Previous Lesson -- Next Lesson
a) Mwujiza wa kuvua samaki wengi (Yohana 21:1–14)
Yohana 21:7-8
“Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini. Na hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata diraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki.”
Mwinjilisti (Yohana) alitambua kwamba kupata samaki wengi namna hii haikutokea hivi hivi tu. Ingawa naye alikuwa chomboni, alifahamu kwamba yule mtu pale pwani si mwingine ila ni Yesu mwenyewe. Yohana hakutamka jina la Yesu, lakini kwa heshima alisema, “Ndiye Bwana!”
Hilo lilimshtusha Petro alipokumbuka kwamba Kristo sasa alifundisha mara ya pili somo maalum kwa njia ya kuvua samaki. Alienda kuchukua nguo zake na kuvaa haraka, maana hakupenda kutokea mbele za Bwana wake akiwa uchi. Alijitupa majini na kuogelea kumwelekea Bwana, hivyo akaacha chombo, rafiki zake na samaki wabichi nyuma. Alisahau kila kitu, kwa sababu moyo wake ulimwelekea Yesu tu.
Yohana alibakia chomboni, ingawa upendo wake ulikuwa nyofu, sawa na ya Petro. Basi huyu kijana pamoja na wenzake wakapiga makasi kwa nguvu kuelekea pwani kama meta 100 zilizobakia. Mwishowe na wao wakafika ufuoni na kushughulikia samaki wengi waliokamatwa.
Yohana 21:9-11
“Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki na mkate. Yesu akawaambia, Leteeni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi. Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka.”
Wanafunzi walipofika pwani, waliona moto wa makaa ikiwa na samaki juu yake. Basi toka wapi moto uliletwa, pia na samaki na mkate? Alikuwa amewaita toka umbali wa meta mia moja, maana hawakuwa na chakula. Kufika tu wakaona samaki waliokaangwa tayari, akawakaribisha wale. - Yeye ndiye Bwana na vilevile ni mkaribishaji kwa wakati moja. Kwa upole aliwapa nafasi katika kutayarisha chakula zaidi. - Yeye anaturuhusu na sisi kushirikiana katika kazi zake na katika matokeo. Kama wanafunzi wasingalitii agizo lake, wasingalikamata kitu. Lakini yupo hapo akiwakaribisha wale. Kiajabu, Bwana asiyehitaji chakula cha dunia hii, akainama na kushiriki pamoja nao chakula kile, ili wasikie na upole na shauku yake kwao.
Hesabu ya samaki 153 inarejea kwa hesabu ya aina za samaki zilizojulikana wakati ule, hii ni kufuatana na mapokeo ya zamani. Basi ilikuwa kana kwamba Yesu anawaambia, “Msivue aina moja ya wanadamu tu, lakini waleteni kutoka kwa mataifa yote.” Wote wanaombwa kuingia uzima wa Mungu. Jinsi ambavyo hata jarife haikupasuka kwa sababu ya uzito, hivyo hata Kanisa halitapasuka au kupoteza umoja wa Roho Mtakatifu, hata ikiwa baadhi ya washiriki wao wakiendelea na maisha ya umimi na bila upendo. Kanisa la kweli litakuwa mali yake na litakuwa lenye nguvu.
Yohana 21:12-14
“Yesu akawaambia, Njooni mfungue kinywa. Wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza, U nani wewe? Wakijua ya kuwa ni Bwana. Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa, na samaki vivyo hivyo. Hiyo ndiyo mara ya tatu ya Yesu kuonekana na wanafunzi wake baada ya kufufuka katika wafu.”
Yesu aliwakusanya wanafunzi wake wazunguke ile moto wa upendo wake. Hakuna aliyethubutu kusema neno, maana wote walijua kwamba huyu mgeni ndye Bwana mwenyewe. Walitamani sana kumkumbatia, lakini hofu na kicho ziliwazuia. Yesu alivunja ukimya na kuwabariki alipoanza kuwagawia chakula. Kwa njia hii aliwasamehe na kuwafanya wawe wapya. - Wanafunzi wote hata sasa huishi katika uradhi wa Bwana wao daima; bila uaminifu wake kwa ajili ya agano lake nao, wangepotea tu. Wote ni wazito kutegemea au kutumaini. Yeye hapo hakuwakemea, lakini aliwaimarisha kwa chakula chake cha kimwujiza. Hata hivyo, Yesu na Mungu wanakuhitaji ushirikishe kwa wengine Habari Njema mbali na dhambi na uzembe wa moyo. Hii ndiyo taratibu anayofuata Yesu kwa kutenda miujiza baada ya ufufuo wake.
b) Petro athibitishwa katika huduma ya kundi (Yohana 21 : 15-19)
Yohana 21:15
“Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je, Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu.”
Kwa neno hilo la AMANI, Yesu aliwasamehe wanafunzi wake pamoja na kukana kwake Petro, alipowatokea mara ya kwanza. Lakini kule kukana kwa Petro kulihitaji dawa ya pekee. Hapo rehema zake ikajionyesha katika maneno ya Bwana, yeye anayechunguza mioyo. Hakutaja lolote kuhusu jambo lile la kukana, ili ampatie nafasi ya kujipima na kujitambua mwenyewe. Akamtaja Petro kwa jina lake la awali, Simoni, mwana wa Yona (Biblia ya Kiswahili inasema “Yohana”, lakini kiingereza na kijerumani inasema “Yona”), kwa ajili ya kurudi kwake katika mwenendo wake wa awali. –
Namna iyo hiyo Yesu akuuliza leo, “Unanipenda? Umeshika maneno yangu na kutegemea ahadi zangu? Umeshika kabisa asili yangu na kuja karibu nami? Umejiunga na daraja langu na kuacha mali yako, muda na nguvu kwa ajili yangu? Mawazo yako kila wakati yako kwangu na umepata kuwa kitu kimoja nami? Unaniheshimu kwa maisha yako?”
Yesu alimwuliza Petro, “Unanipenda kuliko hawa?” Petro hakujibu, “Hapana, mimi si bora kuliko wenzangu wote; nimekukana.” Petro bado alikuwa na tegemeo juu ya nafsi yake na kujibu “ndiyo”, lakini alionyesha mipaka ya upendo wake kwa kutumia tamko la kigriki kwa neno la upendo, wala si upendo tukufu kutokana na Roho Mtakatifu na tegemeo la imani.
Petro hakukemewa kwa ajili ya upendo wake dhaifu, lakini alishurutishwa na Bwana kuthibitisha upendo wake kwa njia ya kuwatunza wafuasi wake. Yesu alimtuma huyu mwanafunzi wa kusitasita aende kuwachunga hao wachanga wake wa imani. - Mwana Kondoo wa Mungu alijinunulia kondoo wawe wake. Je, u tayari kuwahudumia wa namna hiyo, kuchukuliana nao, kuwaongoza kwa uvumilivu, na kungoja wapate kukomaa? Au unatazamia mengi zaidi toka kwao kuliko uwezo wao? Au umewaacha wakasogea mbali na kundi na mwishowe kuraruka kabisa na kuacha? Yesu alimtaka Petro kwanza awachunge wale walio wachanga kiimani.
Yohana 21:16
“Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu.”
Yesu hakumwacha Petro hivi hivi tu kana kwamba kusema, “Hukunijibu haraka uliposema, Ndiyo nakupenda? Je, upendo wako si ya kibinadamu tu na ya upungufu? Je, upendo wako si ya maono ya urahisi tu, au kweli ni ya msingi wa moyo mweupe?”
Swali hilo liligusa moyo wa Petro, akaitika kwa unyenyekevu, “Bwana, wewe wajua kila kitu, unafahamu mipaka yangu na uwezo wangu pia. Upendo wangu kwako haufichiki. Nakupenda kwa kweli na niko tayari kutoa maisha yangu kwako. Nimekosa na nitarudia kukosa. Lakini upendo wako umechochea upendo wa daima ndani yangu.”
Yesu hakukataa matetezi ya Petro, lakini alimwambia, “Jinsi unipendavyo, basi upende na washiriki wazima wa Kanisa langu. Kuwatunza vema kichungaji si rahisi. Wengi wao ni wakaidi, wenye kurudi nyuma, na kila mmoja akifuata njia yake mwenyewe. Uko tayari kubeba kondoo zangu mabegani mwako bila kuchoka? Wewe unawajibika kwa ajili yao.”
Yohana 21:17
“Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwuliza mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.”
Petro alikuwa amemkana Bwana wake mara tatu, basi Yesu aligonga mlangoni mwa moyo wake mara tatu na hivyo kujaribu ukweli wa upendo wake. Alikazia kabisa haja ya upendo tukufu wa kutoka kwa Roho Mtakatifu, wakati Petro alitakiwa kugundua ndani yake kwamba: Hakuwa nao mpaka wakati wa Roho Mtakatifu kushuka juu yake siku ya Pentekoste. Aliendelea kumchunguza, “Kweli umeungamana nami zaidi kuliko kwa ushirikiano mwingine yoyote ya kibinadamu, kwa kiasi cha kukubali kutoa uhai wako kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu?” Na kwa mara ya tatu Petro alijibu kwa huzuni na aibu, akaongeza kwamba Bwana ajua moyo wake.
Petro alikiri kwamba Yesu alikuwa sawa katika kutabiri mara tatu kukana kwake, na ya kwamba Kristo alifahamu mambo yote. Basi Petro alimwita Mungu wa kweli, ajuaye ya ndani kabisa ya nafsi yake. Haya, hii ndiyo shughuli ya kicchungaji iliyokabidhiwa kwake Petro - kuwachunga kondoo.
Je, wewe ni mchungaji anayeangalia juu ya kundi la Mungu? Unaona mbwa mwitu na roho mbaya zinazovizia kundi? Kumbuka, sote tu wenye dhambi, tusiostahili heshima hiyo ya kuchunga watu wa Mungu, isipokuwa kwa uwezo wa msalaba. Bila shaka, wachungaji huhitaji masamaha zaidi kila siku kuliko kondoo; mara nyingi hawajali kwa kutosha kuwajibika kwao.
Sala: Bwaba Yesu Kristo, wewe ndiwe Mchungaji Mkuu. Umeniita niwe mchungaji, wala mimi sistahili huduma hii. Nakufuata na kusita. Umekabidhi kondoo wa rehema zako za upendo kwangu. Mimi nawakabidhi kwako, nikikusihi uwatunze, ukiwahakikishia uzima wa milele, ukiwalinda mikononi mwako, ili yeyote asiweze kuwanyang’anya. Uwatakase, na utujalie uvumilivu, unyenyekevu, tegemeo, imani na tumaini kwa kushika mizizi ndani ya upendo wako. Hutaniacha, bali kunipenda bila kikomo.
Swali 131: Jambo gani limekugusa zaidi katika mazungumzo ya Yesu na Petro?