Previous Lesson -- Next Lesson
c) Wanasheria wamleta mwanamke mzinzi kwake Yesu ahukumiwe (Yohana 8:1-11)
YOHANA 8:1-6
“Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu alienda mpaka mlima wa mizeituni. Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hili wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi.”
Wajumbe wa baraza waliondoka kwenda kwao wakikasirika, kwa sababu Yesu aliwaponyoka mikononi mwao. Makutano walidhani kwamba viongozi walimruhusu Ye.su kwa uhuru kusema tena hekaluni. Lakini wajumbe hao waliendelea kumchunguza ili wapate kumtega. Yesu alienda nje ya kuta za jiji jioni, akavuka bonde la Kidroni. Asubuhi yake alirudi katikati ya mji, akiingia hekaluni palipojaa watu. Hakutoroka mji mkuu wakati wa mwisho wa sikukuu wa vibanda, bali aliendelea kuzunguka katikati ya adui zake. Mafarisayo walifanya kazi kama polisi ya nidhamu, kipekee wakati wa sikukuu ambapo ilikuwa ni nafasi kwa uchangamfu na kulewa divai. Basi wakamshika mwanamke aliyekuwa anazini. Wakatumia nafasi hii ya kumjaribu Yesu kwa kesi hii. Huruma yoyote katika jambo hilo ingeonekana mbele za Mungu na mbele za watu kama uhalifu kwa mapokeo ya kitaifa. Lakini kusisitiza adhabu ya kisheria ingethibitisha ukali wake na hivyo kupoteza hali ya kupendwa na watu. Basi hukumu yake kwa mwanamke huyu ingekuwa ni hukumu kwa mtu yeyote aliyeaibika na athari ya maadili. Hivyo wakangojea kwa shauku tamko lake la hukumu.
YOHANA 8:7-9a
“Nao walipozidi kumhoji, alijiinua akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao.”
Wakati Mafarisayo walipomshitaki yule mwanamke mzinzi mbele ya Yesu, aliinama chini na kutumia kidole chake kwa kuandika ndani ya udongo. Ila hatujui aliyoandika - pengine aliandika amri mpya kwa neno moja - upendo.
Hao wazee walishindwa kuona sababu ya kusitasita kwake, hawakutambua kwamba hakimu wa ulimwengu anayo subira naye alikusudia kuchoma dhamiri zao. Walifikiri kwamba walimshika ndani ya nyavu zao. – Yesu akainuka na kuwatazama kwa huzini; ilikuwa ni mtazamo tukufu, na neno lake ilikuwa kweli, na halikuweza kukataliwa. Akasema kama katika hatua ya kuhukumu, “Yeye asiye na dhambi kati yenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.” Yesu hakubadilisha tamko lolote la amri. Bali aliikamilisha. Yule mama mzinzi alistahili kifo; hilo Yesu alikubali.
Kwa kutenda kwake Yesu aliwahukumu “wacha Mungu” sawa na wazinzi. Hivyo aliwachokoza ili wathibitishe hali yao kuwa bila dhambi kwa kutupia jiwe la kwanza. Kwa tendo hilo alirarua kifuniko cha nyuso zao, mwigo wa “wacha Mungu” kutoka katika nyuso zao. Hakuna mtu asiye na dhambi. Wote tu wadhaifu, tukijaribiwa na kukosa kushinda mabaya. Mbele ya Mungu hakuna tofauti kati ya wahalifu na wachaji wanafiki. Maana wote tumepotea na kupevuka. Yeyote aliyevuka amri moja tu, amevunja sheria yote, na hivyo kustahili kupotea milele.
Wazee na wanasheria walikuwa wanatoa sadaka za wanyama hekaluni ili kutakaswa na dhambi zao, kwa kufanya hivyo walikiri kwamba nao ni wenye dhambi. Basi maneno ya Yesu yaligusa dhamiri zao. Walikuwa wakitamani kumfunga huyu Mnazareti, lakini ilikuwa ni yeye aliye fichua ukorofi wao na kuwahukumu. Wakati huo huo yeye alitimiza sheria kikamilifu. Washitaki wakainamisha vichwa vyao, wakijisikia kuwa kwenye eneo la kuwepo kwa Mwana wa Mungu, wakitishwa na utakatifu wake. Basi, wazee na waliowapendelea wakajiendea, uwanja ukaachwa tupu, - Yesu akabakia peke yake.
YOHANA 8:9b-11
“ …na yule mwanamke akasimama katikati. Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke,wako wapi wale washitaki wako? Je, hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako;wala usitende dhambi tena“.
Yule mwanamke alisimama pale akitetemeka. Yesu akamwangalia kwa huruma na kwa uadilifu akimwuliza, „Wako wapi washitaki wako? Hakuna aliyebaki kuamua na kukulaumu?“ Alijisikia kwamba Yesu, Mtakatifu hatamwadhibu, iwapo yeye peke yake ndiye aliyekuwa na haki ya kumhukumu.
Yesu huwa awapenda wenye dhambi; yeye alikuja kuwatafuta waliopotea. Hakuweza kumwadhibu yule mama mwenye dhambi, bali kumwonyesha rehema zake. Maana alijitwisha makosa yetu yote, tayari kuifia ulimwengu. Yeye mwenyewe alibeba na adhabu ya mwanamke huyu.
Hivyo anakutolea na wewe msamaha kabisa, kwa vile amekufia na wewe. Amini tu upendo wake, ili aweze kukuweka huru na hukumu. Na umkubali na Roho yake mwenye kusamehe, ili na wewe usije ukawahukumu wengine. Daima usisahau kwamba wewe nawe ni mwenye dhambi, wala hujawa mtu bora kuliko wengine. Ikiwa jirani yako amefanya uzinzi, je, wewe huna uchafu na wewe? Kama mwingine ameiba, wewe nawe ni mwaminifu katika yote? Usihukumu, ili wewe nawe usije ukahukumiwa. Kwa kipimo kile unachotumia kupima matendo ya mtu, wewe nawe utapimiwa. Kwa nini unaona sana kibanzi katika jicho la ndugu yako, na hujali boriti ndani ya jicho lako?
Yesu alimwomba yule mama asije akarudia kutenda dhambi kuanzia hapo aliposamehewa. Amri ya Mungu kwetu kuwa safi ni wazi na hakika, wala isilegezwe. Alimwongoza yule mwanamke aliyetamani upendo, aje akamrudie Mungu, na azikiri dhambi zake. Na hivyo apokee nguvu ya Roho Mtakatifu kutoka kwa damu ya Mwana-Kondoo. Hakika Yesu alihitaji jambo kwake ambalo haliwezekani kwake, lakini alimpatia na nguvu ya kushinda ipatikanayo kwa wenye mioyo iliyovunjika kwa kujuta; ili naye aishi katika utakatifu. – Hivyo anahitaji na kwako uache tu dhambi mbeleni; yu tayari kusikiliza maungamo ya moyo wako.
SALA: Ee Bwana Yesu, mimi nasikia haya mbele ya uso wako, maana mimi si bora kuliko yule mama mzinzi. Nisamehe na mimi kwa ajili ya kuwahukumu au kuwaumiza wengine. Unisafishe na machafu yote. - Nakushukuru mno kwa kunirehemu mimi. Ninakutukuza kwa ajili ya uvumilivu na rehema zako kwangu. Nisaidie nisitende dhambi tena kuanzia leo. Imarisha uamuzi wangu huo na unihakikishe katika usafi wako. Uniongoze kwenye maisha ya utakatifu.
SAWLI:
- Kwa nini hao washitaki wa yule mwanamke mzinzi walitoka usoni pa Yesu?