Previous Lesson -- Next Lesson
b) Mtu hahesabiwi haki kwa kutahiriwa (Warumi 4:9-12)
WARUMI 4:9-12
"9 Basi je! Uheri huo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa twanena ya kuwa kwake Ibrahimu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki. 10 Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa. 11 Naye alipokea dalili hii ya kutahiriwa, muhuri wa ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa, apate kuwa baba ya wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki. 12 Tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Ibrahimu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa.“
Paulo alishambulia imani za Wayahudi, akavunja moja ya taratibu zao takatifu, ambao ni tohara. Watu wa jangwani waliangalia dalili hiyo kuwa ndiyo moja ya alama kuu ya agano la kale. Yeyote aliyepata kutahiriwa aliangaliwa kuwa mali ya Mungu, na yule asiyetahiriwa aliangaliwa kuwa mnajisi. Kwa hiyo, Wayahudi walimtaka kila mwamini mpya apate kutahiriwa kama dalili ya utakaso wake maalum, ambayo ilimstahilisha kuingia ndani ya agano na Mungu.
Paulo aliwathibitishia Wayahudi halisi kwa njia ya mwenendo wa Ibrahimu kwamba, mtu huhesabiwa haki si kwa kutahiriwa, bali kipekee kwa imani; tangu Ibrahimu mwenyewe aliposikia wito wa Bwana wake, na kuuamini kabla ya kutahiriwa. Hivyo basi, imani yake ilikuwa ni sababu na msingi wa kuhesabiwa kwake haki. Tohara kwake ilikuwa kama muhuri, wala si haki ya kuweza kumrudia Mungu. Basi haikuwa tohara iliyomsaidia, kwa sababu alitangulia kuingia katika agano na Mungu kwa imani.
Paulo alithubutu kusema kwamba, Ibrahimu alitangulia kuwa baba wa waumini wote wenye asili ya kimataifa kabla hajawa baba wa waliotahiriwa; kwa sababu alihesabiwa haki wakati alipokuwa bado mtu wa mataifa bila tohara. Kwa hoja hilo Mtume wa watu wa Mataifa alithibitisha kwamba, wa Mataifa wanaoamini wako karibu zaidi na Mungu kuliko waliotahiriwa wasioamini ndani ya Kristo. Mungu hutukuzwa kwa imani ya kweli na badiliko la moyo, wala si kwa alama za nje na desturi za kanuni za dini.
Wayahudi waliwaka kama moto katika hasira, Paulo alipowawekea wazi hali yao ya kujidanganya wenyewe na alipokanusha uhakika wao wa uongo. Hata hivyo, aliwashuhudia Wayahudi washupavu kwamba, wangeweza kuwa na Ibrahimu kuwa baba yao, ikiwa wakiamini ndani ya injili ya neema. Njia inayoelekea kwake Mungu si ya mapokeo, wala si ya tohara; lakini kumegemea Msulibiwa. Kwetu sisi jambo hilo linamaanisha kwamba, si kila Mkristo aliyebatizwa anahesabiwa haki kwa sababu ya ubatizo wake, asipoamini kweli; maana mtu huhesabiwa haki mbele za Mungu, si kwa desturi fulani au alama za nje, bali kipekee kwa imani.
SALA: Ew Baba Mtakatifu, hatustahili kukukaribia, kwa sababu ya maasi na makosa yetu. Lakini Mwana wako mpendwa alitufunulia upendo wake kwetu na kutujalia haki msalabani; nasi tunaliamini neno lake, tunatamani kuwa naye binafsi, tunajijenga juu ya wokovu wake nasi twafuata mfano wake, kwa sababu ulituhesabia haki na kututakasa kwa uhuru kabisa pamoja na wote wanaokupenda kote ulimwenguni.
SWALI:
- Kwa nini mwanadamu huhesabiwa haki si kwa kutahiriwa, bali kwa imani tu?