Previous Lesson -- Next Lesson
4. Baba alitukuzwa katikati ya fujo (Yohana 12:27-36)
YOHANA 12:27-28
“Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. Baba, ulitukuze jina lako. Basi, ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.“
Yesu aliteseka ndani ya kiini cha nafsi yake. Yeye ndiye Mfalme wa uzima, lakini akajinyenyekeza hadi kifo, ili ammeze. Yeye ndiye Mfalme wa Wafalme, lakini alimwachilia shetani, mtawala wa enzi ya kifo, amjaribu na mamlaka yake yote. Yesu alibeba dhambi zetu zote kwa hiari, ateketee badala yetu katika miali ya moto ya ghadhabu ya Mungu. Yeye ndiye Mwana ndani ya umoja na Baba tangu milele. Kwa ajili ya wokovu wetu Baba alimwachilia katika upweke, ili sisi tuweze kuunganika naye baada ya hapo kwa neema. Hakuna awezaye kutambua kwa ndani hasa maumivu na uchungu wa Mwana na Baba. Umoja wa utatu ulikuwa taabuni kwa ajili ya kutuokoa sisi.
Mwili wa Kristo haukuweza kuvumilia mshindo wa kupondekwa hivyo. Alilia: “Baba, Uniokoe katika saa hii!” Akasikia sauti ya Roho ikiitika waziwazi moyoni mwake, “Umezaliwa kwa ajili ya saa hiyo. Saa hii ndiyo lengo la tangu milele. Uumbaji wote pamoja na Baba walitazamia kwa shauku dakika hii, ambapo ubinadamu upatanishwe na Mungu, uumbaji wote na Mwumba wake. Hapo hapo mpango wa wokovu utakuwa umekamilika.”
Kwa kuthibitishiwa hayo, Yesu akalia wazi, “Baba, utukuze jina lako!” Mwana asingeweza kujali sauti ya mwili wake. Aliomba kwa kupatana katika umoja wa Roho Mtakatifu, “Litukuzwe jina lako, ili ulimwengu upate kutambua kwamba wewe siyo Mungu wa kutisha, uliye mbali na bila kujali, bali u Baba wa kupenda, ajitoaye ndani ya Mwana, ili awaokoe walio waovu na wenye kupotea.”
Mungu hakusita kujibu kilio cha Mwanaye. Alijibu toka mbinguni: “Nimetukuza jina langu ndani yako. Wewe ndiwe mwanangu mtiifu na mnyenyekevu. Yeyote akuonaye wewe aniona mimi. Wewe ni mpendwa wangu, ndani ya huduma yako nimependezwa kabisa. Sina furaha nyingine zaidi kuliko hilo la kubeba msalaba wewe. Katika kifo chako kwa niaba ya binadamu, humu nitadhihirisha kiini cha utukufu wangu katikati ya dhoruba ya mazito ya maisha. Msalabani unatangaza maana ya utukufu na utakatifu wa kweli. Ni ukuu wa ajabu wa upendo na sadaka na kujitoa kabisa kwa ajili ya wasiostahili na wenye mioyo migumu.”
Sauti ya mbinguni iliendelea kurudia waziwazi, “Nitatukuza tena jina langu, hapo utakapofufuka kutoka kaburini na kupaa kwangu, ili uketi pamoja nami katika utukufu, ukimimina Roho yangu juu ya wapendwa wako. Ndipo jina langu la ki-baba litainuliwa mno kwa ajili ya kuzaliwa kwa upya watoto wasioweza kuhesabiwa, yote kwa huduma ya Roho Mtakatifu. Kuwepo kwao kutaniheshimu mimi; mwenendo wao wa nguvu utanitakasa mimi. Kifo chako msalabani ndiyo sababu ya kuzaliwa kwa watoto wa Mungu. Maombezi yako yenye utukufu yatakuwa thibitisho la kufaulu kwa Kanisa. Ndani yako pekee Baba hutukuzwa daima bila kukoma. “
YOHANA 12: 29-33
“Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika alisema naye. Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu. Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu. Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa.”
Makutano waliomzunguka Yesu hawakuweza kutambua kwamba Yesu aliongea na Mungu, bali walifikiri ilikuwa ni sauti ya ngurumo ya radi. Hawakuweza kutofautisha au kutambua kwamba Mungu ni upendo tupu, wala hawakuweza kusikia sauti yake laini, tena walishindwa kuelewa kwamba kwa kufunuliwa kwa utukufu wa Mungu ndani ya Mwana hukumu juu ya ulimwengu ulikuwa umeanza.
Shetani alinyang’anywa na mshiko kwa watumwa wake; tangu Kristo alipoinuliwa juu ya msalaba na kutupatia uzima kwa njia ya kifo chake. Huyu Mwovu aliondolewa na utawala wake kwa njia ya utoaji wa Mwana chini ya mapenzi ya Baba. Yesu alimwita huyu ibilisi kuwa ni Mfalme wa dunia hii, kwa kuzingatia ukweli huo kwamba ulimwengu mzima uliwekwa ndani ya utawala wake. Kwa kutazama hali hii halisi ya kuumiza na ya uchungu, Yesu hakusita hata kidogo, bali alimpiga Shetani kwa upanga wa haki yake, akitimiza mpigo wa kufisha. - Sasa sisi tu huru, watoto katika jina la Yesu.
Sisi sasa tunavutwa kwa msalaba wake. Shetani alimchukia kiasi cha kuzuia Yesu asife chini ardhini au kitandani mwake, bali aliwafanya wamwinue afe juu ya msalaba wa aibu. Lakini jinsi yule nyoka alivyoinuluwa kule jangwani wakati wa Musa alivyoleta mwisho wa adhabu ya Mungu juu ya walioamini, hivyo ndivyo msalaba inajumlisha hukumu yote mabegani mwa Kristo. Mungu haangamizi tena wale wanaomtazama Msulibiwa. Imani yetu ndani ya Kristo inatusulibisha pamoja naye na kutuunganisha ndani ya kifo chake. Tutakuwa tumefia dhambi na kuishi kwa ajili ya haki.
Umoja wetu na Kristo unatuunganisha pia na nguvu na utukufu wake. Jinsi yeye alivyoshinda dhambi na mauti katika utakatifu, ndivyo naye atatuvuta nyuma yake na kutukaribisha kwenye utukufu wake. Wote wanaomtegemea yeye hawatapotea kabisa, bali watakuwa na uzima wa milele.
YOHANA 12:34
“Basi mkutano wakamjibu, Sisi tumesikia katika torati ya kwamba Kristo adumu hata milele; nawe wasemaje ya kwamba imempasa Mwana wa Adamu kuinuliwa? Huyu Mwana wa Adamu ni nani?”
Wayahudi walijaribu kumshurutisha Yesu, wakimtaka atoe thibitisho la wazi na ya kukubalika kiakili, ili waweze kuridhika bila kuchunguza zaidi kutokea kwake. Walifahamu maelezo ya kitheologia ya kitabu cha Danieli, sura ya 7, ambapo Masihi aitwa Mwana wa Adamu na Mhukumu wa ulimwengu. Hata hivyo walitamani kusikia toka mdomoni mwake akijiita Mwana mtukufu. Hawakufanya hilo kwa ajili ya kujitoa wenyewe na kujaribu kuamini, mbali na hilo wangetoa tamko la kusadiki la juujuu, kama yeye angethibitisha kwamba, yeye ndiye yule aliyedai kuwa. Baadhi yao walikuwa ni maadui wenye makusudi maovu, wakitamani kumtega katika tamko la kukufuru, kama yeye angetamka wazi kabisa kwamba yeye ndiye Mwana wa Adamu. Yesu huwa hajifunui mwenyewe kwa wachunguzi wa njia ya kiakili tu, ila hujifunua mwenyewe kwao waaminio kwa moyo mweupe, wanaoitika kwa mvuto wa Roho Mtakatifu, na wanaokiri kwamba Mwana wa Adamu ndiye Mwana wa Mungu, hata kabla hawajapokea mathibitisho ya kiakili.
YOHANA 12:35
“Basi Yesu akawaambia, Nuru ingaliko pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo nuru hiyo, giza lisije likawaweza; maana aendaye gizani hajui aendako.”
Yesu ndiye nuru ya ulimwengu, tukitambua kwamba nuru haihitaji maelezo ya kinaganaga. Inatambulukana kwa sababu watu wa kawaida waweza kuona nuru na kuitofautisha na giza. Muda wote ambapo bado ni mchana, mtu aweza kusafiri au kutembea, hata kukimbia. Usiku mtu hawezi kufanya kazi. Wakati jua linapowaka ndiyo muda wa kufanya kazi na kushughulika. Yesu aliwaeleza Wayahudi kwamba, ni muda mfupi unaobaki kwao kuingia ndani ya eneo lake la nuru, ikiwa wanapenda. Wakati kama ule ulihitaji kuamua, kujitoa na kuimarika.
Hata hivyo, yeyote aikataaye nuru, atabakia gizani bila kujua njia yake. Hayo ndiyo mambo ambayo Yesu aliwatabiria Wayahudi mapema, na kwamba wataendelea kutapatapa gizani, bila kuwa na mwelekeo au shabaha na bila tumaini. Giza la namna hii lisichanganywe na giza la kawaida ya usiku, ambayo ni nje ya nafsi zetu. Ni giza lile la ndani, linalotengenezwa na roho mbaya ndani ya mtu. Hivyo mtu wa namna hii anakuwa giza ndani yake na mwenye huzuni maisha yote. Yeyote asiyemwelekea Kristo, hatimaye atakumbwa na giza . - Je, wewe waweza kuona, kwa nini mataifa fulani ya “kikristo” wamebadilika kuwa kama asili ya giza ndani ya ulimwengu? Siyo kila mtu aliyezaliwa “kikristo” ametoa maisha yake kwa Kristo. Ni wachache waliopo walio Wakristo wa kweli. Mtu yeyote atashikwa na giza asiyeingia ndani ya eneo la nuru ya Yesu. Hutaweza kurithi baraka za Injili kutoka kwa wazazi wako na kwa kufuata kwa kawaida tu. Ni juu yako wewe binafsi kuitika, kukubali na kujitoa kwake Kristo.
YOHANA 12:36
“Maadamu mnayo nuru, iaminini nuru hiyo, ili mpate kuwa wana wa nuru . Hayo aliyasema Yesu, akaenda zake, akajificha wasimwone.”
Kujiunga na Kristo wewe kwa imani, hayo yatakubadilisha kabisa kabisa. Injili inamwaga miali ya utukufu wa Mungu, ambayo ni yenye nguvu zaidi kuliko miali ya atomik. Lakini iwapo miali ya atomik huharibu, miali ya nuru ya Kristo huumba uzima wa milele ndani yetu, na hivyo mwamini anakuwa mtoto wa nuru na nyumba yenye nuru kwa ajili ya wengi. Je, umeingia ndani ya upana wa kumbatio wa Kristo, ukijaa tele ukweli, usafi na upendo? Yesu akuita utoke kwa giza lako, uje ukaingie kwenye nuru yake ya ajabu na uwe mtakatifu.
Baada ya kumaliza hotuba yake kabla ya kuingia kwake Yerusalemu hakujitwalia enzi kwa nguvu au kwa kuwashambulia Waroma au Mfalme Herode akitumia silaha, hapana. Mashindano yake yalikuwa yamemalizika na hukumu ya ulimwengu ilikuwa ni giza. Nuru hung’aa gizani; waumini wakawa wamesalimika na wasioamini kupotea. Mgongano kati ya mbingu na dunia ilikuwa imefikia kilele chake. Mungu huwa hawalazimishi watu waamini. Je, wewe umepata kuwa mtoto wa nuru, au unabakia kuwa mtumwa wa giza?
SALA: Tunakushukuru, Bwana Yesu, kwamba umejifunua kuwa ndiwe nuru ya ulimwengu. Utuvute ndani ya miali ya rehema yako na kutufanya tuwe wenye rehema. Badilisha mwangalio wetu toka kwenye pesa, madaraka au ushindi wa kidunia, hata tuweze kukufuata katika maisha ya kila siku, na tukadumu kuwa watoto wa nuru yako.
SWALI:
- Sisi kupata kuwa wana wa nuru inamaanisha nini?