Previous Lesson -- Next Lesson
d) Usalama wetu ndani ya umoja wa Baba na Mwana (Yohana 10:22-30)
YOHANA 10:22-26
„Basi huko Yerusalemu ilikuwa sikukuu ya Kutabaruku; ni wakati wa baridi. Naye Yesu alikuwa akitembea hekaluni, katika ukumbi wa Sulemani. Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi. Yesu aliwajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu, ndizo zinazonishuhudia. Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu.“
Sikukuu ya Kutabaruku ilikuwa ni tokeo la furaha na uchangamfu kwa ajili ya kukumbuka hekalu lilivyojengwa tena baada ya Wayahudi kupelekwa Babeli na kurudi mwaka 515 kabla ya Kristo. Wamakabayo ndiyo walioijenga tena katika mwaka 165 kabla ya Kristo. Sikukuu yenyewe iliadhimishwa mwanzo wa Desemba, wakati wa baridi na mvua, maana Yerusalemu iko juu ya milima kwenye meta 750 juu ya bahari.
Kwa tukio hilo Yesu aliyekwisha kudhulumiwa, aliendea tena hekalu, akihubiri kwenye ukumbi wa Sulemani, ambapo watembeleaji wa hekalu wangeweza kumsikiliza. Ukumbi huo wa upande wa mashariki inatajwa tena katika kitabu cha Matendo ya Mitume 3:11 na 5:12.
Hapo ndipo Wayahudi walijitayarisha kumshambulia Yesu. Walidai kwamba atangaze wazi hadharani kama ndiye Masihi aliyetazamiwa au siye. Yale ambayo aliwahi kutangaza juu yake mwenyewe yalikuwa bora sana na yenye upana zaidi kuliko matazamio ya watu juu ya Masihi wao. Hayo aliyoongeza juu ya ubora wake yaliyopita matazamio yao yakawa ni sababu la kujikwaa kwao. Hata hivyo baadhi yao waliamini kwamba labda Yesu aweza kuwa Masihi kweli, kwa sababu nafsi yake, mamlaka na matendo yake yalithibitisha kwa uzito.
Hivyo, walijaribu kumlazimisha Kristo atangaze wito wa kugusa kwa ajili ya mwamko wa Kikristo wa taifa lake. Nafasi ya sikukuu hiyo ilikuwa kumbukumbu ya mapinduzi ya Wamakabayo. Walitumaini kwamba atadai hadharani haki yake kuwa Mfalme wa nchi, akiwaita watu wake kukamata silaha. Walikuwa tayari kumfuata vitani na kutupa mbali aibu ya kutawaliwa na Warumi. Yesu alikuwa na mipango mingine: unyenyekevu, upendo na mabadiliko ya mioyo yao. Hakuwaambia wazi Wayahudi kwamba yeye ndiye Masihi, iwapo alitamka hayo kwa yule mke toka Samaria. Naye alishuhudia kwa yule aliyezaliwa kipofu kuhusu utukufu wake wa kimungu. Wayahudi walimtaka Masihi wa kisiasa na awe mkorofi; Yesu alikuwa mwokozi wa kiroho na mwenye huruma. Ndoto ya watu ilikuwa enzi, uhuru na heshima. Yesu akaja na kudai kujikinahi, kutubu na kufanywa upya. Alitangaza ukuu wake, lakini walishindwa kuyaelewa, maana walidai jambo ambalo kwake halikuwepo. Matazamio yao hayakukutana na ya kwake, na imani haikujionyesha mioyoni mwao. Hawakufungua mioyo yao kwa roho ya Jesu. Miujiza yake yalitendeka katika jina la Baba yake, aliyemshika na kumwongoza hadi ushindi.
Wayahudi walikataa kusikia kuhusu unganiko kati ya Mwana na Baba yake kuwa msingi hasa wa taifa lao. Walidai juhudi, pesa na kuongezwa cheo - na ni hivyo hadi leo.
YOHANA 10:27-28
“Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu.”
Yesu ndiye kondoo wa Mungu mpole; awaitaye wafuasi wake kondoo na wana-kondoo, wale wanaopokea tabia zake. Sifa zao za kwanza ni kusikiliza, kwa sababu Roho Mtakatifu alifungua akili na mioyo yao, ili kwamba sauti ya Yesu na mapenzi yake zididimie ndani ya utu wao kabisa na kuwageuza kuwa viumbe vipya. Tabia ya usikivu ndiyo mwanzo wa ufuasi wao.
Kristo awafahamu wote wanaokimbilia kwa Neno lake binafsi; awapenda, aona siri zao, naya afahamu ile sura, ambayo anakusudia kuwaumbia. Wakristo wa kweli hawadidimii ndani ya hali isiyo na shabaha au kutokushughulika. Waonekana kwa bidii zao. Na mbinguni majina yao yajulikana na kuorodheshwa. Kila mmoja ni mwujiza wa pekee, ni kiumbe kipya cha Mungu.
Yesu afanana na mchungaji mwema; kondoo zake wamezoea sauti yake, na wanamfuata na furaha ya kujikabidhi kabisa kwa uongozi wake. Hawatamani chochote mbali na mapenzi ya Mchungaji wao. Mawazo yote ya ukaidi hayana nafasi mioyoni mwao; huwa ni wana-kondoo wapole kweli.
Badiliko hilo lilitendeka ndani ya tabia zao kwa sababu ya kazi za Kristo ndani yao. Yeye aliwapatia upendo wa Mungu, pia na nguvu ya kushinda dhambi na kifo. Hawatakufa kiroho bali kuishi daima, kwa sababu wanabeba uzima wake, zawadi kuu ndani yao. Wako huru na hukumu na upotevu, pia na kifo cha milele; wamehesabiwa haki kwa damu ya Kristo.
Hakuna hata mmoja kati ya hao walionunuliwa kwa damu ya Kristo atakayepotea. Yeye aliachilia utukufu wa mbinguni, ili aokoe binadamu, akateseka ili awapatie uzima. Alikusudia kuwatunza kwa gharama yoyote ile. - Je, wewe wajisikia salama mikononi mwa Bwana wako? Ulichagua enzi ya Kristo na uwezo wake? Upande moja unaishi katika dunia ya dhambi ukizunguka-zunguka bure, au umewekwa huru kwa kufanywa mwana wa Mungu kwa njia ya Kristo na kujaliwa Roho Mtakatifu wake. Ulinzi wa Bwana wetu unapitiliza kabisa bidii zetu zote za kuweza kujilinda wenyewe, maana huo ulinzi unaenea kote, ng’ambo ya upeo wa ufahamu wetu. Tupo imara tukisimama sambamba na Mshindi wetu.
YOHANA 10:29-30
“Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu Umoja.”
Baadhi ya waumini wataweza kuwa na mashaka na wazo kwamba kijana Yesu kweli ataweza kuwalinda na kifo, Shetani na ghadhabu ya Mungu. Kweli jambo hilo lapita uwezo wa ufahamu. Lakini ndiyo sababu Yesu aliwaelekeza wanafunzi wake kwa Baba yake na uenyezi wake. Ni yeye aliyemchagua kila mmoja kipekee kuwa mfuasi wa Yesu. Hakuna amfuataye Yesu isipokuwa kwa mapenzi ya Mungu mwenye enzi na chaguo lake.
Mungu Baba anawajibika kwa wale wote wanaoshikamana na Mwana wake. Baba ndiye aliye Mkuu, mwenye uenyezi wote. Yesu hakujipendeza mwenyewe, bali alinyenyekea kwa kwa kumwachia kila kitu Babaye.
Kwa kiasi hicho cha kujikinahi mwenyewe, ukamilifu wa uungu ulikuwa ndani yake. Wako wanaosema kwamba Kristo ni mdogo kwa Baba yake. Lakini asili ya Roho Mtakatifu inatueleza kwamba, yeyote anayejiinua atashushwa, na yeyote anayejishusha atainuliwa. Kwa vile Yesu alimpa Baba utukufu wote, aliweza kusema: “Mimi na Baba tu Umoja”. Uwazi huo ulikanusha ubishi wa wale wasemao kwamba, tunamwunganisha mwingine na Mungu. Hapana, hatuabudu miungu mitatu, tunamwabudu Mungu mmoja. Watu wanaokataa umoja huu wa Kristo na Babaye ulio kamili, basi wanao kiburi, na wasiotambua kwamba, njia kwenda kwa ukuu unaanza kutoka kwa unyenyekevu.
SALA: Bwana Yesu, wewe ndiwe Mchungaji Mwema. Wewe ulitoa uhai wako kwa ajili ya kondoo. Unatuhakikishia uzima, hivyo hatutakufa. Tunakushukuru sana; hutuachii kifoni, wala kwa Shetani, dhambi na ghadhabu ya Mungu. Hakuna awezaye kutunyakua toka mkononi mwako. Utufundishe unyenyekevu wako, ili tuweze kumfahamu Baba ndani yako; Na tuweze kujikinahi wenyewe, ili na uwezo wako uonekane ndani ya udhaifu wetu.
SWALI:
- Jinsi gani Kristo anaongoza kundi lake?