Previous Lesson -- Next Lesson
2. Utatu utakatifu huwashukia waumini kwa njia ya Mfariji (Yohana 14:12-25)
YOHANA 14:15
„Mkinipenda, mtazishika amri zangu“.
Uinjilisti unatendeka kwa sababu ya shukrani kwa ajili ya Golgotha. Yeye asiyeshiriki katika kueneza Injili, basi hajafahamu uhuru wa Kristo. Ukiona kwamba maombi yako na ushuhuda wako hazileti matunda, ujipime mwenyewe, kama kweli unadumu ndani ya upendo wa Kristo, au dhambi zako zinazuia baraka hizo. Basi ukiri upungufu wako mbele ya Yesu, ili mto ule wa baraka usikatwe kwa ajili ya wengine. Bwana ametupatia maagizo mengi: Wapende adui zako; ukeshe na kuomba, ili usiingie majaribuni. Uwe mkamilifu, jinsi Baba yako wa mbinguni alivyo mkamilifu; njooni kwangu ninyi nyote mlio na kazi nyingi na mizigo ya kulemea, nami nitawapumzisha. Maagizo hayo yanajumlishwa katika tamko hilo la dhahabu: mpendane jinsi mimi nilivyowapenda. Amri zake sio mizigo mizito, bali ni msaada kwa ajili ya maisha, nazo ni kama daraja kwa ajili ya imani na upendo.
Yeyote anayeendelea kujua ukombozi wa Yesu, basi hawezi tena kuishi kwa ajili yake mmwenyewe tu, bali atamtumikia Kristo Mwokozi.
YOHANA 14,16-17
„ Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu“.
Mtu anayejaribu kuishi kufuatana na maagizo ya Yesu kwa nguvu zake mwenyewe, atapotea kwa kukata tamaa. Kwa sababu hii Yesu alituombea kwa Mungu, ili atutumie Mfariji, yaani Roho Mtakatifu. Yeye anayo kazi mbalimbali ndani yetu. Yeye ni Roho wa kweli, anayetuonyesha ukubwa wa dhambi zetu. Ndipo anatuonyesha wazi mbele zetu sura ya Yesu aliyesulibiwa, akituhakikishia kwamba ndiye Mwana mtukufu, anayekuwa radhi na dhambi zetu. Ndiye anayetujalia haki mbele za Mungu kwa neema. Huyu Roho mbarikiwa atupatia hatua ya kuzaliwa mara ya pili. Atufungulia midomo yetu tuweze kumwita Mungu „Baba yetu“. Ndipo twajisikia na uhakika kwamba kweli tu watoto wa Mungu kwa Roho huyu wa kuchaguliwa. Mwishoni, anakuwa mtetezi wetu anayetulinda. Husimama upande wetu na kutuimarisha usoni pa manong’onezo ya Shetani, na kutuhakikishia kwamba wokovu umekamilika. Hatuwezi kupata uhakika katika mahangaiko yetu wala maridhisho duniani humu isipokuwa kwa njia ya huyu Mfariji aliyetumwa na Yesu kwetu.
Hakuna mtu anayejaliwa Roho kwa hali ya kawaida, hata mtaalamu au mtunga mashairi wala mwonaji, hakuna. Roho huyu si wa dunia hii, na anawajia tu wale waoamini ndani ya damu ya Yesu. Yeye asiyempenda Yesu kwa moyo na kumkubali, basi hawezi kuwa na Roho huyu akikaa ndani yake. Lakini ampendaye Yesu na kukubali wokovu wake ataona furaha tele katika mwenendo wake. Pamoja na huyu Roho Mtakatifu mioyoni mwetu tunatambua nguvu za Mungu hata katikati ya madhaifu. Yesu akuhakikishia kwamba huyu Mfariji hatakupotosha hata kifoni wala hukumuni, maana yeye mwenyewe ndiye uhai wa milele.
YOHANA 14:18-20
„Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu.“
Wakati msaliti alipoenda nje, Yesu aliwajulisha wanafunzi kwamba mwenyewe ataondoka kwao hapo karibuni, na wao wasiweze kumfuata. Lakini aliongeza kwamba atarudi kwao binafsi. Alitambua hofu zao, na kwamba maneno yake yalikuwa na maana mbili: Kwanza, kuja kwa Roho Mtakatifu, kwa vili Bwana ndiye huyu Roho. Pili, kurudi kwake katika utukufu mwisho wa wakati. Kwa sababu hizo mbili, ilimpasa aondoke kwao na aende kwa Baba yake. Bila kuachana nao namna hii, Roho Mtakatifu asingaliweza kuja kwao.
Huyu Roho ndiye afunguaye macho na mioyo mara moja wamtambue. Tunaelewa kwamba, Yesu hakutulia kaburini kama watu wengine, bali twatambua kwamba yu hai akiwa pamoja na Baba sasa. Uhai wake ndiyo msingi wa ulimwengu wote na wa wokovu wetu. Kwa sababu alishinda kifo, aweza kutupatia uhai na sisi, ili hata sisi tuweze kushinda kifo kwa imani, na kuishi ndani ya haki ya Kristo. Dini yetu ni dini yenye uhai unaojaa tumaini.
Huyu Roho wa kweli mwenye kutufariji ndiye Roho wa Mungu, ajaye kwetu na kutawala ndani yetu; na anatuhakikishia kwamba Mwana ni ndani ya Baba na Baba ndani ya Mwana, wakiwa katika umoja kamili. Ufahamu huo wa kiroho juu ya Umoja Utakatifu si kama vili elimu au masomo ya mahesabu, bali inakuwa ikikamilika ndani ya mwumini, na ya kwamba tutaunganishwa na Mungu jinsi Yesu alivyo. Siri hizo za kiroho zinakaa ng’ambo ya utambuzi wa akili yetu sisi kama wanadamu.
Sasa Yesu hasemi kwamba, anataka kuishi ndani yako tu kipekee, „lakini naishi ndani yenu ninyi nyote mnaoniamini.“ Mkristo mmoja peke yake siyo hekalu la Roho; Yesu ni kama jiwe la msingi ndani ya makao matukufu. Waumini wote wanaunganika ndani ya ushirikiano huo wa kiroho. Ahadi hiyo imetolewa katika namna ya wengi, „ Ninyi wote mko ndani yangu na mimi ndani yenu.“ Ushirikiano wa watakatifu ndipo hapo ambapo Yesu hujifunua kwao. - Umetambua kwamba Bwana anakamilisha ahadi hiyo pamoja na agizo „Mpendane ninyi kwa ninyi jinsi mimi nilivyowapenda“ ? Basi si mimi peke yangu niliyefungwa hivyo na Kristo, bali sisi sote tutajazwa hadi ukamilifu wa Mungu uonekane.
SALA: Twainama mbele zako, mtakatifu Mwana Kondoo wa Mungu; kwa kifo chako tumepokea uzima wa milele. Utusamehe imani yetu haba, hali yetu ya kutokutambua, ili pasiwepo kizuizi chochote kati yako na sisi. Tusaidie tuweze kukuona ndani ya taabu zetu zote, na tuishi kwa raha katika utambuzi wa uwepo wako kwetu. Twakushukuru kwamba Mfariji wetu ametujia, huyu Roho wa kweli, anayetuunganisha daima.
SWALI:
- Zipi ni sifa, ambazo Yesu anazitaja juu ya Roho Mtakatifu?