Previous Lesson -- Next Lesson
2. Yesu anahojiwa mbele za Anasi na kukana kwake Petro mara tatu (Yohana 18:15-27)
Yohana 18:15-18
„Wakamfuata Yesu, Petro na mwanafunzi mwingine. Na mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika behewa ya Kuhani Mkuu. Lakini Petro akasimama nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine aliyejulikana na Kuhani Mkuu akatoka, akasema na mngoja mlango, akamleta Petro ndani. Basi yule kijakazi, aliyekuwa mngoja mlango, akamwambia Petro, Wewe nawe je! Hu mwanafunzi mmojawapo wa mtu huyu? Naye akasema, Si mimi. Na wale watumwa na watumishi walikuwa wakisimama, wamefanya moto wa mkaa; maana ilikuwa baridi; wakawa wakikota moto. Petro naye alikuwapo pamoja nao, anakota moto.“
Yohanan na Petro walimfuata Yesu usiku ule kutoka mbali kidogo. Kwa vile Yohana alikuwa wa ukoo wa Kuhani Mkuu, aliweza kuingia kwa uhuru ndani ya ua la kuhani. Petro hakuweza kufanya hivyo, kwa sababu mlango ulingojewa na mtumishi.
Yohana alisikia usumbufu wa moyoni mwa Petro, akisimama gizani mlangoni. Kwa kutaka kumsaidia, Yohana akasema na msichana mngoja mlango. Yule hakuridhika kabisa na kumhoji Petro, „Wewe nawe je, hu mmojawapo wa wanafunzi wa yule mtu?“ Akajibu, „Hapana!“ na akajifanya kana kwamba hajui kitu, na hana sehemu katika kesi ile, na baada ya hapo akajaribu kupata joto kwenye moto, maana ilikuwa baridi.
Yohana 18:19-24
„Basi Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu habari ya wanafunzi wake, na habari za mafundisho yake. Yesu akamjibu, Mimi nimesema na ulimwengu wazi wazi; sikuzote nilifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri sikusema neno lolote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena. Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema, Wamjibu hivi Mkuhani Mkuu? Yesu akamjibu, Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini? Basi Anasi akampeleka hali amefungwa kwa Kayafa, Kuhani Mkuu.“
Uchunguzi uliotangulia haikuwa kuhusu hatia ya Yesu, wala kuhusu nafsi yake au madai yake aliyoyatamka. Ilikuwa kuhusu wanafunzi wake na namna alivyofundisha. Wakati ule yalikuwepo mashirika mengi ya kisirisiri. Wachunguzi walitaka kugundua kwa haraka, kama kulikuwa na hatari ya fujo kwa upande wa wanafunzi wake, ili waweze kukomesha fujo yoyote mapema.
Yesu alikataa kwa kuwepo kwa shirika fulani ya namna hii, bali wao wenyewe walijua kwamba, alifundisha wazi saa za mchana ndani ya masinagogi pia na hekaluni, ambapo wengi walihudhuria kumsikiliza. Ikiwa hao viongozi walipenda kumfahamu kwa kweli, wangeweza kwenda mahali pa kukutanika kwake na kusikiliza kinaganaga matamshi yake na wito wake.
Namna hii Yesu aliitika kwa Kuhani Mkuu wa awali bila hofu. Hapo kwa kushitua, mmoja wa watumishi akampiga Yesu, hali akitamani kupata sifa mbele ya Kuhani Mkuu. Yesu hakurudisha pigo wala kuonyesha hasira. Hata hivyo hakupunguza uzito wa tendo hilo la kuvunja sheria, lakini alimtaka yule aliyefanya hilo kosa atamke sababu ya kumjeruhi. Kwa vile Yesu alikuwa bila kosa, yule mtumishi angetakiwa kuomba msamaha na kuonyesha sikitiko.
Jibu hilo la Yesu kwa kweli lilimlenga Anasi, maana yule aliwajibika kwa mtumishi wake na mwenendo wake. Yeye aliruhusu hilo jambo baya. Aina hii ya mshtaka hata siku hizi hufanywa kwa yeyote ampigaye mtu bila sababu ya wazi, au anawaruhusu wafuasi wake kumtisha yule asiye na kosa. Bwana wetu huwapenda wale wadogo wasiohesabiwa na kusema, „jinsi mlivyowatendea hao wadogo wa mwisho, mlinitendea mimi.“
Baada ya Anasi kutambua kwamba Yesu hakushitushwa na matisho yake, bali alisimama kama mwenyewe ni hakimu na kumhoji kuhusu kweli na haki; basi akamtuma Yesu kwa mkwewe Kayafa, aliyejulikana kama mbwa mwitu mjanja, ili asihangaike zaidi na shida hiyo.
Yohana 18:25-27
„Na Simoni Petro alikuwa akisimama huko, anakota moto. Basi wakamwambia, Wewe nawe je! Hu mwanafunzi wake mmojawapo? Naye akakana, akasema, Si mimi. Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule aliyekatwa sikio na Petro, akasema, Je! Sikukuona wewe bustanini pamoja naye? Basi Petro akakana tena, na mara akawika jimbi.“
Kayafa alimhoji Yesu kuhusu wanafunzi wake. Wawili wao walikuwa wakisimama uani, lakini hawakukiri kuwa ni wafuasi wa Bwana. Katika nuru ya miali ya moto Petro alionekana kama mgeni, na watumishi walikuwa na mashaka kama kweli anahusika na Yesu. Na tena Petro alijibu kwa baridi, “Hapana,hapana”. Mmoja wa wale waliomfikiria akatamka kama mashitaka tena. Basi wote walimtupia macho, akachangamka, hasa wakati mmoja wa wale watumishi aliposema, „Mimi nakujua; nimekuona kule bustanini“. Hatari ilifikia kileleni, maana msemi huyu alikuwa jamaa ya yule, ambaye Petro alikata sikio lake. - Yohana hapo haelezi kinaganaga malaumu ya Petro au namna alivyomkana Yesu, lakini anathibitisha hali yake ya Petro mwenye hofu, asiyestahili kuwa mtume kiongozi. Kuwika kwa jimbi ilikuwa kama mlio wa tarumbeta wa hukumu kwa masikio ya Petro.
Yesu hakumpata mwanafunzi hata mmoja aliyekuwa tayari kumfuata hadi kifoni. Wote wao walikuwa wamekimbia, walifanya dhambi, walisema uongo au kumkataa yeye. Wala Yohana hatuelezi habari ya machozi ya Petro au kuungama kwake, lakini Yohana anakazia hatari ya jambo la kumkana Bwana wetu. Jogoo aliwika mara tatu kwa kumchokoza Petro. - Mungu atujalie na sisi tuwe na jimbi atakayewiki kila tunaposema uongo au tunapoogopa kumkiri Bwana wetu. Roho wa kweli anatamani kuja juu yetu na kutuongoza. Umwombe Yesu kukupatia ulimi wa kweli na moyo mnyofu na akili wa kutulia katika kweli.
Sala: Bwana Yesu, tunakushukuru kwa sababu wewe ni Kweli , Uvumilivu na Enzi binafsi. Tusamehe namna zozote za uongo na za kutia chumvi. Wewe ulibeba vifungu vyote vya binadamu, sasa utufunge na Roho yako, ili ndimi zetu zisiweze kutamka maongo tena. Tushike mizizi ndani ya kweli yako, na utufundishe kushuhudia katika jina lako kwa unyenyekevu, kwa hekima na kwa ushujaa.
Swali 111: Kulikuwa na uhusiano gani kati ya Yesu na Petro wakati Yesu alipohojiwa mbele za Anasi ?