Previous Lesson -- Next Lesson
1. Mpango wa ukombozi wa Mungu unatuahidi utukufu utakaofunuliwa (Warumi 8:28-30)
WARUMI 8:28-29
"28 Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.“
Yeyote anayemjua Mungu anatambua ya kwamba yeye ni mwenye enzi zote. Hakuna lolote linalotokea ulimwenguni asilolijua na kukusudia. Yeye ndiye Mwenyezi. Hata hivyo, sisi hatuamini habari ya kuamriwa hali ya kila mtu ya baadaye, jinsi watu wa dini zingine wanavyoamini, kwa sababu tunajua kwamba, Mungu mkuu ndiye Baba yetu mwenye huruma, anayetuchunga kwa kuendelea daima, wala hawezi kutudhuru, kutupuuza wala kutuacha. Na kwa sababu hiyo tunamwomba aimarishe tegemeo letu ndani ya upendo wake, ili imani yetu isipotee katika shida zote na maonezi tunazopata. Ili kuimarisha tegemeo letu ndani ya pendo la Mungu kwetu, Paulo anatuandikia mfululizo wa mathibitosho kuhusu wokovu wetu wa binafsi, ili tusiingiwe na mashaka, wala kutingiswa kiimani.
Mungu alikuchagua kabla hujazaliwa, maana ulikuwa wazo moyoni mwake. Alikufahamu hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu. Hivyo, anafahamu mahali pa ndani pa utu wako, asili yako na makusudi ayko. Uhusiano wako na Mungu una kina kirefu kuliko unavyodhani. Wewe si mgeni, bali wa karibu na kujulikana naye kabisa. Anakungojea, kama vile baba anavyongojea kurudi kwake mwana mpotevu. Mungu anakutamani zaidi sana kuliko wewe unavyomtamani yeye.
Mungu wa milele alikufahamu kabla ya nyakati zote zilizokwisha kupita. Na kwa yale yajayo, anakuwekea shabaha yenye utukufu mbele zako, maana alikuchagua mbele kwa ukamilifu wa mapenzi yake matukufu uwe mwana wake kwa njia ya Yesu Kristo, aliyebeba dhambi zako, pia na kushinda mwili wako wa dhambi msalabani kwake. Kipekee ndani ya Kristo, chaguo lako limekamilika. Yeyote anayekamatana na ukombozi wa Mwana hatasogezwa kotoka katika hali hiyo, kwa sababu Mtakatifu naye ni mwaminifu, Kwa hiyo, tambua kwamba Mungu ameweka shabaha kwa maisha yako, pia na kukuchagua upate kuwa tukufu katika mfano wa sura ya Kristo, akaaye mkononi mwa kulia wa Babaye. Mungu hapendi kuwa na daraja mbalimbali za wana, bali atawaongoza wote kwenye ukamilifu wa uvumilivu na unyenyekevu, ili uweze kujinyima mwenyewe na kutembea namna Kristo alivyotembea duniani kwetu.
WARUMI 8:30
"30 Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.“
Mungu ameyafanya mawazo ya upendo wake kuwa ni watu wenye nafsi na utambuzi, naye amekusema wewe binafsi!
Je, umesikia sauti yake chini kabisa moyoni mwako? Na wito wake umedidimia ndani mahali pa chini kabisa ya ugumu wa utu wako? Kumbuka kwamba, Mungu alikuchagua wakati ulipokuwa bado mwenye dhambi, na hivyo alikuchagua uwe mtoto wake. Alikusudia kukutengeneza kwa upya wewe uliye mfu kwa kiburi na tamaa, ili upate kung‘aa katika usafi kabisa, unyimivu, uaminifu na unyofu. Hakuna nguvu lolote ndani yako kwa maisha matakatifu kama haya, isipokuwa neno la Mungu, linalofanya kazi ndani yako. Kwa hiyo soma Biblia Takatifu bila kukoma, kwa maana kwa njia ya herufi hizo nyeusi Mungu anasema nawe moja kwa moja.
Katika uamuzi wake wema Mungu aliweka msingi wa kweli wa wokovu wako, ambao hauwezi kusogezwa kwa malalamiko ya shetani. Mungu wetu mwenye haki zote alikujalia haki hiyo kwa kifo cha kafara ya Mwana wake, naye akafuta makosa yako yote mara moja. Sasa wewe umewekewa haki ndani ya uadilifu wa haki ya Kristo, na umehesabiwa kuwa safi ndani ya ukombozi wake. Basi, ni lini utakapomshukuru Bwana wako kwa upendo aliyokujalia? Lini utaamini uongozi wake na kusifu neema yake ya uaminifu?
Katika enzi yake Mungu aliainisha na mengi kuliko hayo kwa ajili yako. Alikupatia na sehemu ya Roho Mtakatifu kuwa dhamana ya uhai wake tukufu ndani yako. Kwa sababu hiyo utukufu wa asili ya Mungu umefichika ndani yako leo. Jinsi Kristo alivyotokea tu kwa macho ya waumini, ndivyo hata upendo wake, ukweli na kazi yake ya subira ndani yako. Roho wa Mungu mwenyewe ataleta matunda ndani yako kwa nguvu zake, ukidumu ndani ya Mwokozi wako. Paulo hakusema kwamba, Mungu atakutukuza hapo mbeleni, lakini kwa imani alikiri kwamba, yeye amekwisha kukutukuza hapo nyuma, maana Paulo alikuwa na uhakika kwamba, Yesu ndiye mwanzilishi na mwenye kukamilisha imani. Kwa hiyo, yeye aliyeanzisha wokovu ndani ya roho yako ni mwaminifu. Yeye anakufundisha, kukuimarisha na kukukamilisha tu kwa sababu ya ustahilifu wake.
Je, unayo matatizo maishani mwako? Unayo njaa au wewe ni mgonjwa? Unatafuta kazi? Labda umeshindwa shuleni? Mambo hayo yote sio ya maana zaidi, kwa sababu Mungu yu pamoja nawe. Yeye anakupenda, anakuchunga na anakulinda kama mboni ya jicho lake. Hawezi kukusahau, lakini anakamilisha mpango wake kwako hadi mwisha. Huyu Mtakatifu alikuchagua wewe hasa akupokee kuwa mtoto wake. Basi, ujikinahi, ujitwishe msalaba wako ukamfuate Mwana wa Mungu kutokea msalabani hadi kaburini na ndipo mpaka kwenye utukufu, maana mambo yote hufanya kazi pamoja kuwa mema kwa wale wampendao Mungu. Je, unampenda yeye aliyekupenda kwanza?
SALA: Ewe Mungu mtakatifu, uliye Utatu ndani ya mmoja, tunakuabudu kwa sababu ulituchagua, ulitujua tangu awali, na ulituchagua ndani ya Kristo, ili tuvishwe utukufu wa upendo wako. Sisi tuna nini hata ututamani? Utusamehe makosa yetu, na utufungulie masikio yetu, ili tuweze kusikiliza wito wako ndani ya Biblia Takatifu. Tukubali kujaliwa haki yetu kwa damu ya Mwana wako na tukushukuru daima kwa upendo wako wa uaminifu. Tunataka kuamini uongozi wako, na tunakusihi utuimarishe katika uhakika, ili tusisogezwe toka kwako kwenye siku za mbeleni zilizo ngumu, bali tumtambue Roho Mtakatifu akitawala ndani yetu kama dhamana ya utukufu utakaokuja.
SWALI:
- Kwa nini mambo yote hufanya kazi pamoja kuwa mema kwa wale wampendao Mungu?
Katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao kuwapatia mema
(Warumi 8:28)