Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- John - 041 (Jesus withdraws from the clamor for his crowning; Jesus comes to his disciples in distress)
This page in: -- Albanian -- Arabic -- Armenian -- Bengali -- Burmese -- Cebuano -- Chinese -- Dioula? -- English -- Farsi? -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Kyrgyz -- Malayalam -- Peul -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Thai -- Turkish -- Twi -- Urdu -- Uyghur? -- Uzbek -- Vietnamese -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

YOHANA - Nuru inaangaza gizani
Somo la Injili ya Kristo kufuatana na Mtume Yohana
SEHEMU YA 2 - Sehemu ya pili: Nuru inang’aa gizani (Yohana 5:1 - 11:54)
B - Yesu ni chakula cha (mkate wa) uzima (Yohana 6:1-71)

2. Yesu anajiondolea kwenye kelele ya kutaka kumfanya awe mfalme (Yohana 6:14-15)


YOHANA 6:14-15
14 „Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. 15 Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.“

Yesu alikuja ulimwenguni ili kushinda juu ya binadamu. Baada ya kuwalisha elfu tano, watu wakamzungukia kwa shauku. Wakapiga makofi na kurukaruka kwa kumpatia heshima kama mfalme. Walitambua kwamba huyu Mgalilaya ni mtu wa Mungu. Sauti ya Mungu ilisema kupitia kwake, na enzi ya Aliye Juu ikaonekana ndani yake. Enzi za asili zilimtii. Alikuwa amewapa mkate jinsi Musa alivyowafanyia jangwani. Bila shaka ndiye Nabii aliyeahidiwa, ili kuongoza taifa lililotawanyika wafikie kwenye ukweli (Kumb. 18:15). Pia walifikiri kwamba, kama Yesu atakuwa mfalme wao, hawatahitaji tena kufanya kazi wala kuchoka hapo mbeleni. „Tutakuwa na muda wa kusoma na kuchunguza maandiko na kuomba, naye atatupatia chakula bure. Mfalme wa namna hii pia atakuwa na nguvu ya kutosha kushinda majeshi ya vita ya Waroma. Pengine atashusha na moto toka mbinguni ili kuwameza. Basi tumwekee taji na kumtangaza kuwa mfalme. Wote kwa umoja wakamwelekea ili kumbeba mabegani. Wamwimarishe kwa kutegemea kwamba atawategemeza na mahitaji yao yote.

Msimamo wa Yesu ilikuwa nini katika mkupuo huo? Je, alifurahia kuinuliwa kwa maendeleo yake na kuwashukuru kwa kumtegemea yeye? Je, alishindwa katika jaribu hilo na kujenga ufalme wake kwa msaada wa wasioamini? Au alikemea mipango yao? Hapana, hakusema neno, akajiendea kwenye upweke wa jangwani. Hakutaka kuegemea watu, aliridhika na Mungu kusimamiwa na yeye tu. Yesu alielewa hali ya hao watu waliochangamka, wakilewa na shangilio la mvuto wa wengi, bila nafasi ya kusikiliza mwongozo wake. Walikuwa na umoja wa kisiasa juu ya wazo moja tu.

Yesu hakuwa na hamu ya kujenga ufalme wa kidunia, bali alitaka kumwongoza mmoja mmoja ajitambue katika ungamo kweli na azaliwe kwa upya. Maana hakuna awezaye kuingia ufalme wa mbinguni, isipokuwa kwa kuzaliwa mara ya pili. Umati wa watu walishindwa kuelewa shabaha ya miujiza na matendo yake ya pekee. Walifikiria mkate wa kidunia; yeye alisema habari ya Roho Mtakatifu awezaye kuridhisha njaa ya moyoni. Wao walimaanisha ukuu wa kidunia na utukufu wa kupotea; yeye alichagua msalaba kuwa msingi wa ufalme wake. - Bila ungamo na kuzaliwa mara ya pili hutaweza hata wewe kufurahia karibisho la Kristo.

Yesu hakuhitaji kupewa heshima kubwa kutoka kwa umati wa watu. Hakutaka kupokea utukufu kutoka kwa watu, bali daima alisikiliza sauti ya babaye. Alifunga moyo wake kwa majaribu ya Shetani. Hivyo alijiondokea kimya kimya kwa nafasi ya kuomba, amshukuru Baba na kumsihi, ili macho ya hao vipofu yafumbuliwe kwa msaada wa Roho. Hakuweza kukubali kufanywa mfalme kwa watu, akifahamu kwamba, watamtukuza kwa „Hosana“siku moja, na siku nyingine kulia „Msulibishe!“. – Kristo ajua mioyo yetu, wala hapotei kwa hilo.


3. Yesu anawafikia wanafunzi wake wakiwa taabuni (Yohana 6:16-21 )


YOHANA 6:16-21
16 „Hata ilipokuwa jioni wanafunzi wake wakatelemka baharini, 17 wakapanda chomboni, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. 18 Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu. 19 Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa. 20 Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope. 21 Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia nchi waliyokuwa wakiiendea.“

Ilipofika jioni, wanafunzi wake walitelemka ziwani, wakapanda chombo na kuanza kuvuka ziwa kuelekea Kapernaumu. Tayari ikawa giza, naye Yesu hajaonekana. Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ukaanza kuvuma. Walipokuwa wamevuta makasia kama maili tatu au nne, wakamwona Yesu akitembea juu ya maji na kuwakaribia hapo chomboni. Waliogopa kweli, lakini aliwatuliza kwa kusema: Ni mimi, kwa nini kuogopa? Basi wakafurahi kumpokea chomboni, na ajabu, mara hii chombo chao kikafikia nchi kavu walikotaka kufikia.

Wakati Yesu alipokuwa faraghani kwenye milima ya Golan, aliwaona wanafunzi wake wakiwa mbali wakihangaika na mvumo wa upepo ziwani. Kwa vile usiku ulikaribia, aliwaendea kwa miguu juu ya mawimbi ya maji. Hakuwaacha peke yao hatarini, ingawa walimdhania kuwa pepo wa njozi na kuogopa. Wavuvi mara kwa mara wanafikiria kwamba, wanaona roho ziwani, kwa vile wanatumia muda mwingi usiku juu ya uso wa maji. Yesu akawajia na kusema nao wazi na kwa upole, „Ni mimi“. Hapo baadaye tamko hilo likawa ni msingi wa imani ya Mitume. - Kwenye Agano la Kale tunakuta neno linalofanana: „Mimi ndimi“, wakati wa kuonyesha kwamba Bwana yu pamoja na waumini wake. - Hapo wanafunzi wakatambua kwamba Yesu alikuwa na uwezo wote juu ya nguvu za asili: Mkate ukawa nyingi sana mkononi mwake - mawimbi ya maji yakambeba kwa urahisi - mvumo wa upepo ukakomeshwa kwa agizo lake. Kwa kutambua hayo yote wakazidi kwenye hofu ya mshangao. Basi akawaomba, wasiogope kabisa. Agizo hilo, „Msiogope“, ni kwa ajili ya wafuasi wake wakati wowote; nalo latokea mara 365 ndani ya Biblia, mara moja kwa kila siku mwaka mzima. Kutegemea ukaribu wa Kristo kunashinda hofu zetu. Si kitu hali yako ni yenye shida gani, au tatizo la namna gani likuhangaishe, Yesu asema: „Ni mimi, usiogope“.

Wanafunzi wake walipomtambua Yesu, wakashangaa, wakamkaribisha ndani ya chombo. Ila hapo hapo wakawa wamefikia pwani. Hilo ilikuwa ni sehemu ya tatu ya mwujiza kwa siku hiyo moja. - Yesu ndiye Bwana wa kila mahali na wa wakati wote; aweza kuongoza chombo cha Kanisa kwenye misukosuko na mawimbi ya taabu ya aina zote na kuifikisha salama. Anawapenda wanafunzi wake na kuwakaribia; analohitaji tu ni kutegemewa nao kikamilifu. Huwa anaimarisha tumaini lao ndani yake, hata wakiwa katikati ya giza au masumbufu, ili hofu liondolewe, nao waweze kushikamana naye daima.

SWALI:

  1. Kwa sababu gani Yesu alikataa kufanywa Mfalme na umati wa watu?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on October 07, 2013, at 11:57 AM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)