Previous Lesson -- Next Lesson
2. Kristo aliyefufuka anakamilisha haki yake ndani yetu (Warumi 5:6-11)
WARUMI 5:6-8
"6 Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. 7 Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. 8 Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.“
Baada ya kufunuliwa kwa ghadhabu ya Mungu na hukumu yake ya haki, Paulo anatuongoza tufikie toba la kweli, na kuvunjika kwa utu wetu wa umimi, ili tupate kuwa tayari kupokea kufanywa haki kwa imani, kushikamana na tumaini kuu, pia na kuendelea katika upendo wa uaminifu wa Mungu. Ingawa tumeingia katika wokovu huo, pia tunahitaji kukumbuka yale yaliyopita maishani mwetu, ili tusije tukapata kuwa wenye kiburi.
Vipawa vyote vya kiroho, amani, neema, upendo, kutakaka, imani, tumaini na uvumilivu hazitokezwi kwa nguvu zetu sisi wenyewe, wala si kwa nguvu yoyote ya kibinadamu. Zote hizi ni matunda ya kifo cha Yesu, aliyetoa uhai wake si kwa ajili ya ndugu zake wapendwa wake, bali kwa ajili ya walio kinyume cha Mungu, ambamo Mungu anatuona na sisi tumo. Mtu wa asili ni kama bomu ya uovu. Hajipotoshi mwenyewe tu, bali wengine nao. Hata hivyo Kristo alitupenda kiasi cha kutufia.
Kutokana na unyenyekevu huo tunaona upendo kuu wa Mungu. Basi ni shida sana kumpata mtu aliye tayari kutoa kwa sadaka mambo kama raha yake, muda, utajiri na maendeleo yake ya starehe, au hata kutoa uhai wake, ili aendeleze hali bora ya ndugu yake aliye mgonjwa. Pengine mtu fulani atathubutu kutoa maisha yake kwa ajili ya nchi yake ya nyumbani, au labda kwa ajili ya watoto wake; labda yawezekana mama atoe sadaka maisha yake kwa ajili ya watoto wake ikipasa; lakini hakuna kabisa atakayekuwa tayari kutoa maisha yake kwa ajili ya wahalifu sugu na maadui wanaokataliwa, hakuna, ila Mungu tu.
Taratibu hiyo inatia maana kuu kwenye kilele cha imani yetu. Wakati tulipokuwa bado maadui wasiomtii Mungu, huyu Mtakatifu alikuwa anatupenda. Akaambatana na wenye dhambi, ndani ya Mwana wake, akafa kwa ajili ya malipo ya dhambi za wauaji wake. Hakuna kabisa aliye na upendo kubwa zaidi kuliko huo, yaani kuweka maisha yake kuwa sadaka kwa ajili ya rafiki zake. Kutokana na neno hilo la Kristo tunagundua kwamba, aliwaita maadui yake “rafiki zake”, kwa sababu aliwapenda wote, hadi kuwafia.
Upendo wa Mungu kwetu ni kubwa mno kwamba, alitusamehe dhambi zetu kule msalabani hata kabla hatujatenda mabaya hayo, na hata kabla ya kuzaliwa kwetu. Kwa sababu hiyo hatuna haja kufanya bidii zozote za kutuweka katika hali ya haki sisi wenyewe, bali tunatakiwa tu kukubali ile neema tukufu, na kuamini kwamba, tumewekewa haki; na baada ya hapo, enzi ya wokovu wa Yesu itaanza kupata sura ndani yetu.
WARUMI 5:9-11
"9 Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. 10 Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. 11 Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.”
Sasa basi, furahini na kuruka kwa shangwe! Kwa maana tumekwisha kupata haki mbele za Mungu kutokana na umoja wetu wa imani pamoja na Kristo. Shetani hana haki tena kulalamika dhidi yetu. Damu ya Kristo inatusafisha kote, katika miili yetu na rohoni pia. Hali hiyo mpya itadumu daima, kwa sababu maombezi yake Yesu yatatuokoa na ghadhabu ya Mungu kwenye siku ile ya hukumu.
Paulo anatujenga imara katika uhakika wa kweli kwa mambo hayo yafuatayo:
Kwanza: Tulipatanishwa na Mungu wakati ambapo bado tuliishi katika uadui na fujo dhidi yake. Upatanisho huo ulifanyika pasipo kibali chetu, na malipo kwa ajili ya gharama yake. Kwa kweli, sisi hatukuwa na uwezo wowote wala hatukustahili kuanzisha upatanisho huo, ambao ni zawadi tupu ya neema.Upatanisho huo uliwezekana tu kutokana na Mwana wa Mungu, aliyepata kuingia mwilini mwetu na kutufia.
Pili: Ikiwa kifo chake Yesu kilileta matokeo ya kubadilisha namna hiyo, kiasi gani zaidi maisha ya Kristo aliye hai yatatuletea wokovu! Sasa sisi baada ya kupatanishwa na Mungu kwa mapenzi yake na kwa shabaha yake pia, sisi sasa tunataka kutenda kufuatana na mapenzi yake, tena kwa moyo wetu wote, ili na nguvu yake ipate kutenda kazi ndani yetu. Hivyo, uzima wa milele, ambao si jambo lingine, ila ni maisha ya Kristo mwenyewe, uzima hua umetujia kwa njia ya imani yetu ndani ya Mwana Kondoo wa Mungu, ambaye naye ni Roho Mtakatifu, asili ya upendo wa Mungu. Mistari hii tukufu inajenga mioyoni mwetu amani, furaha, utulivu na shukrani kwake. Roho wa Bwana ndiye uthibitisho kuhusu yale yaliyo mbele yetu yenye utukufu, maana yeyote atakayedumu ndani ya upendo, naye atadumu ndani ya Mungu na Mungu ndani yake.
Tatu: Kutokana na hayo Paulo alithubutu kupanda kwenye hali ya juu katika utukufu aliposema, “Sisi pia tunafurahia ndani ya Mungu”, ambalo linamaanaisha kwamba, huyu Mtakatifu mwenyewe huishi ndani yetu, na sisi tunaendelea ndani yake, maana hatukupatanishwa kwake tu, bali na Roho Mtakatifu, ambaye ni Mungu mwenyewe, aliifanya miili yetu kuwa ni hekalu kwa ajili ya Mungu aishi ndani. - Je, unashangilia kwa ajili ya kuwepo kwake Mungu ndani yako? Basi upate kuwa mtu aliyevunjika, mwenyewe kuwa si kitu, umwabudu Bwana wako, ukashangae kwa daraja la ajabu, ambalo kifo cha Kristo kimekuinulia.
SALA: Tunapiga magoti mbele ya enzi ya upendo inayotangazwa kwa njia ya Yesu Msulibiwa, nasi tunatolea miili yetu kwa makusudi ya upendo tukufu, ambayo inatukumba na sisi tulioshusha roho zetu kwa unyenyekevu. Hatutaki tena kuwaza habari zetu tu, bali kuzama ndani ya ziwa la upendo tukufu la kutoka kwako.
SWALI:
- Jinsi gani upendo kuu wa Mungu ulijionyesha?