Previous Lesson -- Next Lesson
d) Baraza la Wayahudi walimhukumu Yesu afe (Yohana 11:45-54)
YOHANA 11:45
“Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Mariamu, na kuyaona yale aliyoyafanya, wakamwamini.”
Lazaro akawa hai baada ya kufa kwake, akila, akinywa na kuzungumza. Watu wakakutana naye akiwa hai barabarani na nyumbani. Wengi walishangaa sana kwa uweza wa Yesu, wakaamini kwamba ndiye kweli Masihi, Mwana wa Mungu aliye hai. Basi wanafunzi wakazidi kuongezeka, na watu wakakimbilia nyumbani kwa Mariamu wawatazame Yesu na Lazaro.
YOHANA 11:46-48
“Lakini wengine wakaenda zao kwa Mafarisayo, wakawaambia aliyoyafanya Yesu. Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu anafanya ishara nyingi. Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa letu.”
Baadhi ya wale walioshuhudia huo mwujiza wakawakimbilia Mafarisayo, wawapashe habari kuhusu shughuli za Yesu. Hao bado walikuwa watu wasioamini, na hukumu ya Bwana juu yao imedokezwa katika mfano wa “Mtu Tajiri”, ambaye alipokuwa jehanum, Ibrahimu alimjibu, “wasipomsikiliza Musa na manabii, watakataa pia kumwamini mtu akifufuka kutoka kwa wafu” (Luka 16:31). Roho wa Mungu hataweza kubadili mioyo ya mawe inayokataa kumtegemea Yesu, hata ikiwa miujiza mikuu kabisa itaonyeshwa kwao.
Mafarisayo walikuwa na maongozi makubwa katika baraza kuu la kidini. Kiasi cha kumfanya kuhani mkuu akubali kusisitiza kwao.Washiriki sabini waliitwa kuhojiana jambo hilo. Masadukayo, watu waliokataa ufufuo, walikaribisha sana neno kuu la kikao. Washiriki hawakuwa na maoni ya namna moja, wakachanganyikiwa, kwa vile Yesu hakutenda dhambi fulani ili afungwe. Hata hivyo kulikuwa na mwamko wa kikristo kati ya umati wa watu kabla ya sikukuu ya Pasaka, ambapo makumi elfu ya waenda haji walimiminwa kwenye mji mkuu. Katika mahojiano yaliyofuata washiriki wa baraza walimtaja Yesu kama mtu wa kawaida, wala si mtu wa Mungu au nabii. Ingawa walimkataa kiasi hicho, walishindwa kukataa miujiza yake ya kushangaza mno.
Kadiri walivyoendelea kuhojiana, hofu ilifunika hali ya mjadala ndani ya baraza, kwamba enzi ya ufalme wa kirumi watambue jambo hilo na kuingilia. Kukusanyika kwa umati wa maelfu wanaomzunguka mtu atendaye miujiza katika namna ya Masihi inaelekeza kwenye hatari ya maasi. Kwa jambo kama hilo Warumi wangezuia hekalu, mahali pa utawala wa Mungu. Hivyo ibada za hekaluni zingekoma pamoja na sadaka, sala na mibaraka.
YOHANA 11:49-52
“Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, ninyi hamjui neno lolote; wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima. Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi yake, bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa hilo. Wala si kwa ajili ya taifa hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili wawe wamoja.”
Wakati ghasia na fujo ndani ya baraza ilipofikia kileleni, Kuhani Mkuu Kayafa akainuka na kuanza kukemea viongozi wa taifa, akiwashitaki ujinga na ya kutokutafakari. Alikuwa na namna ya haki katika matamshi yake, kwa vile alikuwa ni mwenyekiti wa baraza kwa cheo chake cha Kuhani Mkuu. Alikuwa ametiwa mafuta kichwani kwa ishara ya utakatifu, lakini alikuwa ni Mpinga-Kristo. Alitazamiwa kujazwa na Roho Mtakatifu, ili Mungu aseme naye kama kiongozi wa taifa. Hata hivyo alifuata kosa na ubadilifu. Kwa kushikilia madaraka ya nabii iliyounganika na cheo cha Kuhani Mkuu, aliwaeleza watu wake wote kuwa wajinga.
Katika namna ya “roho ya majuto” iliyojionyesha katika matamshi ya Kayafa, kwa vile shetani alisema kwa sauti yake, kwa kadiri ionekanavyo akatumika kwa shabaha za Mungu, ingawa kwa hali halisi alitenda kinyume. Bila shaka lolote, ilikuwa ni bora kwa watu kwamba Mwana Kondoo wa Mungu afe kwa niaba yao, ili wao waweze kupishwa ghadhabu ya Mungu na kujaliwa uzima wa milele. Lakini msemi wa Shetani alitamka mawazo hayo kwa ajili ya sababu za kisiasa, „Yesu afe ili atuokoe na hasira za Warumi.“ Kwa unabii huo wa kishetani maneno ya Kristo yakathibitishwa kwamba, shetani ndiye baba wa kiroho wa Wayahudi wengi, kwa vile ndiye mwongo na baba wa maongo.
Ingawa tabia hiyo ya kishetani ilijionyesha, mwinjilisti Yohana alitambua kwamba Kayafa alitamka kusudi ovu, ambalo kwa kweli ilikuwa ni ukweli tukufu. Kayafa alitumiwa kueleza kifo cha Yesu kuwa ni wokovu kwa wote, hata bila kutambua maana halisi la juu ya maneno yake „yenye amri“. Hapo mjinga ambaye hakutafakari kwa kutosha alikuwa ni Kayafa, kwa sababu hakumwamini Yesu, wakati Roho Mtakatifu alimwongoza atamke maneno halali kuhusu kifo cha Kristo cha kulipia makosa. Alishindwa kuelewa maana ya maneno yake mwenyewe, kwa vile yeye alikusudia yaliyokuwa kinyume.
Yohana alitambua maana ya tamko hilo katika upeo wa kusudi lake kuwa wokovu kwa ulimwengu. Yesu hakufa kuwa sadaka kwa dhambi za watu wake tu, bali kwa ajili ya mwumini yeyote kati ya mataifa. Wote wanaomtegemea yeye ni watoto wa Mungu; kwa njia ya tumaini lao ndani ya Mwokozi wanapokea uzima wa milele pamoja na nguvu na uweza wake.
Shabaha ya imani yetu sio wokovu wetu wa binafsi tu, lakini umoja wa watoto wote wa Mungu wawe wamoja katika Kristo. Upendo wake ndiyo alama na nguvu ya ukristo. Jina lake linaunganisha wafuasi wake. Wakati wowote wanapounganika na kiini chao, pia wameunganika wao kwa wao. Basi tuamke na kuhimizana kuelekea kwake, tutambue kwamba wote tu ndugu na wadada ndani ya familia ya Mungu, hata tuwe karibu zaidi ya ujamaa wa kimwili.
YOHANA 11:53-54
„Basi tangu siku ile walifanya shauri la kumwua. Kwa hiyo Yesu hakutembea tena kwa wazi katikati ya Wayahudi; bali alitoka huko, akaenda mahali karibu na jangwa, mpaka mji uitwao Efraimu; akakaa huko pamoja na wanafunzi wake.”
Baadhi ya wanachama wa baraza walichokozwa na utabiri kali wa Kayafa, kwa vile walijisikia upande wa Yesu, bali wengi wao walifurahia, wakisadiki kwamba Mungu alisema kwa maneno ya Kayafa kupitisha hukumu juu ya mdanganyi huyu na kuokoa taifa. Kwa upatano baraza lilithibitisha hukumu na kuafiki shauri la Kayafa kumwua Yesu. Bila shaka wengine kati yao waliokuwapo, wale wenye unyofu zaidi, walikataa, lakini hakuna aliyewasikiliza. Mjanja Kayafa aliwaongoza vibaya kwenye mpango kumharibu Yesu, tena kuitmiza kwa siri; ili kupisha vurugu kati ya watu.
Yesu alipata habari ya hiyo hila, na pengine alitambua hayo kwa utambuzi wa ki-mungu. Aliondoka katika eneo la utawala wa baraza akaenda maeneo ya bonde la Yordani, mashariki ya Nablus, akingojea hapo pamoja na wanafunzi wake wakati wa kusulibiwa na kufufuka kwake.
Mpaka hapo “eneo la mapigano” likawa wazi: Kuhojiana kwake na makuhani tangu kusafisha Hekalu - pamoja na kushindana na wanasheria kuanzia uponyaji wake siku ya Sabato - sasa ikafikia kilele kwa kumfufua Lazaro. Hivyo, viongozi wa watu wakaamua kumwua mfadhili wao mara moja.
Nuru yang’aa gizani, wala giza halikuliweza (Yoh.1:5) Ndugu mpendwa, umeona kwamba Kristo ndiye nuru? Je, Injili yake imemulikia mawazo yako na kutengeneza moyo wako? Uzima wake wa milele umekujia, na Roho yake amekuongoza ukatubu na kuungama dhambi zako na kuumba imani ndani yako upate kubarikiwa na kukutakasa? Kama bado, basi fungua moyo wako na kumruhusu Roho wa Kristo akuvute kwake, ukitoa maisha yako na siku za mbeleni mikononi mwake, ili usipate kukubaliana hata bila kutaka na maadui wa Yesu katika hukumu yao juu yake. Bora uungane na wanafunzi wake, ukaendelee kumwelewa zaidi na zaidi huyu Mtakatifu, ili na wewe upate kukiri kwa furaha, “Tumeona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.” ( Yoh.1:14b)
SALA: Bwana Yesu Kristo, asante sana kwa kutokukataa kweli katika saa ya hatari kwako; wewe siku zote ulimtukuza Baba yako wa mbinguni. Uwe radhi kwa imani yetu dhaifu na ya kulegea. Utuvute ndani ya ushirikiano wako na Baba, ili tuishi katika uzima wa milele na kukutumikia bila kukoma. Pokea maisha yangu, ili niwe sifa kwa ajili ya neema yako tukufu.
SWALI:
- Kwa nini baraza la kiyahudi walimwua Yesu?
NAMBA - 4
Mpendwa Msomaji, ututumie majibu sahihi kwa maswali 15 katika hizo 17. Ndipo sisi tutakutumia somo linalofuata katika mfululizo wa masomo hayo.
- Jinsi gani Yesu aliwathibitishia Wayahudi kwamba, wao sio watoto wa Ibrahimu?
- Tabia za Ibilisi ni zipi, ambazo Yesu alitufunulia waziwazi?
- Kwa nini Wayahudi walitaka kumpiga kwa mawe Yesu?
- Kwa nini Yesu alimponya yule mtu aliyezaliwa kipofu?
- Kwa nini Wayahudi walikataa uwezekano wa kumponya mtu aliyekuwa haoni tangu kuzaliwa?
- Jambo gani huyu kijana alifaulu kutambua polepole wakati alipohojiwa?
- Kuinama chini mbele ya Yesu kunaonyesha nini?
- Baraka za Yesu anazoziweka juu ya kondoo zake ni zipi?
- Jinsi gani Yesu anapata kuwa Mchungaji Mwema?
- Jinsi gani Kristo anaongoza kundi lake?
- Jinsi gani Yesu alitangaza uungu wake?
- Kwa nini Yesu alisema habari ya utukufu wa Mungu, iwapo Lazaro alikufa?
- Kwa nini Yesu aliendelea kwa ki-ushindi ili amwokoe Lazaro?
- Jinsi gani sisi tunafufuka toka kifoni siku hizi?
- Kwa nini Yesu alifadhaika na kwa nini alilia machozi?
- Jinsi gani utukufu wa Mungu ulijionyesha wakati wa kumfufua Lazaro?
- Kwa nini baraza la kiyahudi walimwua Yesu?
Kumbuka kuandika jina lako na anwani yako kamili kwenye karatasi ya majibu ya quiz, wala si kwenye bahasha tu. Halafu uitume kwa anwani hii:
Waters of Life
P.O.Box 600 513
70305 STUTTGART
GERMANY
Internet: www.waters-of-life.net
Internet: www.waters-of-life.org
e-mail: info@waters-of-life.net