Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- Romans - 050 (The Spiritual Privileges of the Chosen)
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hebrew -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Malayalam -- Polish -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Turkish -- Urdu? -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
SEHEMU 2 - HAKI YA MUNGU HAISOGEI HATA BAADA YA WATOTOWA YAKOBO, WATEULE WAKE, KUFANYA MIGUMU MIOYO YAO (Warumi 9:1-11:36)

2. Mapendeleo ya kiroho ya hao watu waliochaguliwa na Mungu (Warumi 9:4-5)


WARUMI 9:4-5
"4 ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa Torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; 5 ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhidimiwa milele, Amina.“

Paulo alitaka kukumbusha kanisa la Rumi habari ya mapendeleo ya kiroho pamoja na haki za watu wake. Pamoja na hayo alikiri kwamba, mapendeleo hayo hayakumsaidia yeye mwenyewe pamoja na watu wake kumtambua wala kumkubali Masihi wa kweli; ndiyo maana walikuwa wamemchukia, kumkataa kabisa, pia na kumwonea wivu kiasi cha kumtolea asulibiwe, huku wakifanya migumu mioyo yao, hata dhidi ya Roho Mtakatifu. Jinsi giza inavyoingia kila jioni polepole na si kwa mara moja, ndivyo hali ya kuwa ngumu kimoyo iliwaangukia watu wake.

Tuone tena, hii mibaraka waliojaliwa hao jamaa za Paulo ilikuwa ya namna gani na hata kuwatofautisha na watu wengine?

Jina lao la kiasili lilikuwa ni „Watoto wa Yakobo“, yule mdanganyi, wala si „Watoto wa Israeli“.

Lakini baba yao, aliyekuwa na madhambi, hakuachana na Bwana, hadi Bwana alipomjalia baraka.

Kwa sababu ya imani yake imara ya Yakobo, Bwana alibadilisha jina lake liwe Israeli, maana yake, „yule aliyeshindana na Mungu, „El“, na kushinda kwa imani yake“. Si kwamba Yakobo alikuwa mwenye nguvu sana za kimwili, wala hakuwa na adabu ya pekee, ila imani imara ilitawala ndani yake, na hiyo ilimsalimisha na ghadhabu ya Mungu na hukumu yake (Mwanzo 32:22-32).

Yakobo alipata kuwa mmoja wa mababu wa ukoo, ambamo Yesu alizaliwa. Yesu ndiye Mwana Kondoo wa Mungu aliyechukua dhambi za ulimwengu, na aliyeshindana pamoja na Mungu, ili kutuokoa na hukumu ya dhambi zetu. Alishikamana na Mungu kwa imani, na hakuachana naye hadi Mungu alipotubariki sisi sote. Huyu Mwana wa Mariamu ndiye Mwokozi wetu aliyetuweka huru na hukumu. Hapo tunaona, mshindanaji wa kweli wa kushindana na Mungu, sio Yakobo, bali ni Yesu, ambaye yeye pekee ndiye Israeli wa kweli, aliyetukomboa na hasira ya Mungu.

Wayahudi, Wakristo na hata Waislamu wasiomkubali huyu mpatanishi, aliyehangaika kwa ajili ya hao wote, hawataweza kushiriki katika mibaraka yake, wala hawatakuwa sehemu ya watu wake wa kiroho aliyewachagua. Ufahamu huo ndiyo uliojaza moyo wa Paulo na huzuni, maana aliona jinsi wengi wa watu wake hawakutambua haki zao walizoahidiwa, bali waliyakataa hayo kwa ukaidi katika upofu wao wa kiroho na kiburi chao kilichopita kiasi.

Bwana Mungu alimwagiza Musa aelekee kwa Farao wa Misri na kumwambia kwamba, hao watoto wa Yakobo ni wana wake wa kwanza (Kutoka 4:22; Kumbukumbu la Torati 14:1; Hosea 11: 1-3). Bwana alikuwa akihuzunika kutokana na ukaidi wa watoto wake, ambao hawakumheshimu, ingawa aliwajalia haki ya kuitwa watoto wake. Walikuwa hawakuzaliwa mara ya pili, hata hivyo walikuwa na haki ya wazaliwa wa kwanza wa Bwana.

Utukufu wa Bwana ulitawala mahali patakatifu pa patakatifu penye chumba cha ndani kabisa cha hekalu, hata wakati watu wake wateule walipozunguka jangwani. Bwana aliwalinda na kuwaongoza kati ya hatari kadhaa, naye aliwatendea miujiza mingi (Kutoka 40:34; Kumbukumbu la Torati 4:7; Wafalme I,2:11; Isaya 6:1-7; Ezekieli 1:4-28; Waebrania 9:5). Hata hivyo, Bwana aliwaadhibisha wateule wake na kuwatisha hata na mauti kutokana na kutokuamini kwao, ila maombezi ya Musa na Haruni yaliwaokoa na ghadhabu yake tukufu (Hesabu 14:1-25).

Basi Paulo anawakumbusha hao Wayahudi na mapendeleo mengine yanayoonekana katika mfululizo wa maagano, ambao yanashuhudia matamko makuu na yenye enzi ya Mungu, kwamba Bwana, Mwumbaji wao na Hakimu mwenye haki, amejifunganisha mwenyewe kwa hilo taifa ndogo kwa daima. Biblia Takatifu linatueleza habari ya maagano hayo yafuatayo:

Agano la Mungu na Nuhu (Mwanzo 6.18 na 9:9-14).
Agano la Mungu na Ibrahimu (Mwanzo 15:18 na 17:4-14).
Agano la Bwana na Isaka na Yakobo (Mwanzo 26:3 na 28:13-19; Kutoka 2:24).
Agano la Bwana na Musa (Kutoka 2:24 na 6:4 na 24:7-8 na 34:10 + 28).

Lakini, la kusikitisha ni kwamba, Biblia Takatifu lashuhudia kwa kurudia kwamba, hao watu wa Agano la Kale waliachana na hizo ahadi za Mungu tena na tena, kwa hiyo nabii Yeremia alitamka kwamba, Bwana aliamua kutengeneza Agano lingine Jipya nao, pamoja na kuzaliwa kwa upya kiroho hao watu wake, ambao hawakumtii (Yeremia 31:31-34) Amri za Mungu ndizo msingi za Agano la Bwana na watu wake kwa mkono wa nabii wake Musa. Kitabu kile cha Agano lenye Amri Kumi kilikuwa ni chanzo cha jumla ya maagizo 613, yaliyogawanyika katika maagizo 365 ya kukataza jambo fulani na maagizo 248 ya kuwataka kutenda jambo fulani, kutokana na Maimonides (Myahudi aliye mfilosofia na mtaalamu wa Torati).

Mwanzoni mwa amri hizo twasoma moja kwa moja tamko hilo: „Mimi ndimi Bwana, Mungu wako. Usiwe na miungu mingine mbele zangu“ (Kutoka 20:1-3).

Mtu anayechunguza kusudi la amri hizo, atakuta tena amri hiyo: „Uwe mtakatifu, maana Bwana, Mungu wako ni mtakatifu“ (Mambo ya Walawi 19:2). Ndipo kiini cha amri hizo ni: „Mpende Bwana, Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa nguvu zako zote (Kumbukumbu la Torati 6:5), na pia „Umpende jirani yako kama nafsi yako (Mambo ya Walawi 19:18).

Lakini basi tunakuta kwamba, hakuna ila Yesu tu, aliyezitimiza amri hizo zote (Zaburi 14:3 na Warumi 3 :10-12).

Ibada mbele za Sanduku la Agano, na baadaye ndani ya Hekalu la Yerusalemu, kwanza kabisa ilidai takaso la mtenda dhambi kwa njia za sadaka kadhaa za damu, ili aweze kuruhusiwa kumwelekea Mungu na kumwabudu katika hali bila dhambi. Tena hali hiyo ilifikiwa kwa njia ya kutamka zaburi, nyimbo na maombi, ungamo la dhambi, kushika taratibu zote na kwa kuabudu. Mtu anayeingia sana ndani ya kitabu cha Zaburi na cha Torati, atakuta wazi roho hiyo ya uhusisho na matamko hayo. Jambo la muhimu katika vitendo hivyo vya ibada, mbali na kutoa sadaka, ilikuwa ni habari ya kupokea baraka.

Hatua hizo za ibada zilifikia kilele chake wakati wa sikukuu, hasa hasa siku ya Pasaka, ya Pentekoste, ya Sanduku la Agano, na ya Yom Kippur (siku ya upatanisho).

Jambo kuu hasa la Mungu kuishi ndani ya Hekalu la Yerusalemu ndilo lililoimarisha umoja wa lile taifa la Waisraeli. Lakini mbali na mahali pa kiini chao cha kiroho, vilikuwepo na vijiji vingi vilivyotengeneza madhabahu kwa ajili ya Ma-Baali na hivyo kutoa sadaka kwa miungu mingine, wakiinua sanamu zao na mifano, vilivyochokoza hasira ya Mungu dhidi yao.

Agano la Kale inajaa na ahadi kuu kadhaa, ambamo ndani yake tutakuta makusudi matatu:

a) Kuwepo kwa Mungu wao, msamaha wake, ulinzi wake na faraja yake (Kutoka 34:9-11)
b) Ahadi ya kuja kwake Masihi, au Kristo, Mfalme wa amani, na aliye Mwana Kondoo wa Mungu mnyenyekevu (Kumbukumbu la Torati18:15 na 2.Samweli 7:12-14 na Isaya 9:5-6; 49:6 na 53:4-12)
c) Kumwagwa kwa Roho Mtakatifu juu ya watu walioteuliwa na juu ya wenye mwili wote (Yeremia 31:31-34; Ezekieli36:26-27 na Yoeli 3:1-5).

Lakini ole ! Wayahudi, wengi wao hawakutambua kuja kwake Mwana Kondoo wa Mungu, Mfalme wa watu wake. Walipuuza kumwagwa kwa Roho Mtakatifu, hali wametazamia tukio la utawala wa kisiasa wenye nguvu. Kwa sababu hiyo hawakujitambua kuwa wenye dhambi, wala hawakutazamia mwamko mpya wa kiroho. Ahadi nyingi zilikuwa zimetimia kwa matendo ya Yesu na kumwagwa kwa Roho Mtakatifu juu ya wafuasi wake, hata hivyo sehemu kubwa ya watu waliochaguliwa na Mungu hawakutambua wala kukubali kutimizwa kwa ahadi hizo kwa ajili yao.

Wakina baba wa hao wateule hawakuwa wataalamu wa filosofia, bali walikuwa ni wachungaji na makuhani kwa ajili ya wengine wao. Walikuwa ni mawakili wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, kwa maana imani yao ya kweli ilishinda udhaifu wao. Bwana wa Agano alikuwa anaitwa Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Yakobo (Mwanzo 35:9-12; Kutoka 3:6 na Mathayo 22:32).

Wala Musa, au Mfalme Daudi, au Eliya, au nabii mwingine mkubwa wa Agano la Kale hakuna aliyeanzisha Chuo Kikuu au shule ya hali ya juu, lakini waliona na kufahamu kwa kurudia mara nyingi ukweli na enzi ya Bwana, mbali na maasi ya watu. Waliishi kufuatana na imani yao, nao wakapata kuwa mifano bora kwa watu wao, tena wakawa kama chemchemi ya baraka kwa watoto wao na vizazi vilivyozaliwa baadaye.

Mbali na hayo yote, pendeleo kuu na heshima ya watu wa Israeli ikawa ni kuja kwake Kristo mtazamiwa, Mfalme wa Wafalme, Kuhani Mkuu wa kweli, pia na Neno la Mungu lililoingia mwilini, ambaye ndani yake tunaona enzi, nguvu na upendo wa Mungu akiwepo katikati ya watu. Alisema: „Mimi ndimi nuru ya ulimwengu,“ kwa sababu upendo wa Mungu uliishi ndani yake, tena Roho Mtakatifu alimtukuza yeye. Yeye na Mungu ni mmoja, jinsi alivyokiri mwenyewe: „Mimi na Baba ni mmoja“ (Yohana10:30). Kufuatana na ukweli huo, Mtume Paulo alimwita „Mungu“. Hakusema „mungu fulani“, bali „Mungu wa kweli“, jinsi makanisa yote yanavyokiri kwamba, Kristo ni Mungu kutoka kwa Mungu – Nuru kutoka kwa Nuru. Mungu kweli kutoka kwa Mungu kweli; mfanyika, wala si kuumbwa, bali mwenye asili moja na Baba.

Wayahudi walighadhibishwa, walifanya fujo, nao wakawalaani Wakristo kwa sababu ya kukiri kwao jinsi Paulo alivyotamka katika waraka wake kwa kanisa la Rumi. Sehemu kubwa ya Wayahudi walimwona Yesu kama mpotoshi, anayemdharau Mungu, na mchokozi dhidi ya Mungu. Basi wakamtolea kwa Warumi, waliokuwa wakoloni wao, ili apate kusulibishwa. Ndipo wakaendelea katika ugumu wa mioyo yao, walivyofanya tangu enzi za nabii Isaya, miaka 700 kabla ya Kristo (Isaya 6:9-13; Mathayo 13:11-15; Yohana 11:40 na Matendo ya Mitume 28:26-27).

Katika mistari hii tutakuta habari ya ugumu wa mioyo yao na hali hii ilivyoendelea kuzidi na kujionyesha waziwazi. Hawakuungama kabisa hayo madhambi yao, bali walijihesabu kuwa wenye haki, kwa sababu walijijua kwamba, wanashika sheria za Musa, huku wakiwaangalia wengine kuwa kama takataka.

Waakati wa kuendelea kufanya migumu mioyo yao basi, Yohana Mbatizaji alitokea atayarishe njia kwa ajili ya Kristo, na sehemu ya watu wakapata kubatizwa naye. Walisikia kwake kwamba, Yesu ndiye Mwana Kondoo wa Mungu, na wakaelewa pia kwamba, Yesu atawabatiza na Roho Mtakatifu, ili aanzishe ufalme mpya wa kiroho. Na wote waliobatizwa na yule aliyelia nyikani walikuwa wametayarishwa kumpokea Kristo. Basi Yesu hakuwaita wale wenye elimu na uwezo, waliojiona wasafi, au wasomi waje kumfuata, bali aliwaita wale waliokiri dhambi zao mbele ya Mbatizaji, nao wakapata kuwa wanafunzi wake na pia kujazwa na Roho Mtakatifu. - Basi, mwujiza katika wale waliochaguliwa sio elimu yao, wala utajiri, wala si uzoefu wa utaalamu wa kisiasa, wala ukuu wowote, bali ilikuwa ni ungamo wa makosa yao na kuvunjika kiroho. Wale waliokiri dhambi zao kwa ukweli wakapokea kwake Kristo wokovu na uzima wa milele.

Mapendeleo ya halali, ambayo watu wa Israeli waliofurahia, pamoja na kuwepo kwake Mungu kati yao, yote ambayo yalileta matokeo ya kutokuwafaa juu ya jumla ya Wayahudi. Wakapata kuwa wenye kiburi na kujisikia bora kuliko watu wa mataifa mengine, wakijiona wenye haki, na hivyo bila haja ya ungamo. Hawakutambua dhambi zao, lakini walifanya migumu mioyo yao tangu miaka mingi dhidi ya Mungu, dhidi ya Kristo, pia na dhidi ya Roho yake safi, wakawa watajiri wa haki za binafsi, lakini maskini kiroho.

Paulo, katika maisha yake yaliyotangulia, yeye naye alikuwa mmojawao wao hao walioelezwa hapo juu, mshupavu na mwenye kiburi. Aliwatesa sana hao wafuasi wa Kristo. Aliwalazimisha baadhi yao kukana imani yao, na akawaua wale waliokuwa imara katika imani yao. Lakini kukutana kwake na Kristo, alipomtokea katika utukufu wake wa kung‘aa mno kule karibu na Dameski, jambo hilo lilitowesha ndoto zake, matazamio yake na kiburi, na lilimfanya aungame chuki na dharau yake. Alipata kuvunjika kimoyo kwa neema ya Kristo, akazaliwa mara ya pili kwa Roho Mtakatifu, halafu kuwa mtume wa Bwana Yesu.

Paulo alitambua sana kwamba, lile linalomwokoa mtu si hali ya kuwa wa ukoo wa mbegu ya Ibrahimu, wala si kutahiriwa, lakini kujaliwa haki kutokana na malipo au kafara ya Kristo, ndipo kujazwa na Roho yake Mtakatifu. Namna hiyo basi, mtu amepandwa ndani ya mwili wa kiroho wa Kristo na kuwa kiungo ndani yake. Kwa njia ya kuhubiri Injili kwa kizazi kipya cha Ibrahimu, Paulo alipata kuelewa wazi kwamba, ufalme wa kiroho wa Mungu hauwezi kabisa kuwa sawa na serikali ya kisiasa ya Israeli. Kinyume cha hayo, mwili wa kiroho wa Kristo unaumia na mateso ya ujeuri nchini Israeli siku hizi. Paulo hakusema lolote kuhusu serikali ya kisiasa, bali kuhusu ufalme wa kiroho wa Kristo unaojionyesha katika tabia safi, uaminifu, na adabu nzuri kote ulimwenguni.

SALA: Ee Baba wa mbinguni, twakushukuru kwa uvumilivu wako kwa watu wako uliowachagua, na tunakutukuza kwa ahadi ulizozifanya katika Agano la Kale kwa ajili ya hao watu walioasi, hata mbali na maonyo yako na maadhibisho. Utusamehe pamoja na watu wetu kote ambapo hatukurudisha upendo wako kuu kwa imani na uaminifu. Twaomba uwaokoe wengi wa watoto wa Ibrahimu, ukifanya upya tabia zao na kutakasa mioyo yao kwa Yesu Kristo aliye hai. Amina.

SWALI:

  1. Mapendeleo mangapi Paulo alitaja kuhusu watu wa Agano la Kale? Ipi katika hizo unaona ni muhimu zaidi kwako?
  2. Kwa nini neema ya Mungu haikufaulu kuwaokoa wengi wao wa wateule wake, nao wakaanguka katika hukumu moja hadi nyingine?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on November 17, 2022, at 03:19 AM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)