Previous Lesson -- Next Lesson
4. Shuhuda nne juu ya Uungu wa Kristo (Yohana 5:31-40)
YOHANA 5:41-44
41 “Mimi sipokei utukufu kwa wanadamu. 42 Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. 43 Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo. 44 Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti?”
Yesu alitikisa silaha za adui zake, akawaonyesha hali halisi ya mioyo yao na ajali yao ya mbeleni. Alidokeza kwa makusudi yao maovu, kiini cha tabia yao ya upotovu.
Yeye hakuwa na haja ya kupongezwa na watu au viongozi wao, maana alikuwa na uhakika juu ya ujumbe wake. Thibitisho hilo haikuwa na msingi katika matokeo ya wazi ya huduma yake. Kama alipewa heshima, aliipitisha kwa Babaye. Alifundisha kusali kwanza kwa Baba, wala si kwake mwenyewe, alifundisha Ukristo kwa kutamka: “Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje. Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.” Yesu alijikana mwenyewe katika kutokukusudia kutafuta heshima au utukufu. Utukufu wa babaye ilikuwa ndiyo shabaha yake. Wivu kwa haki za Mungu zilimmeza. Upendo wa Mungu ndiyo madhumuni katika uumbaji, ukombozi na katika ukamilisho. Huu ni kiini cha msingi wa Utatu Utakatifu. Tena ni ukamilisho wa sheria au torati, na dhamana ya ukamilifu huo inathibitisha upendo hasa. Yeye aliyo nayo upendo huo, haishi kwa ajili yake mwenyewe, wala hajiheshimu mwenyewe, bali anawaheshimu wengine, akiwahudumia kwa kujinyima mwenyewe. Anatoa yote aliyo nayo kwa maskini. Upendo haushindwi wakati wo wote.
Hakuna mtu ampendaye Mungu kwa mapenzi yake mwenyewe, ila yule anayeumizwa na uchafu wa dhambi zake, akiungama na kuamini upendo wa Mungu ndani ya Kristo. Atakiri kwamba upendo wa Mungu umemiminwa ndani ya mioyo yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu tuliopewa, jinsi alivyofanya Paulo. Upendo huo unajionyesha katika kujitolea kabisa, kwa unyenyekevu na uvumilivu. Yeyote anayefungua moyo wake kwa Roho wa Mungu atapenda huo Utatu Utakatifu, pia na watu wote. Lakini anayejisifu mwenyewe, akifikiri yeye ni mwema, yeye si wa kutubu kweli, bali yu kinyume cha Roho wa Mungu. Kwa ndani ni wa kujipenda tu. Hahitaji kufanywa upya , wala hatambui haja yake kuwa na mwokozi, bali anaendelea kufanya ngumu moyo wake. Kristo hakuja duniani katika jina la uungu geni usiojulikana, bali katika jina la Baba, ili afunue upendo wa Mungu na rehema zake. Wote wanaomkataa Kristo, wanathibitisha kwamba akili zao zimefungwa kwa upendo wa Mungu. Wanapenda giza kuliko nuru, na hivyo wanawachukia wale waliozaliwa na nuru.
Kristo aliwajulisha adui zake kwamba, atatokea yule aliye kinyume cha Kristo (Anti-Christ), atakayewakusanya wote wanaojipenda wenyewe na kujisifu, ili awaongoze kwenye maasi dhidi ya upendo wa Mungu. Yeye atatenda miujiza na kumwiga Kristo.
Wengi hawawezi kuamini, wakipendelea kusita-sita katika nia zao kuliko kuungama kweli. Wanajifikiria kuwa wema wenyewe, wenye nguvu na akili. Hawatetemeki mbele za Mtakatifu, na hawatambui kwamba yeye pekee ndiye mwema. Kujifikiria kuwa na haki mwenyewe ndiyo sababu ya kutokuamini, na kiburi ndiyo alama ya shabaha hiyo bovu.
Yeye anayemfahamu Mungu na roho yake mwenyewe, anavunjika mbele yake na kuungama makosa yake, akikataa sifa na heshima yoyote, lakini akitoa utukufu kwa Baba na Mwana daima. Anatukuza neema inayookoa. Anaamini kwamba sote tu wenye dhambi tuliosamehewa, tuliowekwa huru na majivuno katika kuishi kwetu. Tunajua sisi tu wakina nani, tena na Mungu ni nani. Upendo unaeleza ukweli kwa rafiki; ila mwenye kiburi atajidanganya mwenyewe na wengine, akienda mbali na uongozi wa Roho wa Mungu anayetunyenyekeza.
YOHANA 5:45-47
45 “Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. 46 Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mgeniamini mimi, kwa sababu yeye aliandika habari zangu. 47 Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini wapi maneno yangu?”
Kristo aliendelea kupooza kiburi cha hao wasimamizi wa sheria akisema, “Mimi siye wa kuwashitaki mbele za Mungu ili kuwahukumu. Musa mwenyewe atatoa mashitaka. Ndiye aliyewapa amri za agano, na hizo zitawahukumu. Ninyi mmeshindwa kutambua upendo, na kutamani kuniua katika jina la sheria. Kwa kwenda mbali na Mungu mnatanga-tanga gizani. Mimi nimemponya mgonjwa siku ya Sabato, nanyi hamkupenda kazi hii ya Mungu; bali mnanichukia, mimi niliye upendo wa Mungu mwilini. Mnakataa kuamini kwamba hizo ni kazi za Masihi: Roho zenu ni za kuasi na kukwaruza. Mungu aliwapa sheria ili mpate kuishi, wala sio kufa. Ikiwa mgekuwa wa kutubu, mgetamani kumpata mwokozi. Torati na manabii ni matangulizi kwa ajili ya Yule Anayekuja. Ninyi mmepindua makusudi ya sheria , na kuruhusu mapenzi yenu kuhukumu amri za Mungu. Mnashindwa kuelewa unabii. Roho zenu mbaya zinawazuia msitambue ukweli. Mtaendelea kwa hali ya kutokutambua na uziwi, mkizuia Roho wa Mungu. Kwa sababu ya ukaidi wenu mnakataa kuamini Neno la Uzima.”
SWALI:
- Kwa nini Yesu hakupokea utukufu kwa ajili yake mwenyewe, jinsi ambao watu wengine wangalifanya?
NAMBA - 2
Mpendwa Msomaji, ututumie majibu yaliyo sawa kwa maswali 17 kati ya hizo 19. Ndipo tutakutumia mafuatano ya mfululizo wa masomo haya.
Maswali:
- Kwa nini Yesu alitembelea Hekalu na kuwafukuza nje wafanyi biashara?
- Ni nini tofauti kati ya uchaji wa Mungu wa Nikodemo na malengo yake Kristo?
- Ni nini dalili za kuzaliwa mara ya pili ndani ya waumini?
- Ni jinsi gani Kristo anafanana na nyoka ile ya shaba jangwani?
- Kwa nini waumini wa Kristo hawatatokea kwenye hukumu?
- Kwa maana gani Kristo anafananishwa na Bwana Arusi?
- Jinsi gani tunapokea uzima wa milele?
- Jambo gani ni zawadi anayotupatia Yesu? Na ni namna gani tabia na sifa zake?
- Jambo gani linazuia Ibada ya kweli, na jambo gani linaifanya liwe la kweli?
- Jinsi gani tunaweza kumiminiwa na maji yaliyo hai?
- Jinsi gani tutapata kuwa wavunaji wa kufaa kwa ajili ya Yesu?
- Zipi ni hatua za kukua kiimani, ambazo yule diwani alizipitia?
- Jinsi gani Yesu alimponya yule mwenye kupooza kwenye birika la Bethzatha?
- Kwa nini Wayahudi walimhukumu Yesu?
- Jinsi gani na kwa nini Mungu hufanya kazi na Mwana wake?
- Zipi ni kazi muhimu mbili, ambazo Baba alimpa Kristo azikamilishe?
- Uhusiano kati ya Baba na Mwana ni nini, jinsi alivyotueleza Yesu mwenyewe?
- Zipi ni zile shuhuda nne, na kwa jambo gani zinashuhudia?
- Kwa nini Yesu hakupokea utukufu kwa ajili yake mwenyewe, jinsi ambao watu wengine wangalifanya?
Usisahau kuandika jina lako na anwani yako wazi kwenye karatasi ya majibu ya quiz, wala si kwenye bahasha tu. Ndipo uitume kwa anwani hii:
Waters of Life
P.O.Box 600 513
70305 STUTTGART
GERMANY
Internet: www.waters-of-life.net
Internet: www.waters-of-life.org
e-mail: info@waters-of-life.net