Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- Romans - 057 (Is Israel Responsible for their Unbelief?)
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hebrew -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Malayalam -- Polish -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Turkish -- Urdu? -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
SEHEMU 2 - HAKI YA MUNGU HAISOGEI HATA BAADA YA WATOTOWA YAKOBO, WATEULE WAKE, KUFANYA MIGUMU MIOYO YAO (Warumi 9:1-11:36)
4. Haki ya Mungu hupatikana tu kwa imani, wala si kwa kujaribu kutimiza sheria (Warumi 9:30 - 10:21)

d) Je, Israeli inawajibika kwa ajili ya kutokuamini kwao? ( Warumi 10:16-21)


WARUMI 10:16-21
"16 Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? 17 Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. 18 Lakini nasema, Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. 19 Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa asema, Nitawatia wivu kwa watu ambao si taifa, Kwa taifa lisilo na fahamu nitawaghadhibisha. 20 Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema, Nalipatikana nao wasionitafuta, Nalidhihirika kwao wasioniulizia. 21 Lakini kwa Israeli asema, Mchana kutwa naliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi."

Paulo alilishuhudia kanisa la Rumi kwa ya tamko lake la dhahiri iliyotangulia kwamba, wengi zaidi kati ya Wayahudi waliokuwa wakimngojea Masihi hawakumtambua, wala habari njema ya ushindi ndani yake, lakini walilipinga neno la Mungu wakati wowote. Jambo hilo lilikuwa wazi nyakati za nabii Isaya, aliyekuwa amejaa huzuni naye alihangaika katika sala zake kwa ajili ya watu wake miaka 2700 iliyopita, akisema: „Nani aliamini habari zetu?“ (Isaya 53:1).

Wayahudi wengi walisikia Injili. Lakini hawakuielewa wala kuiamini. Baadhi yao walisikia neema moyoni iliyotolewa kwao, lakini hawakuwa tayari kuitii. Walipenda zaidi mazingira yao ya kutokuamini na hali yao ya taifa lililo gumu kuliko kumpenda Bwana aliyewaokoa, nao waliogopa watu kuliko Mwumbaji wao mwenye rehema.

Paulo aliitika kwa hiyo hali yao ya kuchuchia na jumla ya hotuba yake iliyotangulia; kwamba imani hutokana na mahubiri. Jambo lililo muhimu hapo sio namna injili inavyokufikia; kama ni kwa njia ya wimbo, au kwa mstari fulani wa Biblia, bali kwamba Mungu anapogonga mlangoni pa moyo wako, mara moja wewe umfungulie; la sivyo utakuwa hatarini kwamba, atakupita na kwenda zake. Hao wote wanaoleta injili kwa watu haiwapasi kuileta katika maneno ya kielimu sana na matamko ya jamala, ambayo hayaeleweki kwa watu wa kawaida, bali kwa maneno rahisi, ambayo wasikilizaji waweze kuelewa. Inampasa msemaji kuleta ujumbe wa Mungu kwa lugha ya wale wanaomsikiliza. Pia anatakiwa kuleta ujumbe kamili, wala si kwa sehemu tu. Mhubiri yeyote inampasa kujizoeza sana na alete pia mifano kutoka kwa maisha ndani ya hotuba yake, naye atamke kwa urafiki na katika namna ya kugusa watu binafsi. Sala nazo lazima zisindikize kazi hiyo ya kueneza neno na mapenzi ya Mungu. Na mhubiri lazima aamini kila neno analolitamka, akifikia kilele cha ushuhuda wake na sifa na kumshukuru Mungu.

Kuhubiri sio aina ya kufundisha kiakili, bali ni wito toka kwa Bwana, kwenye msingi juu ya maagizo yake na ujumbe kwa wale waliotiwa nguvu naye. Kwa hiyo, imani yetu ndani ya Bwana ni muhimu zaidi kuliko ufahamu wetu wa injili, maana Bwana alitupatia neno lake kwa kulipeleka kwa wale walio tayari kusikiliza; waonywe nalo, wafundishwe nalo, waitwe, watiwe moyo na kuwatingisa. Haimpasi msemaji kusema badala ya Kristo, bali bora awe mjumbe mwaminifu kwake, jinsi Mtume Paulo alivyosema: „Haya basi, tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinvya vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu (II.Wakorintho 5:20).

Paulo alijiuliza: Pengine wengi wa Wayahudi hawajasikia habari ya wokovu wa Kristo. Labda hakuna aliyewaeleza waziwazi habari ya Mwokozi wa pekee. - Sisi twapata jibu kwa maswali ya mtume katika Zaburi ya 19:5; neno la Mungu ni kama jua la haki. Linapanda toka mashariki ya mbinguni na kuzunguka mpaka upande wa pili; na hakuna linalositirika na hari yake. Jinsi jua linavyomulika dunia yote, ndivyo na injili inavyomulika dunia. Wakati wa Yesu, umati wa watu walikimbia waone miujiza yake na kusikiliza maneno yake. Siku hizi twasema, yeyote atakaye kusikia, anapata nafasi ya kusikia; na yeye anayetafuta, ataona. Redio na mipango katika TV zinasaidia, hata yeyote atakaye kusikia aweza kusikia injili.

Siku hizi watu wajiuliza: Je, nichague nini: Pesa au vinywaji vikali? Pesa au Mungu? Nitafute sifa, uwezo, mambo ya wanawake, au mambo ya kujifurahisha? Au je, nitake kusikiliza na kutii neno la Mungu? Watu hujitoa kwa hali ya kuridhika katika maeneo yote ya maisha. Haya, nani basi yu tayari kusikiliza na kumtumikia Mwumbaji wake? Paulo anaendelea kujiuliza: Pengine watoto wa Yakobo hawakuelewa hayo waliyoambiwa! Pengine injili haikupelekwa kwao kikamilifu! Lakini tayari Mungu alikuwa amejibu swali hilo kwa njia ya Musa aliposema: „Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu; wamenikasirisha kwa ubatili wao; nami nitawatia wivu kwa wasio watu; nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo“. (Kumbukumbu la Torati 32:21).

Katika tamko hilo kwake Musa, Bwana alikusudia kuwaambia watu wake: „Kwa vile hujawa tayari kusikiliza neno langu, mimi nitajifunua na kutoa upendo wangu kwa watu ambao hawakuchaguliwa nao ni watu bila elimu. Nitakufanya wewe kuwa na wivu na kukasirika utakapoona watu wasiochaguliwa wanajaliwa nami badala yako uliye taifa lenye kiburi na majivuno. Nitawaongoza wale wapate kunipenda na kuniheshimu.“

Mungu alikuwa amemjulisha nabii wake Isaya miaka 600 kabla ya Kristo: „Watu wasionitaka wanauliza habari zangu; nimeonekana na hao wasionitafuta, naliliambia taifa lisiloitwa kwa jina langu“ (Isaya 65:1 na Warumi 9:30).

Siku hizi twaona kwamba, Mungu huwapinga wale wasioamini katika njia zao kwamba, wapate kutambua kwamba, Mungu yupo. Huwa anasema na wale wasiomjali kwa njia za ndoto, matukio fulani au hata kwa magonjwa. Katika ulimwengu unaoendelea kielimu, tunawaona watu wengi wenye elimu ya juu wasiopata jibu kwa maendeleo ya walimwengu, isipokuwa kwa kukiri kwamba yuko Mwumbaji, wakati ambapo watu wa Mungu wenyewe wanampuuza Bwana wao na kumwacha. - Basi Mungu anayo maelfu ya njia za kuwafanya watu wengine wasiojulikana wawe watu wake. Jambo hilo basi lilikuwa ni siri ambayo Paulo aliliona kwa huzuni, lakini upande wa pili pia kwa furaha wakati wa safari zake za kueneza Injili (Matendo ya Mitume 28:24-31).

Mungu naye alikuwa amemwambia Isaya: „Nitazameni, nitazameni! Mchana kutwa nimewanyoshea mikono yangu watu walioasi, watu waendao njia isiyo njema, wakifuata mawazo yao wenyewe, watu wanikasirishao mbele za uso wangu daina“ (Isaya 65: 2-3a). Kwa tangazo lake Bwana anataka kutuambia kwamba, alinyosha mikono yake kwa watu wake wasiotii, jinsi mama anavyomnyoshea mikono mtoto wake, ili asianguke na kupata taabu. Namna hiyo basi, Bwana alitamani kuwaokoa watu wake, lakini alitambua kwamba, hawakuwa tayari kumsikiliza. Kwa makusudi hawakutii neno lake na kwa ukorofi walifanya uasi dhidi yake.

Jinsi ulivyo kuu upendo wa Mungu, ambaye hawasahau hata wale wanaomwacha na kuishi kwa kutokujali, wakinang‘ania katika uasi wao. Hata hivyo yeye aendelea kuwapatia upendo wake wakati wowote. Mwishoni basi, Hakimu atatoa hukumu yake dhidi ya sehemu kubwa ya wateule wake. Wao kwa kusudi hawakumtii yeye, wala hawamtaki awaokoe. Basi, wako kama kipofu ambaye, ingawa ameonywa habari ya shimo, bado kwa kusudi anajikwaa na kuanguka ndani yake. Hivyo basi, Bwana aliwaambia wazi hao Waisraeli kwamba, wao peke yao tu ni wenye wajibu kwa ajili ya hali yao mbaya, hata mbali na upendo wake kwa ajili yao.

SALA: Ee Baba wa Yesu Kristo, wewe pia ni Baba yetu, unayetunyoshea mikono yako, jinsi mama anyosheavyo mikono yake kwa mtoto wake, ili asianguke. Tunakuabudu kwa ajili ya upendo wako, na tunakuomba ufungulie masikio ya watoto wa Yakobo kwamba, wasikilize neno la Yesu, walitii kwa furaha na shukurani. Amina.

SWALI:

  1. Jinsi gani mtu yeyote anaweza siku hizi, kama anataka, kusikia, kuelewa na kukubali injili?
  2. Kwa nini Mungu alifanya watu wapya kutoka kwa mataifa yoyote kuwa wateule wake?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on November 17, 2022, at 07:16 AM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)