Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- Romans - 079 (The Continuation of Paul’s List of the Saints)
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- French -- Georgian -- Greek? -- Hausa -- Hebrew -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Malayalam -- Polish -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish? -- Tamil -- Telugu -- Turkish -- Urdu? -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
Maongezo kwa SEHEMU ya 3 - Maelezo ya pekee juu ya msimamo wa Paulo kwa viongozi wa kanisa la Rumi (Warumi 15:14 – 16:27)

5. Mwendeleo wa orodha ya Paulo ya watakatifu waliojulikana kwake ndani ya kanisa la Rumi (Warumi 16:10-16)


WARUMI 16:10-16
"10 Nisalimieni Apele, mwenye kukubaliwa katika Kristo. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Aristobulo. 11 isalimieni Herodioni, jamaa yangu. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Narkiso, walio katika Bwana. 12 Nisalimieni Trifaina na Trifosa, wenye bidii katika Bwana. Nisalimieni Persisi, mpendwa aliyejitahidi sana katika Bwana. 13 Nisalimieni Rufo, mteule katika Bwana, na mamaye, aliye mama yangu pia. 14 Nisalimieni Asinkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma, na ndugu walio pamoja nao. 15 Nisalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa, na watakatifu wote walio pamoja nao. 16 Salimianeni kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo yawasalimu."

Paulo alijulisha kanisa la Rumi habari ya majina ya washiriki wote waliojulikana kwake, ambao walifahamu mafundisho yake na mwenendo wake kati yao. Aliwathibitishia viongozi wa kanisa kwa njia ya orodha hii kwamba, yeye hakuwa mgeni katika Rumi, bali wajumbe wake waliotenda kazi ndani ya kanisa la Rumi walijulikana na kukubalika.

Apele alikuwa na jina la mchoraji Myunani mwenye sifa sana. Alikuwa ni mshiriki mwenye uzoefu sana katika kanisa la Rumi, aliyeendelea kuwa mwaminifu kwake Kristo, mbali na mateso na mahangaiko. Ndugu za wale wa nyumbani mwa Aristobulo wanafikiriwa kuwa ni waachiliwa huru kutoka utumwani, ambao hawakujulikana binafsi, bali Paulo aliwaita „ndugu“, kwa sababu ya imani yao ndani ya Kristo, Mwana wa Mungu, Mwenyezi aliwapokea kuwa watoto na kuwafanya kuwa wapya.

Herodioni alikuwa ni Mkristo wa asili ya Kiyahudi, aliyejaribu kushika sheria za Musa, na wakati uo huo pia kumfuata Kristo. Alikuwa ni wa jamaa ya Paulo kufuatana na kabila lake.

Kuhusu nyumba ya Narkiso, Paulo hakuwafahamu kwa majina, lakini walipata kuwa Wakristo waaminifu, mali ya Bwana Yesu, nao walishuhudia mwenendo wao wa kiroho. Trifania na Trifosa walikuwa dada wawili waliojulikana kuwa ni wafanya kazi wa bidii sana wa Bwana. Persisi alikuwa ni mtumishi wa tatu wa Bwana, ambaye Paulo alimwaita mpendwa kufuatana na mwenendo wa kiroho, kwa sababu hakuwa mwumini tu, lakini aliishi kabisa maisha ya kuonyesha imani yake, naye akafanya kazi kwa ajili ya Yesu.

Paulo alimjalia Rufo cheo cha pekee, “Mteule katika Bwana“, na hilo linadokeza kwamba, alikuwa ni mwana wa Simoni wa Kirene, aliyebeba msalaba wa Yesu (Marko 15:21). Mke wa Simoni, ambaye ni mamaye Rufo, anafikiriwa kumtumikia Paulo katika maeneo ya Mashariki ya Kati, kwa sababu Paulo anashuhudia kwamba, huyu mwanamke mwema alikuwa kama mama kwake, katika kumtunza na kumfariji.

Paulo alituma na salamu kwa vikundi viwili vya waumini, naye akataja vyote viwili kwa majina, kwa sababu alitia fikira kwamba, hali yake ya kuwafahamu ipate kujulikana ndani ya kanisa. Asinkrito, Flegoni, Herme, na ndugu waliokuwa pamoja nao, hao ndiyo kundi la kwanza, ambao aliwaita ndugu ndani ya Bwana Yesu. Kundi la pili ndilo: Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa, na watakatifu wote waliokuwa pamoja nao; hao wote walikuwa ni washiriki katika kanisa la nyumbani mwao. Wote waliotajwa hapo waliishi chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, na matunda ya Roho Mtakatifu yalijitokeza kati yao kiasi cha kuwaita watakatifu. Katika maisha yao ya kila siku walimtambua huyu Msulibiwa aliyefufuka kutoka kwa wafu kuwa ndiye Bwana na Mwokozi wao, nao wakapokea kipawa cha Roho Mtakatifu na nguvu zake za milele.

Paulo alifunga orodha ya watakatifu wa Rumi, akiwataka wasalimiane kwa busu takatifu, kama ishara ya uhusiano yao ya kindugu, takatifu na kiroho ndani ya Kristo. Na zaidi ya hapo, Paulo anawasalimia waumini wote na makanisa kule Rumi katika jina la makanisa yote ya eneo la Mashariki ya Kati, akitumia uwezo wake kama wakili wao.

Yeyote anayechunguza kwa uangalifu orodha hii, inayojumlisha majina 25, atatambua kwamba, makanisa ya nyakati zili yalikuwa si makanisa ya mawe (majengo) tu, bali ni mashirika ya waumini, waliokutana pamoja katika vikundi vya kiasi ndani ya nyumba zao, ambavyo Paulo aliwatambua wote pamoja kuwa ndiyo hekalu la Roho Mtakatifu kule Rumi. Walitokana na maen eo mbalimbali na kukutana kwenye jiji kuu, ambapo waliunda kanisa la kimataifa walipoishi na lugha na mapokeo mbalimbali. Lakini wote walishuhudia kwa ulimi moja habari ya jina la Kristo na damu yake, na kuhusu haki yake waliojaliwa naye. Pengine tunasoma katika orodha ya majina hayo habari ya wafia dini kadhaa, ambao waliuawa wakati wa udhalimu mkuu chini ya Nero, huyu mjeuri mkuu wa Rumi. Aliwafunga Wakristo, aliwatundika, na alimwaga vitu vilivyowaka moto kwenye miili yao, ili wafanywe kama mienge inayowaka moto, au alichoma miili yao juu ya pao la chuma chenye moto chini yake.

SALA: Ee Baba wa mbinguni, tunakuabudu kwa sababu ulikusanya kanisa la Yesu Kristo kule Rumi, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, tena kwa lugha mbalimbali; na kanisa hilo likapata kuwa mfano wa uumbaji mpya, kwa sababu uzima wa milele uliishi ndani yake. Twaomba utujalie pia nguvu tusiwe walegevu, lakini tuwatafute na kuwakubali wote wanaompenda Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, ambaye ni Mungu mmoja.

SWALI:

  1. Tunaweza kujifunza nini kutokana na majina ya watakatifu wanaotajwa ndani ya orodha?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on November 17, 2022, at 01:05 PM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)