Previous Lesson -- Next Lesson
a) Watu walianza kumwegemea Yesu (Yohana 2:23-25)
YOHANA 2:23-25
23 “Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizozifanya. 24 Lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa aliwajua wote; 25 na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu”.
Wakati wa sherehe ya Pasaka mati ya watu walikuja Yerusalemu, pakuu pa kuabudia. Walikuwa wanafikiria habari ya kondoo ambaye aliwalinda babu zao zamani za Misri wasihukumiwe na Mungu, kwa hiyo walikula pamoja nyama ya dhabihu wakati wa chakula.
Yesu, aliye kondoo teule wa Mungu, sasa alifikia Yerusalemu na kutenda ishara nyingi akionyesha upendo na uwezo wake. Wakati huo alipata kujulikana sana na umati na jina lake lilitajwa na wengi. Walikuwa wakinong’onezana, “Je, huyu ni Nabii, au Eliya anayemtangulia, ama labda Masihi mwenyewe?” Wengi walivutwa kwake na kuamini kwamba ametoka kwa Mungu.
Yesu alitazama mioyoni mwao, wala hakuchagua hata mmojawao kuwa mwanafunzi wake. Bado hawakutambua kwamba yeye ndiye Mungu, ila walifikiria mambo ya kidunia. Katika mawazo yao walitazamia kuondolewa utumwani mwa Warumi, kazi nzuri na maisha ya raha hapo mbeleni. Yesu aliwajua watu wote; hakuna moyo iliyofishwa machoni pake. Hakuna hata mmoja aliyemtafuta Mungu kwa makini. Kama wangalimtafuta Mungu kwa moyo kweli, wangalibatizwa Yordani wakiungama na kuomba msamaha kwa dhambi zao.
Kristo anajua na moyo wako, fikira zako, maombi yako, pia na kila dhambi. Anafahamu mawazo yako na mianzo yake. Anakuelewa wewe kwamba unatafuta maisha ya maana na ya haki. Ni lini kiburi chako kitingishwa? Na lini utaacha kujikuza mwenyewe na kumruhusu Roho Mtakatifu akutawale na kukuongoza?
b) Haja ya kuzaliwa mara ya pili (Yohana 3: 1-13)
YOHANA 3:1-3
1 “Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa wayahudi. 2 Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu. Kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. 3 Yesu akajibu akamwambia, Amin, amin, nakwambia, mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu”.
Toka kwa umati wa watu alitokea mmoja aliyeitwa Nikodemo, mwenye msimamo wa kidini na pia mkuu wa wayahudi, mmoja katika wale sabini wa baraza la Sanhedrin. Alitambua nguvu za Mungu ndani ya Kristo. Labda alipenda kujenga uhusiano kati ya nabii huyu mpya na shirika la wayahudi. Pamoja na hayo alimhofu kuhani mkuu na watu wa taifa lake. Alikuwa na shaka juu ya huyu mtu Yesu. Alimjia Yesu kwa siri gizani, akitamani kumjaribu Yesu kabla ya kujiunga na kundi lake.
Kwa kumwita Yesu kwa cheo cha “mwalimu”, Nikodemo alitamka maoni ya watu wengi ambao wanamwona Kristo kama mtu ambaye anafundisha maandiko vema, na akiwa na kundi la wafuasi. Alikubali kwamba Yesu alitumwa kutoka kwa Mungu, akithibitishwa na miujiza. Alikiri, “Tunaamini kwamba Mungu yu pamoja nawe na kukuthibitisha. Labda unaweza kuwa Masihi?” Hii ilikuwa zaidi ya thibitisho la kutosha.
Yesu alijibu swali lake, bila kutegemea maongezi kati ya hao viongozi wa watu na Kristo tu. Alitambua moyo wa kutangatanga wa Nikodemo, dhambi zake na hamu yake ya kutambua ukweli na haki. Angeweza kumsaidia tu baada ya kumwonyesha upofu wake wa kiroho. Mbali na uchaji wake wa Mungu, Nikodemo hakumjua Mungu kwa kweli. Yesu alikuwa wazi kabisa kwake na kumwambia: “Kweli hakuna mtu anayeweza kumjua Mungu kwa uwezo wake mwenyewe; anahitaji kutengenezwa kwa upya kwa njia ya Roho wa mbinguni.
Tangazo hili ilikuwa ni hukumu ya Kristo juu ya mafunzo ya ki-theologia na taratibu za kidini zenye msingi wa kiakili tu. Maana ufahamu wa kweli juu ya Mungu haupatikani kwa mafunzo ya elimu ya juu, lakini kwa kuzaliwa kwa upya. – Kwenye redio, tofauti na TV, unaweza kuzungusha kifungo chake upendavyo, lakini hutapata picha yoyote. Picha zinahitaji chombo tofauti kabisa na redio. Ndivyo ilivyo na mtu wa asili, hata awe mcha Mungu na mwenye bidii kweli, hataweza kumtambua Mungu kweli, sio kwa wazo, wala si kwa kujisikia. Utambuzi huu wa kiroho unahitaji mapinduzi, ambayo ni kuzaliwa kwa upya toka mbinguni, inayomfanya kuwa kiumbe kipya.
YOHANA 3:4-5
4 “Nikodemo akamwambia, “Awezaje mtu kuzaliwa akiwa mzee? Anaweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili , akazaliwa?” 5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, “Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu!”
Jibu la Kristo kwa Nikodemo, ambalo lilimtambulisha kwamba hajamfahamu Mungu, lilimzungusha akili. Alikuwa hajasikia habari ya kuzaliwa mara ya pili. Kusikia hayo, akapata kuchanganyikiwa kwa kuhisi kwamba, mzee angeweza kurudia tumboni mwa mamaye. Jibu kama hilo lilitokana na mawazo ya mwenendo wa kawaida wa maisha, ambayo kiroho ni mawazo mafupi. Hakuweza kuelewa kwamba, Mungu Baba aweza kujipatia watoto kwa njia ya Roho yake.
Yesu alimpenda Nikodemo; baada ya kumwongoza atubu ya kwamba, hajajua njia ya kuingia ulfame wa Mungu, ndipo alimsisitizia ukweli kwamba, yeye ndiye Kweli nafsini mwake. Tunapaswa kuamini kwamba, hatuwezi kuingia ulfame wa Mungu bila kuzaliwa mara ya pili - ndiyo njia ya pekee.
Kuzaliwa mara ya pili ni nini? Ni kuzaliwa, ndiyo, lakini si mtungo wa mimba, wala haitokani na nguvu au bidii ya mtu, kwa sababu hakuna mtu anayeweza kujizaa mwenyewe. Mungu ndiye mzazi na mtoa uhai. Kuzaliwa hivyo kiroho ni neema tupu, si kubadilishwa kwa tabia ya utu, wala si maadili ya jamii. Watu wote wamezaliwa katika dhambi, watenda maovu tangu utoto wao na wako bila matumaini ya kujiboresha. Kuzaliwa kiroho ndio kuingia kwa uhai wa Mungu ndani ya binadamu.
Mambo haya yanatendeka namna gani? Yesu alimwambia Nikodemo kwamba, inawezekana kupitia maji na Roho. Maji yanasimamia ubatizo wa Yohana, pia na mabalasi ya maji ya utakaso wakati wa arusi kule Kana. Washiriki wa nyakati za Agano la Kale walifahamu kwamba maji yalitumika kwa mwosho kuwa mfano wa kusafisha dhambi. Kana kwamba Yesu alikuwa akisema, „Kwa nini hutelemki kwa Mbatizaji, ukaungame dhambi zako na upate kubatizwa?“ Mahali pengine Yesu alisema, “Kama mtu akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwishe msalaba wake na anifuate.“ - Ndugu, ungama dhambi zako, kubali hukumu ya Mungu kwa ajili ya hatia zako! Wewe umeharibu na rushwa na unaenda kupotea!
Yesu hakuridhika na ubatizo wa maji, lakini aliwabatiza wanaoungama kwa Roho Mtakatifu, ili aumbe maisha mapya ndani ya wale walio na moyo wa kuvunjika na kutubu. Baada ya kusulibishwa kwake tunajifunza kwamba, kuoshwa kwa dhamiri zetu ni kwa damu yake ya thamani. Kutakaswa hivyo ndiyo kazi ya Roho Mtakatifu. Wakati mtu anapovutwa na Roho, anajazwa na uhai wa milele na matunda yake. Tabia yake inakuwa safi, akiongozwa na Yesu. Kubadilishwa hivyo inachukua muda; kama vile ilivyo kwa mtoto anavyokua tumboni mwa mamaye ndipo akazaliwa. Ndivyo ilivyo kuzaliwa mara ya pili kwa mwumini.
Yesu alifanya mambo hayo kuwa shabaha ya mahubiri yake, au shabaha ya ufalme wa Mungu. Na sasa ufalme huu ni nini? Sio mwendo fulani wa siasa ama njia ya kupata pesa au utajiri, lakini ni ushirikiano wa wazaliwa wa mara ya pili pamoja na Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Roho huyu wa baraka anawajia kadiri wanavyojitoa kwake Kristo na kumtambua kuwa Mfalme ambaye wanastahili kumtii.
SALA: Bwana Yesu, nakushukuru kwa kunizaa kiroho mara ya pili kwa rehema pekee. Umenifumbua macho ya kiroho. Unitunze ndani ya upendo wako. Na wafumbulie macho wale wanaokutafuta kwa moyo wote, wajua dhambi zao na kukiri, ili wafanyike wapya pia kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Wapate nao kutegemea damu yako iliyotiririka, ili wasikose kuingia katika ushirikiano na wewe kwa hali ya kudumu.
SWALI:
- Ni nini tofauti kati ya uchaji wa Mungu wa Nikodemo na malengo yake Kristo?