Previous Lesson -- Next Lesson
1. Kumponya aliyepooza kwenye birika la Bethzatha (Yohana 5:1-16)
YOHANA 5: 10-13
10 “Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. 11 Akawajibu, Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende. 12 Basi wakamwuliza, Yule aliyekuambia, Jitwike, uende, ni nani? 13 Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maana Yesu alikuwa amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale.”
Watu waliokuwako pale ndani ya malango ya Bethzatha walifurahia sana, isipokuwa wale wanasheria washupavu. Hao jamaa walikuwa wachoyo wakali, na hasa hasa kwa sababu uponyaji huo ulitendeka siku ya Sabato. Mbali na kazi ya Yesu kumponya yule ambaye hakujiweza, alimwagiza kubeba godoro lake kwenye barabara za mji. Walona kwamba hii ilikuwa ni dhambi kubwa dhidi ya Mungu na taratibu za Sabato, maana lazima kazi zote ziachwe siku hiyo ya mapumziko.Mwenye kuvunja sheria hii alikuwa anastahili kufa (Hesabu 15:32-36). Wayahudi walihisi kwamba Masihi hatakuja, hadi taifa lote washike taratibu za Sabato kikamilifu.
Wayahudi hao wasingempiga mawe hapo hapo huyu mtu aliyebeba godoro lake, maana iipasa kutoa onyo kabla ya kuthibitisha hukumu. Kule kukataa kazi aliyoifanya kulikuwa ndiyo onyo. Mponywa alijitetea kwa kutamka agizo la Yesu kwake. Kubeba godoro kulikuwa ni thibitisho la kupona kabisa.
Hao wanasheria wakachemka na hawakufurahia tendo la kuponya. Wala hawakutambua enzi ya upendo, ambalo Yesu aliionyesha katika uponyaji huu. Walianza kujadiliana kwa choyo na chuki nafsi ya huyu mponyaji. Maana alithubutu kumwagiza yule maskini abebe godoro lake siku ya Sabato. Hivyo kwa maoni yao Yesu alikuwa mvunja sheria anayestahili kufa.
Mwenye kupona hakumfahamu mponyaji wake, maana Yesu alikuwa ni mgeni kwake, aliyetembelea kwa mara ya kwanza Bethzetha. Baada ya kumponya ikawa amepotea. Yesu hakutafuta imani ndani ya nafsi yake kwa msingi wa miujiza, bali kwa ajili ya utu wake wa upendo.
YOHANA 5: 14-16
14 “Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi. 15 Yule mtu akaenda zake, akawapasha habari Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima. 16 Kwa sababu hiyoWayahudi wakamwudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya Sabato.”
Yesu akamtafuta yule aliyeponywa, ili akamilishe uponyaji kwake kwa kumweka huru na dhambi zake. Akamkuta huyu mtu hekaluni akimsifu Mungu. Alikuwa amejaa hofu na furaha wakati moja alipomwona Yesu. Tunafahamu Yesu alimwambia nini:
Wewe umepata kupona. Tambua ukuu wa mwujiza uliokujia. Ulikuwa huwezi kwa miaka thelathini na nane. Hili lilikuwa tendo tukufu kwako, wala si tendo la kibinadamu. Mungu aliye mwilini amekufungulia macho ya moyo wako.
Umetambua makosa yako. Maisha bila Mungu yametokeza msiba huu mkubwa kwako. Kwa kukuponya, pia dhambi zako zimesamehewa. Ili tiba lifikie na utu wake wa ndani, Yesu alimtaka awe mtiifu, wala asitende dhambi tena. Kwa kupokea msamaha kunahitajika uamuzi wa kutokurudia dhambi ile. Anayekubali neno la Kristo lenye nguvu maishani mwake, naye akikiri makosa yake kwa huzuni, basi pamoja na msamaha anapokea nguvu tukufu, ili ashinde maovu kwa msaada wa Mungu. Kristo hatazamii kwetu jambo lisilowezekana, lakini anatujalia Roho yake, maana nguvu yake inaweza kushinda majaribu yetu ya kimwili pamoja na kukasirika kwetu. Huyu Roho wa kweli anatuwezesha kujikinga na maovu na kuyapinga.
Mara kwa mara maradhi na maumivu yanaongozwa na Mungu, ili katika kutushughulikia kwa upendo wake apate nafasi ya kuturudisha kwake. Wakati mwingine hata raha na starehe yanaweza kuwa mapigo matukufu dhidi ya ugumu wetu kwa Mungu. Hivyo mtu aweza kupatwa na mapepo, mwishowe kupotea milele. Usichezeshe dhambi, bali ukiri kufungwa kwako katika kosa fulani, ukamwombe Kristo akuweke huru. Vunja kona lile la ki-dhambi. Umwahidi Mwokozi wako kwa kufanya mapatano ya kutokurudia. Atakuokoa kabisa hadi mwisho.
Sasa mshangao gani! Baada ya kupata mwongozo wa Yesu, huyu aliyeponywa alikimbilia kwa Wayahudi, akawaeleza kwamba mtu wa Nazareti alimponya na kumwongoza vibaya kinyume cha sheria ya Sabato. Wanasheria walitegemea kwamba, atamvizia Yesu na kuwapatia sababu ya kumfunga kwa urahisi zaidi.
Chuki iliyoonyeshwa na makuhani wakati Yesu aliposafisha hekalu haikuwa kali sana kama wakati Mafarisayo walipoanzisha chuki dhidi ya Yesu baada ya uponyaji huo. Kristo alikuwa amefunua “haki”yao, na kuwaonyesha kwamba haki yao haitegemei kushika tu sheria. Mungu anahitaji kuona rehema na upendo. Utakatifu bila upendo siyo wa kweli. Mungu anatafuta rehema ndani yetu, wala si kutimiza taratibu fulani. Tushukuru kwamba Mungu ametuweka huru na maelfu ya sheria au maagizo, akitujalia upendo kuwa ndiyo agizo lake la pekee.
SWALI:
- Kwa nini Wayahudi walimhukumu Yesu?