Previous Lesson -- Next Lesson
3. Yesu anaombea mitume wake (Yohana 17:6-19)
YOHANA 17:14
“Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.”
Yesu alishuhudia ndani ya sala zake kwamba, aliwatolea wanafunzi wake maneno ya Baba, akiwafunulia jina lake la ubaba pamoja na maana yake. Kwa njia ya mafunuo hayo alitangaza ule Utatu Utakatifu kwetu. Ufunuo huo wa kimwujiza kuhusu asili ya Mungu iliwagusa sana wanafunzi. Uliwabadilisha na kuwajaza na nguvu, wakaweza kuwa viungo katika mwili wa kiroho wa Kristo.
Kutokana na sifa hizo na uwezo wake ulimwengu unawachukia, jinsi walivyomchukia Yesu. Jinsi asili yake Kristo ilivyokuwa toka kwa Mungu, na uhai wake ulikuwa umefichwa ndani ya Mungu tangu awali na hata milele, vilevile wote waliozaliwa mara ya pili wataishi milele.
YOHANA 17:15
“Mimim siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu.”
Yesu hakuwapeperusha wanafunzi wake mbinguni, wala hakuwasafirisha kwenye eneo la upweke, ingawa dhiki na magumu yakawapata pande zote. Akamwuliza Babaye awalinde wafuasi wake kutoka kwa ushawishi wa kishetani na udanganyifu wa wasemaji pamoja na roho mbaya. Bwana wetu anatuombea kweli. Kila mwumini aishi ndani ya kumbatio lake, akihakikishwa na kuwekwa muhuri. Damu ya Yesu hutulinda, na kwa sababu ya sadaka yake Mungu yu pamoja nasi. Hakuna awezaye kutushitaki au kutuharibu. Tumepata kuwa wenye haki, bila kufa tena, tukibebwa na rehema yake huyu Mtakatifu. Tusipogeuka kuwa wenye kutokutii na kufuata mivuto yetu ya dhambi fulani ya pekee; basi atatuacha tuanguke katika majaribu, maana dhambi iliyomo bado ndani yetu inaweza kujitokeza na kufunuliwa wazi kuwa aibu kuu. Ndipo tutatetemeka na tutatubu na machozi, tukilia: “Baba, usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu.” Yule anayejaribu kugombana na Shetani na kifo katika nguvu zake mwenyewe na ushupavu wa kibinadamu peke yake, atajidanganya mwenyewe. - Kimbilia kwenye kingo la damu ya Kristo na maombezi yake, yeye pekee ndiye Mwokozi wetu.
YOHANA 17:16-17
“Wao si wa ulimwengu, kama mimi si wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndilo kweli.”
Katika sala zake Yesu alirudia ushuhuda wake kwa wanafunzi, kwamba hawajaondoka kutoka kwa dunia hii ovu, ingawa wao nao ni wenye miili na kuelekea kwenye maovu kama wengine. Wangeendelea kuwa wabaya, lakini kwa sababu ya neema ya Mungu kuna damu ya Kristo inayowaweka huru kisheria kutoka kwa gereza la yule Mwovu. Wameesha kuwa wageni duniani humu na kuwa wenyeji wa mbinguni.
Katika hali hiyo mpya ya hao waumini wenye mwili na roho, bado kuna mgongano unaoendelea maisha yote bila huruma na bila kukoma. –Roho Mtakatifu anaumizwa tunapojipenda wenyewe, kazi zetu, hata familia zetu zaidi ya watu wengine. Bidii zetu zote za kujipendeza wenyewe itaumiza dhamiri zetu. Kila neno la uongo linachoma ndani ya kumbukumbu kama mwanzi unaowaka moto kwa kutoa moshi. Roho wa Mungu hatakuruhusu kuweka mali iliyoibiwa nyumbani kwako. Kama umemwumiza mtu kwa udanganyifu au tendo ovu, Roho wa kweli atakusukuma uende na kuomba radhi kwake. Kwa sababu huyu Roho Mtakatifu hufichua maovu yote, udanganyifu na yaliyopinda maishani mwako, naye atakuhukumu ipasavyo.
Kristo alimwuliza Babaye atutakase, maana asiye mtakatifu hawezi kumfanya mwingine kuwa takatifu. Basi hiyo takaso inatendeka kwa kutuvuta kwenye kweli yake. Kwa kiasi kile ambacho tunatambua upendo wa Mungu na kudumu ndani ya neema ya Mwana na kuishi katika nguvu ya Roho Mtakatifu, tunaendelea kufanywa takatifu. Kuwepo kwake Mungu ndani ya maisha yetu inatubadilisha. Mungu mwenyewe anatimiza makusudi yake ndani yetu, “Uwe mtakatifu maana mimi ni mtakatifu.” Damu ya Yesu inatutakasa mara moja kwa maisha yote, jinsi pia Roho Mtakatifu ndani yetu hapungukiwi na lolote. Imani yako ndani ya namna ya Utatu Utakatifu inatutakasa kikamilifu.
Kutakaswa hivyo kunatendeka upande wa Mungu kwa njia ya kuingia ndani ya Neno Lake. Injili ndiyo chemchemi ya kutakaswa kwetu, pia na mzizi wa kutii kwetu. Maneno ya Kristo ndani ya Injili yanatuongoza tuweze kuamini, kujikinahi, pia na upendo kwa kuabudu, ili tuweze kuwa wa kufaa kumwelekea Mungu bila kizuizi chochote. - Basi fungua moyo wako kwa neno la Baba yako, maana Mungu ni upendo, na yeyote adumuye upendoni, atadumu ndani ya Mungu, na Mungu ndani yake.
YOHANA 17:18
“Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.”
Baada ya Yesu kuwaombea wanafunzi wake akiomba kwamba watakaswe, akawatuma wakiwa wapya ndani ya dunia ya maovu mengi. Alituokoa ili atutakase maisha yetu; ndipo akatutuma ndani ya ulimwengu, ili tuwaokoe wengi na kuwatakasa. Kanisa sio mkusanyiko linalopatikana kwa urahisi, linaloweza kujifurahisha lenyewe na maneno safu na hukumu za haki, hapana. Kanisa ni shirikiano la utendaji kazi, likiingilia boma la Shetani kwa imani, likilenga kwa maombi na kuvumilia kupata kuwaokoa waliopotea. Kanisa linatangaza ufalme wa Baba na kushughulika kufaulu mapenzi yake ya uinjilisti ulimwenguni kote. - Je, wewe umepata kutambua maombezi ya Kristo kwa ajili ya bidii katika uinjilisti?
Yesu anakuheshimu kwa kukutuma kwao waliopotea, jinsi Baba alivyomtuma yeye kwanza. Shabaha ni ileile pamoja na vifaa vyake pia. Anakutolea kipekee mafunuo kuhusu ukweli wote juu ya Mungu ndani ya Kristo. - Yesu naye akuita kwa huduma ya utendaji, wala si kwa mapumziko au madanganyo. Roho yake Mtakatifu ndiye uwezo wako.
YOHANA 17:19
“Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.”
Yesu alifahamu kwamba hakuna kati ya wanafunzi wake aliyeweza kufanya uinjilisti au kuendeleza ustawi wa kiroho, na kwamba wote wataanguka na majeraha ya ajali mioyoni mwao na katika dhamiri zao, lakini utakatifu wa Mungu uliwazunguka. Kwa sababu hiyo Mwana akawa kafara, akijitakasa mwenyewe, ingawa alikuwa takatifu tangu awali. Kwa njia ya kifo chake akatimiza matakwa yote ya utakatifu, ili na mashitaka ya Shetani yafutike kwa imani yetu ndani ya damu ya Yesu. Kwa msingi wa kifo chake cha kuridhisha, hao wanafunzi waliweza kupokea Roho Mtakatifu, aliyewafanya wawe vyombo vya kubeba maji ya uhai, pia na mashahidi wa mahubiri ya Yesu katika jina lake.
Hivyo wakapata kuwekwa huru na udanganyifu, na midomo yao kusafishwa na sumu ya hila. Wakapokea ujasiri wasiseme kinyume cha haki; pia na kufunua dhambi, ingawa hilo lingeweza kutatiza dhamiri za watu, lakini mwishowe yatawaongoza kwenye wokovu. Mvutano huo wa kusema uongo, na mengine kama uzinzi na kiburi inaweza kushinda tu kwa ulinzi wa damu ya Kristo na uhodari wa maombezi yake.
SALA: Utusamehe chuki, maongo na kiburi ndani ya mioyo yetu. Tangu asili tu waovu, na wewe u mtakatifu. Utulinde na mitego ya Shetani. Utueleze vema Injili, ili maneno yako yatutakase kweli, na tuweze kuishi kufuatana na yale tunayoyahubiri.
SWALI:
- Jinsi gani Yesu alimwomba Baba yake atulinde na maovu?