Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- John - 080 (Men harden themselves)
This page in: -- Arabic -- Armenian -- Bengali -- Burmese -- Cebuano -- Chinese -- English -- Farsi? -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Kyrgyz -- Malayalam -- Peul -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Thai -- Turkish -- Twi -- Urdu -- Uyghur? -- Uzbek -- Vietnamese -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

YOHANA - Nuru inaangaza gizani
Somo la Injili ya Kristo kufuatana na Mtume Yohana
SEHEMU YA 3 - Nuru yang’aa ndani ya shirika la Mitume (Yohana 11:55 - 17:26)
A - Utangulizi kwa Juma Takatifu (Yohana 11:55 - 12:50)

5. Watu huendelea kuwa wagumu wenyewe wakielekea hukumuni (Yohana 12:37-50)


YOHANA 12:37-41
“Walakini ijapokuwa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini; ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana,ni nani aliyezisadiki habari zetu? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena, Amewapofusha macho, ameifanya mizito mioyo yao, wakafahamu kwa mioyo yao, wakaongoka, nikawaponya. Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake.”

Yesu alitenda mujiza mingi kuwaonyesha makusudi yake ya upendo hapo Yerusalemu. Wote waliokuwa na mioyo ya hamu, wakatambua uwezo wake, pia na alikotoka. Bali wale wenye mawazo mafupi, waliofungwa na maoni ya awali, hao walishindwa kumtambua Yesu, kwa vile walimpima Yesu kwa misimamo yaliyopinda na ushupavu wao.

Watu wengi huwa wanajaa na mawazo yao ya ajabu na wanashindwa kusikiliza sauti ya Mungu. Roho Mtakatifu huwa anasema kwa upole na sauti nyembamba na anahitaji usikivu wa moyo.

Lakini waasi wakapinga Roho Mtakatifu anayesema ndani ya Injili, na hivyo wanaendelea kufanya gumu mioyo yao, na zaidi ya hapo, Mungu katika haki na ghadhabu yake huondoa uwezo wao wa asili ya kusikiliza na kuamini, na hivyo wanaendelea kuwa gumu zaidi. Matokeo yake ni kwamba hapo mbeleni hawataweza tena kutambua haja zao. Basi, Mungu ndiye mtendaji wa wokovu pia na wa hukumu.

Tunatambua kwamba baadhi ya familia, kabila na mataifa yaonekana kwamba zinaishi chini ya ghadhabu ya Mungu. Yeye hawatambui tena wanaoondoka kwake tena na tena, baada ya juhudi zake kuwarudisha chini ya uongozi wake. Mungu huwa anawafanya wagumu wale wasiotii sauti ya Roho Mtakatifu wake. Wote wanaokanyaga upendo wake kwa makusudi na kukataa mvuto wa Kristo wataangukia ndani ya uharibifu. Kwa ajili ya utakatifu wake inampasa Mungu kuwafanya wagumu wasiotii hatua kwa hatua hadi kupotea milele.

Mpango huo wa Mungu kuwafanya wagumu wanaomkataa sio msimamo wa kimawazo tu, lakini unahusika sana na utukufu wake. Isaya alifahamu jambo hilo, alipomsikia Bwana akimtuma sio kuwaokoa watu wake, bali kufanya migumu mioyo yao (Isaya 6:1-13). Kuhubiri habari ya upendo ni rahisi kuliko kuhubiri maonyo kuhusu ghadhabu ya Mungu na hukumu yake. Upendo wa Mungu umeunganishwa na utakatifu, kweli na haki. Uovu wowote hauwezi kusimama katika kuwapo kwake, bali utakimbia mbali na miali ya utukufu wake. Kwa vile Yesu ndiye upendo takatifu mwilini, nafsi yake huwatenganisha watu. Kwa ushujaa Yohana anathibitisha kwamba yule Mmoja akaaye kwenye kiti cha enzi, jinsi Isaya alivyomwona, ndiye Yesu, kwa sababu Mungu na Mwanawe ni mmoja katika utakatifu na utukufu.

YOHANA 12:42-43
“Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.”

Mwinjilisti Yohana alijulikana na familia ya kuhani mkuu (Yoh.18:15). Atueleza kwamba, ingawa umati wa watu kwa jumla walijitenga na Yesu, baadhi ya watu wa maana na heshima nao walimwamini. Walitambua wazi kwamba Mungu alikuwa pamoja naye, na maneno yake yalijaa enzi na kweli, ila hawakushuhudia hayo wazi hadharani.

Kwa nini watu kama hao walikubali hukumu iliyoenda kinyume cha dhamiri zao? Waliwaogopa Mafarisayo, wakipendelea usalama na kujulikana mbele za watu kuliko ukweli. Mafarisayo walikuwa wamewatisha wenyeji wa Yerusalemu na hatua ya kumtenga yeyote atakayempendelea Yesu. Hivyo hao wajumbe walikuwa wakichukia hatua ya kupoteza heshima zao na kuwa hatarini kukataliwa na kuonewa. Yeyote aliyekataliwa na taifa basi hakuweza kuuza au kununua kitu, tena alikataliwa kuoa au kusali pamoja na watu wake. Alihesabiwa kama mwenye ukoma aambukizaye jamii.

Kwa nini hao wajumbe hawakukiri, ijapokuwa walikuwa wakiamini kisiri? Walipendelea heshima za watu kuliko ukuu wa Mungu. Basi, kumpendeza Mungu mtakatifu haikuwa lengo lao; walijipenda wenyewe kuliko Bwana wao.

Ole wake yeye aaminiye kisirisiri tu, na kuendesha maisha yake kana kwamba hamjui Yesu. Mtu wa namna hii atamkana Bwana wake saa fulani ya hatari. Atapendelea usalama na heshima yake kuliko heshima ya Mungu na ulinzi wake. - Basi ndugu, umkiri Bwana na Mwokozi wako, ukitegemea kwamba atakuongoza vema kufuatana na mapenzi yake mema kwako.

YOHANA 12:44-45
“Naye Yesu akapaza sauti akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka.”

Yesu aliwaita watu wake watubu, akitoa kiini cha mafundisho yake kwa maneno magumu, Lakini wakati uo huo kuyafanya rahisi kwa namna ya kiroho. Kwanza maneno hayo yanaonekana yakipingana, kana kwamba akisema,”Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi!” Yesu hamfungi mtu kwake binafsi tu, bali Mwana huwaongoza wafuasi wake wote moja kwa moja kwa Baba. Anajimimina kuwa tupu, pasipa na haki za pekee, wala hatazamii watu wamtegemee yeye peke yake. Mwana hamnyimi Mungu imani za watu; hivyo hapunguzi lolote kwenye enzi ya Mungu, anaifunua na kuitukuza daima.

Mambo kinyume cha hayo nayo ni kweli: Hakuna awezaye kumjia Baba ila kwa njia ya Mwana; hakuna imani ya kweli ndani ya Mungu isipokowa kwa njia ya Mwana. Baba alimzawadia waumini wote wawe watu wake pekee, na akamvisha na sifa zote tukufu. Hivyo Mwana aliye mnyenyekevu anaweza kusimama bila majivuno na kutamka: “Anitazamaye mimi anamwona yeye aliyenipeleka.” Yesu ndiye Mtume wa pekee toka kwa Mungu, abebaye enzi na utukufu wa Mungu kwa kumtii kikamilifu. Yesu ni wakili wa kiini cha uhai wa kimungu, nuru na fahari yake. Hatumjui Mungu mwingine, tofauti na mfano ule ambao Yesu aliirudisha kama katika kioo maishani mwake na katika ufufuo wake. Unyenyekevu wake ulimwinua kwenye usawa na Baba. Kweli, yule Mmoja ambaye Isaya alimwona alikuwa ni Yesu mwenyewe, maana hakuna utofauti wowote kati ya Baba na Mwana.

YOHANA 12:46-48
“Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulumwengu, ila niuokoe ulimwengu. Yeye anikakaaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho.”

Tauni ya hatari ilitokea katika vijiji fulani bara Afrika. Hapo watu walijirusha juu kwa fujo ndani ya vibanda vyao vya msituni kwa sababu ya homa. Daktari aliyekuja haraka vijijini alitambua kwamba virusi vya msiba huo vingeangamizwa, kama wagonjwa hao wangetembea penye nuru kali ya jua. Basi akalia kwa sauti kuu: „Njooni hapo nje ya vibanda vyenu vya giza, nanyi mtapona. Virusi hivi vitaangamia juani.“ Wengi wao wakaenda nje kwenye jua kali na kupona. Wengine hawakumwamini yule daktari kutokana na maumivu yao; wakabaki ndani wakafa. Daktari na wengine waliopona waliwaona baadhi yao waliohangaika kufa, wakawauliza, “Kwa nini hamkutoka na kuja juani?” Wakawajibu, “Ole wetu, hatukuamini maneno yako, yalisikika rahisi mno. Tena tulikuwa wenye maumivu na bila nguvu.” Daktari aliwajibu, “Basi, hamtakufa kwa sababu ya ugonjwa, bali kwa sababu hamkuamini maagizo yangu.”

Mfano huo unatueleza uwezo wa Kristo. Yeye ndiye Jua la Haki lililotokea juu ya giza la dhambi, Mshindi juu ya asili ya maovu. Yeyote aingiaye kwenye nuru yake ya ajabu, atakuwa ameokoka. Kristo hana lengo lingine, ila kuokoa binadamu kutoka dhambi na kifo. Maneno yake yaweza kutuweka huru na nguvu zote za uharibifu. Asikilizaye maneno yake, kuyategemea na kuyaamini, atamjia yeye na kumtii na ataishi daima. Kifo haitaweza kuwa na nguvu juu yake.

Lakini yeyote asikiaye maneno yake bila kuyatunza moyoni mwake, atadidimia ndani ya dhambi na kuendelea hadi hukumuni na katika giza la nje. Hivyo Injili kwa wasioamini inapata kuwa kama hakimu na jambo moja zito katika kupotea kwao. - Je, umemkubali Yesu kuwa Mwokozi wako? Unakariri maneno yake na kuyatimiza katika nia ya moyo wako?

YOHANA 12:49-50
„Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.“

Yesu ndiye Neno la Mungu. Analoliwaza Mungu tu na kulihitaji, ndilo tunalolisikia anaposema Yesu. Kristo ndiye ujumbe wa Mungu moja kwa moja kwako. Mwana akawa mtiifu, alisikiliza sauti ya Baba yake na kulitafsiri katika lugha za kibinadamu. Kwa njia yake Mungu anasema na ulimwengu yenye hatia. Ni kana kwamba kusema: “Mimi ndimi ni wa milele nami nitakuwa Baba yenu. Kwa neema nitawajalia uzima wa milele. Ingawa mnastahili ghadhabu ya Mungu na kuharibika, mimi nawapendeni hata hivyo; namtoa dhabihu Mwanangu Mtakatifu kwa niaba yenu, nanyi hivyo kupewa haki mtapokea pia Roho Mtakatifu. Wala hamtakufa. Nawaagizeni kupokea uzima wa milele kwa mkono wa Masihi wangu. Yeyote asiyepokea hayo, basi hataona Paradiso wala uzima wa kweli.” Kwa maneno kama hayo Mungu anatolea ulimwengu wokovu ulio bure. Lakini yeyote asiyemjali Kristo au kumkataa, ataanguka ndani ya shimo la kwenda chini kabisa, kwa sababu atakuwa ameyarudisha maneno ya Mungu ya kumwomba apokee uzima.

SALA: Baba, twakushukuru sana kutujalia uzima wa milele. Tunakuhimidi na kukusifu kwa furaha. Ulitusafirisha toka kifoni hadi uzimani, kutoka kwa utawala wa dhambi ndani ya upendo wako. Tusaidie tuweze kutunza maneno ya mwana wako ndani yetu na kuyaimarisha mioyoni mwetu na kwenye ufahamu wetu, ili tuweze kuleta matunda mema. Uwahuishe na wengine wengi kwa njia ya Injili yako. Tufundishe kupeleka ujumbe wako kwa wote, ili wao nao wapate kuishi na wasife.

SWALI:

  1. Lipi ni agizo la Mungu ndani ya Kristo kwa wanadamu wote?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on September 01, 2014, at 04:34 PM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)