Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- Romans - 056 (The Absolute Necessity of the Testimony of the Gospel)
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hebrew -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Malayalam -- Polish -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Turkish -- Urdu? -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
SEHEMU 2 - HAKI YA MUNGU HAISOGEI HATA BAADA YA WATOTOWA YAKOBO, WATEULE WAKE, KUFANYA MIGUMU MIOYO YAO (Warumi 9:1-11:36)
4. Haki ya Mungu hupatikana tu kwa imani, wala si kwa kujaribu kutimiza sheria (Warumi 9:30 - 10:21)

c) Ulazima kabisa wa ushuhuda wa Injili kwa ajili ya watoto wa Yakobo (Warumi 10:9-15)


WARUMI 10:9-15
"9 Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako, ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako, ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. 11 Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. 12 Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; 13 kwa kuwa, Kila atakayeliita Jina la Bwana ataokoka. 14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? 15 Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!“

Mtume Paulo alianza kuelekea kwenye vita vya kiroho na kanisa la Wakristo wa asili ya Kiyahudi kule Rumi. Aliwaeleza kwamba, kule kuhubiri kuna hatua na vipengele mbalimbali. Imani ya kweli huanza moyoni, maana mwanadamu huamini ndani ya moyo wake. Imani hiyo ina maana kwamba, mwumini kwa moyo wake wote na kwa karibu sana ameunganika na yule anayemwamini.

Tena pamoja na imani inapasa kuwa na ushuhuda kwa maneno, maana ukweli unapasa kutupa mbali giza lolote. Imani na ushuhuda zinaenda pamoja. Ushuhuda hutamka habari ya imani kwa namna kwamba, upande moja wasikilizaji waweze kuelewa, na upande wa pili ni kwamba, mshahidi mwenyewe aendelee kupata uhakika zaidi ndani ya imani yake mwenyewe.

Uhakika wa imani, ambayo Paulo mwenyewe na mashahidi wengine wa Kristo walioitolea, inayo kanuni fulani pia na mafundisho:

1. Yesu ndiye Bwana. Yeye ni mwenye ulimwengu, na enzi zote amekabidhiwa yeye. Mfalme Daudi alishuhudia wazi: Bwana asema kwa Bwana wangu: „Uketi mkono wangu wa kuume, hata niwafanyapo adui zako kuwa chini ya miguu yako“ (Zaburi 110:1). Mtume Yohana alieleza kinaganaga habari ya Kondoo wa Mungu akaavyo kwenye kiti cha enzi (Ufunuo 5:1-14); na Paulo alishuhudia katika matamshi yake ya kumtukuza Msulibiwa aliyefufuka kutoka kwa wafu kwamba, kwa jina la Yesu kila goti litapigwa, ya walio mbinguni, na ya walio duniani, na ya walio chini ya ardhi na kwamba, kila ulimi ukiri kwamba, Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba (Wafilkipi 2:5-11).

Tamko hilo fupi „Yesu ni Bwana“ ndiyo uti wa mgongo wa imani ya kikristo. Ina maana kwamba, Yesu Kristo ndiye Mungu kweli katika ushirikiano wa Utatu Utakatifu. Anaishi na kutawala katika mapatano kamili na Baba yake wa mbinguni.

2. Huo tukuzo kwake Kristo una msingi wake kwenye tendo lile la Mungu Mtakatifu kwamba, yule aliyesulibiwa na kufa kabisa, alimfufua toka mautini awe hai tena. Ufufuo wa Kristo ndio nguzo ya pili ya imani ya Kikristo; maana ikiwa Mwana wa Adamu hakufufuka kweli, basi mwili wake umeoza kabisa. Lakini alifufuka kutoka kwenye kaburi lake, naye alitembea kupitia katika miamba na kuta kwa mwili wake wa kiroho. Yesu yu hai, wakati waanzilishi wengine wote wa dini zingine walikufa na miili ya kuoza. Ufufuo wa Kristo pia ni thibitisho la utukufu wake, ushindi wake, enzi yake, na ukombozi wake kamili.

3. Yeyote aaminiye mambo hayo moyoni mwake, naye akiyashuhudia hayo aliyohakikisha, basi ameokoka. Matumaini hayo yanamwongoza mwumini ashuhudie kwa uthabiti na furaha kwamba, Yesu ndiye Mshindi. katika ushuhuda wake anashiriki uhai, Roho na amani ya Kristo. Yeye aliyesimama kwenye msingi wa Kristo, naye amtegemeaye kweli, daima hatakosa kabisa.

4. Kwenye matumaini hayo yanayoendelea kukua, Paulo anasema kwamba, yeye aaminiye ndani ya Bwana Yesu Kristo, atakuwa amejaliwa haki na Mungu mtakatifu, naye amefunguliwa na dhambi zake zote, kuachiliwa katika hukumu ya mwisho, naye amejaliwa kuwa mshiriki ndani ya familia ya kiroho ya Mungu na kupandikizwa ndani ya mwili wa kiroho wa Kristo. Kwa kifupi, mwumini hujiunga kwa uimara na kwa daima pamoja na Yesu. Wokovu kamili na kujaliwa haki zapatikana kwa njia ya ushuhuda wa imani yake kwamba, yeye ni mtenda dhambi aliyejaliwa haki, anayekubaliwa na Mungu. Hivyo, ushuhuda sio sababu ya wokovu, maana haki ya kweli inapatikana tu kwa imani. Zaidi, ushuhuda unatambua na kuimarisha hali hiyo ya kujaliwa haki kwa mwumini kwa kusudi kwamba, wokovu wake katika maisha ya kila siku uendelee kuimarika. Kujaliwa haki na ukombozi zinatokana na Kristo, nazo zapatikana kwa njia ya ushuhuda wa mwumini juu ya Bwana wake aliyemwokoa.

5. Baada ya utambulisho huo wa imani ndani ya Agano Jipya, pia na kujaliwa haki kwa neema tu, Paulo anaelekea kutamka shindo: Hakuna kabisa utofauti kati ya Myahudi na Mkristo kama wote wawili wanaamini ndani ya Kristo na kufanywa wapya kwa neema yake. Kweli kuna Bwana mmoja tu, Mwokozi mmoja, Mkombozi mmoja kwa ajili ya wote. Wayahudi hawaokoki kwa njia ya Ibrahimu au Musa, ila kwa Yesu tu. Wokovu wa Kristo, enzi yake, uzima na upendo zinahusiana na wote, Wayahudi na Wakristo kwa namna moja kabisa. Popote hakuna mwingine aliyesulibiwa na kujitoa mwenyewe kwa malipo kwa ajili ya kila mtu, hakuna ila huyu Mwana Kondoo wa Mungu mpole, aliyepeleka mbali dhambi ya dunia yote.

6. Paulo anaonyesha waziwazi kwamba, Yesu ni mtajiri, naye huwafanya wote wanaomwuliza kuwa washiriki katika utajiri wake wa kiroho (Warumi 10:12-13). Yeye hutoa Roho yake Mtakatifu, enzi yake tukufu, pia na upendo wake wa daima kwa yeyote amwombaye; mtu anapomwaga moyo wake mbele ya Yesu Kristo aliye hai binafsi, bila kurejea kwa watakatifu au kwa bikira Mariamu. Bila hatua yako kuombea wokovu, kutaka kutakaswa na kuokolewa, hakuna litakalotendeka kwako. Ila neema hupatikana kwa wote, lakini inatupasa kuitafuta (Yoeli 2:32). Kwa kusihi tutasikia sauti ya Roho Mtakatifu ndani yetu ikilia: „Abba, Baba“ (Warumi 8:15-16).

WARUMI 10:15
"15 Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!“

Roho huyu hutufundisha kukiri dhambi zetu kwake Mwana Kondoo wa Mungu, tukimshukuru hasa kwa ajili ya kutufia, kufufuka kwake, na kwa ajili ya utayari wake wa kutuokoa na ghadhabu ya Mungu inayokuja.

Hii roho wa kuomba ndani yetu isijifikirie tu yenyewe. Yeye aaminiye ndani ya Kristo haombi kwa ajili yake mwenyewe tu, lakini pia kwa ajili ya wale wote ambao huyu Roho Mfariji anaweka mbele yake. Hapo mwanzo wa Ukristo wana wa Yakobo (Wayahudi) waliomba namna hiyo kwa ajili ya wale walioenda kupotea kati ya Mataifa; na kwa namna iyo hiyo na sisi tunatakiwa kuomba siku hizi kwa ajili ya wote, Wayahudi na Waislamu. Shabaha ya huyu Roho ni mwamko wa kuhubiri kutoka kwa Mwana Kondoo wa Mungu mwenyewe (Matendo ya Mitume 1:8 na Ufunuo 5:6).

7. Mtumne Paulo aliwaeleza waumini wa Kristo walio watoto wa Yakobo kule Rumi jinsi ya kutangaza injili kwa maisha ya kila siku, jinsi ya kushinda hali ya kujisikia kuwa watu wa kuchaguliwa, na jinsi Roho Mtakatifu alivyowaongoza kutenda kazi kwa busara.

Jinsi gani Bwana huwaita watu wowote wasioamini ndani yake? Na jinsi gani watapata kuamini ndani yake, ikiwa hawajasikia habari zake kwa karibu? Watasikiaje juu yake bila mhubiri mwaminifu? Na jinsi gani mtangazaji atahubiri, kama hakutumwa na Kristo? Basi si watu tu wasioamini ni wenye lawama, lakini pia wale ambao hawakuwaeleza ukweli wa wokovu, ambao wao wenyewe wameipokea. Paulo anapumua kwa nguvu anapokariri neno la Bwana kwa Isaya (52:7): „Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima miguu yake aletaye habari njema, yeye aitangazaye amani, aletaye habari njema ya mambo mema, yeye autangazaye wokovu.“

Habari hiyo njema, kufuatana na Paulo, inabeba ndani yake shuhuda kwamba, Yesu yu hai naye anatawala, na pia kwamba, wokovu wake unaendelea kuenezwa. Ufalme wa Mungu ndani ya Yesu Kristo ndiyo sababu ya furaha ya mwumini. - Haya basi, nani ni mwenye furaha siku hizi akiamini kwamba, Kristo anatawala naye atashinda? Je, sisi sote tumelegea na kuchoka na imani yetu? Nani anaamini siku hizi itiko la kufaa kwa ombi lile, „Ufalme wako uje“ na kusema: „Ndiyo Bwana, ufalme wako uje kabisa nchini kwangu“?

SALA: Ee Baba wa mbinguni, tunakuabudu, kwa sababu ulimwinua Yesu juu mbinguni, nawe ukamfanya kuwa Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme. Utusaidie kukiri hadharani na pia kwa hekima habari ya kufufuka kwake toka mautini na kwamba, anaketi pamoja nawe. Twaomba cheche ya uzima wa milele iweze kuingia ndani ya mioyo ya wengi wanaosikia habari hiyo.

SWALI:

  1. Je, uhusiano kati ya imani na ushuhuda ni nini?
  2. Jinsi gani imani na ushuhuda zinaendelea kukua maishani, kufuatana na mtume Paulo?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on December 14, 2023, at 01:21 AM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)