Previous Lesson -- Next Lesson
1. Asili na kazi ya Neno kabla ya kufanyika mwili (Yohana 1:1-5)
YOHANA 1:1
1 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu”
Mwanadamu hueleza mawazo na makusudi yake kupitia kwa maneno yake. Yale usemayo ndio yanayokueleza. Na maneno yako ndio jumlisho la nafsi na maisha yako yakidhihirisha na hali ya roho yako.
Kwa maana ya kikamilifu zaidi, Neno la Mungu laeleza Uungu, utakatifu na nguvu zake zinazofanya kazi kwa Neno lake takatifu. Kwamba hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi kupitia kwa Neno lake la enzi. Na aliposema, “na iwe”, ikawa (au ilifanyika). Mpaka leo nguvu za Mungu zingali na uwezo ule ule katika Neno lake. Unajua kuwa injili iliomo mikononi mwako inajaa mamlaka makuu ya Mungu? Kitabu hiki kina uwezo kuliko bomu ya nguvu za hewa kwa sababu kinaangamiza uovu ndani yako na kukujenga tena upya kwa mambo yaliyo mema.
Siri ya ndani inayoelezwa na tamko la “neno”, jinsi ilivyo mara kwa mara katika injili ya Yohana, kwamba katika lugha ya kinyunani ina maana mbili. Ya kwanza ni “pumzi” inayosukuma sauti itoke mdomoni na kutamka maneno. Ya pili ni ya “nafsi ya kiume wa Roho”, na nafsi hiyo ndiye Yesu. Hizi maana mbili zaonekana hata katika lugha ya Kiarabu kwa jinsia inayopewa Neno. Kwa kiingereza haya mawili hutofautishwa kwa jinsia ya “he” au “it” inayotangulia Neno. Wafasiri wa Biblia walijitahidi kuonyesha jambo hili kwa Kiswahili walipotamka sehemu ya pili ya aya ya kwanza (Yoh.1:1b): “… naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu”, wala si “…nalo Neno lilikuwako kwa Mungu, nalo Neno lilikuwa Mungu”, ili kuonyesha maana ya Neno kuwa ni nafsi ya Yesu. Hii pia ni sababu ya kuanzisha “Neno” kwa herufi kubwa (Capital Letter). Hata kwa Biblia ya kiingereza iliandikwa “Word” kwa herufi kubwa, jinsi isivyo katika maandishi ya kawaida.
Maneno ya aya ya pili na kuendelea hadi 14 yanaendelea kumweleza huyu Neno kuwa ni Uzima, pia na Nuru, naye ndiye aliyefanyika Mwili, na hata hivyo kuendelea kuwa Mwana pekee wa Mungu. Hii ndiyo ajabu na siri kuu, isiyoweza kuelezwa zaidi, bali tunaiamini.
Misemo tofauti jinsi Yohana anavyotamka mwanzoni: “Hapo mwanzo kulikuwako Neno” na kuelezea kwenye sentensi ya pili akisema “Neno alikuwako tangu mwanzo kwa Mungu”, basi hayo yaonyesha ukuu wa siri ya nafsi ya Yesu Kristo, ambayo Yohana alijibidiisha kuifafanua.
Yesu ametoka kwa Baba kama vile maneno yetu ya kawaida hutoka mdomoni. Kristo ndiye utimilifu wa mapenzi ya Mungu na mawazo yake. Ni ajabu kwamba twaona matumizi haya yakiwepo hata katika dini zingine, yaani kwamba Kristo anatajwa kuwa Neno la Mungu na Roho atokaye kwake Mungu. Hakuna mwanadamu yeyote ulimwenguni mwenye tabia na uwezo wa kimbinguni, ila HUYU tu aliyezaliwa na bikira Mariamu. Kufanyika kwake kuwa mwili huko Bethlehemu haikuwa mwanzo wa kuwepo kwake. Alikuweko pamoja na Baba kabla ya vizazi vyote na kabla ya ulimwengu kuumbwa. Yaani Kristo ni wa milele, kama vile Baba alivyo wa milele na habadiliki, na kama vile neno la Mungu halibadiliki kwa namna yoyote daima.
Yohana alituonyesha uhusiano wa pekee kati ya Kristo na Babake. Hakutengana naye Baba, kama vile maneno tunayotamka yanavyokwenda mbali nasi na kupotea hewani. Bali Kristo alikaa ndani yake Mungu na kudumu kwake. Maelezo “Alikuwa na Mungu” yamaanisha kwa kigriki (Kiyunami) kuwa neno lilikuwa likisogea kwake Mungu na kuingia ndani ya Mungu. Hivyo Kristo alielekea daima kwake Mungu Baba. Mwelekeo huu pia ni jambo la asili kwa wote waliozaliwa na Roho Mtakatifu, kwa maana Kristo ndiye chanzo cha upendo. Wala upendo huu haujipendelei bali unaendelea kuelekezwa kwa chanzo chake Mungu na kudumu ndani yake.
Mungu hakumwumba Kristo toka kwa kisiokuwepo, jinsi alivyofanya kwa viumbe vingine vyote kwa uwezo wa Neno lake. Bali Mwana ndiye Neno la uumbaji na hubeba enzi ya Babake mwenyewe. Mwisho wa aya hii ya kwanza twaona tamko la ajabu, lakini lililo dhahiri kwamba Neno lenyewe ni Mungu. Kwa njia hii mwinjilisti Yohana atuambia kuwa Kristo ni Mungu toka Mungu, Nuru toka kwa nuru, Mungu wa kweli toka Mungu kweli, aliyezaliwa na wala si kuumbwa. Yeye ni wa asili moja na Baba, wa milele, mwenye enzi, Mtakatifu na mwenye huruma. Yeyote anayekiri kuwa Kristo ni neno la Mungu atakubaliana na maelezo haya kuhusu umungu wake.
SALA: Bwana Yesu Kristo, tunakuinamia kwa kuwa ulikuwa pamoja na Baba kabla ya uumbaji wote, ukiwa unaelekea kwake Baba daima. Tusaidie ili tusijitenge naye, bali kila wakati tujitoe kwa Mungu na kudumu katika upendo wake. Twakushukuru, Bwana Yesu, kwa sababu una kuja kwetu katika injili yako kwa maneno ya kueleweka, ili kwamba mamlaka yako ionekane maishani mwetu kwa njia ya imani kupitia kwa Neno lako. Amina
SWALI:
- Ni neno gani hili linalorudiwa tena na tena kwenye aya ya kwanza ya Yohana sura ya kwanza, na maana yake ni nini?