Previous Lesson -- Next Lesson
a) Awahukumuye wengine hujipatiliza mwenyewe (Warumi 2:1-11)
WARUMI 2:3-5
"3 Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je! 4 Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu? Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu? 5 Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu,“
Uliwahi kutambua kwamba, uchafu kuu wa kuchukiza hasa sio uzinzi wala kiburi, au hata chuki kwake Mungu, bali ni unafiki? Mnafiki hujifanya kuwa mwenye haki, mnyofu na mcha Mungu, wakati mle ndani yake amejaa na maongo, machafu na udanganyifu. Yeye basi ni chukizo kwake Bwana. Yule Mtakatifu ataondoa kile kifuniko toka usoni mwako, na kukuweka wazi mbele za watu wote, malaika na watakakatifu, ule ukweli juu ya dhambi zako, maana ulijifanya kuwa takatifu mbele zao. Uzinifu wako uko kubwa zaidi unavyodhania. Usijidanganye na matumaini ya uongo. Jinsi wasafiri wasioruhusiwa kuingia kwenye ndege mpaka wamelazimika kukaguliwa kabisa, ndivyo hakuna awezaye kuingia uzima wa milele isipokuwa ameitwa kwanza kwenye hukumu ya haki, ambayo hakuna awezaye kuikwepa. Kwa nini karibu watu wote wanaogopa saa ya kifo chao, nao wanatetemeka kwa kufika kwake yule aitwaye „mvunaji mwovu“? Basi kwa sababu katika dakika hizo za kuchungulia kaburini watu mara moja wanatambua kwamba, wameikosa shabaha ya maisha yao, na kwamba sasa wanasimama mbele ya saa ya hukumu.
Kwenye siku ile kuu ya hukumu ya mwisho watu wote wa dunia hii, weusi, wanjano, wekundu, wa rangi ya udongo na weupe, wakijumlishwa watajiri na maskini, watu wa juu na wa chini, werevu na wajinga, wazee na vijana, wanaume na wanawake, wafungwa na walio huru, wote watakutana mbele za Mungu. Ndipo vitabu vitafunguliwa vyenye kumbukumbu za matendo, maneno na mawazo ya watu. Si vigumu kwetu sisi tunaoishi wakati wa vyombo vya kutega maneno na kila sauti, video cameras na micro films, kuweza kuelewa jinsi ilivyo rahisi sana kwa Muumbaji wetu ajipatie kumbukumbu ya kila mmoja wa viumbe vyake. Hakutakuwa na muda wala haraka katika enzi ya milele; na Mungu atakuwa na nafasi ya kutosha achunguze habari zako kwa kinaganaga. Hutahitajika hata kutamka neno kwa kujikinga mbele zake Bwana, achunguzaye moyo na ubongo, na pia itakuwa bila sababu kueleza ma-udhuru juu ya wengine, au kuwaaibisha wazazi wako, walimu au watu wengine. Wewe ni mwenye makosa, na Mungu atakuhukumu. Basi, ujitayarishe hata uweze kusimama mbele za Hakimu Mkuu, maana hutaweza kutoroka ile saa ya hukumu yake.
Ujue leo hii, katika ufunuzi wa utukufu wa Mungu kwamba, wewe umekuwa najisi. Usianze kunung’unika kwa sikitiko na huzuni, lakini ukiri dhambi zako mbele za Mungu, ujikane na kujipatiliza mwenyewe, na kuyataja uliyoyatenda. Usifiche yoyote ya matendo yako maovu, lakini uyaungame mbele za Yule Mtakatifu kwamba, wewe ni mwovu katika makusudi yako yote.
Kuvunjika namna hii kiroho ya utu wako, maana ndiyo njia pekee kwa wokovu wako. Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita ndani ya tundu la sindano kuliko kwa mtu mwenye kiburi kuingia ndani ya ufalme wa Mungu.
Hata hivyo, Mungu ni mwenye rehema. Yeye hatawaangamiza viumbe vyake bila huruma, bali huwapenda wenye dhambi watubuo, walioweka nia kabisa kuziondoa dhambi maishani mwao. Mungu ajua kwamba, watu wote wamechafuka, na hakuna aliye mwenye haki mbele za utakatifu wake, lakini yeye ni mvumilivu, amejaa upendo na upole; na kwa sababu ya upole wa upendo hakusudii mwenye dhambi afe mara moja. Uadilifu wake unadai hukumu na kupatiliza kwa kila mtu leo, lakini wema wake watupatia nafasi nyingine ya kutubu. Sisi sote tunaishi kutokana na taratibu za Mungu. Bila shaka lolote anayo haki na uwezo wa kuweka mwisho kwa ulimwengu wetu kwa mpigo moja, lakini Mungu, anayetutunza na kutuhurumia, hatendi mambo kwa haraka, lakini anatazamia kwamba, wote watageuka na kubadilisha mioyo yao.
Je, umekwisha kuungama kwake Mungu kwa masikitiko na kumwuliza akuumbie ndani yako moyo safi, pia na kufanya upya roho iliyo sawa ndani yako? Unatumia wema wa Mungu kwa nafasi ya kutimiza dhambi zako chini ya funiko la vazi la haki? Je, unadharau upendo wa Mungu kwa kugeukia mafundisho yasio sawa au mawazo ya filosofia, ukitafuta nafasi ya kutoroka wazo la hukumu? Hukumu ya Siku ile Kuu ni ya hakika, basi yeyote asiyejikana mwenyewe na kufia tamaa zake za kimwili, anamdharau anayepima mioyo na nia, asiyesinzia wala kulala, lakini anayetambua kikamilifu tabia ya kweli ya kila mtu.
Shikamana kabisa na wema wa Mungu, nawe utakuwa salama. Ujiingize kwa chini kabisa ndani ya toleo la rehema yake, nawe utajaliwa tumaini. Ubadilishe tabia yako, na utambue sana upendo wa Mungu, ili ufahamu zaidi Mungu ni nani. Yeye ni baba mwenye rehema, wala si mtawala wa peke yake asiyejali, na anayetenda atakavyo bila kumfikiria mtu mmoja mmoja. Mungu huona, husikia na kufahamu kila kitu cha kwako. Anawafahamu babu zako sawasawa na mapokeo yako na mazingira na hali zote zilizogeuza tabia yako. Yeye naye anajua majaribu yako na mapenzi yako ya kudanganyika. Mungu hawezi kuwa bila haki. Yeye yu mwema, huweka taratibu kwa kutenda haki na kujalia rehema.Yu tayari kukusamehe na anakusudia kukutakasa, ikiwa utajitoa kabisa kwake, ukichukia roho yako ya ukorofi, kuikiri ukorofi huo, na kuamua kabisa kuutupa mbali katika jina lake.
Ole wako ukifahamu utakatifu na rehema ya Mungu na hata hivyo kuacha kuungama! Maana ndipo moyo wako utaendelea kuwa ngumu zaidi na akili yako itapofuka. Mnafiki mpumbavu atakuwa mnajisi rohoni mwake wala hawezi kugeuka tena. Hataweza tena kusikia wala kutambua kwa urahisi sauti ya Mungu zaidi ya hapo. Atakuwa akisoma neno la Mungu bila kuguswa. Kwa sababu hizo, ungama mapema ambapo bado panaitwa „Leo“, na ujibidiishe kwa uangalifu kuhakikisha wokovu wako, kabla ya kukosa kabisa nafasi ya kutenda hivyo.
Kwenye saa ile ya kuogofya, ghadhabu ya Mungu itakuwa imechochewa hasa hasa dhidi ya wale waliosikia habari ya wema wake wakiipuuza, wala hawakumgeukia na mioyo iliyopondeka. Hao hawatakuwa na tumaini lolote kwenye Siku ya Hukumu, kwa sababu walitapanya mali yao ya kiroho, na hawakupeleka chochote kwake Mungu ila hatia tu, machukizo, chuki, makosa na kutokuwa haki. Hao itawapasa kuwekwa wazi, kuaibishwa na kuhukumiwa kwenye Hukumu ya Mwisho, kwa sababu hawakuungama wala kukiri dhambi zao.
SALA: Ee Mungu Mtakatifu, nijalie ungamo wa kweli kutokana na uongozi wa Roho wako Mtakatifu. Unirudishe kwako, kwa sababu kurudi kwangu peke yangu sio kamili. Nisaidie ili nisilegee kutambua utakatifu na upendo wako, bali nitambue ndani ya subira yako hali ya kutokusubiri kwangu. Ee Bwana, mimi nafaa kuangamizwa tu katika ghadhabu yako ya haki. Usinihukumu kwa hasira yako kali, bali unirudi katika uvumilivu wako. Naomba vunja kila namna ya kiburi ndani yangu, ili nipate kufia umimi wangu na kuishi na wema wako tu. Niweke huru na kila namna ya unafiki na usiniachilie niingie katika hali ile ya kupata moyo mgumu zaidi. Wewe ndiwe Hakimu wangu na Mwokozi wangu. Ndani yako nategemea.
SWALI:
- Zipi ni zile siri, ambazo Paulo anatufunulia kuhusu hukumu ya Mungu?