Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- John - 047 (Sifting out of the disciples)
This page in: -- Albanian -- Arabic -- Armenian -- Bengali -- Burmese -- Cebuano -- Chinese -- Dioula? -- English -- Farsi? -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Kyrgyz -- Malayalam -- Peul -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Thai -- Turkish -- Twi -- Urdu -- Uyghur? -- Uzbek -- Vietnamese -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

YOHANA - Nuru inaangaza gizani
Somo la Injili ya Kristo kufuatana na Mtume Yohana
SEHEMU YA 2 - Sehemu ya pili: Nuru inang’aa gizani (Yohana 5:1 - 11:54)
B - Yesu ni chakula cha (mkate wa) uzima (Yohana 6:1-71)

5. Kupepetwa kwa wanafunzi (Yohana 6:59-71)


YOHANA 6:66-67
66 “Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. 67 Basi Yesu aliwaambia wale Thenashara, Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka?”

Mwujiza wa kuwalisha watu elfu tano ulitokeza shauku kati ya umati mkubwa. Hata hivyo, Yesu alionyesha uongo uliyokuwa nyuma ya hiyo shauku, iliyowafanya wengi waondoke kwake. Yeye hahitaji bidii ya kujifanya au uchaji wa Mungu, wala si usadiki tupu kwa makusudi ya mashaka. Anahitaji kuona kuzaliwa mara ya pili, imani ya kweli ya kumtamani yeye bila kujizuia kwa jambo lolote. Wakati uo huo wapelelezi toka baraza kuu la Yerusalemu walipenya kati ya wafuasi wake. Waliwatisha wale kwamba, wao wanafaa kuondolewa kati ya Wayahudi, kama watanag’ania kumfuata yule waliyemwita mdanganyifu. Basi wengi wa Kapernaumu waliondoka kwake, hata umati wa watu wa kawaida wakawa dhidi yake Yesu. Hata wale waaminifu wakaanza kuhofia mamlaka ya baraza kuu. Wakajisikia kwamba kanuni za Yesu zinapita kiasi. Kundi ndogo tu la wafuasi wa kweli waliendelea naye. Bwana alikuwa akipepeta ngano kutoka kwa makapi.

Kabla ya hilo Kristo alikuwa amewachagua mitume kumi na wawili kutoka kwa hao wafuasi wake, kulingana na makabila kumi na mbili za watu wake Waisraeli. Nambari hii inajumlika na namba tatu mara nne, sawa na mbingu na nchi, au kwa kueleza zaidi, ni Utatu utakatifu na pembe nne za nchi. Hivyo, katika kundi la wanafunzi wake mbingu na nchi zimechangamana.

Baada ya mgawanyo huo, Yesu zaidi akawajaribu hao aliowachagua, ili kuthibitisha wito wao na kusema: “Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Kwa swali hilo aliwashurutisha wanafunzi wake waamue waende wapi siku za mbeleni. - Kwa njia hii Yesu anakuuliza na wewe na rafiki zako, je, wakati wa hofu au saa za mateso, utataka kumwacha au utanang’ania kwake? Mambo gani kwako ni muhimu zaidi: mapokeo, shauku za kujisikia furaha, elimu ya juu au usalama kwa ajili ya mali, hayo yote kwa upande moja, au upande wa pili uhusiano kamili na Bwana Yesu?

YOHANA 6:68-69
68 “Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. 69 Nasi tumesadiki, tena tumejua ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”

Petro alionyesha wazi thibitisho la unabii wa Kristo, kwamba yeye ndiye mwamba imara. Alisema kwa niaba ya wenzake wote akitamka: “Bwana, tuende kwa nani? Wewe pekee ndiwe asili ya uzima wa milele.“ Pengine hakutambua kabisa makusudi ya Yesu, lakini ndani sana nafsini mwake alitambua kwamba, huyu mtu Yesu wa Nazareti ndiye Bwana toka mbinguni, na kutoka kwake yatokea maneno yenye uwezo wa kuumba na ya kuhuisha, wala si maneno ya mtu wa kawaida tu. Petro aliamini kwamba, Bwana alikuwapo hapo pamoja naye. Alishiriki katika kugawa mikate. Mkono wa Yesu ulimshika wakati alipokuwa karibu kuzama majini. Moyo wa Petro uliambatana na Yesu, alimpenda Bwana wake kuliko chochote kingine, wala asingeweza kumwacha. Petro alimchagua Yesu, kwa sababu Yesu alikuwa amemchagua kwanza.

Kiongozi wa Mitume alijumlisha ushuhuda wake na maneno haya: “Tumeamini na kujua”. Angalia, yeye hakusema, “Tulijua na ndipo tuliamini”. Maana ni imani inayofungua maoni ya moyo. Ni imani yetu inayomulikia akili zetu. Hivyo Petro na wenzake walijitoa kwa mvuto wa Roho wa Mungu, aliyewaongoza kumwamini Yesu na kuwamulikia kutambua kweli. Wakakua katika utambuzi wao kuona utukufu wake ambao haujawa wazi. Utambuzi wowote kumhusu Yesu moja kwa moja ni zawadi ya ukarimu wa Mungu.

Jambo gani ilikuwa ni msingi wa imani ya wanafunzi ndani ya Yesu? Jambo gani ilikuwa , ni kiini cha imani hii? Walikuwa wameambatanishwa na Masihi Mtukufu, ambaye ndani yake ukamilifu wa Roho ulitawala. Aliunganisha ndani ya nafsi yake huduma zote za kikuhani, za kifalme na za unabii. Wafalme, makuhani wakuu na manabii ndani ya Agano la Kale walikuwa wenye kumiminiwa mafuta na Roho Mtakatifu. Hivyo ndani ya Kristo zimeunganishwa nguvu na baraka zote za mbinguni. Yeye ndiye Mfalme Mtukufu ulimwenguni kote; pamoja na hili yeye ni Kuhani Mkuu anayepatanisha wanadamu na Mwumbaji wao. Anayo uwezo wa kufufua wafu; naye atahukumu ulimwengu. Kwa imani Petro alitambua utukufu wa Kristo.

Wanafunzi kwa pamoja walimwamini; na pamoja na Petro kama msemaji wao walishuhudia utoaji wa ushuhuda huo wa kuhakikisha: Huyu ndiye Yesu, Mtakatifu wa Mungu, wala si mwanadamu wa kawaida, bali pia ni Mungu kweli. Tabia zote za Mungu zilikuwa ndani yake, akiwa Mwana wa Mungu. Akadumu bila dhambi, akatimiza shabaha yake kama Mwana Kondoo wa Mungu, jinsi Mbatizaji alivyotabiri juu yake. Wanafunzi wake walimpenda na kumheshimu, maana walitambua kwamba, kuwepo kwake ilimaanisha kuwepo kwa Mungu mwenyewe. Ndani ya Mwana walimwona yeye Baba na kujifunza kwamba Mungu ndiye upendo.

YOHANA 6:70-71
70 “Yesu akawajibu, Je, mimi sikuwachagua ninyi Thenashara na mmoja wenu ni shetani? 71 Alimnena Yuda, mwana wa Simoni Iskariote; maana huyu ndiye atakayemsaliti; naye ni mmojawapo wa wale Thenashara.”

Yesu alikaribisha ushuhuda huo wa Petro kwa furaha, maana ilionyesha kukua kwa imani yao. Hata hivyo alitambua kwamba mmoja kati ya nambari yao alikuwa kinyume chake kwa matokea kadhaa. Moyo mgumu wa huyu mtu ukaendelea kuwa ngumu zaidi kiasi cha kumfanya Yesu kumwita “shetani”. Mitume wote walikuwa wamechaguliwa, walipovutwa na Baba kwake Mwana, lakini hawakuwa kama mashine mkononi mwa Mungu. Waliendelea kuwa huru kutii sauti ya Roho au kuipuuza. Yuda Iskariote kwa makusudi alifunga akili yake kwa sauti ya Mungu na hivyo akajikabidhi kwa Shetani, aliyeweka kiungo cha akili kati yake na yeye.Yuda hakuondoka kwa Yesu peke yake kama wengine walivyofanya waliomwasi, bali akaendelea kusindikizana na Yesu – mnafiki aliyejifanya tu kwamba anaamini. Akawa mwana wa “Baba wa uongo” akazidi kuendelea katika udanganyifu. Hapo Petro alipokiri huduma ya Yesu ya Masihi, Yuda alikaribisha mawazo ya kumsaliti Kristo kwa baraza kuu. Kwa kuchochewa na chuki kwa siri alipanga kusudi lake la udanganyifu.

Huyu mwinjilisti hakufunga sura yake hii muhimu kwa matendo ya ajabu kutokana na uwezo waliopewa Mitume, hapana. Bali aliona bora aonyeshe kwamba hata katika shirika la waaminifu kulikuwa na msaliti. Yesu hakumfukuza, wala hakufunua jina lake kwa hao wengine. Bali alimvumilia kwa upole, kwa nafasi kwamba labda Yuda apate kutubu ubaya wa moyoni mwake.

Ndugu mpendwa, ujichunguze kwa unyenyekevu. Wewe ni mtoto wa Mungu au mtoto wa shetani? Wajifungua wazi kwa mvuto wa Roho Mtakatifu, au unaelekea kwa mapatano na shetani? Angalia sana usije ukakosa shabaha ya maisha yako. Bwana wako anakupenda, naye amekuokoa. Hata hivyo ukijizuia na wokovu wake, utapelekwa polepole kwenye njia za uovu na kudidimia ndani ya kifungo cha shetani. Rudi kwake Kristo, maana anakungojea sana.

SALA: Bwana Yesu Kristo, wewe ndiwe Mwana wa Mungu, takatifu, mwenye rehema, mwenye enzi na ushindi. Nisamehe makosa yangu na kuniimarisha ndani ya agano lako, ili niweze kuishi katika utakatifu na kuendelea machoni pako, na hivyo kubadilishwa ndani ya mfano wako. Watakase wafuasi wako, wapate kukua katika imani na ufahamu, pia na washuhudie kwa wote kwamba, wewe pekee ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Amina.

SWALI:

  1. Maana halisi ya ushuhuda wa Petro ni nini?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on October 07, 2013, at 11:56 AM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)