Previous Lesson -- Next Lesson
2. Yesu awatokea wanafunzi wake kwenye chumba cha orofani (Yohana 20:19-23)
Yohana 20:20
„Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.“
Ufufuo wa Kristo ndiyo thibitisho kwamba upatanisho na Mungu umekamilika. Mungu hakumwacha Mwana wake kaburini, wala hakumwondosha kwa sababu ya dhambi zetu alizozibeba. Aliridhika na dhabihu safi kabisa, alimwinua mshindi juu ya kaburi na kuishi naye kwa maeleano kamili pamoja naye Baba. Zaidi ya hapo, alikubali msalaba bila kufanya lolote ila mapenzi ya Baba. Msalaba ilikuwa ndiyo kusudi la kuja kwake duniani, tena ndiyo namna ya pekee ya kukomboa ulimwengu. Basi, namna gani watu wengine wanasemaje kwamba Yesu hakufa msalabani ?
Kristo alionyesha wazi kwamba yeye hakuwa njozi tu au roho aliyejificha. Aliwaonyesha kovu za misumari kwenye kitanga cha mikono yake. Aliwaonyesha na ubavu wake waone na alama ya mkuki iliyomchoma. Basi wakaona kovu za misumari wakavutwa kwamba yeye ndiye yule aliyekuwa nao, wala si namna ya kimungu kigeni, bali ndiye mwenyewe aliyesulibiwa . Mwana kondoo wa Mungu ndiye mshindi. Aliyepigwa kufa ndiye aliyeshinda mauti.
Polepole wanafunzi wakaanza kutambua kwamba Yesu hakuwa pepo au kivuli tu, lakini mtu kweli aliyepo pamoja nao. Namna yake mpya ilikuwa ndiyo sababu ya furaha yao. - Ndiyo bora na kwetu tuamini na kutambua kwamba Yesu ndiye Bwana aliye hai, aliyefufuka kutoka kwa wafu. Sisi sio yatima waliotupwa. Ndiye Ndugu yetu akiwa katika umoja na Baba yake na Roho Mtakatifu akitawala walimwengu daima.
Furaha ya wanafunzi ikaongezeka kutokana na ushindi wa Kristo juu ya mauti. - Tangu hapo yeye akawa ni tumaini hai kwa ajili yetu sisi, tuliokuwa tunapotea. Kaburi wazi bado si mwisho wetu, lakini uzima wake ni wa kwetu pia. Jinsi yeye alivyoitaja akiwa anastahili utukufu, akisema, „Mimi ndimi ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa, ataishi. Naye aishiye na kuniamini mimi, hatakufa kabisa.“
Wanafunzi walipoanza kutambua kwamba Yesu anasamehe dhambi zetu, wakashangilia zaidi. Anatuhakikishia kwamba alilipia dhambi zetu zote. Kwa hiyo tunayo amani na Mungu kutokana na jeraha zake.
Je, wewe unashiriki katika furaha yao ya Pasaka? Unainama mbele zake aliyefufuka, kwa vili naye yupo karibu, akikuhakikishia tumaini na kibali kabisa kuwa radhi? Yesu kweli yu hai, na ni juu yetu kufurahi. Kwa hiyo mtume Paulo analiambia Kanisa hivyo: „Furahini katika Bwana daima, na tena nasema, furahini. Wema wenu na ijulikane kwa watu wote. Bwana yu karibu.“
Sala: Bwana Yesu, tunakuhimidi na kukushukuru, maana ndiwe pekee tumaini letu na kutujalia maana kuu kwa maisha yetu. Jeraha zako zinatufanya kuwa na haki, na kuwepo kwako kunatupatia uhai na sisi. Ufalme wako na uje, na ushindi wako utambulikane, ili na wengi wainuke toka kifo cha dhambi na waishi kwa kutukuza Ufufuo wako.
Swali 124: Kwa nini wanafunzi walifurahi?