Previous Lesson -- Next Lesson
1. Mashaka ya Paulo kwa ajili ya watu wa taifa lake waliopotea (Warumi 9:1-3)
WARUMI 9:1-3
"1 Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, 2 ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu. 3 Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili;“
Mtume Paulo anaanza maelezo ya hali ya Wayahudi, watu wake, waliofanya migumu mioyo yao, akitumia maneno hayo ya kushangaza: „Nasema ukweli katika Kristo“. Hatolei namna ya filosofia, wala si maoni yake ya binafsi, bali anatamka kutokana na ufahamu chungu na uhakika baada ya kupitia kwenye mateso, ambayo hayakutokana na nafsi yake, bali kwa sababu ya kudumu kwake ndani ya Kristo. Hashirikishi nasi imani yake ya binafsi, badala yake ni Yesu asemaye ndani ya matamshi yake; maana Bwana ndiye kichwa cha kiroho, na wafuasi wake ni mwili wake wa kiroho na viungo vyake vya kutenda kazi.
Paulo anawahakikishia wasomaji wa waraka wake kwamba, maungamo yake ya dhati ni kweli, kwa maneno haya, „Nayaandika, wakati dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu“. Kristo wangu ndiye Mwokozi, ambaye ndani yake Roho wa ukweli hufanya kazi. Roho huyu hawezi kuruhusu uongo, au kupinda maneno, au kupiga cheng a, au kudhania tu, ila inasukuma na kuongoza wafuasi wa Kristo wawe mashahidi wa ukweli na kwamba, matamshi yao yawe thabiti na ya kukomaa.
Dhamiri ya mtume ikawa ni dira yake ya kiroho. Yeye hakutenda mbalimbali akiongozwa na hali alivyojisikia mwenyewe tu, kwa vile moyo wake ulifanywa kuwa mpya na kutolewa kabisa kwa uongozi wa Roho Mtakatifu.
Roho huyu tukufu ulihakikisha amani katika dhamiri yake, pia na maneno yake yaliyokuwa wazi kabisa. Hivyo, ushuhuda wake ulikuwa ni wa kweli kwa namna yoyote ile.
Haya basi, ni nini, ambayo Paulo aliyoshuhudia baada ya mashauri hayo marefu ?
Alishuhudia kwamba, alikuwa na huzuni nzito kwa ajili ya watu wake, ambao hawakumtii Mungu wao. Mtume alikuwa na masikitiko mno kwa ajili ya jamaa zake wapendwa nao aliowajua sana, hata hali ya kusikia majonzi haikumwacha kabisa.
Huzuni hiyo kuu, kutokana na kukuza hali ya kuwa na mioyo migumu kwa mambo ya kiroho katika taifa lake, ilikuwa inaishi moyoni mwake na kumsindikiza wakati wote. Moyo wake ulisikitishwa kwamba, wengi sana katika watu wake walionekana kuwa vipofu kiroho, wasiweze tena kutambua kweli za kiroho zilizofunuliwa kwao. Kwa hiyo, mtume alitamani kuwaokoa, lakini wao hawakutaka kuokolewa, maana walijifikiria kwamba, wao wenyewe walikuwa na haki, na kwa hiyo hawakuwa na haja ya kupokea wokovu, ambao Paulo alisema habari zake.
Basi huzuni zake Paulo zilienda mbali kiasi cha kuwa tayari kubeba adhabu ya watu wake, kama hatua hiyo ingeweza kuwa njia ya kuwapatia wokovu. Upendo wake kwa ajili ya watu wake ilikuwa na uzito kwamba, alikuwa tayari kukataliwa na Yesu, Mwokozi wake, kama hatua hiyo ingesaidia lolote kwa ajili yao.
Paulo aliona watu wake walivyopotea kama familia yake na kabila lake. Aliwachukulia kama ndugu na jamaa zake, kwa vile walitokana na babu zake yeye mwenyewe. Alikuwa tayari kufanya na kutoa kila kitu, mradi wao wapate kuokolewa na ghadhabu ya Mungu.
SALA: Ee Bwana Yesu Kristo, wewe ulilia kwa ajili ya Yerusalemu (Luka 19:41), na kuhangaika kutokana na kutokutii na kuwa na mioyo migumu kwa watu wako, lakini uliwasamehe dhambi zao kule msalabani ulipoomba: „Baba, uwasamehe, kwa sababu hawajui wanalolitenda“ (Luka 23:34) Utusaidie, Ee Bwana, tuwapende watu wetu, pia tuhangaike kwa sababu ya hali yao inayoongezeka kuwa ya kutokutii. Tusaidie kuwaombea, na pia kwa ajili ya wana wote wa Yakobo, ili wapate kuungama kweli, wakutambue wewe na kukupokea. Amina .
SWALI:
- Huzuni kuu ya Paulo ilikuwa na sababu gan?
- Paulo alikuwa tayari kutoa sadaka gani kwa ajili ya wokovu wa watu wake?