Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- Romans - 029 (The Faith of Abraham is our Example)
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hebrew -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Malayalam -- Polish -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Turkish -- Urdu? -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
SEHEMU 1 - HAKI YA MUNGU INAHUKUMU WENYE DHAMBI WOTE NA KUJALIA HAKI PAMOJA NA KUWATAKASA WOTE WAMWAMINIO KRISTO (Warumi 1:18 - 8:39)
B - Njia Mpya Ya Kuhesabiwa Haki Kwa Imani Iko Wazi Kwa Wanadamu Wote (Warumi 3:21 - 4:22)
3. Ibrahimu na Daudi wakiwa mifano ya kuhesabiwa haki kwa imani (Warumi 4:1-24)

d) Imani hodari ya Ibrahimu ni mfano wetu (Warumi 4:19-25)


WARUMI 4:19-22
"19 Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa ya tumbo lake Sara. 20 Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; 21 huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi. 22 Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.“

Ibrahimu alisikia neno la Mungu la unabii kwamba, alichaguliwa kuwa baba wa watu wengi. Neno hilo la mafunuo makubwa lazima lilimshangaza Ibrahimu, ambaye hakuwa na mwana, lakini alilikubali kwa imani. Aliamini kwamba, Mungu hutoa tumaini hata wakati ambapo tumaini lote la kibinadamu limepotea. Tayari, Ibrahimu alikuwa amekosa katika mvutano wa ki-imani, wakati Ishmaeli alipozaliwa kwake kutoka kwa mtumwa Mmisri. Ndipo, ilipoonekana haiwezekani tena kwa mkewe aliyezeeka kuzaa mtoto, yeye hakuangalia taratibu ya asili, lakini alimwangalia Mwumbaji wa asili kwamba, ataweza kubadilisha taratibu za asili. Ibrahimu hakujidanganya mwenyewe kwa wazo kwamba, haiwezekani tena kwake kuwa na mwana kutoka kwa Sara mkewe. Badala yake alitia moyo imani yake, akashikamana na neno la Mungu, akitegemea ndani ya ukweli wa daima, naye alijua hakika kwamba, Bwana wa utukufu hasemi uongo, pia na kwamba, hatakosa kutimiza ahadi yake, hata wakati akili ya kibinadamu haikuona njia ya kutimiza hiyo ahadi.

Shikamano hilo imara na uaminifu wa Mungu katika mvutano huo wa imani yake ilihesabiwa kwake Ibrahimu kuwa ni haki. (Mwanzo 15:1-6 na 17:1-8).

Kristo akuita siku ya leo, ushiriki imani ya Ibrahimu. Tunapojiangalia sisi wenyewe na kuchunguza ndani kwa chini katika makanisa yetu, tutakuta kwamba, mashirika yetu yamechoka kiroho, bila uwezo na karibu kufa. Hata hivyo, Kristo anatamani kutoa uzima wa milele kwa mamilioni ya watu, kwa njia ya imani yako, sawa na ya imani yangu. Yeye apenda kubariki ushuhuda wetu kwamba, upendo wake upate kuwa na sura ya kimwili na kuongezeka sana kama nyota za angani. Je, unaamini ndani ya ahadi na wito wa Yesu kwamba, utakuwa na watoto wa kiroho kwa njia ya neno lako la imani? Unaamini kwamba, Mungu anaweza kushinda kutokuweza kwako, afufue kanisa lako lenye uvuguvugu, naye aweza kujiinulia watoto wa roho yake kutoka kwa mioyo ya kijiwe, jinsi alivyosema Yohana Mbatizaji: „Je, Mungu aweza kujiinulia watoto wa Ibrahimu kutoka katika mawe yaliyozagaa nyikani, kama ninyi hamtatubu kwa kweli?“ Je, mnamheshimu Mungu? Mnamtegemea Bwana wa utukufu na kumwamini, badala ya kuangalia yote kwamba yatakuwa mabaya, hasa kuhusu kanisa lenu lenye uvuguvugu na tabia zenu za ovyo? Yeye aweza kuwatumia, ili kubeba nguvu ya uhai wake kwa watu wengi. Mwe na uhakika kwamba, Mungu wa Ibrahimu, Bwana wa Paulo, ndiye yule yule jana, leo, na pia siku zote za mbeleni. Basi anatazamia imani yako, maana ndiyo ushindi uliofaulu ulimwenguni - ni imani yetu. Usilale! Usipoteze tumaini, hata kama mashindano ya imani yako yamekwisha kuendelea kwa miaka, hata makumi ya miaka, jinsi ilivyotokea maishani mwake Ibrahimu, hadi mwishoni tunda moja ndogo lilikomaa ndani yake, ambalo lilikuwa ni Isaka mchanga. Mbali na matatizo yake Ibrahimu, Bwana alimwimarisha kiroho na kumfanya hata kuwa baba wa manabii. - Na Bwana wako yu hai, naye anataka kukujalia haki kwa imani yako. Basi, uinue moyo wako, imarisha mikono yako yaliyolegea, hata na magoti yako hafifu, maana Bwana wako anaishi, naye anakutangulia katika vita vyako vya kiroho.

WARUMI 4:23-25
"23 Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesbiwa kwake, 24 bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; 25 ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.“

Ufahamu wa imani yetu ulikua hata kufikia uhakika kamili, kwa ajili ya ufunuo kwa Ibrahimu. Siku hizi Mungu hajionyeshi tu kama mweza yote, mkuu, na asiyeonekana, lakini alitutumia Mwana wake Yesu, ili tupate kutambua ndani ya upendo wake Mungu aliye Baba. Jambo ambalo lilionekana haliwezekani, basi lilitokea, na Mwana wa pekee wa Mungu alikufa kwa kufuta dhambi zetu. Mungu mtakatifu hakuwaangamiza waovu, kwa ajili ya ukorofi wao, lakini alijiangamiza mwenyewe, ili sisi tulio waovu tupate kuokolewa. Namna hiyo ya Mungu kuwa mwenye rehema na upendo, aliyejitoa sadaka yeye mwenyewe, mtoaji na mwenye uvumilivu, ndivyo Mungu wetu alivyo.

Kristo alipofufuka kutoka kwa wafu, shangilio la dhabihu yake likasikika. Baba yake hakumwacha, alipomwaga ghadhabu yake yote juu ya Mwana Kondoo aliyesulibiwa, lakini alimfufua Mwana wake asiyekuwa na kosa, na hivyo kuthibitisha wazi kwamba, dhabihu yake ya pekee ilifuatana na mapenzi yake tukufu. Hivyo, ufufuo wa Kristo unahakikisha ukweli wa kuhesabiwa haki kwetu. Haikuwezekana kwamba, Kristo apaae mbinguni kabla ya kuzikwa kwake na kuwa karibu na Mungu Babaye tena. Hapana! Mungu alimfufua toka kwa wafu, ili na sisi tupate kuona na kuwa na hakika kwamba, upatanisho kati ya Mungu na ulimwengu ulikamilika pale msalabani.

Siku hizi Mwombezi wetu wa pekee huketi mkononi mwa kulia kwa Mungu. Anapatanisha kati ya Mwenye Utakatifu na sisi na kutumia matokeo ya dhabihu yake, ili sisi tusiwe tena na mashaka, lakini badala yake tudumu ndani ya imani yetu, na tuamini kwamba, Kriso anaweza kuwaokoa kabisa kabisa wale wanaomjia Mungu kwa njia yake, kwa vile anaishi milele kwa kufanya maombezi kwa ajili yao.

Basi je, imani yako iko wapi katika matatizo yote, hofu na hatari? Iko wapi tumaini lako kuhusu kuja kwa ufalme wa Mungu siku hizi, na kwa kuzaliwa mara ya pili kwa mamilioni ya watu? Kristo alitupatanisha na Mungu, naye yu hai leo, ili athibitishe kujaliwa haki kwetu kutokana na maombezi yake. Uamini basi kwamba, mito ya maji ya uzima yatatiririka kutoka kwa imani yako kwenye mioyo iliyo bila faida au iliyokufa. Uamini, wala usiwe na shaka wakati wowote, kwa sababu Kristo anaishi kweli.

''SALA: Ee Bwana Mungu, unaishi na unatutuma kuhubiri ulimwenguni. Mtumishi wako Ibrahimu aliamini kwamba, yeye na mkewe Sara, katika umri wao mkubwa, wataweza kuzaa mtoto wa rehema yako, ambaye kwa yeye watu wote wabarikiwe. Ushinde imani yetu ndogo, na uimarishe tumaini letu kwamba, tukutegemee wewe dhidi ya majaribu yetu, hata nguvu yako ikamilike ndani ya udhaifu wetu. Asante sana, kwa sababu ulituhakikishia kwamba, mamilioni ya watu watazaliwa mara ya pili katika siku zetu, maana wewe unaishi na kutawala milele.''

SWALI:

  1. Tunajifunza nini kutokana na mashindano ya imani ndani ya Ibrahimu?

Basi, tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani,
na mwe na amani na Mungu,
kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

(Warumi 5:1)

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on November 15, 2022, at 11:39 AM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)