Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- Romans - 034 (The Believer Considers Himself Dead to Sin)
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hebrew -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Malayalam -- Polish -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Turkish -- Urdu? -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
SEHEMU 1 - HAKI YA MUNGU INAHUKUMU WENYE DHAMBI WOTE NA KUJALIA HAKI PAMOJA NA KUWATAKASA WOTE WAMWAMINIO KRISTO (Warumi 1:18 - 8:39)
D - Uwezo Wa Mungu Hutuokoa Na Nguvu Ya Dhambi (Warumi 6:1 - 8:27)

1. Mwumini hujifikiria mwenyewe kwamba, amefia dhambi (Warumi 6:1-14)


WARUMI 6:5-11
"5 Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhakika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; 6 mkijua neno hilo, ya kuwa utu wenu wa kale ulisulibiwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena; 7 kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi. 8 Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye; 9 tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena, wala mauti haimtawali tena. 10 Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu. 11 Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.“

Je, umefahamu kwamba, Yesu aliteseka na kufa kweli msalabani, kwa sababu ya dhambi zako chafu? Kwa ajili ya madhambi yako na maasi yako unastahili adhabu kali hadi kufa, na kuonja mateso mabaya ya jehanum milele. Haya basi, Yesu alibeba hukumu ya Mungu kwa ajili ya kuasi kwako, akakubali kusulibiwa badala yako kwenye mti uliolaaniwa.

Kama umepokea upendo wa kuokoa na kazi zake Yesu, wewe ungeona aibu sana kwa ajili ya dhambi zako, na usingetaka kabisa kutenda au hata kuwaza maovu tena. Na hivyo, ungejitweza na kujikinahi mwenyewe. Usingejitambua mwenyewe, bali kujihukumu na hata kukubali kuhukumiwa. Ungejihesabu kuwa umekufa na kufutika kabisa. Hakuna hata kidogo wokovu mwingine kwa ajili ya utu wako wa kuasi, ila kukamilisha kifo hiki cha kiroho ndani yako, ili Kristo apate kuishi ndani yako.

Haiwezekani kumfuata Kristo bila kujikana mwenyewe. Paulo anayo ushuhuda muhimu, anayorudia katika waraka zake: Tumekwisha kusulibiwa na kufufuliwa pamoja na Kristo, ili tuweze kuishi kwa kukubaliana naye; tena kwa kutambua kwamba, aliyesulibiwa hawezi tena kutenda inavyompendeza, lakini ametukuzwa, naye anaendelea kufia utu wake wa kale kwa maumivu mengi.

Paulo anashuhudia kwamba, kifo hiki cha utu wetu kilitendeka wakati tulipoanza kuamini ndani ya Msulibiwa. Ndiyo hapo hapo tuliunganishwa na kifo cha Yesu, nasi tulikiri kwamba, kifo chake kilikuwa na cha kwetu. Tulikufa kihalali, nasi hatuna tena haki au mambo ya kutaka katika maisha haya, maana ghadhabu ya Mungu amekwisha kutuharibu kabisa ndani ya Kristo.

Jinsi ambavyo sheria ya serikali haiwezi kutoa haki yoyote kwa ajili ya aliyekufa, ndivyo hata sheria ya Mungu haina nguvu tena juu ya mtu mfu. Majaribu nayo hayaoni mahali pa kuanzia ndani ya miili yetu miovu, maana tuiyahesabia kuwa imekufa.

Hata hivyo, kuna baadhi ya watu ambao karibu wamekufa, au wamekufa nusu, lakini bado wanayo pumzi kidogo ya uhai. Watu wa namna hii pengine bado wanaweza kutembea. Lakini umfikirie mtu mfu anainuka na kutembea na mwili wake wa kuchakaa barabarani katika mji wako! Basi, kila mtu atamkimbia, kwa sababu ya harufu yake mbaya. Hakuna kilicho kibaya zaidi kuliko Mkristo anayegeukia tena kwenye dhambi zake za awali, na akivaa tena mwili wake mbovu na kuwa mfungwa wa tamaa zake dhilifu. Kujikinahi bila kukoma ndiyo hali ya imani yetu. Inatupasa kujihesabu kuwa wafu ndani ya Kristo siku zote.

Imani yetu hata hivyo haitahukumu tu mambo yasiyofaa, kana kwamba tunaendelea kuvua ule utu wa kale, na kujihesabia wenyewe kuwa tumesulibiwa na kufishwa. Hapana, maana imani yetu ni dhahiri. Ni imani ya uhai, maana umoja wetu na Kristo katika upendo inatufanya kuwa washiriki wa ufufuo wake, shangilio na enzi. Jinsi Yesu alipotoka kaburini mwake kimya-kimya na kupita na mwili wake wa kiroho katika miamba na kuta, ndivyo yule aaminiye anajivisha ndani ya Yesu akijua kwamba, maisha ya milele ya Bwana wetu yanatiririka ndani yake anayeshikamana naye kabisa.

Kristo hafi tena wakati wowote. Yeye ameshinda kifo, maana huyu adui hasa hakuweza kuwa na nguvu juu yake aliye Mtakatifu. Yesu alikufa kuwa Kondoo wa Mungu kwa ajili ya dhambi zetu. naye akapokea ule ukombozi wa daima. Yeye alikufa kwa ajili ya kuwatumikia Mungu na watu. Kwa kiasi gani zaidi atatoa maisha yake leo kwa ajili ya Mungu na watu, maana yu hai, akimtukuza Baba yake wakati wowote, ili watoto waume na wa kike wengi wazaliwe kwake, wakitakasa jina lake la milele kwa njia ya maisha yao safi.

Je, unafahamu alama ya imani yetu? Ni Msalaba. Tulijikana sisi wenyewe kabisa tulipokiri dhambi zetu zote na kuunganishwa na Msalaba. Ndiyo maana Yesu alipanda ndani yetu nguvu ya maisha yake, ili tuweze kupaa kiroho, na kuishi kwa ajili ya Mungu kwa utakatifu na kwa furaha katika haki ya milele, jinsi Yesu alivyofufuka kutoka kwa wafu, akiishi sasa na kutawala daima.

Basi, kuna tofauti ya maana sana hata hivyo, kati ya Kristo na sisi wenyewe. Yeye alikuwa takatifu ndani yake tangu milele, mbali na sisi tuliopokea tu utakatifu kwa njia ya imani yetu katika umoja na Yeye. Huyu Mtume hakukutaka tu wewe umtumikie Mungu, lakini anakushawishi umtumikie Yeye ndani ya Kristo. Hatustahili kumkaribia huyu Mtakatifu sisi wenyewe, lakini tunapojizamisha ndani yake Mwokozi, na umimi wetu ukifa ndani ya upendo wake nasi tukiendelea ndani yake, ndipo nguvu yake, wema na furaha zake zitafanya kazi ndani yetu, ili tupate kushinda kwa kiasi kikubwa mapungufu yetu yote kwa njia yake yeye aliyetupenda. Tunaweza kushiriki tu katika pendeleo hilo kwa njia ya imani na mapenzi ya binafsi yaliyovunjika. Je, unaamini kwamba, umesulibishwa kweli na kuzikwa na Kristo, na umefufuka kweli kwa njia ya ufufuo wake?

SALA: Ee Bwana Kristo mtakatifu, wewe ndiwe ulienda badala yangu msalabani. Ndiwe uliyebeba dhambi zangu na lawama yangu. Asante sana kwa ajili ya ukombozi huo mkuu na wa upendo. Kamilisha ndani yangu hali ile ya kujikana, na uniimarishe ndani ya ufahamu kwamba, nilikuwa nimestahili hukumu ya kufa, ili nijifahamu kuwa nimekufa ndani ya kifo chako. Nakushukuru kwa uvumilivu wako na makusudi yako kwa ajili yangu. Nakutukuza kwa ajili ya kupanda uhai wako ndani yangu, ili niweze kuishi kwa ajili yako, nimtukuze Baba yako, na niwe nimeunganika nawe kiimani. Ee Bwana mtakatifu, wewe unatengeneza watakatifu kutokana na wahalifu, na kutokana na yatima unafanya watoto wa Mungu wanaoishi kwa ajili yake. Jinsi neema yako ilivyo kuu mno! Twaomba ukubali ibada zetu na maisha yetu nayo.

SWALI:

  1. Jinsi gani tumesulibiwa na Kristo na kufufuka ndani ya uhai wake?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on November 15, 2022, at 12:28 PM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)