Previous Lesson -- Next Lesson
f) Ibilisi, mwuaji na mwongo (Yohana 8:37-47)
YOHANA 8:37-39
„Najua ya kuwa ninyi ni uzao wa Ibrahimu lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halimo ndani yenu. Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo. Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiyo Ibrahimu! Yesu akawaambia, Kama mgekuwa watoto wa Ibrahimu, mgezitenda kazi zake Ibrahimu.“
Wayahudi walijijua wenyewe kuwa ni wazaao wa Ibrahimu, na kwa sababu hiyo wakadhania kwamba, kiungo hiki na Baba wa imani inawarithisha ahadi, ambazo Mungu aliziweka juu ya mtumishi wake mtiifu.
Yesu hakukataa faida za uhusiano huo, lakini alihuzunika kwamba watoto wa Ibrahimu walikuwa hawana roho ile ya babu zao. Roho hiyo ingaliwajalia uwezo wa kusikiliza sauti ya Mungu na kushika Neno lake. Lakini kwa hali hiyo walifunga mioyo yao kwa maneno ya Yesu. Hilo neno lilishindwa kuingia mioyoni mwao au kuwamulikia. Waliendelea bila kutambua na bila kuamini.
Matamshi ya Kristo hayakuleta matunda katika umati huo ila kukataa na kuchukia tu. Bila shaka, wengi wao hawakufikia hali ya kukusudia kumwua Yesu. Ila Yesu akafunua makusudi ya mioyo yao na kujua kwamba chuki ndiyo utangulizi wa uuaji. Alifahamu baadaye mapema watalia kwa sauti „Msulibishe, msulibishe“ (Mathayo 27:21-23; Yohana 19:15 ).
Ibrahimu alikuwa msikivu wa sauti ya Mungu na mara akamtii. Na kwa ajabu zaidi, Yesu hakusikiliza tu daima sauti ya Babaye, lakini zaidi aliona kazi ya Mungu na enzi yake. Mafunuo yake yalikuwa kamili, yakichipuka kutoka katika ushirikiano wake wa karibu na Mungu. Yesu ndiye Roho kutokana na Roho wa Mungu na upendo kutokana na upendo wake.
Lakini Wayahudi walimchukia Huyu aliyetokana na Baba. Hii ilithibitisha kwamba, wao hawakutoka kwa Mungu wa kweli. Chimbuko la mafikara yao haikuwa ya ki-mbinguni. Kwa hatua hiyo ya mjadala, Yesu alijaribu kuwavuta wafikirie msimamo wa “mababa” yao. Basi, hakuwa ni Ibrahimu.
YOHANA 8:40-41
“Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo. Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani Mungu”.
Wayahudi waliudhika na maneno ya Kristo, kwa sababu aliwasuta kwamba hawamo katika namna ya roho ya Ibrahimu. Tumaini lao kwamba ni uzao wa Ibrahimu lilitengeneza msingi wa imani na tumaini lao pamoja na kujivuna. Basi, namna gani Yesu alithubutu kuona kosa katika uhusiano wao na Ibrahimu na kuifuta tu?
Yesu naye aliwaonyesha kwamba kazi zake Ibrahimu alizitenda katika utiifu kwa imani yake kwa Mungu, alipoondoka na kusafiri kama mhamiaji. Tumaini lake ndani ya uaminifu wa Mungu lilijitokeza alipokubali kumtoa mwanawe Isaka awe sadaka; pia na unyenyekevu wake aliyoonyesha kwa mpwa wake Lutu. Lakini Wayahudi walipanua ukaidi, uasi na kutokutii kwao. Roho zao zilikuwa kinyume kabisa na ya Kristo. Hivyo wakajadili Ukweli uliyoingia mwilini na kusimama katikati yao - wala hawakusikiliza sauti ya Mungu iliyowajia kwa njia yake Kristo. Yesu hakuja kama Mwana wa Mungu akizungukwa na malaika katika utukufu, hapana. Lakini kama mtu wa kawaida, akiwa na enzi ya Neno lake tu. Hakuwashurutisha watu kukubali Injili yake. Alifunua upendo wa Mungu, neema yake, pia na jina lake. Walikataa habari zake njema kwa dharau. Wakacheza na wazo la kumwua. Hayo yalikuwa kinyume kabisa na sifa na matendo ya Ibrahimu. Maana yeye alisikiliza, akatii, akaishi na kutimiza kufuatana na mafunuo ya Mungu kwake.
YOHANA 8:42-43
“Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma. Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu”.
Yesu aliwathibitishia Wayahudi kwamba, Ibrahimu sio baba yao; naye akawaongoza watambue jina la baba hasa waliomfuata (shetani). Jinsi alivyokuwa, ndivyo walivyokuwa.
Wayahudi walijisikia kwamba, Yesu alionyesha wazi utofauti uliokuwepo kati yake na wao. Waliitika kwamba wao si watoto waliozaliwa kwa zinaa, jinsi walivyokuwa Wamoabu na Waamori waliozaliwa kwa zinaa ya maharimu (Mwa. 19:36-38). Wala hawakuwa taifa la kuchanganyika kama vile Wasamaria, bali walisisitiza kwamba Mungu ndiye Baba yao, wakitegemea maandiko ya Kutoka 4:22 na Kumb.32:6, pia na Isaya 63:16. Basi Yesu aliposisitiza kwamba Mungu ndiye Baba yake, wao walirudisha kwa nguvu kwamba yeye ni Baba yao pia kufuatana na Maandiko. Hii ilikuwa ni kanuni ya imani yao, ambayo waliipigania, pia na kuteswa kwa ajili yake. Bali ushuhuda wao ulikuwa si kweli. Yesu alionyesha kwa kifupi kwamba walijidanganya wenyewe. Aliwaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana Mungu ni upendo wala si chuki. Yeye humpenda mwanawe atokaye kwake, naye Mwana anabeba namna yake”. Yesu hakuwa na namna ya kujitegemea, mbali na Baba, hata dakika moja; lakini alimtii kama Mtume mwaminifu.
Ndipo Yesu aliuliza umati wa watu, “Mbona mnakosa kuelewa lugha yangu? Mimi sisemi kwa ulimi wa kigeni, lakini naliwatolea Roho yangu kwa maneno rahisi, kwamba hata wadogo hao wangeshika na kuelewa”. Yesu alijibu maswali yake mwenyewe, akiwaambia adui zake, “Mwashindwa kunisikiliza; ninyi hamko huru, ninyi ni watumwa; uhai wenu wa kiroho umepotea. Mnafanana na viziwi wasioweza kusikia wito.”
Ndugu mpendwa, hali ya kusikiliza kwako kiroho ina hali gani? Unasikia neno la Mungu moyoni mwako? Unasikia sauti yake inayokusudia kukusafisha na kutengeneza utu wako wa ndani? Au unayo kiburi, bila usikivu, kwa sababu roho fulani ya kigeni imekushika? Je, unafanya kazi kwa ajili ya Mungu katika nguvu ya Injili, au roho mbaya inaishi ndani yako, ukifuata mwongozo wake?
SWALI:
- Jinsi gani Yesu aliwathibitishia Wayahudi kwamba, wao sio watoto wa Ibrahimu?