Previous Lesson -- Next Lesson
1. Mwumini hujifikiria mwenyewe kwamba, amefia dhambi (Warumi 6:1-14)
WARUMI 6:1-4
"1 Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? 2 Hasha! Sisi tuliofia dhambi, tutaishije tena katika dhambi? 3 Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? 4 Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.“
Katika sura 1 – 5 mtume Paulo ametuonyesha kwamba, kila mtu aaminiye ndani ya Kristo amehesabiwa haki kihalali na kuokolewa na ghadhabu na kuhukumiwa na Mungu. Anawaeleza wakristo Warumi kwamba, kuhesabiwa haki hivyo inatuingiza katika hali ya amani na Mungu na upendo kwa ajili ya ulimwengu.
Baada ya toleo hili la mwanzoni, mtume anajibu swali lile muhimu, lililoulizwa kwa namna ya kukashifu na maadui wa kuhesabiwa haki kwa uhuru: Je, tuendelee kutenda dhambi, ili neema na izidi, na uaminifu wa Mungu upate kuonekana?
Katika jibu lake kwa swali hilo bovu, Paulo anachora njia inayoongoza kwenye ushindi wa mwisho juu ya dhambi maishani mwetu kwamba, mwumini yeyote hawezi kupona asiposoma fungu linalofuata na kuitumia ndani ya maisha yake. Maana mjadala wetu sio namna ya somo la kimawazo tu, bali ni mwongozo kwa kuishi katika utakatifu.
Mtume hakusema: „Hangaika na dhambi unazozijua na uzishinde“, maana alijua kwamba, hakuna awezaye kuzishinda dhambi zake kwa nguvu zake mwenyewe. Paulo hakuiti uhangaike dhidi yako mwenyewe, lakini anakuita ushuhudie kwamba, hakuna jibu lolote lingine kwa ajili ya hali yako ya umimi na tabia ya kuasi, ila njia ya kufa kwa wema wa binafsi.
Je, tutawezaje kufia nguvu ya dhambi ndani yetu? Paulo anajibu kwa urahisi: „Tumekwisha kufa“, kana kwamba ni rahisi kuharibu uovu! Anaeleza hayo katika muda uliokwisha kupita, kana kwamba tendo la kufa ilimalizika ndani yetu. Basi, haitegemei bidii yetu ya binafsi, wala hatuna haja ya kuihangaikia tena. Jinsi ilivyo, anatuonyesha kwamba, ubatizo wetu ndiyo alama ya mauti ya utu ule ovu na kifo cha uchoyo wetu. Ubatizo wa kikristo sio desturi ya nje tu; sio tendo la kusafishwa kwa nje tu, wala si kumwagiwa maji tu kwenye mwili, hapana. Ni hukumu, kifo na kuzikwa. Kwa ubatizo wako unashuhudia kwamba, Bwana wako amekupatiliza kufa, unatimiza hayo kwa kuzamishwa majini. Kuoza, kutupilia mbali utu wa kale, hayatendeki kwa uhalisi mwilini, lakini kiroho, unapokubali kabisa kifo cha Kristo badala yako. Ubatizo wetu huonyesha unganisho letu kamili na Kristo ndani ya agano la upendo, uwazi wetu wa upendo wetu kwake, na kuendelea kwetu ndani ya mfano wake wa uaminifu.
Kristo alipotuondolea dhambi zetu, tulifia pamoja naye hali yetu ya kiburi. Hivyo maana ya msalaba pia ni kuchoma utu wa uasi. Yeye aaminiye anajikana mwenyewe na kujitwisha msalaba, akikiri kwamba, watu wote wanastahili kuharibiwa kila siku. Kifo chetu hiki hakitendeki kwa vita ya ki-saikologia (psychological). Ilikwisha kutendeka hapo zamani, Kristo alipolia pale penye mti uliolaaniwa, „Imekwisha“. Unapoamini, utaokolewa na kuwekwa huru kutokana na nguvu ya dhambi.
Kristo alikufa na kuzikwa si kwa ajili ya kutuunganisha na kifo na kuzikwa kwake tu, lakini alifufuka kutoka kwa wafu, akituvuta na sisi kwenye ufufuo wake na kutujalia uzima wake wa milele. Sisi pamoja na kujikana wenyewe, pia tuliunganishwa na Kristo katika nguvu ya uhai wake mwenyewe. Kutokana na hayo, imani yetu haimaanishi tu ufahamu na kanuni fulani, bali ni nguvu inayokua ndani yetu, kana kwamba Kristo amezaliwa ndani yetu. Yeye anakua, anatenda kazi, anashangilia na kushinda maovu ndani ya miili yetu. Sio sisi tunaofaulu kupata ushindi, lakini ni Yeye anayeshangilia ushindi ndani yetu.
Ufufuo kutoka kwa wafu ndiyo ulikuwa ushindi mkubwa na yenye utukufu wa Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa njia ya ufufuo wake ametangaza utukufu wake wa milele na haki isioweza kutingishwa kwa kuridhika na upatanisho wa Mwana wake, ushindi wake juu ya kifo, na ufunuo wa maisha yake matakatifu. Enzi ya Mungu ilitenda kazi waziwazi ndani ya ufufuo wa Kristo, na ule upya wa maisha yake matakatifu inatenda kazi ndani ya waumini waliofunganishwa na Kristo kwa imani. Ukristo sio dini ya hofu au kifo. Ni dini ya tumaini, uhai na nguvu.
Sisi kwa kumwabudu Kristo tunakiri kwamba, haishi mbali nasi, juu ya nyota, au kwamba anatufikiria tu mara chache. Badala yake tunakiri kwamba, amefunganishwa nasi kwa agano lisiloweza kuvunjwa, na ya kwamba, anaishi ndani yetu kwa ukamilifu wa nguvu yake, anakaa nasi siku sote, na anatuongoza tuendeshe maisha yetu kwa utakatifu. Hivyo, ubatizo wako ni umoja pamoja na Kristo, kifoni na maishani, na imani yako nayo ni agano jipya kabisa kwako. - Yeyote anayejiunga na Kristo, anakiri kwamba, amekufa naye msalabani, naye amefufuka ndani yake kwa maisha mapya ndani yake.
SALA: Ee Bwana Kristo, uliyemaliza kifo changu msalabani, ulitamka na uhai wangu ndani ya ufufuo wako. Nakuabudu pamoja na wale wote wanaokuamini, waliokufa nawe pia kiimani, nao wakafufuka pamoja nawe kiroho. Nakuabudu wewe, Baba wa utukufu, nikikushukuru kwa ajili ya ufunuo wa hali yako ya utukufu kutokana na ufufuo wa Mwana wako, na kwa ajili ya kutujalia uhai ndani yako. Tusaidie kuendelea ndani ya neema yake, na kutembea kufuatana na maagizo yake katika usafi, hali ya kujinyima, uaminifu, upendo na subira, ili uhai wako upate kuonekana ndani ya waumini wote.
SWALI:
- Maana ya ubatizo ni nini?
Tubuni,
mkabatizwe kila mmoja
kwa jina lake Yesu Kristo,
mpate ondoleo la dhambi zenu,
nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
(Matendo ya Mitume 2:38)