Previous Lesson -- Next Lesson
4. Yesu anawapa watu chaguo: “Kubali au kataa!” (Yohana 6:22-59)
YOHANA 6:22-25
22 „Siku ya pili yake mkutano waliosimama ng’ambo ya bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja, tena ya kuwa Yesu hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake walikwenda peke yao. 23 (Walakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia mpaka karibu na mahali pale walipokula mikate, wakati Bwana aliposhukuru). 24 Basi mkutano walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu. 25 Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa?“
Watu walipotambua kwamba Yesu hakuondoka akitumia mashua, walishangaa kwamba alifaulu kuwaepuka. Alikuwa ameondoka usiku sirini.
Basi maelfu wakarudi Kapernaumu, wakitegemea habari ya mikate iliyotolewa kwa wingi bure. Watu walishangaa na kuwa na wivu, wakitamani kushiriki katika ukarimu huo. Umati wakakimbia kumtafuta Yesu manyumbani kwa wanafunzi wake, hadi wakampata akiwa kati yao. Wakaanza kutambua ukweli wa sharti ya Ukristo: „Watu wawili au watatu wakiwa wamekutanika katika jina langu, mimi niko kati yao“.
Wale waliotamani mno kuona ishara, sasa wakatambua mwujiza mwingine mpya. Wakauliza: „Lini na namna gani ulifika hapa?“ Yesu hakujibu swali hilo. Badala yake kwa kujali hali yao ya kiroho, aliweka wazi maana ya imani, akitamani kuvuta wale wenye nia ya kweli kati ya hao waliochangamka, watambue upendo wake, akiweka wazi hila na kule kukataa kwa adui zake. Yesu hakupenda hali ya uvuguvugu, akaanza kutenganisha kundi la waumini kutoka katika umati wa watu waliojionyesha kuwa wa kidini kwa nje tu.
YOHANA 6:26-27
26 „Yesu akawajibu, akasema, Amin,amin, nawaambieni, ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27 Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani Mungu.“
Kwa wazi kabisa Yesu aliwaonya watu waliokusanyika: Hamnipendi wala hamnitafuti kwa sababu yangu, wala hamtafakari mawazo yaliyo sawa kumhusu Mungu. Bali mnafikiria matumbo yenu tu na mikate. Hamjaelewa ishara: kusudi langu haikuwa kushibisha njaa yenu tu na mkate, lakini ilikuwa kuwasaidia mpate kunifahamu na nguvu zangu. Mnatafuta zawadi na huku hamjali mtoaji. Mnajadiliana mambo ya kidunia, wala hamwamini kwamba mimi ndimi Mungu.
Msifanye kazi kutwa kwa ajili ya chakula na vinywaji tu, bali mchukue nafasi ya kuwaza habari ya nguvu ya Mungu. Msiwe kama wanyama tu wanaoishi kwa ajili ya kula tu, bali mmkaribie Mungu aliye Roho. Yeye yu tayari kuwafanya mwe washiriki katika uzima wake wa milele.
Zaidi ya hapo Yesu akaeleza: Nimekuja ulimwenguni, niwapatie zawadi kuu ya Mungu. Mimi siye mtu wa kawaida tu mwenye mwili na damu. Bali nabeba zawadi ya Mungu ndani yangu mpate kubarikiwa naye. Mungu amenitia muhuri wa Roho yake Mtakatifu, ili kuwashirikisha maisha ya kiroho na kuwahuisha kwa nguvu za mbinguni.
Kwa tamko hilo Yesu aliwatangazia ile siri kuu, kwamba Mungu awashughulikia wote, awalisha wanadamu wote na kuwapenda. Yeye siye Mungu mwenye hasira anayesisitiza kutimiza sheria zake zote kabla ya kuwabariki. Yeye huwabariki wenye haki na waovu, na kufanya jua lake kuangaza juu ya wote bila kutofautisha, hata kwa wasiomwamini kabisa na wanaokufuru. Mungu ni pendo, na Kristo alijibidiisha kwa ajili ya umati wa watu wasifikirie ya kimwili tu, bali awarudishe kumtegemea Mungu aliye Baba wa wote. Hivyo alisisitiza kwamba ufalme wake sio wa dunia hii, wenye msingi wa chakula, utajiri na utawala, bali ni ufalme wa kiroho unaofurika uhai kweli kweli, akiwajia katika nafsi ya Kristo, anayewapa Roho wote wanaomwomba.
YOHANA 6:28-29
28 “Basi wakamwambia, Tufanyeje, ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? 29 Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.”
Umati wa watu walishindwa kuelewa wazi mafundisho ya Yesu, ila walitambua kwamba, alitaka kuwatolea zawadi kuu kutoka kwa Mungu, na wote walitamani kupokea uzima huu wa milele. Hata walikuwa tayari kufanya kitu kwa ajili ya zawadi hiyo. Wakawa tayari kutimiza amri, kutoa sadaka, kufunga, kusali na kwenda kuhiji Yerusalemu - ili kuipata kama mshahara kwa matendo yao. Basi, hapo tunaona upofu wao. Wote walikuwa ni watu wa sheria, wakiwa na shauku ya kupatiwa wokovu kwa bidii zao wenyewe. Hawakutambua kwamba hilo haliwezekani, kwa vile walikuwa na hatia na wenye kupotea. Kwa kiburi walifikiri kutenda kazi za Mungu, wakidhani kwamba wanao ubora wa kutosha na nguvu ya kutenda hayo. Mwanadamu ni kipofu kiasi cha kutokuona hali halisi ya moyo wake, bali anajihisia kuwa kama mungu mdodo, akitazamia kwamba Mungu anaridhika naye.
Yesu aliwaonyesha kwamba, haihitajiki kitu kwao kama kutimiza wajibu fulani au matendo. Waliitwa tu kumwamini yeye mwenyewe aliyekuwa kati yao. Mungu hahitaji bidii au nguvu zetu, bali anapenda tumwelekee Yesu na kumtegemea yeye tu. Maneno hayo yalikuwa ni kikwazo kwa watu; na hivyo mgawanyiko ikaanza kati ya Yesu na umati wa watu. Zaidi aliwaeleza kwamba kazi ya Mungu ilikuwa waamini ndani yake. “Mkifungua roho zenu kwa Roho Mtakatifu, mtafahamu uweza wangu, shabaha na upendo wangu. Ndipo mtatambua kwamba mimi si nabii tu, bali ni Mwumbaji, Mwana aliyetumwa na Baba kwenu. Nanyi mtabadilika kutoka kwa mawazo yenu ya kidunia na kuwa watoto wa Mungu”.
Kumwamini Yesu ni kushikamana naye na kumruhusu kutenda kazi maishani mwenu, ni kukubali uongozi wake na kupokea uzima wa milele kwa njia ya enzi yake. Imani ni kufungamana na Yesu wakati huu na hata milele. Hii ni kazi ya Mungu, anayewaambatisha waumini kwa Mwana wake, ili dhambi ianze kupotea maishani mwao na waendelee kudumu pamoja naye daima.
YOHANA 6:30-33
30 “Wakamwambia, Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani? 31 Baba zetu walilia mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale. 32 Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. 33 Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
Sisitizo la Yesu kwa kujitoa kwake kabisa, kwa watu hao ilikuja kama mstusho mkali. Walijisikia kwamba Yesu alitazamia jambo kwao ambalo lingeweza kutolewa kwake Mungu tu. Hivyo wakamtaka atende jambo la kuthibitisha dai lake. Kana kwamba wangesema: “Utupe thibitisho la uungu wako; Musa aliwapa mkate ( mana ) kule jangwani, kila siku kwa upya. Lakini wewe ulitupa mkate mara moja tu. Musa alitoa chakula kwa mamia ya maelfu, wewe ulitoa kwa elfu tano tu. Tuonyeshe mwujiza mwingine, ndipo tutakuamini.” Hayo ni ugonjwa wa kibinadamu. Mwanadamu hukataa kuridhika na upendo wa Yesu bila masharti, bali anasisitiza kupata thibitisho kwanza. Lakini Yesu asema, “Heri wale wanaoamini bila kuona. Hao ndiyo wale wanaoniheshimu kwa tumaini lao.” Yesu ndiye kiongozi mkuu kabisa, awaongozaye wasikilizaji wake hatua kwa hatua kutoka kwa mawazo ya kisheria na wafikie imani wazi wazi ndani yake tu. Aliwaweka huru watu kutoka kwa tamaa ya chakula, akawamulikia maisha yao; yeye mwenyewe ndiye zawadi ile kuu ya Mungu kwao.
Kama sehemu ya dhihirisho hilo la hatua kwa hatua, Yesu naye aliwaweka huru kutoka kwa mawazo yao ya kinyume juu ya maana ya maandiko ya Agano la Kale, kwamba ni Musa aliyewapa ile mana. Ilikuwa ni Mungu ambaye kwa kweli ndiye aliyewapa, yeye mtoaji wa ukarimu wote. Aliwafikisha mahali pa kutulia na kutafakari kwanza, ili watambue kwamba Mungu anawatolea mkate bora, na chakula cha mbinguni kisichoharibika daima. Kwa kusikiliza kwa makini wangetambua ya kwamba Yesu alijitangaza kuwa ndiye Mwana wa Mungu, maana alimwita Mungu kuwa Baba yake. Hata hivyo, wengi wao waliendelea kufikiria chakula cha kawaida tu, hata kile kilichotoka mbinguni kwa mkono wa Musa.
Yesu aliinua kule kuelewa kwao kufikia ufahamu kwamba, mkate kutoka kwa Mungu siyo wa kumeza hadi tumboni, bali ni nafsi ya Kristo anayeshibisha njaa ya watu ya kutamani ukweli na uhai tele. Yule Mtoaji wa hayo ameshuka toka mbinguni, akibeba baraka za Mungu na enzi yote. Mkate wa Mungu sio wa kawaida ya asili na wa kuharibika, bali ni ya kiroho naya kudumu. Haikutokea kutoka chini ardhini jinsi ilivyokuwa na ile mana, bali ilishuka kutoka juu kwa Mungu, tena ya kutosha kwa binadamu wote tena kwa wakati wote. Wala haikufungwa kwa uzao wa Ibrahimu tu. Mungu Baba awashughulikia wote ulimwenguni kote.
SALA: Bwana Yesu, utuzuie na vitendo vya binafsi tu. Utuumbie ndani yetu imani nyenyekevu, tuweze kukusikiliza unalotutaka tufanye. Na ufanye kazi ndani yetu kwa uwezo wako. Utuhimize tufikie umoja kamili na wewe. Ridhisha njaa za mioyo yetu kwa kuwepo kwako ndani yetu. Ututayarishe kwa kushiriki uzima wa milele. Tunakushukuru Baba, kwa kuja kwako kwetu, ukituhakikishia uwezo na baraka.
SWALI:
- Jinsi gani Yesu aliwaongoza watu watoke kwenye hamu ya mkate, na wapate imani ndani yake?