Previous Lesson -- Next Lesson
b) Petro athibitishwa katika huduma ya kundi (Yohana 21:15-19)
Yohana 21:18-19
“Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka. Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo, akamwambia, Nifuate.
Yesu alielewa moyo wa Petro, mwanafunzi wake, kuwa ni yenye bidii na tabia ya kuvutwa kwa urahisi. Mara nyingi tunakuta tabia hii ya ujasiri katika mwenendo wa vijana wanapoonyesha imani mara ya kwanza ndani ya Kristo. Mara wanapotambua nguvu ya Roho Mtakatifu, wanachangamka na kufanya haraka kuwaokoa wengine. Lakini mara nyingi, wanahudumia kwa uchangamfu ya kibinadamu tu, sio ndani ya uongozi wa Yesu, ambaye ni mwenye upole, maombezi na kwa kushirikiana.
Hata hivyo, Yesu alimtabiria Petro kwamba atatumia sana tegemeo lake ndani ya nafsi yake na polepole kukomaa kiroho, akijitoa zaidi kwa Bwana wake, kama mwenye kushikwa na upendo wake, akitamani yale tu yanayompendeza Kristo.
Petro aliendelea kukaa Yerusalemu, wala hakwenda kwa mataifa mengine. Alikuwa anapigwa na kutupwa gerezani mara kwa mara; wakati fulani alifunguliwa na Malaika wa Bwana. Mara nyingine aliongozwa na Roho Mtakatifu kwa nyumba ya Kornelio, akida wa kirumi, alipogundua kwamba, Roho Mtakatifu aliweza kushuka juu ya wapagani, ambao hadi hapo walihesabiwa kuwa wanajisi. Kwa hatua hii katika uinjilisti Petro alifungua mlango kwa huduma ya utume (missioni) ulimwenguni kote.
Baada ya kufunguliwa kwenye gereza la Herode, Petro alizungukia makanisa machanga yaliyoanzishwa, hasa baada ya Paulo kutupwa gerezani. Hivyo, huyu mtume mkuu alitembelea Wakristo waliotoka kwenye upagani, akiwatia moyo kwa ujumbe wa ki-baba hapa na pale. Mapokeo ya awali yanasema kwamba alifia Rumi wakati wa fukuzo la Kaisari Nero.
Akijihesabu mwenyewe kwamba hastahili kifo cha msalaba kama Bwana wake, aliwaomba wauaji wake wamsulibishe juu chini, yaani kichwa chini. Yesu alikuwa ametaja hilo, aliposema, Petro atamtukuza Mungu hivyo katika kifo chake.
Kabla ya hapo, Petro alikuwa amedokeza kwa Yesu, kwamba yu tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya Bwana wake. Hapo Yesu alimjibu, “Huwezi kunifuata sasa, lakini utafanya hilo mwishoni.” (Yohana 13:36) Yesu aliunganisha wanafunzi wake kwa nguvu na utukufu wake wawe kitu kimoja naye, pia na Baba na Roho Mtakatifu. Aliwafanya wawe washiriki katika mateso na kufo chake, ambazo ndizo tangulizi za utukufu. Utukufu ndani ya Injili haimaanishi kung’aa au kuwa na heshima kwa namna ya kidunia, lakini kuvumilia hadi msalaba kwa ajili yake Yeye atupendaye. Petro hakuweza kumtukuza Mungu kwa namna yake mwenyewe, lakini damu ya Kristo ilimsafisha, na nguvu ya Roho ilimtakasa, hata akajikana mwenyewe, akaishi kwa ajili ya Bwana wake, akafa pia kwa kumtukuza yeye.
Mwishowe, Kristo alimpa Petro agizo la kijeshi: “Nifuate!”. - Kwa kadiri tunavyomfuata yeye maishani hata kifoni, tutachumilia matunda ya upendo na kutukuza jina la Baba mwenye rehema.
Sala: Bwana Yesu Kristo, tunakushukuru kwa sababu hukumkataa Petro, iwapo alikukana, lakini ulimwita kutukuza Utatu Utakatifu kwa maisha na kifo chake. Chukua pia maisha yetu, na utusafishe, ili tuweke mapenzi yetu kabisa chini ya uongozi wako, tuendelee kuzishika maagizo yako, tupende hata adui zetu, na tukuheshimu kwa utii katika imani hadi mwisho, ili na maisha yetu yapate kuwa sifa kwa neema yako.
Swali 132: Jinsi gani Petro alimtukuza Mungu?