Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- John - 092 (Abiding in the Father's fellowship appears in mutual love)
This page in: -- Arabic -- Armenian -- Bengali -- Burmese -- Cebuano -- Chinese -- English -- Farsi? -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Kyrgyz -- Malayalam -- Peul -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Thai -- Turkish -- Twi -- Urdu -- Uyghur? -- Uzbek -- Vietnamese -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

YOHANA - Nuru inaangaza gizani
Somo la Injili ya Kristo kufuatana na Mtume Yohana
SEHEMU YA 3 - Nuru yang’aa ndani ya shirika la Mitume (Yohana 11:55 - 17:26)
D - Kuagana njiani kwenda Gethsemane (Yohana 15:1 - 16:33)

2. Kudumu kwetu ndani ya ushirikiano na Baba huonekana katika upendano kati yetu sisi na yeye (Yohana 15:9-17)


YOHANA 15:9
“Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu.”

Baba alivyompenda Mwana kiasi cha kupasua mbingu wakati wa ubatizo wake katika mto Yordani. Roho Mtakatifu alishuka katika mfano wa hua, pia na sauti ikasikika, “Huyu ndiye Mwanangu mpendwa ninayependezwa naye.” Tangazo hilo la Utatu Utakatifu wakati Yesu alipotwishwa dhambi za wanadamu chini ya alama ya ubatizo, hapo basi ilikuwa ni chanzo cha njia ya kafara ya Mwana Kondoo wa Mungu. Mwana alikamilisha mapenzi ya Baba, akijimwaga kabisa kwa ajil ya ukombozi wetu. Upendo huu haukukoma kwa Baba na Mwana, lakini wako wamejiunga pamoja katika upendo kwa ajili ya dunia hii ovu, wakitayarisha huo ukombozi kuu.

Yesu atupenda kwa kipimo cha upendo wa Baba; wakati yeye alipokuwa mtii; sisi hapana, hatukutii. Hakuna kati yetu aliyefanyika tangu milele, ni Yesu tu. Jambo lililotendeka ni kwamba, Mwana alituchagua sisi watenda dhambi na kutusafisha. Alitupatia kuzaliwa mara ya pili kwa njia ya Roho na kututakasa. Hatuangaliwi kama vitu tu vya kuchezewa mkononi mwake, hata kutupwa chini akitaka, hata kidogo. Yeye anatufikiria mchana kutwa , akituchunga kwa shughuli tukufu. Hutuombea daima na kutuandikia barua za upendo ndani ya Injili. Anatutia moyo tuamini, tuwe na upendo na tumaini. Kama tungeweza kukusanya upendo wote unaotolewa na wakina baba na mama wote duniani wakati wowote, pia na kuweza kusafisha upendo huo na machafu yote na namna za kibinadamu, hayo yote yangonekana kidogo sana kulingana na upendo wa Yesu kwetu, ambao hauwezi kukosea wakati wowote.

YOHANA 15:9-10
“Kama Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.”

Yesu anakuonya, “Usijitenge na upendo wangu. Ninakupenda na kutazamia kupata thibitisho la upendo wako kwangu. Sala zako ziko wapi? Yako kama kiungo chako cha simu kwenda mbinguni? Je, matoleo yako kwa ajili ya wenye shida yanalingana na ukuu wa kazi yangu ya kukuokoa? Ninakusihi utende yale yaliyo mema, ya kupendeza, yenye huruma na takatifu. Udumu ndani ya upendo wangu. Roho Mtakatifu atakusukuma kutenda mema, jinsi Mungu atendavyo mema daima.”

Ni dhambi kutokupenda jinsi Mungu anavyopenda. Kristo anakusudia kutupandisha kwenye usawa wa rehema ya Mungu; “Uwe mwenye rehema jinsi mimi na Baba tolivyo na huruma”. Pengine unajisikia kwamba hii haiwezekani. Uko sawa, kama jambo hilo lingekuwa kwenye eneo la uwezo na kufikiri kwetu. Basi bado hujaelewa linalohitajika na Kristo, ambalo yeye anaweza kutenda ndani yako. Anamimina Roho yake ndani yako, ili uweze kupenda jinsi yeye anavyopenda. Katika roho huyu Paulo anasema, “Nayaweza mambo yote katika Kristo anitiaye nguvu.” (Wafil.4:13)

Yesu alishuhudia wazi jambo hilo kwamba kwa wakati wote hakuvuka mipaka ya mambo yaliyolingana na mapenzi ya Baba yake; alidumu ndani ya mapenzi ya Mungu daima. Kristo ndiye anayetokeza amani ya Mungu ndani yetu, pia na sala za kiroho na huduma zenye upendo.

YOHANA 15:11
“Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.”

Tamaa inafahamu hali ya moyo wa binadamu, kwamba inahangaika wakati wote inapokuwa mbali na Mungu. Kristo aliyedumu ndani ya pendo la Babaye alikuwa anajaa furaha na raha. Ndani ya utu wake kulikuwa na kuimba na kutukuza bila kukoma. Naye anatamani kutupatia, ikiwa ni pamoja na wokovu wake, bahari ya upendo wa undani. Mungu ni Mungu wa furaha, raha na heri.

Upendo hufuatwa na furaha, ambayo ni tunda la pili katika orodha ya matunda ya kiroho. Ambapo dhambi inakataliwa, kufurahi kunatawala moyo. Kristo anapenda kutuimarisha ndani ya furaha ya wokovu, ili iweze kufurika na kwa wengine. Mtu mwenye furaha hawezi kuzuia hiyo furaha ndani yake mwenyewe tu, lakini anapenda kuwaokoa na wengine wafikie changamko la kusamehewa na furaha ya hakika ya kutulia ndani ya Mungu. Ikiwa hivyo, furaha yetu itakamilika kwa ajili ya wengi watakaopata kuokoka. Jinsi Mtume alivyosema, “Mungu anataka wote waokolewe na kufikia ufahamu wa ukweli”. Uinjilisti ndiyo chemchemi ya furaha hata kati ya masumbufu na kuteseka.

YOHANA 15:12-13
“Amri yangu ndiyi hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake”

Yesu atupenda, afahamu majina yetu, tabia zetu, pia na yote yaliyoyapita maishani mwetu. Anasumbuka kwa ajili ya masumbufu yetu na shida zote. Yeye anayo mpango kwa ajili ya yote yajayo maishani mwetu akiwa na msaada. Yuko tayari daima kuongea nasi katika sala zetu, yu tayari kufuta makosa yetu na kutuvuta tuingie ndani ya maisha matakatifu katika kweli na usafi.

Jinsi Yesu anavyotupenda, basi hutamani nasi tupendane sisi kwa sisi. Tunapata kutambua zaidi hali ya jamaa na marafiki zetu, hata tunasumbuka pamoja na magumu na shida zao. Tunaanza kutambua makusudi yao na hali za nafsi zao. Twagundua maelezo kwa ajili ya shida zao na kuwapatia msaada wa kufaa na faraja, tukitumia muda wa kukaa nao. Wakifanya makosa, tunawapa pole na kuvumilia nao, bila hata kutaja yasiyo sawa na makosa yao.

Yesu ndiye aliyetokeza kilele cha upendo ndani ya maisha yake. Yeye hakuwa mwenye kusema na kusaidia tu, bali alijitoa kabisa kama sadaka kwa ajili ya wenye dhambi. Si kwamba aliishi tu kwa ajili yetu, lakini alikufa badala yetu. Msalaba ndiyo taji la upendo, ikitueleza habari ya upendo wa Mungu. Anatutaka na sisi tupeleke ujumbe huo wa wokovu kwa wengine, tukitoa sadaka za muda wetu na pesa zetu. Anapotuita kushirikisha Injili kwa wengine, pia tukitenda mbele zao yale aliyoyatenda Yesu kwa ajili yetu, anatutazamia tutoe za kwetu, mali yetu na nguvu zetu. Anawaombea hata wale wanaomdharau, akiwachukua kama marafiki. Aliwaombea hata maadui zake, “Baba, wasamehe, kwa vile hawajui watendalo.” Hakuwaita kama ndugu tu au watoto wa Mungu, lakini aliwaita “Wapendwa”. Kwa ajili ya wale ambao hawakustahili upendo huo, alikufa ili apate kuwakomboa.

YOHANA 15:14-15
“Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.”

Mungu anawaita “Wapendwa”. Tena afanya hayo kwa kila mmoja binafsi. Pengine uko na upweke, huna mtu wa kumwendea. Umtazame Yesu, maana amekufia na kuishi kwa ajili yako. Ndiye rafiki yako bora , akiwa tayari kukusaidia wakati wowote. Anafahamu mawazo yako, na anatazamia kuitika kwako kwa nia njema. Hali ya kudumu katika urafiki wake ni kwamba tunawapenda watu wote kama vile yeye anavyowapenda wote. Wawili hawawezi kuzozana wakati wakielezana wote wawili kumpenda Kristo. Urafiki wake unadai na sisi tupendane. Ametuita wapendwa wake; tu mali yake kwa sababu alituumba, na hivyo angeweza kutufanya kuwa watumwa wake. Lakini ametuweka huru na nira ya utumwa na kutuinua. Anatujulisha habari ya kazi zake tukufu. Hatuachi kama wapumbavu, lakini hutufundisha habari ya jina la baba, enzi ya msalaba na upendo wa Roho Mtakatifu. Kwa kutuonyesha siri ya Utatu Utakatifu anatufunulia kweli za milele zilizokuwa zimesitirika. Baba alikabidhi mambo hayo katika mikono yake Kristo, ili yeye apate kuyafunulia kwetu. Kweli urafiki wake ni kuu, kiasi cha kuturuhusu kushiriki katika kazi zake, fadhili, heshima, enzi na wake. Hashiki hata haki yake ya uwana au kufanywa mtoto, lakini anatuvuta kwake ili nasi tupate kuwa watoto wa Mungu.

YOHANA 15:16-17
“Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lolote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.”

Uhusiano wenu na Yesu hautegemei kwanza mapenzi yenu, kutaka kwenu au uzoefu wenu, bali ni kwa sababu ya upendo wake tu, uchaguzi na wito wake kwenu. Mlikuwa watumwa wa dhambi zenu, mkishikwa na makucha ya Shetani na utawala wa kifo. Mlikuwa hamwezi kuondoka katika gereza hilo, lakini Yesu aliwachagua tangu milele, ndipo kuwaweka huru kwa damu yake ya thamani. Akawafanya kuwa marafiki zake na kuwaamuru kuwa warithi wenye haki ya kuitwa wana. Uchaguzi wake huo ni neema tupu. Upande wenu inabakia jambo moja tu: Ni kumkubali au kumkataa. Yesu aliwachagua watu wote alipolipia adhabu ya dhambi za wote pale msalabani. - Si wote wanaoitika kwa wito wake huo, lakini wanapendelea kudumu ndani ya ziwa la matope ya dhambi. Hawafahamu uhuru wa watoto wa Mungu. Kristo amekuita wewe uje kwenye uhuru kutoka kwa dhambi uje kwenye ushirikianao tukufu. Ujizoeze mwenyewe katika kupenda. Uhuru wako una shabaha moja, kumtumikia Bwana wako na wanadamu wengine kwa hiari. Hakuna shurutisho kama kwa watumwa . Yesu akawa mtumwa kwa hiari kwa ajili ya upendo. Basi hivyo yeye ndiye mfano wetu, bila kujiangalia mwenyewe, bali alijihangaisha kwa ajili ya wapendwa wake.

Kwa sababu hiyo yeye anatamani kwamba na wewe uonyeshe hali ya kuwashughulikia rafiki zako, kama vile mchungaji afanyavyo kwa kondoo zake. Kwa vile uwezo wetu una mipaka, mtu hawezi kumweka huru mtu mwingine kutoka kwa utumwa wa dhambi. Yesu atutia moyo, ili tuombe katika jina lake. Maana tukiomba kwake Yesu kwamba yeye awaongoze wanaowekwa huru kwa nguvu zake na kuwajenga kiroho na katika tabia zao na kuwajalia yote wanayoyahitaji kwa mwili, moyo na roho, Bwana atajibu kufuatana na mapenzi yake mema. Siri ya maombi yanayopata kujibiwa ni upendo. Ukiomba kwa ajili ya rafiki zako katika roho ya namna hii, Yesu atakuonyesha makosa yako uliyo nayo bado mara kwa mara, na atakuongoza kuwa na maisha ya hekima na wa kufaa na kwa maombi ya kweli na katika hali ya kujinahi na ya unyenyekevu. Bwana atajibu, ukimwomba kwa wokovu na utakatifu ili uwafikie rafiki zako. Tunakutaka ufulize katika sala zako bila kuchoka. Yesu hatakuahidi matokeo yanayofifia, bali matunda ya kudumu. Yule atakayeamina kutokana na sala na ushuhuda wako ataishi milele, hali amepita toka kifoni kuingia uzimani.

Zaidi na juu ya imani, maombi na ushuhuda, Yesu akuagiza uwapende rafiki zako, kwa kimoyo, upendo wa unyofu na safi. Uwavumilie bila kujali tabia zao ngumu. Uwe mpole kwao, jinsi Mungu alivyo mpole kwako. Uangaze na mwangazo wa upendo wa Mungu katika ulimwengu uliopotoka na chafu. Ujizoeze katika huduma, kujitoa kabisa, kusikiliza na kuitika jinsi itakavyofaa. Heri upendo wa Kristo upate kun’gaa kutoka kwa maisha yako.

SALA: Bwana Yesu, tunakushukuru kwa sababu umetuweka huru kutoka kwa utumwa wa dhambi na kutufanya tuwe wapendwa wako. Heri tupate kujifunza kuwapenda wote jinsi unavyotupenda sisi. Tunakuabudu na kujiweka kwako upate kututumia. Utufundishe utii, ili tuweze kuleta matunda tele.

SWALI:

  1. Jinsi gani Yesu aliwafanya wale waliokuwa watumwa wa dhambi wapate kuwa Wapendwa wake?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on March 13, 2015, at 11:47 AM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)