Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- Romans - 078 (Paul’s List of the Names of the Saints in the Church of Rome)
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- French -- Georgian -- Greek? -- Hausa -- Hebrew -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Malayalam -- Polish -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish? -- Tamil -- Telugu -- Turkish -- Urdu? -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
Maongezo kwa SEHEMU ya 3 - Maelezo ya pekee juu ya msimamo wa Paulo kwa viongozi wa kanisa la Rumi (Warumi 15:14 – 16:27)

4. Orodha ya Paulo yenye majina ya watakatifu waliojulikana kwake katika kanisa la Rumi (Warumi 16:1-9)


WARUMI 16:1-9
"1 Namkabidhi kwenu Fibi, dada yetu, aliye mhudumu wa kanisa lililoko Kenkrea; 2 ili mmpokee katika Bwana, kama iwapasavyo watakatifu; mkamsaidie katika neno lolote atakalohitaji kwenu; kwa sababu yeye naye amekuwa msaidizi wa watu wengi, akanisaidia mimi pia. 3 Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika Kristo Yesu; 4 waliokuwa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu; ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa ya Mataifa yote pia; nisalimieni na kanisa lililomo katika nyumba yao. 5 Nisalimieni Epaineto, mpenzi wangu, aliye malimbuko ya Asia kwa Kristo. 6 Nisalimieni Mariamu, aliyejishughulisha sana kwa ajili yenu. 7 Nisalimieni Androniko na Yunia, jamaa zangu, waliofungwa pamoja nami, ambao ni maarufu miongoni mwa mitume; nao walikuwa katika Kristo kabla yangu. 8 Nisalimieni Ampliato, mpenzi wangu katika Bwana. 9 Nisalimieni Urbano, mtenda kazi pamoja nami katika Kristo, na Stakisi, mpenzi wangu."

Ndani ya waraka huu Paulo alieleza mambo yafuatayo:

Kwanza: Miongozo ya msingi wa imani ndani ya Kristo.
Pili: Uchaguzi wa Mungu.
Tatu: Mwenendo wa nidhamu ya waumini.

Mwisho wa waraka wake Paulo hasemi tu habari ya miongozo, bali pia anawaonyesha watu waliojulikana kwake na walioko ndani ya kanisa. Anaonyesha wazi kwamba, wao ndiyo thibitisho la kufaa kwa ajili ya kuhakikisha ukweli wa mafundisho yake, kwa vile anawaangalia wao kuwa wenye kuonyesha ujumbe wake, nao wanajitayarisha kwa ajili ya mafundisho yake na kufika kwake. Mtume wa Mataifa hakuwa mgeni kule Rumi, naye aliweza kuonyesha baadhi ya watakatifu waliojulikana kwa ndugu wengine. Aliwaeleza kwamba, hao wote walijenga imani yao ndani ya Kristo, pia wakawa mawe yenye uhai ndani ya hekalu la Roho Mtakatifu, tena ndani ya jiji kuu la serikali ya kirumi jinsi ilivyokuwa wakati ule.

Ni jambo la kushangaza kwamba, Paulo anaanza orodha ya watakatifu na mwanamke, jina lake Fibi, ambaye anamweleza kuwa ni „dada yetu katika Kristo“. Fibi alikuwa ni Mkristo mnyofu, aliyejitoa kabisa kwa ajili ya huduma ya kanisa, pia kwa ajili ya maskini, wagonjwa na wageni waliopita. Alikuwa ni mtumishi wa kawaida wa kanisa la Kenkrea, mji yo bandari upande wa mashariki ya Korintho kule Uyunani. Inajionyesha kwamba, yeye alikuwa ni fundi wa mambo ya sheria, na kwa kushughulikia madai ya ofisi ya ushuru, pia na kuwasimamia wahusika na watu wasiokuwa na haki ya uraia. Alikuwa amemsaidia Paulo na wenzake katika kusafiri kwao, na ikaonekana kwamba, alikuwa tayari kumsaidia pia hapo Rumi, kama pengine akipata matatizo kwa ajili ya kufika kwake hapo. Basi Paulo akawauliza Wakristo wa Rumi wamsaidie pia katika jambo lolote, ambalo pengine atawahitaji; pia akawataka wamkaribishe ndani ya kanisa lao kwa namna inavyowapasa watakatifu. Kwa jumla inasadikika kwamba, Fibi alikabidhi huo waraka wa Paulo kwa kanisa la Rumi. Fibi alikuwa ni mtu maarufu, na ni mmoja wa Wakristo waliojulikana sana katika eneo la Mashariki ya Kati.

Baada ya huyu mpelekaji wa barua katika orodha ya watakatifu pale Rumi, Paulo anamtaja Priska na mume wake Akila. Hao walikuwa wamemtunza Paulo nao wakampatia kazi kwa ajili ya kuweza kupata ridhiki wakati akiwa Efeso (Matendo ya Mitume 18:2-26), ambapo alimweleza kinaganaga zaidi Injili kwa Apele, mhubiri mwenye uwezo. Inafaa kutamka kwamba, Paulo alitaja jina la mwanamke kabla ya jina la mume, huku akikumbuka kwamba, wote wawili walijitoa kabisa kwa ajili ya usalama wa Paulo, wakihatirisha hata maisha yao kwa kumlinda. Hapo waumini wote wa Asia Ndogo waliwashururu huyu mtu na mkewe kwa ajili ya kujitoa kama sadaka na pia kwa huduma yao njema. Inaonekana kwamba, wakati ule wao walikuwa wamesafiri kwenda Rumi, ambapo walipokea kanisa lililozoea kukutana kwa ibada katika jumba lao lenye ukarimu. Paulo vilevile alituma salamu kwa kanisa lililokuwepo katika nyumba yao, akiwahesabia wao wote kuwa ni mashahidi wa mafundisho yake kuhusu neema ya Mungu.

Epaineto anasalimiwa kama mpendwa wake Paulo. Yeye alikuwa ni mmojawao wa wale waliookolewa kwanza kwa imani ya Kristo katika Asia, na waumini walimhesabia kuwa kiungo kati yao na Kristo. Ndipo alisafiri kwenda Rumi na yeye akiendelea kufuata katika nyayo za Yesu kule.

Baada ya Epaineto Paulo anamtaja Mariamu, ambaye alijitaabisha mwenyewe sana katika kanisa la Rumi kwa uaminifu na uvumilivu mwingi, na bila shaka alimsaidia Paulo na wajoli wake kule Uyunani na Anatolia. Paulo anamshuhudia kutenda huduma safi na ya kudumu kwa ajili ya wafuasi wa Kristo.

Ndipo Paulo anawataja Androniko na Yunia, ambao walikuwa waumini wa asili ya Kiyahudi, tena wa kabila la Benjamini, jinsi alivyokuwa na Paulo, ambao waliishi Rumi, nao walikuwa mashahidi wa ukweli kwamba, Paulo alikuwa ni mmoja wa wazao wa Yakobo. Walikuwa wamefungwa pamoja na Paulo na wenzake, walioteseka kwa ajili ya Kristo. Tena walikuwa wameokolewa kabla ya Paulo, nao walikuwa wametukuzwa kati ya Wakristo wa kwanza ndani ya kanisa la Yerusalemu, pia waliheshimiwa kwa urafiki na mitume wengine.

Sasa basi, Paulo anataja majina matatu mageni katika orodha ya watakatifu: Ampliato, Urbano na Stakisi. Ampliano na Stakisi walikuwa bado ni watumwa. Yule wa kwanza Paulo anamweleza kuwa ni mpenzi wake katika Bwana, hivyo akidokeza kwamba, yeye aliyekuwa anadharauliwa na kuumizwa vibaya, baadaye alipata kuheshimiwa sana alipopandikizwa kiroho ndani ya mwili wa kiroho wa Kristo. Yule mwingine, ambaye Paulo anamweleza kuwa mpendwa wake alikuwa ni mtumishi wa kusifiwa ndani ya kanisa. Urbano naye alikuwa ni bwana mheshimiwa wa asili ya Rumi, aliyefanya kazi pamoja na Paulo kwa muda mrefu sana, hata Paulo alimfikiria kuwa mshiriki wake katika utume wake na msaidizi wake katika Kristo. Urbano alikuwa amejulikana katika makanisa yote ya eneo la Rumi.

Ni lazima kutambua kwamba, kanisa la Rumi tangu mwanzo lilijumlisha watu huru na watumwa, ambao wote pamoja waliunda umoja wa kiroho ndani ya Kristo. Hali hii inatujulisha kwamba, Roho Mtakatifu haweki umuhimu kwa tofauti za kikabila au za maisha ya jamii. Hatofautishi kati ya wanaume au wanawake, watu huru au watumwa, watajiri au maskini, Myahudi au mtu wa Mataifa, kwa sababu wote wako na hali moja katika umoja wa kiroho katika Kristo.

SALA: Baba yetu wa mbinguni, tunakutukuza kwa sababu ulijenga ndani ya Kristo na chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu makanisa ya manyumbani mwa watu kule Rumi. Kipekee tunafurahia, kwa sababu makanisa hayo ya Mwana wako yalijumlisha watu huru na watumwa, waume na wake, watajiri na maskini, Wayahudi na watu wa Mataifa, na wote wakawa ni umoja wa kiroho uliobarikiwa.

SWALI:

  1. Tunaweza kujifunza nini kutokana na majina ya washiriki wa kanisa la kule Rumi?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on November 17, 2022, at 12:58 PM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)