Previous Lesson -- Next Lesson
1. Utume kutoka kwa baraza kuu (iitwayo Sanhedrin) unamhoji Mbatizaji (Yohana 1:19-28)
YOHANA 1:19-21
19 “Huu ni ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani? 20 Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. 21 Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La.
Uamsho ulitokea kule bondeni mto Jordani kwa sababu ya Mbatizaji. Maelfu hawakuzuiliwa na barabara mbaya toka milimani hadi bondeni chini sana. Walitelemka kwa Mbatizaji ili wapate kusikia sauti ya huyu nabii mpya na kubatizwa naye wapate ondoleo la dhambi zao. Kawaida mikusanyiko ya wengi si kwamba hawatambui mambo, kama vile walivyodhaniwa na wenye kiburi, lakini walikuwa wenye njaa kweli ya kutamani mwongozo wa kujua ukweli. Kwa haraka hutambua nguvu na mamlaka ndani yao wanaojazwa nayo. Hawakutaka kusikia habari ya sheria au mapokeo, lakini walikuwa wenye hamu ya kukutana na Mungu. Wajumbe wa Sanhedrin, baraza kuu ya kidini ya wayahudi walikuwa wametambua habari ya uamsho huu. Walituma ujumbe wa makuhani na wasaidizi wakali, waliozoea kuchinja dhabiu. Waliagizwa kumwuliza Mbatizaji maswali, ili akipatikana kuwa amefukuru, wawe na sababu ya kumwua.
Kwa hiyo mkutano huu kati ya Mbatizaji na wajumbe wa baraza la Sanhedrin ulikuwa wa hatari sana. Mwinjilisti Yohana alikuwa anawaita watu hao waliokuja kutoka Jerusalem “Wayahudi”. Kwa jina hilo anafunua shabaha moja ya injili yake. Maana wakati ule mawazo ya kiyahudi yalikuwa ya kulinda sheria kwa vikali na wivu, isibadilishwe. Hivyo Yerusalem ilipata kuwa mahali pakuu pa kupinga Roho wa Kristo. Si watu wote wa Agano la Kale, lakini kikundi cha makuhani, hasa mafarisayo, walikuwa waangalifu wa dini, na maadui wa namna yoyote waliohisiwa kubadilisha mipango na uongozi wao. Hii ilikuwa sababu yao ya kutaka kumtega Mbatizaji kwa maswali yao.
“Wewe u nani?” ilikuwa ni swali la kwanza waliomwuliza Yohana, aliyekuwa amezungukwa na mkusanyiko wa kutubu na kumsikiliza kwa makini. “Ni nani aliyekupa ruhusa ya kunena? Wewe umesoma sheria na mafundisho ya dini? Wewe unajiona kuwa umetumwa na Mungu, ama unajiona kuwa wewe ndiye Masihi?”
Yohana Mbatizaji alitambua hila ndani ya maswali yao, naye hakusema uongo. Kama angesema, “Mimi ndiye Masihi”, wangemhukumu na kumpiga kwa mawe. Kama angesema, “Mimi siye Masihi“, watu wangemwacha na kusema yeye hana umuhimu. Wakati huo taifa la uzao wa Ibrahimu waliteseka kwa aibu ya kutawaliwa na Warumi. Walitamani mkombozi ambaye awaokoe kutoka kwa minyororo ya Warumi. Mbatizaji alikiri wazi kwamba, yeye si Kristo, wala yeye si mwana wa Mungu. Hakukubali cheo ambacho si kwa uongozi wa Roho Mtakatifu. Alichagua kunyenyekea na kuwa mwaminifu kwa wito wake, akimtumaini Mungu kwamba yeye kwa wakati wake atadhihirisha ukweli wa ujumbe wake.
Baada ya pigo lao la kwanza, wakaendelea kumwuliza, „Wewe ni Eliya?“ Jina hilo ilihusika kwa ahadi katika kitabu cha Malaki 4:5 inaposema kwamba, kabla ya kuja kwake Masihi atatokea nabii mwenye nguvu na roho kama nabii Eliya, ambaye alishusha moto toka mbinguni. Pia alimfufua mtu kutoka kwa wafu kwa uwezo wa Mungu. Kila mtu alimtambua shujaa huyu kuwa ni kiongozi katika taifa lao. Lakini Yohana alinyenyekea, ingawa kwa kweli yeye alikuwa ni nabii yule wa ahadi, jinsi Kristo alivyomkiri baadaye habari zake. (Mathayo 11:14)
Ndipo makuhani walimwuliza, kama yeye ndiye nabii waliyemngoja aliyetabiriwa na Musa kwamba atakuja nabii kama yeye, naye ataleta agano mpya (Kumbukumbu 18:15) Ndani ya swali lao walitamani kujua ni nani aliyempa ruhusa ya kunena kama nabii. Walisisitiza kwa kumwuliza yeye ni nani na amepewa mamlaka gani, au kama ananena kwa mafunuo ya Mungu au anajisemea mwenyewe tu.
Mbatizaji alichukua wajibu na nafasi kama ya Musa. Hakukusudia kusimamisha Agano Jipya na Mungu, bila kuruhusiwa naye kufanya hivyo. Wala hakuwaongoza wasililizaji wake kwa ushindi wa kivita. Yeye aliendelea kuwa mwaminifu katika majaribio, wala hakujifanya mwerevu au kujivuna. Pia alikuwa mwenye hekima na hakuwajibu maadui hao zaidi ya majibu yaliyohitajika. Ni jambo la maana hata kwa maisha yetu kutumia busara ya aina hiyo.
SALA: Bwana Yesu, tunakushukuru kwa kumtuma Yohana Mbatizaji ulimwenguni, mtu ambaye hakujivuna wakati wowote. Tusamehe kwa kuwa tumejivuna kuwa wakubwa mara kwa mara, na kwamba tu wenye maana kuliko wengine. Utufundishe kuelewa ya kwamba tu watumishi ambao hatuna lolote, ila wewe tu ndiwe mkuu.
SWALI:
- Ni nini shabaha ya maswali yaliyoulizwa na wajumbe kutoka baraza kuu ya dini ya wayahudi?