Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- John - 067 (Jesus is the Good Shepherd)
This page in: -- Arabic -- Armenian -- Bengali -- Burmese -- Cebuano -- Chinese -- English -- Farsi? -- French -- Georgian -- Hausa -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Kyrgyz -- Malayalam -- Peul -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish? -- Tamil -- Telugu -- Thai -- Turkish -- Twi -- Urdu -- Uyghur? -- Uzbek -- Vietnamese -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

YOHANA - Nuru inaangaza gizani
Somo la Injili ya Kristo kufuatana na Mtume Yohana
SEHEMU YA 2 - Sehemu ya pili: Nuru inang’aa gizani (Yohana 5:1 - 11:54)
C - Safari ya mwisho ya Yesu kwenda Yerusalemu (Yohana 7:1 - 11:54) Neno Kuu: Kutenganisha giza na nuru
3. Yesu, Mchungaji Mwema (Yohana 10:1-39)

c) Yesu ndiye Mchungaji Mwema (Yohana 10:11-21)


YOHANA 10:11-13
“Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake.”

Mungu enzi za Agano la Kale aliwavumilia kwa subira wafalme, manabii wa uongo na makuhani waliodanganya, wakiangalia watu wake waliotawanyika kama kondo bila mchungaji. Basi akaamua kumtuma Kristo awe Mchungaji Mwema. Alipofika akasema, “Mimi nipo tayari kuwa Mfalme wa kweli, kuhani mkuu, pia na nabii mwenye ufunuo wa mwisho.” Ndani ya nafsi ya Kristo tunagundua kazi zote njema za kichungaji zimeungana. Yeye aweza kutamka kwa haki, “Njooni kwangu ninyi nyote mliolemewa na mizigo mizito, nami nitawapumzisha.” Sitawatumia kwa ajili ya faida yangu, bali kuwaokoa kutoka kwa maisha yaliyoongozwa vibaya, pia na kutoka katik kila hatari.

Thibitisho kwamba yeye ndiye Mchungaji Mwema kweli ilikuwa ni utayari wake tangu mwanzo kutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Hakusema tu kwamba atatoa mwili wake, bali alitoa mwili, roho na nafsi yake kwa ajili ya wokovu wa kundi la Mungu. Alihangaika tangu hatua ya kwanza katika kuwahudumia wafuasi wake. Kifo chake cha kimwili kilikuwa ndiyo taji ya maisha ya kujitoa. - Kumbuka kwamba Yesu hakuishi wala kufa kwa ajili yake mwenyewe. Aliishi hapo duniani na kufa kwa ajili yako wewe.

Wachungaji wasio na imani wataonekana tu, maana saa ya hatari watakimbia na kujificha, Wakijishughulikia wenyewe tu. Wanawaachia kondo kwa wana-mbwa, ambao vyovyote watakuja tu. Wao wenyewe sio wanyama, ila wanatenda kwa namna ya kinyama; baba yao ndiyo Shetani. Kama mbwa-mwitu wa kwanza, shabaha ya Shetani ni kutafuna tu. Shambulio zake ni kali, ya kuangamiza na kuua. Yeye hutokea na majaribu yanayopendeza na maongo meupe. Sisi wachungaji tusikubali kuvumilia au kutokujali mafundisho yasiyo kweli, tukitumia upendo kama udhuru. Lakini kwa ajili ya upendo tunatakiwa kupigania kweli kwa hekima na kwa nguvu ikipasa. Maisha ya Kristo inatueleza kwamba siku zote alishindana na roho za kishetani. Kwa upendo mwingi alisema kweli tupu kwa watumishi wake, ili wao nao wahudumie kundi lake kwa bidii na kuigombania usoni pa mashambulio ya roho za kishetani. Shabaha ya mwana-mbwa mlafi ni wazi, maana kwa hoja za uongo na dhuluma anatamani kuharibu kanisa la Mungu. - Je, unatafuta huduma na heshima ndani ya kundi la Mungu? Basi, utambue kwamba itamaanisha magumu, mateso na kutjitoa kuwa sadaka, wala haitafuatana na ruzuku au kujifurahisha, bila kutaja hata nafasi kupumzika.

YOHANA 10:14-15
„Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.“

Kristo alirudia kwamba yeye ndiye Mchungaji wa pekee. Sisi sote tunakosa na hatuwezi kuhudumia jinsi itupasavyo, kwa vile hatumjui sana adui, wala hatufahamu sana tabia za kondoo, au namna ya kuwaongoza na kuwafikisha kwenye malisho bora. Kristo amjua kila mmoja mmoja kabisa, tena kwa jina, pamoja na kuelewa mambo ya maisha yake ya nyuma, mawazo yake ya sasa na pia yatakayokuwepo mbeleni.

Yesu aliwachagua kondoo zake, na akawajalia zawadi ya kumfahamu yeye kwa kutosha. Katika hatua za kumwelewa zaidi na zaidi, wanashangaa kwa nini hajawakatalia. Kuwepo kwake kunawaonyesha mapungufu yao. Na kuendelea kujuana hivyo kunazidisha upendo zaidi, ikiwaingiza katika hali ya kushukuru zaidi na kuimarisha maungano na agano la daima na yeye.

Kujuana hivyo kwa ndani kati ya Yesu na kundi lake siyo juujuu tu au ya kidunia, bali ni zawadi ya Roho, maana tunamtambua anavyomwona Baba, na jinsi Baba anavyomjua Mwana. Hii ndiyo siri kuu, ambayo kila Mkristo, kwa kushukiwa na Roho, anajaliwa ufunuo wa kweli katika ufahamu tukufu kwa njia ya Kristo. Hii inamaanisha pia kwamba, Roho wa Mungu anaishi ndani ya kundi lake na kumjalia kila mmoja. Hakuna hata mmoja asiyejaliwa.

YOHANA 10:16
„Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.“

Kristo hakufa kwa ajili ya taifa fulani ya pekee, bali kwa ajili ya wote. Hakuwaokoa wale wakaidi wa Agano la Kale tu, lakini pia kwa ajili ya jamaa wote wachafu kati ya mataifa. Alitabiri kwamba kifo chake kitawaokoa kondoo wengi tu toka pembe zote za dunia. Hakuna walioweza kumjia Mungu kwa uwezo wao; walihitaji kiongozi, Mchungaji Mwema. Na huyu awe ndiye Kristo. Yeye binafsi ndiye mwenye enzi kwa ajili ya mataifa yote na watu binafsi. Uongozi wake wa kiroho unatendeka kwa njia ya neno lake. Kwa vile kondoo wanatambua sauti ya mchungaji wao wenyewe, ndivyo hata kote duniani watu walio tayari wanasikia sauti ya Kristo, na wanaokoka mara. Toka kwa wateule wa Agano la Kale pamoja na waokoka kutokana na mataifa, umoja mpya wa kiroho utatokea chini ya uongozi wa Kristo. Siku hizi watu wa Agano Jipya ndiyo kundi la Mungu, Yesu akiwa Mchungaji wetu. Wote wasikiao injili kwa furaha na kumwamini Kristo, Mwana wa Mungu, ndiyo wanachama wa kanisa la kweli, hata wanapojiunga na madhehebu mbalimbali. Tupo na Roho mmoja, Bwana mmoja na Baba mmoja. Roho huja juu ya wote waliosafishwa na damu ya Yesu. Umoja wa zizi la Kristo ni kubwa kuliko tunavyodhani, ukikusanya kondoo toka kila pembe ya dunia. Mchungaji Mwema huja binafsi awaongoze wafuasi wake waaminifu na wepesi wa kutii, awafikishe kwenye utukufu wake. Ndipo kutakuwa na kundi na zizi moja, pia na mchungaji mmoja. Lakini yeyote anayejaribu siku hizi kuunda kanisa kwa njia na taratibu za kibinadamu na shabaha zilizo za kidunia, huyu atakuwa hatarini kuangukia ndani ya mitego ya mbwa-mwitu mkubwa; huyu atajaribu kuvuta uangalifu wa kundi liondoke kwa Mchungaji wake na lielekee kwake. Hata hivyo, waumini wa mataifa mbalimbali hatuwezi kukaribiana vizuri zaidi pasipo kumkaribia zaidi Kristo.

YOHANA 10:17-18
„Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uwezo wa kuutoa, ninao na uwezo wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.“

Twaamini kwamba Mungu ni upendo, akimpenda Mwanawe daima. Maana Yesu bila kubadilika alitenda yaliyompendeza Babaye. Ndipo tunasoma jambo lililompendeza Mungu kweli - kipekee ilikuwa ni msalaba. Kifo chake Kristo kilikuwa ni kusudi lililopangwa na Mungu. Hakuna kabisa njia nyingine kuokoa kundi kutoka kwa dhambi, isipokuwa kwa kafara hiyo na kutakaswa kwake kwa njia ya damu ya huyu Kondoo.

Kifo na ufufuo wa Yesu ndiyo miujiza mikuu ajabu; aliwaeleza mapema kwamba atakufa, ili aishi. Hakutolewa yeye kwa kulazimishwa, lakini kwa hiari kabisa, kwa sababu alitamani kuwaokoa wenye dhambi. Yeye ndiyo upendo kweli kweli. Baba yake alimkabidhi uwezo wa kuokoa ulimwengu, pamoja na uwezo wa kuchukua uhai wake tena. Hakuna aliyeweza kuzuia huduma ya kukamilisha ushindi huo wa Kristo msalabani. Shetani na jeshi lake walijitahidi sana kuzuia tendo lake la kuokoa; lakini hao wakorofi walishindwa mbele ya enzi ya upendo wa Kristo. Basi haikuwa Kayafa wala Pilato wala wengine waliomshitaki afe; ilikuwa ni yeye mwenyewe aliyekusudia kufa. Hakukimbia alipomwona yule mbwa-mwitu anamkaribia, lakini alijitoa mwenyewe ili atufie. Na hii ilikuwa ni mapenzi ya Mungu kamili. Yesu alishinda katika mgongano huo kati ya mbingu na jehanum pale msalabani. Kuanzia siku ile wote wa kundi lake wanao matumaini yaliyothibitishwa na damu ya Kondoo. Yesu hutuongoza kupitia katika hatari na mateso hadi kwenye utukufu wake.

YOHANA 10:19-21
„Kukaingia tena matengano kati ya Wayahudi, kwa ajili ya maneno hayo. Wengi wao wakasema, Ana pepo huyu, tena ana wazimu; mbona mnamsikiliza? Wengine wakasema, Maneno hayo siyo ya mtu mwenye pepo. Je, pepo aweza kuwafumbua macho vipofu?“

Wale wapelelezi waliotumwa na viongozi wa wayahudi walichachamaa kwa kumsikia Yesu anawaeleza wale wenye mamlaka kati ya Wayahudi kuwa wanyang’anyi na watendaji wa Shetani; pamoja na kujitangaza kuwa ndiye Mchungaji Mwema, na zaidi ya hayo awe pia Mchungaji wa mataifa yote - jambo ambalo kwa Wayahudi lilionekana kama upuzi. Walijiona wenyewe tu kuwa wateule wa Mungu. Basi wakamsema anayo mapepo na mwenye wazimu, wakachukizwa naye. Wengi wa wasikilizaji wakakubaliana na mashitaka hayo. Jumla ya wenyeji basi wakamgeukia Yesu, kwa vile mafundisho yake ya mbinguni yalikuwa ng’ambo ya uwezo wa ufahamu wao.

Hata hivyo, baadhi ya wasikilizaji wake wakawa na uhodari wa kushuhudia wazi mbele zao kwamba wamesikia sauti ya Mungu ndani ya maneno ya Yesu. Maneno yake hayakuwa mawazo matupu tu, lakini yaliyojaa nguvu na yenye uhai. Alikuwa amesamehe dhambi za yule kipofu. Lakini uadui dhidi ya Yesu iliendelea kukua kati ya mati ya watu, wakati huo upendo wake uliendelea kushika mizizi ndani ya waaminifu wachache. Yesu anaongoza na aliongoza wakati wo wote kundi lake kwa Roho mtulivu kwenye shabaha zake.

SALA: Bwana Yesu, uliye Mchungaji wa kondoo, hukuwakataza kondoo wakaidi, lakini uliwatafuta hadi kuwapata, ukatoa uhai wako kwa ajili yao. Utusamehe makosa yetu. Asante kwa kutujalia Roho wa ufahamu, ili tuweze kukuelewa, jinsi wewe unavyomfahamu Baba. Unafahamu majina yetu, wala huwezi kutusahau. Unatutunza pamoja na wafuasi wako wote. Twaomba uchague toka kwa mataifa wale walio tayari kusikiliza, ukawaunganishe. Na uwalinde na yule mbwa-mwitu atakaye kuwameza.

SWALI:

  1. Jinsi gani Yesu anapata kuwa Mchungaji Mwema?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on March 18, 2014, at 11:31 AM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)