UTANGULIZI
Kristo aliwaita wanafunzi kuwa mashahidi wake. Yeye mwenyewe hakuandika habari juu ya maisha yake, wala hakutuma barua yeyote kwa makanisa. Lakini nafsi yake ilifanya tofauti kubwa kwenye mioyo ya wafuasi wake, ambao Roho Mtakatifu aliwaongoza kumtukuza Bwana wao Yesu Kristo. Waliona katika upendo,unyenyekevu, kifo na ufufuo wake kuwa ni utukufu kama ule wa Mwana pekee wa Baba aliyejaa neema na kweli. Wakati wainijlisti Matayo, Marko na Luka wanapoeleza misemo na matendo ya Yesu na ufalme wa Mungu kuwa lengo la kuja kwake, Yohana anaangazia kwa undani habari ya maisha na nafsi ya Yesu na upendo wake takatifu. Kwa sababu hii injili ya Yohana imeitwa injili kuu, ambayo ni taji ya vitabu vyote vya Bibilia takatifu.
Ni nani mwandishi wa injili hii?
Viongozi wa hapo awali wa kanisa la karne ya pili walikubaliana kuwa Yohana ambaye ni mwanafunzi wa Yesu ndiye mwandishi wa kitabu hiki cha ajabu. Sasa mwinjilisti Yohana anataja majina ya mitume wengine, wala humtaji ndugu yake Yakobo au jina lake mwenyewe, kwa sababu hakujiona kuwa anastahili kutajwa pamoja na jina la Bwana na Mwokozi wake. Hata hivyo, Askofu Ireneus wa Lyon huko Ufaranza aliandika wazi kuwa mwanafunzi Yohana aliyemlalia Yesu kifuani wakati wa karamu ya Pasaka ya mwisho ndiye aliyeandika injili hii, wakati akihudumu kanisa la Efeso wa Anatolia, enzi za utawala wa Kaisari Trajan (98-117 B.K).
Baadhi ya wapinzani wa ukweli wanafikiri kuwa Yohana, mwandishi wa injili hii siye yule mwanafinzi aliyefuatana na Yesu, bali mmoja wa wazee wa kanisa la Efeso aliyekuwa mwanafunzi wa Yohana na kwamba iliandikwa muda baadaye. Hao ni waotaji na hawajui Roho wa kweli asiyesema uongo, kwa sababu mtume Yohana aliandika injili yake akijitaja mwenyewe pamoja na wenzake anapoandika: “Nasi tukauona utukufu wake” (Yoh.1:14) Hivyo mwandishi wa injili hii alikuwa mmoja wa mashahidi wa macho wa maisha, kifo na ufufuo wa Yesu. Na marafiki wa Yohana ndio walioongeza mwisho wa injili yake wakisema: „Huyu ndiye mwanafunzi ashudiaye haya na kuandika mambo haya; nasi twajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli“ (Yohana 21:24). Walisisitiza sana tabia ya aina yake Yohana inayomtofautisha na mitume wengine kwa vile Yesu alikuwa akimpenda na kumruhusu alale kifuani mwake wakati wa karamu ya pasaka. Na ni yeye yule aliyethubutu kusema na Bwana akiuliza: „ Ni nani (atakaye kusaliti)?“ (Yoh.13:25)
Yohana alikuwa kijana wakatiYesu alipomwita amfuate, alikuwa mdogo kuliko wote kumi na wawili. Alikuwa mfua samaki. Jina la baba yake ni Zebedayo na mamake ni Salome. Aliishi na familia yake huko Bethsaida karibu na ufuo wa ziwa Tiberia. Alijiunga na Petro, Anderea na ndugu yake mwenyewe Yakobo pamoja na Filipo na Nathanieli walipotelemka pamoja kwenye bonde la mto Jorodani kumwona Yohana Mbatizaji akiwa akiita watu kutubu. Watu walikuwa wakikimbia kwake na mmoja wao ni Yohana mwana wa Zebedayo aliyeomba msamaha na kubatitzwa mto Jorodani kwa mkono wa huyu Mbatizaji. Pia inafikiriwa kwamba alikuwa jamaa ya familia ya Kuhani Mkuu Anasi, kwa kuwa alijulikana kwao na kuruhusiwa kuingia ndani ya jumba lake.(Yoh.18:15). Yaani alikuwa wa karibu na jamii ya ukuhani. Kwa hiyo alitaja kwenye injili yake mambo ambayo wainjilisti wengine hawakutaja, hasa yale aliyotamka Mbatizaji akisema juu ya Yesu kwamba: Yeye ndiye mwana kondoo wa Mungu achukuaye dhambi za ulimwengu.
Kwa njia hii Mtume Yohana, kwa uongozi wa Roho Mtakatifu, akawa mwanafunzi aliyemwelewa Bwana wake Yesu na upendo wake zaidi ya wenzake wote.
Uhusiano wa Yohana na wainjilisti wengine watatu
Yohana alipoandika injili yake, injili za Mathayo, Marko na Luka zilikuwa tayari zimeandikwa na kujulikana makanisani kwa muda. Hao wainjilisti watatu walitoa injili zao kwa msingi wa kitabu cha kiebrania ambacho ndani yake mitume walikusanya kutoka mkononi mwa Mathayo ile misemo ya Yesu, ili yasipotee baada ya kupita muda, na badoYesu hajarudi tena alivyoahidi. Pengine matendo ya Yesu na matukio ya maisha yake yalikusanywa kwenye taarifa nyingine ya pekee. Wainjilisti hawa walichunga kwa tahadhari kuu waandike mambo yote kwa uaminifu sana. Luka yule daktari alitegemea habari za wengine kwa kuwa alikutana na Mariamu mamaye Yesu na mashahidi wengine tofauti.
Yohana hata hivyo, yeye mwenyewe ni kisima cha muhimu cha kuongezea kwa taarifa za hao wengine waliotajwa hapo juu. Hakupenda kurudia habari zilizojulikana tayari kwa makanisa, bali alitaka kuziongezea. Wakati hizo injili tatu za kwanza zikitangaza matendo ya Yesu kwenye maeneo ya Galilaya, zikitokeza ile safari moja tu ambayoYesu alikuwa akielekea Jerusalemu na kukutana hapo na mauti yake, Injili ya nne inatuonyesha mambo ambayo Yesu aliyafanya huko Jerusalemu kabla ya hapo, wakati na baada ya huduma yake kwenye eneo la Galilaya.Yohana alishuhudia kwetu kuwa Yesu alikwenda huko mji mkuu wa nchi yake mara tatu, ambapo viongozi wa taifa lake walimchukia tena na tena. Na baada ya upinzani mkuu ulipoongezeka juu yake walimkabidhi asulubiwe.Hivyo, umuhimu wa Yohana ni kwamba alionyesha huduma ya Yesu kwa wayahudi huko Jerusalemu, ambapo ni kitovu cha historia na mapokezi ya Agano la Kale.
Mwinjilisti wa nne hatoi umuhimu wa miujiza aliyofanya Yesu, akitaja sita tu. Ni nini basi ambalo Yohana alilokusudia kuonyesha? Alitangaza maneno ya Yesu kwa mtindo wa
kumwonyesha huyu aliyetamka: “MIMI NDIMI” na kwa njia hii kujulisha upekee wa Yesu kuwa ni nani. Hao wainjilisiti watatu walielezea matendo na maisha ya Yesu, bali Yohana alikazia zaidi kufunua nafsi ya pekee ya Yesu kuwa ni nani katika utukufu wake mbele ya macho yetu. Lakini ni wapi Yohana alipopata maneno ya aina ile, yasiyopatikana kwa wenzake wengine, na ambayo Yesu aliyasema juu yake mwenyewe? Ni Roho Mtakatifu aliyemkubusha maneno hayo baada ya Pentecoste ya kwanza. Kwa kuwa Yohana mwenyewe alishuhudia sehemu zingine tofauti kwamba wanafunzi hawakuelewa ukweli wa maneno mengine alioyasema Yesu mpaka baada ya kufufuka kwake na kuja kwa Roho Mtakatifu juu yao. Kwa njia hii alielewa baadaye maana ya maneno ya Yesu aliyojisemea mwenyewe na yaliyohusu neno lile “NDIMI”. Ndiyo maneno yanayotofautisha nia na upekee wa injili hii ya ajabu.
Yohana pia anataja maneno ya Yesu alipolinganisha mambo kama vile nuru na kinyume giza, roho na mwili, ukweli na uongo, uzima na mauti, na pia mambo kuwa wa juu au wa chini. Hatuoni mlinganisho wa aina hii katika injili zingine. Lakini Roho Mtakatifu alimkumbusha Yohana kwa muda wa miaka kadhaa baadaye alipoishi katika utawala wa wagiriki juu ya maneno ambayo Bwana aliyasema. Roho alifafanua kwa mwinjilisti huyu kuwa Yesu hakunena tu kwa njia ya Kiebrania, bali akatumia pia misemo ya kigriki kwa mataifa.
Ni nini lengo la injili ya Yohana?
Yohana hakutaka kumjulisha Yesu kwa njia ya kishairi wala Kifilosofia au kwa njia tofauti ya kiroho, lakini alikazia sana juu ya kuingia kwake mwili wa binadamu, kujitwisha udhaifu huo hadi kufikia kiu aliyovumilia pale msalabani. Aliweka wazi pia kuwa Yesu ni mwokozi wa wanadamu, wala si kwa wayahudi tu, kwa sababu “ndiye mwana kondoo aichukuaje dhambi ya ulimwengu.” Alitutangazia jinsi Mungu alivyowapenda wanadamu wote.
Mambo haya tuliotaja hapo juu ndio njia na ushahidi wa kufikia kiini na uti wa mgongo wa injili hii, hasa ya kuwa Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu. Umilele wake ulionyeshwa katika kule kutoshikamana na umungu wake. Na pia katika ubinadamu aliyokubali kuupokea na enzi yake ndani ya udhaifu wake. Hivyo, ndani yaYesu, Mungu akaonekana na kuwepo kati yetu binanadamu.
Lengo la ufafanuzi wa Yohana haikuwa kumtambulisha Yesu kwa njia ya kifilosofia au ya kutafakari juu ya Mungu, bali kumfahamu Bwana kwa njia ya Roho Mtakatifu kwa msingi wa imani wakifu. Kwa hiyo alifunga injili yake na maneno yajulikanayo sana. “Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu, na kwa kumwamini mwe na uzima kwa jina lake”(Yohana 20:31). Imani hai ndani ya umungu wa Yesu ndiyo lengo la injili ya Yohana. Na imani ya namna hii inazaa ndani yetu uhai wa milele iliyo tukufu na takatifu
Ni kwa wakina nani injili ya Yohana iliandikwa?
Kitabu hiki kinachojaa ukweli wa maelezo juu ya Kristo hakikuandikwa ili kuhubiri kwa wasioamini, bali kiliandikwa kwa kusudi la kujenga kanisa na kuliimarisha katika Roho. Mtume Paulo tayari alikuwa ameanzisha makanisa huko Anatolia. Na alipofungwa gerezani huko Rumi, Petro aliyatembelea makanisa hayo na kuwatia moyo. Wakati Petro na Paulo walipoaga dunia, pengine nyakati za mateso chini ya Kaisari Nero huko Rumi, Yohana alichukua nafasi zao na kuishi Efeso, mji iliyokuwa kitovu cha ukristo wakati ule. Alichunga makanisa kadhaa yaliyotawanyika huko Asia Ndogo. Yeyote asomaye barua zake na sura ya pili na tatu ya kitabu chake cha Ufunuo, ataelewa lengo na matarajio ya Mtume huyu, aliyetufafanulia upendo wa Mungu uliyoonekana ndani ya Yesu Kristo akiwa mwilini. Alipigania imani dhidi ya waumini wa kimawazo tu waliovamia kundi lake kama mbwa-mwitu wakipotosha kondoo kwa maneno matupu na sheria zisizokunjika na desturi chafu, wakichanganya ukweli na mawazo yao ya upotovu.
Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji nao aliishi Anatolia na kumheshimu yeye aliyewaita watu watubu, zaidi kuliko Yesu. Walikuwa bado wakimtarajia Masihi aliyeahidiwa wakifikiri kuwa bado hajaja. Kwa njia ya kumweleza Yesu, Mtume Yohana alipinga mafundisho hayo yote yaliyoenezwa kinyume cha Kristo. Aliinua sauti yake na kupinga hizo roho zingine akisema:
”Nasi tuliuona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli”. (Yoh.1:14)
Yaonekana kuwa wengi waliopokea ujumbe wake walikuwa ni waumini toka kwa mataifa, maana Yohana aliwasimulia mengi juu ya mapokeo ya kiyahudi, ambayo Wayahudi wenyewe wasingehitaji kuelezwa tena. Zaidi ya hapo, Yohana hakutegemea katika injili yake maneno ya Yesu yaliyoandikwa wakati ule wa lugha ya Kiaramaiki na kuyatafsiri kwa kigriki, jinsi wainjilisti wengine walivyofanya. Bali alitumia misemo ya kigriki (Kiyunani) iliyojulikana kwa makanisa yake. Aliijaza roho ya injili na kushuhudia maneno ya Yesu kwa lugha ya kigriki sanifu kwa huru kabisa, akiongozwa na Roho Mtakatifu. Hivyo, injili yake inatamka kwa urahisi na kwa kina ya kiroho na ufasaha zaidi kuliko jitihada zote zingine za mafundisho. Hivyo, Roho Mtakatifu anatuletea injili hii, ikiwa ni hazina ya ukweli kwa maneno ya kueleweka, ili kila mtu, hata vijana, waweze kuelewa maana yake ya kudumu.
Ni lini injili hii ya ajabu ilipoandikwa?
Twamshukuru Bwana Yesu jinsi alivyowaongoza wachimbaji wa mambo ya kale katika nchi za mashariki miaka kadhaa iliyopita. Walichimbua kule Misri kipande cha gombo chenye tarehe ya mwaka 100 BK, ambamo sehemu ya injili ya Yohana zimeonekana kwa maandishi ya wazi kabisa. Kwa ugunduzi huu, yale majadiliano mengi kuhusu wakati wa uandishi wa injili ya Yohana, yalifikia kikomo na ubishi wa kupinga ukweli ukakomeshwa. Uchimbaji huu unathibitisha kuwa injili ya Yohana iljulikana mwaka 100 BK, na wala si katika Asia Ndogo tu, bali pia kwa maeneo ya Afrika kaskazini. Hamna shaka kabisa kwamba, ilijulikana huko Rumi pia. Ukweli huu watutia nguvu imani yetu sisi wakati huu, kwamba mtume Yohana ndiye aliyeandika injili hii, akijawa na nguvu ya Roho Mtakatifu.
Ni nini kilichomo katika injili hii?
Sio rahisi kwa mtu kupangisha maneno yenye pumzi ya Mungu. Na pia ni ngumu hasa kugawanya injili ya Yohana katika sehemu sehemu. Hata hivyo twashauri kufuata mpangilio huu:
- Kuangaza kwa nuru tukufu ya Mungu (1:1 - 4:54).
- Nuru yaangaza gizani, wala giza halikuishinda (5:1 - 11:54)
- Nuru yaangaaza kati ya shirika la mitume (11:55 - 17:26)
- Nuru yashinda giza (18:1 - 21:25)
Mwinjilisti Yohana alipanga mawazo yake katika mfano wa duara zinazoshikana, kama katika myororo wa kiroho, na ndani yake kila duara inazunguka shabaha au wazo moja hata mbili. Hizi duara haziachani na zingine, bali mara nyingine shabaha zao zinakutana.
Fikara za Yohana kwa kiebrania pamoja na maoni yake ya kiroho ya ndani sana zinapatana vizuri na uchangamfu wa lugha ya kiyunani, na kutokeza mshikamano wa kupendeza. Roho Mtakatifu naye anatufafanulia misemo ya injili hii vizuri hata leo. Kwetu imetuletea kisima cha hekima na maarifa bila kikomo. Yeyote asomaye kitabu hiki kwa kindani, atainama kwa unyenyekevu mbele za Mwana wa Mungu, akitoa maisha yake kwake katika hali ya kumshukuru na kumsifu sana kwa ukombozi wake wa milele.
MASWALI:
- Ni nani mwandishi wa injili ya nne?
- Ni uhusiano gani ulioko kati ya injili ya nne na zile zingine tatu?
- Lengo la injili ya Yohana ni nini?
- Ni kwa wakina nani injili hii ya ajabu iliandikwa?
- Ni kwa namna gani unaweza kuigawa na kuipanga injili hii kimafundisho?