Previous Lesson -- Next Lesson
3. Kristo afufua wafu na atahukumu ulimwengu (Yohana 5:20-30)
YOHANA 5:20-23
20 “Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizi atamwonyesha, ili ninyi mpate kustaajabu. 21 Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana awahuisha wale awatakao. 22 Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote, 23 ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka.”
Jinsi kazi hizi zilivyo kuu, haziwezekani kwa mtu, bali Yesu aweza kuyatenda. Baba anayakabidhi kwa Mwana, ili azikamilishe. Hapo tunatambua sifa mbili zilizotabiriwa katika maandiko ya kumhusu Kristo. Wayahudi walimtazamia mtu atakayezionyesha: Kuwafufua wafu na kuhukumu kwa haki. Hayo mawili yalikuwa pamoja na Yesu aliyaunganisha na yeye mwenyewe. Kabla ya hapo Yesu alitabiri mbele ya adui zake, kwamba yeye ndiye Bwana wa uhai na atakayehukumu, iwapo wao walimwangalia kama mjinga au mwenye kukufuru. Wakaamua kwamba wamwue. Kwa thibitisho hilo Yesu bado alitamani kuwageuza na kuwaongoza wapate kutafakari yaliyo sawa, ndipo waungame kwa kweli.
Mungu wetu siye wa kuharibu, bali ni mtoa uzima, asiyetamani kifo cha mwenye dhambi, bali ageuke kabisa kutoka kwa ukaidi wake na kuelekea uzimani. Yeye amkataaye Mungu ataharibika pole pole, roho yake, moyo na mwili. Upande wapili amkaribiaye Kristo, atahuishwa na kushiriki uzima wa milele. - Mwokozi anatamani kuokoka kwako na uamke.Utajali sauti yake? Au utanang’ania maisha ya dhambi na hatia?
Tangu milele ulimwengu umewekwa msingi juu ya ukweli. Hata kama watu hawamjali Bwana wao, wakiuana na kudanganyana, hata hivyo ukweli huo haubadiliki. Siku ya hukumu itakuwa siku kubwa ya kuhesabu. Kisasi tukufu itawaangukia wote wenye ukatili, na hasa juu ya wale ambao hawakujali wajane na wasiojiweza. Mungu alikabidhi hukumu yote kwake Kristo. Atawahukumu watu wote, lugha zote na dini. Yesu alikuwa ni mtu asiye na hatia yoyote, lakini anatambua na kusikia madhaifu yetu yote. Hukumu yake itakuwa ya haki kabisa. Atakapotokea katika utukufu wake, makabila yote ya duniani wataomboleza, maana hawakumjali hakimu, kwa kumdhadharau na kumkataa. - Je, wewe unatambua hayo?
Siku ile wote watapiga magoti mbele ya Mwana. Wale waliopuuza kumwabudu Kristo hapa duniani, watamheshimu kule kwa hofu na kutetemeka. Kristo anastahili enzi zote, utajiri, heshima na utukufu (Uf. 5:12). Yeye ameupatanisha ulimwengu na Mungu. Alikuwa ni kondoo mnyenyekevu aliyepigwa kwa ajili yetu. Mungu na Mwana wako sawa katika asili yao ya upendo na mamlaka, wala si kwa kazi zao tu, lakini katika kustahili heshima na kuabudiwa kwao. Hayo ndiyo sababu Yesu hakukataa kuabudiwa na yeyote akiwa hapa duniani. Na sisi inatupasa kumheshimu Mwana sawasawa tunavyomheshimu Baba.
Wote wanaomkataa Kristo au kumwona kuwa mdogo, basi wanamkataa Baba mwenyewe. Yeye aitwaye wa Milele anayo uhuru wa kumchagua Mwana. Sababu hasa kwa watu kukataa uwana wa Kristo na kumwabudu ni nia yao mbovu. Hawataki kumjua, na hivyo hawawezi kumtambua Mungu kwa hali yake halisi alivyo.
YOHANA 5:24
24 „Amin, amin, nawaambia, yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.“
Yeyote asikiaye kwa kufurahia injili ya Kristo, na akiamini uwana wake na sadaka yake kwa ajili ya dhambi atapokea uzima wa milele. Uzima usioanza siku ya kufa, lakina unaopokelewa hapa tukiwa hai duniani kwa njia ya Roho Mtakatifu. Huyu Roho anakushukia kwa sababu unamwamini Baba na Mwana. Sio wote wanaoshika vizuri maana ya maneno ya Kristo, hata baada ya kuyasikia mara elfu, hata kwa kuyasoma na kuchunguza yaliyomo. Hawatasema kuhusu neema ya Mwana, wala hawatembei Rohoni. Imani ya kweli ni tumaini ndani ya Kristo na utii kwake. Kwa kuingia agano la namna hii na Kristo, utakuwa umevishwa haki yake, pia kuwekwa huru na hukumu; maana ni imani inayookoa wala si matendo. Upendo wa Kristo unawafunika wale wanaojikinga kwenye msalaba, na anafuta dhambi zote na kusafisha dhamiri zao. Inatutia moyo sana kumwelekea Mungu. Maana mwenye Umilele ameesha kuwa Baba yetu kwa kuzaliwa kwetu kwa upya. Kuzaliwa kwetu mara ya pili ndiyo matokeo ya kuvishwa haki yake. - Je, ndugu, umetambua ahadi kuu za Kristo? Utakuwa umewekwa huru na kifo na matisho yake. Umefanywa hai milele ndani ya neema ya Kristo. Ghadhabu ya Mungu haitakuangukia.
Imani yako ndani ya Kristo imebadilisha tabia zako; uhai takatifu na wa milele ni wako sasa. Kiungo chetu na Yesu si uamizi rahisi kimawazo tu, lakini kwa matendo, kwa kukamata utu wetu kabisa, tena ni ya mara moja kweli. Hakuna wokovu kubwa zaidi kuliko kudumu ndani ya Kristo. Jifunza mstari huu wa 24 kimoyo, na uunganishe maisha yako ndani yake, ndipo wewe na mimi tutakutana katika maisha ya umilele uso kwa uso.
SALA: Tunakuabudu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, maana umetusamehe dhambi zetu na kutupatia haki. Hatutaingia hukumuni, maana ghadhabu yako imepita juu yetu. Tunakuabudu kwa sababu uhai wako umemiminwa ndani yetu, na kifo kwetu kimefutika. Tunaishi kwa ajili yako milele. Utuimarishe ndani yako, ili tuweze kukuza jina lako tamu.
SWALI:
- Zipi ni kazi muhimu mbili, ambazo Baba alimpa Kristo azikamilishe?