Previous Lesson -- Next Lesson
8. Mauguzi matatu ya kipekee (Warumi 8:18-27)
WARUMI 8:18-22
"18 Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu. 19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. 20 Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha katika tumaini; 21 kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. 22 Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa."
Paulo hakuridhika na imani yake na upendo wake kwa Mungu, lakini alijinyosha mbele kwenye utajiri wa tumaini letu ndani ya Mungu. Je, wewe unatazamia ufunuo wa utukufu wa Mungu? Na hii ndiyo shabaha ya maisha yako? Usiridhike tu na ufumbuzi wa shida zako ndogondogo, maana lengo la Mungu ni kukomboa ulimwengu wote. Basi utazamie zawadi kuu ya mwisho, ambayo ndiyo ni kufanywa upya kwa uumbaji wote kabisa.
Wanyama wanateseka, pia na majani yanatoweka. Ole wake yule mtu anayekusudia maumivu kwa wanyama. Umewahi kutambua kwamba, macho ya wanyama yamefungwa na kuonyesha huzuni? Ni hivyo kwa sababu wao nao wanakufa. Furaha imewatoka, na upweke na shida zimewakumba. Wanyama wote wanatazamia kwa kutokea kwa utukufu wa wana wa Mungu, kwa sababu kwa kurudi kwake Bwana, watoto wale waliozaliwa na Roho yake, wataondolewa na huu mwili wa kuteseka, na utukufu wake utafunuliwa ndani yao. Hapo basi na viumbe vyote watasalimika. Kwenye enzi ile, hata punda hatapigwa tena kwa hasira, wala mbu yeyote hatawauma wale wanaolala usingizi. Mungu ametuahidi amani kamili hapo duniani, ambayo itakamilishwa kwa kuja kwake Kristo mara ya pili pamoja na watakatifu wake wote na malaika. Je, unayo hamu kwa ajili yake?
Uumbaji wote umeteseka kuanzia kwenye mwanguko wa mwanadamu dhambini, maana kwa maasi ya watu, madaraka yake na kila kitu chini ya utawala wake kikaasi. Paulo anaeleza mateso hayo ya viumbe kwa maumivu makali ya mwanamke anapozaa mtoto; na mauguzi hayo yanamleta Mwana wa Mungu karibu zaidi na sisi, maana yeye aliteseka na anaugua pamoja nasi na pia na kila mnyama. Yeye anakusudia kutukaribia kabisa iwezekanavyo kwa ajili ya ukombozi wa wote.
WARUMI 8:23-25
"23 Wala si hivyo tu, ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu. 24 Kwa maana tuliokolewa kwa taraja; lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana, hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho? 25 Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi.“
Wana wa Mungu ulimwenguni kwetu wanaugua kwa nguvu ya Roho wa Bwana katika ufahamu wao wa ndani pasipotambulika vizuri, wakitamani kwamba, kupokelewa kwao kuwa watoto kukamilike ndani yao. Ndiyo, tumekombolewa kwa imani, lakini siku moja tutakombolewa kikamilifu. Siku hizi tunaishi na ukamilifu wa sehemu rohoni mwetu, lakini ukamilifu kamili tunatazamia tujaliwe.
Tumaini na shukrani za kiasi kama zawadi ya kutangulia kabla ya utukufu tunaotazamia ndiyo dalili za msingi za uhai wa kiroho ndani yetu. Hatutamani dhahabu au tamaa za mambo ya kimwili, ila tunatamani kumwona Mungu Baba na Mwana, pia na Roho Mtakatifu.
Je, unatamani kumwona Baba yako? Unatazamia ushirikiano na Kristo,Mkombozi wako? Kumbuka kwamba mwili wako wa kufa utateketea mbele ya utukufu wa Mungu, nawe utabadilika kuwa nuru ya daima ndani yake. Hii ndiyo hali ya kutamanika ya watakatifu, maana uhai wao uliofichwa ndani ya Mungu utadhihirishwa mapema, Hali hiyo haitajaa moyo tu, bali miili yao inayoteseka hadi sasa, pia iliyo na magonjwa na ya hali ya kufa itabadilishwa na kutukuzwa. Sisi sote twahitaji sana subira katika mazingira yetu ya kungojea hayo hapo duniani, maana mambo ya teknologia na ya sayansi yanajaribu sana kupoteza tumaini letu kwa njia ya kututengenezea paradiso isiodumu hapo duniani. Hata hivyo, Roho Mtakatifu ndiye hakikisho letu la utukufu utakaokuja.
WARUMI 8:26-27
"26 Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. 27 Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.“
Roho Mtakatifu mwenyewe anahangaika ndani ya miili yetu midhaifu, akihuzunika juu ya hali yetu ya kushindwa, naye anasikia uchungu kwa ajili ya sala zetu za uchoyo na kuchosha, pia anaugua kwa ajili ya utambuzi wetu unaopungua sana, akihuzunika pia kwa ajili ya upendo wetu dhaifu na kushangaa kwa sababu ya nguvu yetu ndogo sana. Roho wa Mungu mwenyewe huomba na kuwatetea waumini, hata kama hawakuomba, kuugua kiroho kunatokea ndani yao, kufuatana na Sala ya Bwana, ambayo ndiyo sala ya Roho Mtakatifu. Basi, ujitoe kabisa kwa mafunzo hayo ya maombi, ili upate kuachana na uchoyo wako na kuongozwa kwenye mvumo wa shukrani na maombi yenye upendo, kuomba kwa hekima, shukrani na nguvu, maana Roho wa Bwana anaomba ndani yako mchana na usiku kwamba, heri ulimwengu wote ungepata kuokolewa. Haya basi, ni lini utakapoanza kushiriki katika maombezi hayo kwa Baba yako wa mbinguni, ukisali na kushukuru kwa moyo wako wote?
SALA: Ee Baba mtakatifu, tusamehe hali ya sala zetu za kulegea na za umimi, na utuongoze tuweze kutakasa jina lako takatifu, tutukuze ukombozi wa Kristo kwa utu wetu wote na kutenda kazi kwa unyenyekevu kwa nguvu ya Roho yako. Ee Bwana, tufundishe kutambua tumaini la Roho, kuomba inavyompendeza, na tutamani hali ya kuwepo kwako, a kurudi kwake Mwana wako katika utukufu kuu, ili uumbaji wote upate kukombolewa pamoja na wote wenye tumaini hilo katika taifa letu.
SWALI:
- Ni wakina nani hao wanaougua kwa ajili ya kurudi kwake Kristo? Na kwa nini?