Previous Lesson -- Next Lesson
a) Baki takatifu lipo (au: linaendelea kuwepo) (Warumi 11:1-10)
WARUMI 11:1-10
"1 Basi, nauliza,je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa kabila la Benjamini. 2 Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, 3 Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. 4 Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali. 5 Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa, yako mabaki waliochaguliwa kwa neema. 6 Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema. 7 Imekuwaje basi? Kitu kile ambacho Israeli alikuwa akikitafuta hakukipata; lakini wale waliochaguliwa walikipata, na wengine walitiwa uzito. 8 Kama ilivyoandikwa, Mungu aliwapa roho ya usingizi, macho hata wasione, na masikio hata wasisikie, hata siku hii ya leo. 9 Na Daudi asema, Meza yao na iwe tanzi na mtego, na kitu cha kuwakwaza, na malipo kwao. 10 Macho yao yatiwe giza ili wasione, ukawainamishe mgongo wao siku zote.“
Mtume Paulo anaandaa kwa ajili ya hoja juu ya wokovu na uharibifu wa watoto wa Ibrahimu. Anadokeza swali la kutisha: „Je, Bwana wa agano aliwafukuza watu wake wenye mioyo migumu kwa daima?“ (Zaburi 94:14)
Paulo anajibu lile swali akisema, Hapana! Jambo kama hilo lisingewezekana, maana mimi mwenyewe ni thibitisho la neema ya kuokoa ya Bwana. Aliniokoa mimi, niliyekuwa mvunja sheria mwenye dhambi. Kufuatana na mwili, mimi ni wa kabila la Benjamini, na wa uzao wa Ibrahimu. Ila Bwana aliniita, akanisamehe na kunijalia uhai. Nipo hapo kama thibitisho la neema ya Bwana ya kuokoa kwa ajili ya watoto wa Yakobo.
Jinsi nilivyoendelea kuishi ndani ya Kristo, ndivyo Bwana mara kwa mara aliwaita watu binafsi kutokana na makabila yote ya watoto wa Yakobo. Aliwaokoa, akawabariki na ndipo kuwatuma. Kutokana nao Bwana aliunda Ukristo wa asili. Bila hao Wakristo kutokana na Wayahudi, waliojaliwa maisha mapya ndani ya Kristo tusingaliweza kuona maandiko yoyote ya Injili ya Kristo. Wao walikuwa kiini hasa cha ufalme wa Mungu, nao walipanda mbegu za Mungu katikati ya mataifa. Na mavuno kwa kujienda yalizidishwa, na ufalme wa Bwana unakwenda na kukua bila kukoma hata bila kelele.
Mungu anao watu aliowachagua, naye anazo njia zake kwa ajili ya ufalme wake wa kiroho. Hakuwakataa hao wapendwa wake, ingawa hata siku hizi, sehemu kubwa ya watoto wa Yakobo wanamkataa na kumchukia Kristo na wafuasi wake, kwa sababu wao wanafuata miungu mingine. Lakini basi hali ilikuwaje wakati wa nabii Eliya? Huyu nabii mwenye ushujaa alipumua kwa uzito kwa sababu ya waumini wa kweli kuangamizwa kwa kutoa damu, jambo lililoanza upande wa kaskazini wa ufalme, pia na kwa sababu ya tangazo la malkia la kumwua yeye mapema (I.Wafalme 19:10-14).
Hapo Bwana alimjibu Eliya kwa maneno ya kumfariji: „Pamoja na hayo nitajisazia katika Israeli watu elfu saba, kila goti lisilomwinamia Baali, na kila kinywa kisichombusu“ (I.Wafalme 19:18). Hakuna ajuaye hao waumini imara walikuwa wakina nani. Walikuwa ndiyo wale salio takatifu, na tunafikiri ndiyo wale waliofukuzwa na ndipo kuongozwa kwenye utumwa wakati wa kuharibiwa kwa Samaria, ambapo walitangaza imani yao hata mwisho wa dunia. Mungu huwalinda waumini wake, na hakuna awezaye kuwapokonya mkononi mwake. Wala hawaahidii maisha yenye raha au kusaza, bali huwajalia mashahidi wake uhakika wa kiroho wa kudumu daima. (Yohana 10:29-30) Katika mahojiano hayo, Paulo alitoa swali lake: „Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa, yako mabaki yaliochaguliwa kwa neema“ (Warumi 11:5).
Tamko hilo lasimama tangu kuzaliwa kwake Kristo. Alama ya Wakristo waaminifu sio nguvu, wala utajiri, wala heshima, bali kumfuata Yesu, hata katika mateso. Kwa namna hiyo Yesu aliwaambia kundi ndogo wa wafuasi wake: „Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme“ (Luka 12:32 pia 22:28-29).
Mamlaka ya Baba, Mwana na Roho Mtaktifu unaumba siku zote chaguo la baraka katika watakatifu wake wachaguliwa. Paulo na Barnaba waliwaambia wale walioitwa kati ya watu wakati wa safari yao ya kwanza ya kueneza injili: „Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi“ (Matendo ya Mitume 14:22b).
Mtume Paulo anaimarisha ufahamu huo na kushuhudia kwamba, baki la watoto wa Yakobo itaendelea, wala halitaangamizwa, lakini kwa sababu ya neema tu (Warumi 11:6). Bwana analilinda na majaribu ya kishetani siku zile za mwisho, naye ataliongoza kama Mchungaji Mwema. Wala baki hilo si lenye haki, takatifu, au kuchaguliwa kwa ajili ya matendo yao; lakini wema wote lililo nalo ni kutokana na neema tu. Kwa sababu hiyo tunahitaji kuamini ndani ya enzi ya neema ya Kristo iliyo ya kipekee na ya kuenea kote, na inatunza hiyo baki takatifu ya watu wa Israeli. Inatupasa kumshukuru Bwana kwa ajili ya jambo hilo, kwa sababu kuendelea kwake ndiyo pia siri ya kuwepo kwetu sisi wakristo.
Katika Warumi 11:7 Paulo anauliza: Hali yao ya kiroho ya watoto wa Yakobo wakati ule ilikuwaje, na pia siku hizi ikoje? Walimaanisha nini kwa kuifuata sheria (au amri)? Na shabaha ya kicho chao ilikuwaje, ambayo hawakuifikia? Walipoteza shabaha yao, wakamsulibisha Mfalme wao, wakawa wagumu dhidi ya uongozi wa Roho Mtakatifu, kwa kusudi lao wakasogea mbali na umoja wa Utatu Utakatifu, wakatumikia wafalme na viongozi wa nchi zingine waliowatumia kwa faida yao tu, nao wakamngojea mshindani mkuu wa Kristo watawale naye juu ya watu wengine wote. Basi ukweli huo wa kuuma hauwajumlishi watoto wote wa Yakobo, kwa maana sehemu ndogo ya watoto wa Ibrahimu wakawa wamezaliwa mara ya pili kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hao waliyajua makosa yao na kuyaungama hadharani, wakamwamini Mwana Kondoo wa Mungu mnyenyekevu, wakapokea msamaha kamili, nao pia wakapakwa mafuta ya Roho Mtakatifu aliyeahidiwa kwao nao. Wakaishi katika uhai wa Kristo, nao wakapata kuwa washiriki mashuhuli ndani ya mwili wake wa kiroho.
Hata hivyo, shemu kubwa ya taifa lao wakawa wagumu (Kumbukumbu la Torati 29:4 na Isaya 29:10). Wakapokea roho ambayo ilishindwa kutambua mema na mabaya. Kwa hiyo, hawakuwa na uwezo wa kutambua yafaayo na yasiyofaa, bali wakatenda lolote walilopenda, bila kujali habari ya Mungu na hukumu ya mwisha. Maana wakiwa wenye macho, hawakuona, na wakiwa na masikio, hawakusikia, ingawa Mfalme Daudi aliomba kwa Bwana na kumtaka kuwaadhibu wengi wao, na ageuze mipango yao kuwa mtego kwao (Zaburi 69:23-24).
Hata hivyo, Yesu alibadili maneno hayo mazito ya Daudi, naye akawaagiza wafuasi wake: „Wapendeni adui zenu, waombeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni“ (Mathayo 5:44-45).
Baki hilo takatifu la watu waliochaguliwa, pia na Wakristo kote duniani, wote wanathibitisha umuhimu wa kuwepo kwao kwa ajili ya kutimiza maagizo ya Kristo hata katikati ya mateso, msongo na mashitaka ya uongo.
SALA: Ee Baba wa mbinguni, tunakuabudu kwa ajili ya watoto wa Ibrahimu ambao namba yao inaendelea kuongezeka, wanaofungua mioyo yao kwa Roho Mtakatifu yako; watakase wenyewe kwa damu ya Yesu, na wapokee uzima wa milele. Twaomba, waimarishe hao walio wapya kiimani, na uwatunze, ili wapate kutambua kuwepo kwako pamoja nao katikati ya mateso ya kutisha, pia wajalie msaada kwa wenzao kiimani, na wasipate kumezwa na matengano.
SWALI:
- Je, ipi ni maana ya maneno ya Mungu kwa Eliya kwamba, alibakiza watu elfu saba kati ya Waisraeli, wale wote ambao hawakupiga magoti mbele ya Baali?
- Je, ipi ni maana ya maneno ya Paulo kwamba, yeye na wafuasi wote wa Kristo kutoka kwa Wayahudi ni washiriki katika baki takatifu ya wateule wa Mungu?