Previous Lesson -- Next Lesson
1. Kuwalisha watu elfu tano (Yohana 6:1-13)
Kule Yerusalemu Yesu alikuwa amefunua kwamba yeye ni Mungu kwenye siku ya Sabato kwa njia ya kuponya, akionyesha ufa mkubwa kati ya upendo wa Mungu na mawazo batili ya watu wa sheria. Walifikia uamuzi wa kumwondoa kwa chuki. Roho Mtakatifu alimwongoza Yesu aende kaskazini hadi Galilaya, ambapo kati yake na wapingaji wake ule ufa wa kukata shauri ulitaka kufikia kilele. Hata hivyo umati mkubwa hapo kaskazini bado walimfuata kote alikoenda.
YOHANA 6:1-4
1 “Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng’ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. 2 Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. 3 Naye Yesu alikwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. 4 Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu.”
Tangu Kristo alipowakemea watu wa sheria kule Yerusalemu, walifanya shauri dhidi yake na kumchunguza. Lakini saa yake ilikuwa bado haijaja. Basi akajiondokea kwenye eneo la mamlaka ya baraza kuu (Sanhedrin) akienda Galilaya. Tusomavyo katika Injili tatu zinazotangulia, alikuwa ametenda miujiza mingi kule. Ukatokea ghasia nyingi iliposikika kwamba amefika, lakini Yesu hakusituka wala kusumbuka. Alifahamu kwamba nia ya hila aliyoikuta kwenye mji mkuu itafika chini chini hadi vijijini na atatishwa hata pale. Hivyo akaendelea hadi eneo la Golan, mashariki ya mto Yordani, ili awe peke yake na wanafunzi wake. Hata hivyo, umati wa watu wakamfuata, wakiwa na njaa ya neno lake, wakingojea kushuhudia mwujiza wake. Mwaka ule Yesu hakurudia kwenda Yerusalemu kwa Pasaka, kwa sababu saa ya kufa kwake ilikuwa bado. Alisherekea sikukuu hii pamoja na umati wa watu karibu naye badala ya Pasaka; kwa njia hiyo alielekeza kwa sherehe kuu ya mbinguni, ambapo Mwokozi atakapounganika na watakatifu wake katika furaha kuu.
YOHANA 6:5-13
5 “Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? 6 Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. 7 Filipo akajibu, Mikate ya dianri mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. 8 Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, 9 Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? 10 Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapate elfu tano jumla yao. 11 Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. 12 Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. 13 Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula.”
Yesu alipoona umati wa watu wengi waliomjia, aliinua macho yake juu kwa babaye mbinguni, akimpa heshima na utukufu, akimkabidhi Mungu utunzaji wa wenye njaa. Kwa hilo mwujiza ukaanza. Baba akampatia Mwana shughuli ya kufunua mioyo yao.
Kwanza Yesu alijaribu wanafunzi, aone kama imani yao iliendelea kukua, au kama bado walifungwa na mawazo ya vitu vinavyoonekana tu na kufikiria kawaida ya kidunia tu. Ndipo akamwuliza Filipo kuhusu mahali pa kupatikana mkate. Sisi tungefikiria kiwanda cha kutengenza mikate. Yesu alimfikiria Baba yake. Sisi tunawaza habari ya shida ya hela na gharama ya maisha. Yesu aliwaza juu ya Msaidizi Mtukufu. Basi hapo hapo Filipo alianza kukadiria fedha itakayohitajika, badala ya kuelekea kwenye imani. Yeyote aangaliaye fedha tu, atashindwa kuona uwezekano mwingine tukufu. Makadirio ya wanafunzi kiakili yalikuwa sawa: Hapakuwa na kiwanda cha mikate karibu, wala kinu ya kusaga unga, wala muda wa kuoka mikate. Lakini watu wengi walikuwapo, wenye njaa baada ya saa nyingi za kusikiliza hotuba.
Mara moja Roho akamgusa Andrea, aliyemwona kijana mwenye mikate mitano na samaki wawili. Akamwita yule kijana, “Utupatie ulicho nacho cha mkate na samaki”. Andrea alikuwa na mashaka yake, akifahamu kwamba jumla ya chakula hiki hakitoshi cho chote. Lakini Yesu aliwaongoza wanafunzi wake wakiri kukosa kwao. Hawakujua kabisa la kufanya, wala shabaha ya Mungu, wala alilokusudia kufanya Yesu mwenyewe.
Yesu aliagiza wanafunzi wake wawapange wote waliokuwepo, wakawaketisha watu kama kwa sherehe kubwa.
Majani mabichi yalifunika mahali pale kama ishara ya imani iliyoanza kuchipuka kwenye umati wa watu. Wanaume elfu tano pamoja na wake zao na watoto kweli ni nambari kubwa. Wengi wao walikuwa bado hawajamwona Yesu kabla ya hapo, wala kazi zake. Lakini walikaa chini na kutulia kwa neno lake.
Kwa taratibu Yesu alichukua ile mikate akaazimu kufafanua uwezo wake wa kuumba katika tukio hilo. Aliweka mikate hii mbele ya Babaye, akimshukuru kwa hii michache. Aliamini kwamba Mungu atabariki uchache huo na kuukuza kwa wingi, hata kufurisha. Kule kushukuru kwa ajili ya hii michache pamoja na kumheshimu Baba yake yalikuwa siri ya mwujiza huu. - Wewe je, unakubali kwa shukrani kile kidogo ambacho Mungu anakupatia, au unakichukua na kunung’unika? Je, unashiriki kile kidogo na rafiki zako? Yesu alikuwa anawafikiria wengine kuliko mwenyewe; upendo wa Mungu ulikaa daima kwa wingi ndani yake. Alimheshimu Baba na kugawa baraka za Mungu kwa wote.
Mwujiza huu unaoelezwa ndani ya Injili zote nne inasimuliwa bila tangazo la tarumbeta. Inaelekea kuwa wale wachache tu walioketi karibu na Kristo ndiyo walioshuhudia: wakashangaa kuona alipomega mikate hii michache, mingine ikatokea, na kule kuongezeka hakukuwa na mwisho. Waliendelea kugawa, kurudi na kwenda tena kuwagawia wote hadi wa mwisho. Kila mmoja akichukua alichohitaji. Na hii ndiyo alama ya rehema. Mungu hutoa radhi, pia na Roho yake bila kipimo. Chukua unachohitaji; amini kwa kiasi unachoweza. Na ugawe baraka hizo na kwa wengine. Wabariki jinsi wewe mwenyewe ulivyobarikiwa, na hivyo utakuwa chemchemi ya baraka kwa wengine.
Kule Kana Yesu aligeuza maji kuwa divai, na kwenye milima ya Golan aligeuza mikate mitano kuwa nyingi ya kutosha kwa watu elfu tano. Na kinachoshangaza ni kwamba, mwisho wa kuwalisha wote iliyosalia ilikuwa nyingi kuliko kiasi cha kwanza mwanzoni! Hesabu ya vikapu vilivyojazwa na mabaki vilikuwa kumi na viwili. Yesu akaagiza kwamba kisipotee chochote. - Siku hizi kuna aibu kubwa kwamba watu hutupa mabaki yao ya chakula mezani kwenye mapipa ya takataka, iwapo wanaelewa kwamba, kila saa maelfu wanakufa kwa njaa. Usitupe baraka unazojaliwa kwa kutokujali. Bali kusanya vipande vya rehema kwa kazi njema. Wewe utapokea zaidi ya uwezo wako wa kushika kutoka kwa ukarimu wa Mungu.
Jaribu kutambua mshangao wa yule kijana mdogo, wakati Yesu alipochukua ile mikate mkononi mwake, akashuhudia kwa macho yake jinsi ilivyoongezeka kwa ajabu. Macho yake yakafumbuliwa kwa mshangao mkuu. Wala asingeweza kusahau mwujiza huo.
SALA: Asante sana, Bwana Yesu, kwa ajili ya uvumilivu na upendo wako. Tusamehe upungufu wetu wa imani. Tufundishe, tukuelekee wewe kwa shida zetu, wala tusitegemee nafasi zetu, bali tutegemee uwezo wako tu. Twakushukuru kwa utajiri wa kiroho uliotujalia, na hata kwa yale machache tuliyo nayo. Utatubariki hasa kwenye siku za vitu vyetu vichache, na utusaidie tusije tukapoteze chochote au kutokutumia vipawa vyetu.
SWALI:
- Siri ya kuwalisha watu elfu tano ilikuwa ni nini?