Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- John - 086 (The Holy Trinity descends on believers)
This page in: -- Albanian -- Arabic -- Armenian -- Bengali -- Burmese -- Cebuano -- Chinese -- Dioula? -- English -- Farsi? -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Kyrgyz -- Malayalam -- Peul -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Thai -- Turkish -- Twi -- Urdu -- Uyghur? -- Uzbek -- Vietnamese -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

YOHANA - Nuru inaangaza gizani
Somo la Injili ya Kristo kufuatana na Mtume Yohana
SEHEMU YA 3 - Nuru yang’aa ndani ya shirika la Mitume (Yohana 11:55 - 17:26)
C - Hotuba ya kuaga kwenye chumba cha orofani (Yohana 14:1-31)

2. Utatu utakatifu huwashukia waumini kwa njia ya Mfariji (Yohana 14:12-25)


YOHANA 14:12
„Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hisi atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.“

Kumtambua Mungu sio filosofia fulani au utaratibu wa mawazo. Utambuzi wowote wa kiakili unatokeza kiburi, lakini tunaloeleza ndiyo utambuzi wa upendo wa Mungu na wokovu kutokana na Mwana. Dalili yake ni uhuru wa kutumika. Kristo aliwapa wanafunzi wake agizo mpya: „waishi na upendo tukufu maishani mwao kwa kazi na matendo yao pamoja na kusali“.

Wanafunzi walimwomba Yesu awalinde na awaongezee utambuzi wa Mungu, walipoanza kufahamu kwamba ataondoka kwao. Lakini Kristo aliwaimarisha ndani ya Baba, ili wawe wa kufaa kueneza Injili ulimwenguni.

Lililokuwa muhimu sana kwao haikuwa usumbufu wao kwa ajili yao wenyewe, bali matayarisho yao kwa ajili ya hiyo huduma tukufu. Utambuzi kuhusu Baba na Mwana unatulinda na tabia ya kujishughulisha wenyewe tu, na kutuongoza ndani ya huduma kwa unyenyekevu. Yesu alisema: Yeyote ategemeaye ndani ya kazi zangu, hatakuwa mtu wa maneno tu, bali atafuata njia ya kujitoa kabisa. Atafanya hivyo kiasi cha kujinyima mwenyewe na kumkuza Kristo Mwana, aliyefufuka kutoka kwa wafu na sasa kufanya kazi ndani yake na kumjalia baraka za mbinguni. Kwa imani ya namna hii Mitume waliweza kuponya wagonjwa na kusamehe dhambi, hata kufufua wafu katika jina la Yesu baada ya kujaliwa nguvu na Roho Mtakatifu. Walijikana wenyewe, na Kristo aliishi ndani yao. Walimpenda kwa nafsi zao kabisa na kumtukuza kwa yote waliyoyatenda.

Mbali na huduma hizo takatifu Kristo aliwatuma kuendesha utume, ambao yeye mwenyewe hakuweza kukamilisha katika muda wake fupi hapo duniani. Baada ya kupaa kwake akamtuma Roho wake Mtakatifu, ili wengi wapate kufanywa upya kwa kuhubiri kwao. Watoto wa kiroho wapate kuzaliwa kwa Baba wa mbinguni kama umande wakati wa kucha. Hakuna kilicho bora kuliko ushuhuda wetu juu ya Kristo aliyesulibiwa na kufufuka. Kwa kutegemea kabisa ushuhuda huo watu hupokea uhai wa kudumu daima. Roho Mtakatifu huwashukia wale wanaoshikamana na Kristo na kuwafanya kuwa watoto wa Mungu, ili wapate kumtukuza Baba yao wakati wowote wa maisha yao katika uaminifu.

YOHANA 14:13-14
„Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya“.

Je, unaomba? Kiasi gani cha maombi yako yanahusika na matatizo yako na dhambi zako? Na kiasi gani cha muda wako unatumia kwa kumsifu Mungu na kuwahudumia wengine? Unajishughulisha kibinafsi katika maombi yako, au umejaa na upendo kwa Mungu na kwa waliopotea?

Jiulize, kama upendo wa Mungu umebadilisha maombi yako, hata uweze kuwabariki adui zako? Je, wokovu wa Kristo ulikufanya uwe mwenye kuwaokoa wengine katika jina lake? Na sala zako zinalingana na maneno ya Sala ya Bwana? Au unaendelea kuwachukia wengine bila kuwasamehe makosa yao? Ikiwa unaomba katika jina la Kristo, basi utaishi na kutafakari pia kufuatana na Roho yake, jinsi anavyotamani yeye, na moyo wako utajazwa na mawazo ya huruma.

Kristo anatoa ahadi inayotegemea nguvu na baraka za mbinguni. Anafunganisha ahadi hiyo na kanuni la wazi kabisa: „Ukijifungua mwenyewe kwa maneno yangu, yaweze kukubadilisha, mimi nitakuwa mwenye nguvu na ukubwa ndani yako, nami nitawaokoa wengi kutoka kwa uchafu wao kwa imani na sala zako. Kila unapoomba kwa kuongozwa na Roho, hali ukiamini ndani yangu, mimi nitajibu hapo hapo.“

Ndugu, utafakari kwa makini na shukrani kuhusu ufunguo, ambaoYesu ameuweka mkononi mwako. Fungua utajiri wa mbinguni kwa sala zako. „Mimi nitashuka juu ya jirani na rafiki zako pamoja na baraka na wokovu na utambuzi, pia na hali ya kuungama na msaada.“ Umwombe Yesu na kugundua kwamba, anaweza kuchagua watumwa wa taifa lako na kuwafanya wawe watoto wa Mungu. Usiwe mdhaifu katika sala zako; imani yako ndiyo inayohitajika kwa ajili ya kuwaokoa wengi. Amini ndani ya jibu wakati unapoomba; umshukuru mapema hata kabla ya kupata jibu. Waulize ndugu na dada zako waungane nawe katika sala na imani yako. Usichoke katika kusifu na kuabudu. Omba hata Yesu amwage Roho wa kuomba juu yako.

Ukijisikia kwamba Yesu hajibu sala zako, ndipo uungame na kukiri dhambi zako, vunja vizuizi vya sala, ili apate kukusafisha. Atakupatia madaraka ya kuleta ukamilifu wa mbinguni chini duniani. Ukiingia katika maisha ya kusali kwa imani na ushuhuda, utamtukuza Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

SALA: Bwana Yesu, utujalie roho ya kusali, tusije tukajifikiria wenyewe kwanza, bali tuwafikirie wale tunaowajua, hata tusiowafahamu. Utufanye kuwa waumini wenye maisha ya kusali, ili upate kuwaokoa watu wa kwetu. Nakutukuza, umetufungulia mbingu, ili utushushie zawadi zako na ukarimu wako. Jina la Baba yako apate kutukuzwa kutokana na watoto wengi watakaozaliwa kiroho. Jina lako lipate kuadhimishwa kwa sababu ya maisha yao katika utakatifu na kwa nguvu ya Roho.

SWALI:

  1. Utaje kanuni ya lazima kwa kujibiwa sala zako!

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on March 12, 2015, at 04:45 PM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)