Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- Romans - 026 (Abraham’s Faith was Accounted to him)
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hebrew -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Malayalam -- Polish -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Turkish -- Urdu? -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
SEHEMU 1 - HAKI YA MUNGU INAHUKUMU WENYE DHAMBI WOTE NA KUJALIA HAKI PAMOJA NA KUWATAKASA WOTE WAMWAMINIO KRISTO (Warumi 1:18 - 8:39)
B - Njia Mpya Ya Kuhesabiwa Haki Kwa Imani Iko Wazi Kwa Wanadamu Wote (Warumi 3:21 - 4:22)
3. Ibrahimu na Daudi wakiwa mifano ya kuhesabiwa haki kwa imani (Warumi 4:1-24)

a) Imani ya Ibrahimu ilihesabiwa kwake kuwa na haki (Warumi 4:1-8)


WARUMI 4:1-8
"1 Basi, tusemeje juu ya Ibrahimu, baba yetu kwa jinsi ya mwili? 2 Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu. 3 Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki. 4 Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni. 5 Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki. 6 Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo, 7 Heri waliosamehewa makosa yao, na waliositiriwa dhambi zao. 8 Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.”

Paulo alitafuta kuwaongoza waumini wenye asili ya Kiyahudi na kuishi Rumi wapate kuwa na imani ya kweli kwenye daraja la Agano Jipya. Kwa kutumia mifano aliwachagulia Ibrahimu, baba yao, na Daudi kama nabii. Kwa kufanya hivyo alithibitisha kwamba walipokea msamaha wao na kuhesabiwa haki kwa njia ya imani yao, wala si kwa matendo yao.

Ibrahimu aliishi sawa na mtu yeyote mwingine; hakuwa bora wala mbaya zaidi kuliko wengine. Bwana alifahamu makosa yake mengi na moyo wake chafu, lakini alitambua ndani ya Ibrahimu hali ya kumtamani Yeye, na hiyo kuwa utayari fulani wa utii wa kiroho. Mungu alisema na Ibrahimu moja kwa moja na kumwita, na huyu Bedui (Bedouin) mzee aliamini wito wake. Hakuelewa ahadi za Mungu kwa kina wala maana ya ndani, lakini alimtegemea Mungu mwenyewe kwamba, neno lake ni la kweli, na kwamba Yeye ni mwaminifu katika kutimiza ahadi zake. Kwa imani hiyo Ibrahimu alimheshimu Mungu, naye akalitukuza jina la Bwana. Ibrahimu hakufikiria habari ya uwezo wake mwenyewe, wala si juu ya udhaifu wake uliokuwa wazi, bali alikuwa na tumaini imara ndani ya Mungu na enzi yake isiyo na mipaka. Tumaini lake na kujishughulisha na habari za Mungu ilituliza kiu cha moyo wake.

Imani hiyo imara, kamili na kuhakikishwa ilikuwa ndiyo sababu ya kujaliwa haki yake, wala si ufahamu wake wa elimu ya kidini. Ibrahimu alijijua kwamba hakuwa na haki ndani yake, lakini imani yake ilikuwa imehesabiwa kwake kuwa haki. Alikuwa na makosa sawa na sisi, lakini aliitikia chaguo lake Mungu, akasikiliza kwa makini neno lake, akakubali ahadi yake, na akayatunza ndani ya roho yake ya shauku kwa Mungu.

Katika sura hiyo ya 4 tunasoma mara nyingi kwamba, imani ya namna hiyo ilikuwa “ikahesabiwa kwake kuwa haki”. Tamko hilo likawa ni alama ya Matengenezo (ya kanisa). Yule amheshimuye Mungu kwa imani yake, basi anakubali injili ya msalaba, bila kuficha shaka lolote moyoni, na akijenga tumaini lake juu ya Kristo, huku akijijua kuwa na haki kabisa bila matendo ya sheria, pia na bila juhudi za binafsi.

Je, umesikia neno la Mungu likikufunulia habari ya uongo wako, machafu, na ya kupungukiwa upendo? Je, unaamini kwamba, hukumu itakuangukia kwa hayo? Je, unakuwa mwenye kusikitika na kuungama, na unaomba msamaha wa Mungu? Ikiwa unapata kuvunjika kwa habari ya kujivuna kwako, basi Roho Mtakatifu atamvuta Mwana wa Mungu aliyesulibiwa mbele ya macho yako ya kiroho, akinyosha mikono yake kwako na kukuambia: “Mimi nimekusamehe dhambi zako. Wewe hujisikii kuwa mwenye haki mwenyewe tu, bali mimi nakufanya kuwa na haki. Wewe si safi, lakini mimi nakutakasa kabisa.”

Je, umesikia neno la Mungu? Limedidimia ndani ya kiini cha roho na moyo wako wa kijiwe, na pia ndani ya akili yako ya kupurukusha? Kubali tu neno la Bwana; amini ndani ya injili ya wokovu, na ushikamane na habari ya msalaba, ili Mungu aweze kukuhesabia kuwa mwenye haki kweli. Umheshimu Msulibiwa kwa imani yako, nawe utakuwa unatakaswa katika ushirikiano wako na yeye.

Mtunga Zaburi, Mfalme Daudi aliyeongozwa na roho wa Mungu, na hata hivyo kuwa na makosa, alitambua mwenyewe mwujiza wa kujaliwa haki tukufu. Wala yeye hakujisifu kwa ajili ya zaburi zake za ajabu, na pia hakujijua kuwa na haki kwa ajili ya ushindi wake kuu vitani, naye hakujivuna kwa ajili ya sala zake za kuvutia, wala sadaka zake kubwa alizotoa. Badala yake alimsifia „Heri“ mtu aliyejaliwa msamaha wa dhambi zake kutokana na neema ya Bwana wake. Haki unayojaliwa ndani ya Kristo ndiyo zawadi iliyo kuu ya Mungu.

SALA: Ee Mungu mtakatifu, tunakushukuru kwa sababu ulitupatia neno lako ulipomingiza Mwana wako mwilini, nawe ukatuelezea habari ya kutujalia haki katika neema ya msalaba. Utufungulie masikio yetu, ili tutambue ahadi zako, tuyaelewe na kuamini kikamilifu ndani yako. Tunakushukuru kwa sababu ulitujalia haki kwa uhuru, tena pamoja na wote wanaokutumaini kokote walipo. Wasaidie rafiki zetu waweze kukubali wito huo, ili wao nao watambue nguvu ya msalaba wa Mwana wako.

SWALI:

  1. Jinsi gani Ibrahimu na Daudi walipata kuhesabiwa haki?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on November 15, 2022, at 10:54 AM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)