Previous Lesson -- Next Lesson
1. Kutakaswa kwa hekalu (Yohana 2:13-22)
YOHANA 2:13-17
13 „Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu. 14 Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. 15 Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao. 16 Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, „Yaondoeni haya! Msifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara“. 17 Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa: Wivu wa nyumba yako utanila.“
Yesu alitembelea mji wa Yerusalemu wakati wa sikukuu ya Pasaka, mahali ambapo maelfu na maelfu ya wayahudi toka kote ulimwenguni wakikusanyika. Kusudi lao ilikuwa kutoa dhabiu za kondoo kwa kumbukumbu kwamba ghadhabu ya Mungu haikuwapata kwa sababu ya kutoa kondoo wa Pasaka. Bila kumwaga damu hakuna ondoleo la dhambi. Na bila upatanisho ibada haina maana. Kwa hiyo Yesu alijitwisha na kuondoa dhambi zao kama mfano katika ubatizo wa mtoni Yordani. Kwa niaba yao alikubali ubatizo wa kifo kama mfano wa kuchukua ghadhabu ya Mungu. Alijua ndani yake kwamba kweli yeye ndiye kondoo wa Mungu aliyechaguliwa naye kwa kusudi hili.
Wakati alipoingia mji na kuelekea ua la hekalu, hakustaajabu uzuri wa jengo, lakini alikuwa anatafakari juu ya wokovu kwa mwanadamu kwa njia ya kafara yake. Ilimshangaza kwamba, hakuona hali ya utulivu hekaluni kwa ajili ya ibada. Alichopata ni vumbi na makelele za ng’ombe na ugomvi za wafanyi biashara na damu za wanyama. Pia alisikia sauti za wabadilishaji wa fedha za kigeni kwa pesa za kiyahudi, ili waweze kulipia ada zao.
Kelele zilizosikika hekaluni zilidhihirisha kwamba utakaso unaweza kununuliwa kwa fedha na juhudi za pekee. Waenda haji walidhania kwamba neema na utakaso zinanunuliwa kwa dhabihu na kawaida za dini, wala hawakutambua kwamba wokovu hauwezi kupatikana kwa sababu ya matendo mema.
Hapo Yesu alionyesha uchungu wake wa haki. Shauku kwa ajili ya ibada ya kweli ilimsukuma kuwafukuza wafanyi biashara wa ngombe na kutawanya pesa vumbini. Hatusomi kwamba alimpiga yeyote yule, lakini sauti yake ilitamka juu ya makonde ambayo Mungu angewapiga wale ambao hawatulii mbele ya utukufu wa Mungu. Hakuna uchaji wa Mungu hapo duniani inayompendeza, ila moyo wenye kuvunjika na kunyenyekea mbele za Mtakatifu.
Yesu alihuzunishwa na kutokujali kwa watu kwa habari ya utakatifu wa Mungu. Kupuuza na pia kutokuelewa kwao kulijionyesha katika tabia zao za kuabudu juu-juu tu. Hayo yalionyesha giza ambayo ilifunika mioyo na akili zao, ingawa walikuwa na torati na sheria za Musa tangu miaka elfu moja mia tatu kabla ya hapo. Kwa sababu ya haya Yesu alitokeza ghadhabu tukufu na wivu takatifu, ili atakase mahali hapa pa kukutakanika kwa ibada. Mahali pa katikati pa kuabudu ilidhihirisha hali mbaya kwa jumla ya taifa lote. Yesu alidai kufanya upya kiini cha dini yao, mabadiliko kabisa katika mtazamo wao kwa Mungu.
YOHANA 2:18-22
18 „Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya hayo? 19 Yesu akajibu akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha. 20 Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha kwa siku tatu? 21 Lakini yeye alisema habari za hekalu la mwili wake. 22 Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu“.
Makuhani walifahamu habari ya kutakaswa kwa hekalu na huku vilio vya wafanyi biashara, kwa hiyo wakamwendea Yesu kwa haraka na kumwuliza: Nani alikuruhusu kufanya mambo haya? Ni nani aliyekutuma? Tupe ukweli na thibitisho kuhusu mamlaka yako! Hawakupinga kutakaswa kwa hekalu; walihisi kwamba Yesu hakufanya haya kwa hasira ya kibinadamu, lakini kwa juhudi kweli kwa heshima ya nyumba ya Mungu. Walihisi atarejesha roho ya ibada kwa watu wengi. Hata hivyo walitaka kuhakikisha sababu na malengo yake yaliyomsukuma. Kwa hiyoYesu alipata kuwa adui machoni pao, kwa sababu walifikiri alitaka kuleta mageuzi hekaluni bila idhini ya shirika lao la kikuhani.
Yesu aliwakemea kwa sababu ya unafiki wa kufanya ibada zao, kwa sababu walipendelea umati wa waabuduo kwa fujo na uwezo wa utajiri, badala ya utulivu wa uwepo wa Mungu. Kwa uwezo wa unabii Yesu aliona kubomolewa kwa hekalu kama matokeo ya ibada za unafiki na kutokujali kwao. Taratibu za desturi za kidini na maadhimio yaliyopangwa nao hayawezi kumwokoa mtu. Bali ni kubadilishwa moyoni kwa ukweli wa Mungu ndiyo inayookoa.
Kuwepo kwa Yesu aliyezaliwa mwilini ilikuwa ni wokovu katikati yao. Yesu ndiye hekalu la kweli. Mungu alikuwapo kati yao ndani ya Yesu. Kana kwamba Yesu alisema: „Mkabomoe hekalu la mwili wangu kwa sababu hamwezi kuvumilia wivu wangu kwa ajili ya Mungu. Mtafanya yasiyowezekana, yaani kuharibu hekalu hili, lakini nitainua mwili huu katika muda wa siku tatu; nitafufuka kutoka kaburini. Mtaniua, lakini niko hai kwa sababu mimi ndimi uhai. Mungu yumo mwilini, hamwezi kuniua“. Hivyo Yesu alitangaza ukweli wa kufufuka kwake. Na hadi leo ufufuo wake ndiyo mwujiza kuu kuliko yote.
Wajumbe toka kwa kuhani mkuu hawakuelewa mfano huu kuhusu hekalu. Wao walistaajabia uzuri wa nguzo na dari ya dhahabu za hekalu na kumfikiria Yesu kwamba alikufuru mahali tukufu Mungu alipokusudia kukaa kati yao, na lililojengwa kwa miaka arobaini na sita. Wao waliongea juu ya mawe, yeye alimaanisha mwili wake. Mahojiano haya muhimu mwanzoni mwa huduma yake yalitokea tena wakati wa hukumu yake mbele ya baraza kuu la wazee wa kiyahudi, yakigeuzwa kupitia kwa matamshi ya washahidi waongo.
Kwa kweli, watu wa Agano la Kale walishindwa kutambua ukweli wa imani mpya ambayo Kristo aliianzisha. Wala hata wanafunzi wake hawakuelewa maana ya undani wa imani hii mpya hadi wakati wa kifo cha Yesu na kufufuka kwake. Baada ya hapo walipata kuelewa jinsi Mwana alivyolipia dhambi na kufufuka tena.
Siku hizi Kristo yupo pamoja nasi katika hekalu lake la kiroho, ambalo nasi tumejengwa ndani yake kama mawe yalio hai. Roho Mtakatifu aliwaangazia wanafunzi, ili wagundue maana katika vitabu vya zamani, ambazo ziliangaziwa na maneno ya Yesu. Walidumu imara katika imani, na kwa pamoja wakawa hekalu takatifu la Mungu, ambalo ni kanisa lake.
SALA: Ewe Bwana Yesu, wewe ndiwe mahali ambapo Mungu anakaa kati yetu, na mahali Mungu anapokutana na wenye dhambi. Tusaidie ili tufanye ungamo na ibada ya kweli na tupate kujazwa na ukamilifu wako. Hivyo utujenge kuwa pamoja hekalu la Roho Mtakatifu na kumtukuza Baba wakati wote.
SWALI:
- Kwa nini Yesu alitembelea hekalu na kuwafukuza nje wafanyi biashara?