Previous Lesson -- Next Lesson
a) Yesu akiwa ng’ambo ya Yordani (Yohana 10:40 - 11:16)
YOHANA 11:11-16
“Aliyasema hayo; kisha baada ya hayo akawaambia, Rafiki yetu Lazaro amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha. Basi wale wanafunzi wakamwambia, Bwana, ikiwa amelala, atapona. Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu aliwaambia waziwazi, Lazaro amekufa. Nami nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini; lakini na twendeni kwake. Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.”
Lazaro alielezwa na Yesu kama “mpendwa wetu”. Mara niyingi Yesu na wanafunzi wake waliwahi kuwa wageni nyumbani kwake Lazaro. Hivyo alikuwa ni rafiki wa wanafunzi wote. Basi, twaweza kusema, Lazaro kama “mpendwa wa Yesu” lalingana na jina la Ibrahimu aliyeitwa “rafiki wa Mungu”.
Yesu alitumia neno la “kulala” kwa ajili ya kufa, ili akaze hali halisi kwamba, kifo sio mwisho wa maisha yetu. Miili yetu itaharibika, lakini roho zetu zitadumu. Pumsiko letu leo na kesho imo ndani ya Bwana kiimani. Tunaridhika na kutulia ndani ya uhai wake, na tutachunguza atakavyotuamsha siku kuu ya ufufuo. Tutaishi milele.
“Naenda nipate kumwamsha”, akasema Yesu kwa tumaini kuu. Hakusema, “tuombe na kumwulizia Mungu atakavyo tufanye, na namna ya kufariji familia.” Hapana, Yesu alikuwa akiwasiliana na Baba yake kwa siku mbili kabla ya habari kumfikia kwamba, rafiki yake amekufa. Alikuwa na uhakika kwamba kumfufua Lazaro itatangulia ufufuo tukufu.ya kwake mwenyewe. Jambo hilo lilikusudiwa ili kuimarisha imani ya wafuasi wake na kuwathibitishia maadui zake kwamba yeye pekee ndiye Masihi. Ndipo kwa mkazo akaongeza kutamka: “Naenda kumwamsha”, kama vile mama fulani angesema, “Naenda kumwamsha kijana wangu, saa imefika aende shuleni”. Yesu hakuonyesha haraka lolote - yeye alikuwa ni uzima nafsini mwake na Bwana juu ya mauti. Imani ndani ya Yesu inatuweka huru na hofu yoyote, na pia itatuimarisha katika mwenendo wetu.
Wanafunzi walishindwa kuelewa maana ya ushindi wa Kristo wakati ule. Wao walidhani kwamba Lazaro amelala usingizi; basi hapakuwa na sababu ya kwenda kwake na kumwamsha. Na zaidi kwa sababu wangehatarisha maisha yao kwa mikono ya Wayahudi.
Ndipo basi Yesu akazungumza waziwazi habari ya kifo cha Lazaro, akisema, “Yeye amefariki”. Julisho hilo liliwachanganya wanafunzi, lakini Yesu aliwahakikishia kwa kusema, “Mimi nafurahi.” Basi, hiyo ndiyo kuitikia kwake Mwana wa Mungu kwa habari ya kifo. Maana anaona ushindi na ufufuo. Kifo sio sababu ya kuomboleza, bali kwa kufurahi, maana Yesu awahakikishia wafuasi wake uzima kweli. Maana yeye mwenyewe ni uzima; yeyote amwaminiye anashiriki uzima wake.
Ndipo Yesu aliendelea, “Mimi nafurahi kwa ajili yenu, kwamba sikuwapo wakati wa kifo chake, na hivyo sikumponya hapo hapo. Hii ndiyo alama kuhusu mwisho wa kila mtu. Hata hivyo, imani ndani yangu inamwanzishia uhai mpya. Basi twende kwake.” Kwenda hivyo kwa mfu inamaanisha machozi na maombolezo kwa wanadamu, lakini kwake Yesu inasema habari ya ufufuo. Tumshukuru Mungu kwamba Yesu atasema wakati tukilala makaburini kwamba, “Twende kwake.” Kuja kwake kwetu itamaanisha uhuru, uhai na nuru.
Mtume Tomaso alikuwa amempenda Yesu na kuwa mwaminifu kwake. Alipotambua uamuzi wa Kristo kwenda kwa mfu, bila kutambua kwamba shabaha ya Kristo ilikuwa kumnyofoa kaburini, basi Tomaso aliwaelekea wenzake na kuwaambia wazi, “Hatutamwacha Yesu peke yake; twampenda Bwana wetu na kusindikizana naye hadi kufa. Wote tumefungamana naye.” Hivyo Tomaso alikaza uaminifu kwake Yesu hadi mwisho.
SWALI:
- Kwa nini Yesu aliendelea kwa kiushindi ili amwokoe Lazaro?