Previous Lesson -- Next Lesson
a) Kuponya siku ya Sabato (Yohana 9:1-12)
YOHANA 9:1-5
“Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza, wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake. Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka, maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi. Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”
Yesu hakutoroka kwa haraka kutoka kwa maadui zake, waliokuwa wakitaka kumpiga kwa mawe, ila kwa hali hiyo ya hatari kwake akamtambua ndugu mtu mwenye shida kuu. Yesu nafsini mwake ni mpole wa upendo anayekusudia baraka tu. Wanafunzi nao wakamwona yule kipofu, lakini hawakusikitishwa zaidi. Badala yake wakahisia kuhusu kosa lililosababisha balaa kwa huyu kipofu; ndivyo zamani watu wengi walivyofikiri kwamba magonjwa yatokana na kosa fulani fulani, na hivyo yakafikiriwa kuwa adhabu toka kwa Mungu. Yesu hakueleza sababu ya shida hiyo; hakutangaza kamili kwamba wazazi wala huyu mtu kuwa hana hatia, lakini aliona ndani ya shida ya huyu mtu nafasi nzuri kwa Mungu kutenda kitu. Hakukubali wanafunzi wake wamhukumu huyu maskini, au watunge mawazo yao juu ya sababu ya upofu huo. Aliwahimiza waendelee na kuwaonyesha kusudi la mapenzi ya Mungu: Wokovu na uponyaji.
“Nahitaji kufanya kazi”, akasema Yesu. Upendo ulimsukuma, bila hamu ya kuhukumu au kuharibu, alitamani tu kuponya kwa huruma. Kwa njia hii alionyesha upendo wake wa kuokoa, nia na shabaha zake. Yeye ndiye Mwokozi wa ulimwengu, akipenda kuwajenga watu waingie katika maisha tukufu.
Nasi pia twasikia maneno ya Yesu, “Sitendi kazi katika jina langu wala si katika nguvu zangu; badala yake nakamilisha kazi za Baba yangu, katika jina lake, kwa maeleano naye.” Kazi zake aliziita kazi za Mungu.
Yesu alifahamu ufupi wa muda wake, na kifo kuwa karibu. Hata hivyo, alichukua muda wa kumponya huyu kipofu. Yeye ndiye nuru ya ulimwengu, akitamani kummulikia na yule kipofu na nuru ya uhai. Alijua habari ya muda ujao, ambapo hata yeye wala mtu mwingine mtukufu hataweza kufanya kitu. Muda huu wa mchana na yenye nafasi ya kuhubiri, basi tumshuhudie Bwana. Giza itazidi, ulimwengu wetu hauna tumaini lingine bila kurudi kwake Kristo. Ni nani atakayetayarisha mapito yake?
YOHANA 9:6-7
„Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho, akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona.”
Kabla ya hapo Yesu alitenda miujiza yake kwa neno tu. Lakini kwa nafasi hii ya kipofu alitema chini akafanya tope kwa yale mate akafunika macho ya kipofu na tope hilo. Kwa njia hii Yesu alikusudia huyu kipofu asikie kwamba amepata kitu kutoka kwake mwenyewe. Yesu alimhurumia huyu kipofu, naye akamshughulikia kwa namna safi sana, ili amponye. Kiajabu, macho ya kipofu hayakufunguka hapo hapo. Ilimpasa atembee kiasi fulani hadi chini bondeni, ili ajioshe ndani ya birika la Siloamu, maana yake, “Aliyetumwa”; hii ilikusudiwa kuwa ishara kwamba, uponyaji huo ulikuwa ni utume kwa watu wake Waisraeli. Maana wao wenyewe walizaliwa vipofu kiroho katika dhambi na hatia, wote wakihitaji uponyaji uliopatikana kwake Yesu pamoja na wokovu.
Yule kipofu alikubali ahadi ya Kristo, akitegemea kabisa upendo wake, akatii mara. Akatembea huku akijiuliza juu ya agizo hilo. Akaendelea mbele, akanawa macho yake na hapo kupewa kuona. Mara moja akaona watu, maji, nuru, mikono yake mwenyewe na anga ya mbinguni. Akatazama hayo yote kwa kushangaa sana. Sauti yake akaipaza kwa “Haleluya” na sifa kwake Mungu.
YOHANA 9:8-12
“Basi jirani zake, na wale waliomwona zamani kuwa ni mwombaji, wakasema, Je! Huyu siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba? Wengine wakasema, Ndiye. Wengine wakasema, La, lakini amefanana naye. Yeye mwenyewe alisema, Mimi ndiye. Basi wakamwambia, Macho yako yalifumbuliwaje? Yeye akajibu, Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tupe, akanipaka macho akaniambia, Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona. Wakamwambia, Yuko wapi huyo? Akasema, mimi sijui.”
Mwujiza huo haukuweza kufichwa, maana majirani yake walimwona amepona na wakashangaa mno. Baadhi yao hawakuamini kwamba huyu atembeaye wima sasa ndiye yule aliyetembea kwa wasiwasi na kusita katika kusogea, na mara nyingi akiongozwa na jamaa. Lakini walishuhudia juu ya nafsi yake kwamba, ni yule waliyemfahamu na hali ya upofu.
Watu wakaanza kuulizia kinaganaga jinsi alivyoponywa, lakini hawakuulizia habari ya mponyaji, ila kuona tu matokeo hayo. Yule aliyeponywa akamwita mponyaji wake Yesu, Ila hakujua zaidi juu yake. Hakuelewa habari ya uungu wake Kristo, lakini alimwona tu kama mtu wa kawaida, aliyefanya tope na kuipaka kwenye macho yake. Na ndipo kumwagiza aende kunawa, na hivyo akapata kuona.
Hapo wapelelezi wa baraza wakauliza, “Yuko wapi huyu Yesu?” Basi huyu mtu akajibu, “Mimi sijui; hapo nyuma nalikuwa kipofu na sasa naona. Hakuniulizia pesa, wala neno la kushukuru. Nilienda chini kwa birika kunawa, na sasa naweza kuona. Mimi sijui yule ni nani, wala sifahamu alipo.”
SALA: Tunakushukuru, Bwana Yesu; hukumpita yule kipofu bila kumjali. Ulifumbua macho yake ukamfanya kuwa ishara kwa wote waliozaliwa katika dhambi. Usafishe na macho yetu kwa njia ya Roho wako Mtakatifu, ili tuweze kuona nuru yako, hata tukiri jina lako kwa furaha.
SWALI:
- Kwa nini Yesu alimponya yule mtu aliyezaliwa kipofu?