Previous Lesson -- Next Lesson
a) Yesu anamwongoza mwanamke mzinzi apate kutubu (Yohana 4:1-26)
YOHANA 4:16-24
16 „Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa. 17 Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume. 18 Kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. 19 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! 20 Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia. 21 Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. 22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. 23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabuduo. 24 Mungu ni Roho nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.“
Baada ya Yesu kuamsha ndani ya yule mwanamke kiu kwa maji yaliyo hai, na kumjalia haja yake ya kupata zawadi hii ya Mungu, akamwonyesha kizuizi kilichomzuia asipokee zawadi hii - yaani dhambi yake. Hakumkemea vikali kwa kusema, „Wewe ni mzinzi“, bali kwa upole akamwomba kumwita mumeo kwake. Ombi hili liligusa jambo nyeti kabisa ndani yake. Kama kawaida ya wanawake wote yeye naye alitamani kwa maisha yake ulinzi na utunzaji wa mume. Bali alikuwa na ukiwa na kudharauliwa, na bila haja ya kufunua aibu yake kwake Yesu. Basi akajaribu kujilinda kwa kusema „Sina mume“.
Yesu akathibitisha tamko lake kuwa ni kweli, maana alijua siri zote. Alielewa kwamba ametupwa na kuwa na upweke, akitafuta upendo kwa njia ya kuridhisha tamaa, na hivyi kuangukia dhambini tena na tena.
Kila tendo la uzinzi ni msiba mkubwa, likikunja dhamiri zetu, na kutia ugonjwa kwenye kujisikia kwetu, na hasa hasa ndani ya wanawake. Mwanamke huwa ana hamu na mume wake hata baada ya farakano hilo, akitamani kuungana tena, kuelewana na kupatana.
Hapo basi alipata kumtambua Yesu kwamba yeye si mtu wa kawaida; alichoona ndani yake ilikuwa ya unabii. Kwa undani kabisa alianza kutambua kwamba ni Mungu tu aliyeweza kumsaidia. Lakini wapi aweze kumpata? Na jinsi gani ? Sala na ibada kwake haikuwa na maana tena. Kwa miaka alikuwa hakushiriki katika ibada, lakini hata hivyo alitamani sana ukombozi na amani na Mungu.
Baada ya Yesu kuamsha ndani yake kiu cha kusafishwa, akaendelea kumpeleka hatua nyingine atambue kwamba, mahali pa kuabudu si jambo muhimu sana, bali swali kuu ni kujua ni nani wa kuabudiwa. Akamfahamisha kwamba Mungu ndiye Baba wa mbinguni. Na hivyo akamtwisha shauri la wokovu wake mwenyewe katika asili ya kumfahamu Mungu. Akatumia tamko muhimu la „Baba“ mara tatu. Basi, si jambo la akili sana au la uchaji wa Mungu linalotokeza ufahamu wa Mungu, bali ni imani ndani ya Kristo peke yake.
Yesu aliweka wazi kwamba, si kila aitwaye mungu anastahili kuwa na cheo cha „Baba“. Wasamaria huwa waliabudu miungu kadhaa. Bali Wayahudi walikuwa wakifahamu ni nani aliye Bwana, aliyejifunua kwao katika historia yao, naye aliyewaahidi kwamba Mwokozi atatokea kwa ajili ya ulimwengu wote, akiwa wa ukoo wa mfalme Daudi.
Dini ya kibiblia ilitakiwa kuwa ya ki-ulimwengu, kwa wanadamu wote. Tangu hapo kumwabudu Mungu iliwekwa huru na vifungu vya hekalu la pekee mahali fulani. Waumini wakapewa kuwa hekalu la Mungu, na Roho Mtakatifu akiwatawala; maisha yao yote yakapewa kuwa ibada kwa utukufu wa Mungu. Wokovu wa Kristo ukawa ndiyo sifa zao, wakiwa wanajiachilia ndani ya ukuu wa upendo wake. Wamechagua maisha ya unyofu, yenye heshima, na safi kwa nguvu yake Yesu. Baba yao wa mbinguni amewafanya kuwa wapya. Wanavyosujudu kwa moyo wote, wanajaa sifa. Inampendeza Mungu sana, watoto wake wakimwelekea na sifa kwa hiari, wakimshukuru kwa moyo wa ibada na kutamka „Baba yetu uliye mbinguni“.
Mungu ni Roho, wala si sanamu au tukio la njozi, hapana. Yeye ndiye Baba yetu, nasi twatambua Roho yake. Yeye anafahamu udhaifu wetu na kutokuweza kwetu kumfikia. Basi akaja kwetu ndani ya Mwana wake, akatusafisha kwa sadaka yake, ili tuweze kupokea Roho yake. Mungu apenda kuwa na watoto wengi; ni hao watoto wake tu wawezao kumwabudu katika roho na kweli. Tunaomba kwa Baba atujalie na Roho yake vipawa vya kweli na neema, ili maisha yetu yapate kushuhudia upendo wake.
Hakuna awezaye kumwabudu Mungu ipasavyo, basi Yesu akatupatia kipawa cha Roho. Ndani yake tu twapata kuwa waombaji waaminifu, watumishi wenye furaha, na mashahidi wajasiri. Hivyo maisha yetu yatakuwa ibada kwa Baba mpendwa katika nguvu ya Roho inayotiririka kutoka kwa msalaba wa Kristo.
Kristo alisafisha na kutakasa hekalu, ili aanzishe ibada ya kweli. Baba alikuwa akifunuliwa kwa yule mwanamke mwenye dhambi. Katika kukiri makosa yake na kwa kutamani maji ya uzima, Bwana Yesu akamjalia rehema zake.
SALA: Baba wa mbinguni, twakushukuru kwamba unatamani kupewa heshima toka mioyoni mwetu, na hivyo kutukuzwa na mwenendo wetu, tukisifu neema yako. Takasa ibada zetu. Tufanye kuwa watumishi wanaomfuata Mwana wako, anayekutukuza daima. Utujalie moyo wa kuomba, pia tukiitika kila wakati kwa neno lako linalomiminika kutoka kwa injili yako.
SWALI:
- Jambo gani linazuia ibada ya kweli, na jambo gani linaifanya liwe la kweli?
YOHANA 4:25-26
25 „Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote. 26 Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye.“
Mwanamke huyu akasikia nguvu na ukweli wa maneno ya upendo wa Yesu. Alitamani kuona kutimizwa kwa ahadi ambazo yeye alimpatia. Alikumbuka unabii uliotamka ukaribu wa kutokea kwa Masihi. Tegemeo lake aliliweka kwenye jina lake, akiamini kwamba ni yeye tu awezaye kumjulisha kuhusu ibada ya kweli wa Mungu.
Kiajabu, Yesu hakujifunua mwenyewe waziwazi mapema zaidi penginepo, jinsi alivyofanya mbele ya mwanamke huyu. Maana alimwambia wazi kwamba, yeye ndiye yule mtazamiwa, aliyetumwa na Mungu, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu akisema: „Mimi ndimi zawadi ya Mungu kwa wanadamu; ni Neno la Mungu lililoingia mwilini na hivyo kuwa Wokovu kwa ajili ya wote“
Yule mwanamke alishindwa kuona kwamba Masihi ndiye mfalme wa wafalme, mkuu wa manabii wote, tena kuhani mkuu. Pengine aliwahi kusikia kwamba, kuja kwake, kungeleta ufufuo na kueneza amani duniani; labda naye alikuwa na habari ya matazamio ya kisiasa ya Wayahudi. Lakini alichotamani binafsi ilikuwa ni kuokolewa na maisha yake ya dhambini. Na akaamini kwamba, Kristo angeweza kumtendea hili.
Hapo Yesu akasema: „Mimi ninayesema nawe, ndiye!“ Katika tamko hilo mipango ya mbinguni na ahadi za manabii zilikuwa zinakutana. „Mimi ndimi!“ Hakuna ambaye angeweza kutamka kwa uwazi zaidi kwamba mwenyewe ndiye Masihi. - Mpinga-Kristo anayetazamiwa kutokea siku moja, ndiye ambaye pengine atajieleza kwa uongo kuwa ni Kristo. Lakini Kristo ndiye upendo ulioingia mwilini, asiyeweza kumkatalia yeyote akimjia na makosa yake, atakuwa na rehema kwake, kama alivyokuwa hapa kwa huyu mwanamke Msamaria. Yeye ndiye N e e m a, wala si hukumu.