Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- Romans - 015 (He who Judges Others Condemns Himself)
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hebrew -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Malayalam -- Polish -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Turkish -- Urdu? -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
SEHEMU 1 - HAKI YA MUNGU INAHUKUMU WENYE DHAMBI WOTE NA KUJALIA HAKI PAMOJA NA KUWATAKASA WOTE WAMWAMINIO KRISTO (Warumi 1:18 - 8:39)
A - Ulimwengu Wote Umekaa Chini Ya Utawala Wa Yule Mwovu, Na Mungu Atahukumu Wote Kwa Uadilifu (Haki) (Warumi 1:18 - 3:20)
2. Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa dhidi ya Wayahudi (Warumi 2:1-3:20)

a) Awahukumuye wengine hujipatiliza mwenyewe (Warumi 2:1-11)


WARUMI 2:1-2
"1 Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale. 2 Nasi twajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao hayo.“

Taji ya dhambi ni unafiki. Watu hujifanya kuwa wenye haki, wenye hekima na wacha Mungu, ingawa wanafahamu kutoka kwa ushuhuda wa dhamiri zao kwamba, kulingana na utakatifu wa Mungu, wako waovu sana. Zaidi na juu ya unafiki huo, wako wakiwahukumu rafiki zao kwa chuki, nao huwasema kwa dharau, kana kwamba wao wenyewe ni mifano bora ya kicho, na rafiki zao ni kama takataka.

Basi, Paulo anavunja kuringa kwako. Anakuondolea mwigo wako wa bandia, akikuonyesha kwamba, huna uamuzi wa kukubalika. Je, unamfahamu yeyote asiye mwaminifu? Wewe mwenyewe huna uaminifu zaidi ya yule. Je, umemwona mwuaji? Wewe ni mwenye kuua zaidi ndani ya chuki yako kuliko yule. Mawazo yako juu yako mwenyewe sio ya kweli. Roho wa Mungu anakuhukumu. Yeye kwanza anawahukumu wale waalimu wakuu wa kicho, wanaojihesabu kuwa bora kuliko watenda dhambi wengine, lakini hawajafahamu kabisa lolote kuhusu kicho cha kweli. Yesu hakusulibiwa na watu wa ghasia, lakini na wale waalimu wakuu wa dini, wenye kiburi na unafiki, wanaoringa na kujivuna kama tausi katika kujionyesha kuwa na kicho, wakati ndani yao wako kama makaburi yaliyojaa mambo yote yaliyo najisi.

Mungu anakuhukumu si kwa ajili ya kazi zako tu, lakini pia kwa sababu ya makusudi yako, mawazo na mapendeleo. Hata ndoto zako ziko ovyo tangu utoto. Katika shabaha zako zote wewe wajiangalia tu. Unakataa kumtii Mungu, unakuwa kinyume cha maazimio yake, unavunja sheria zake na kuwadharau jamaa zako. Wewe ni mwenye mawazo ya kuzini, na umejitenga na Muumbaji wako. Mawazo yako mabovu yatoka moyoni mwako. Kwa vyovyote, katika hukumu ya mwisho utasikia maneno yako yaliyoandikwa, na utaona kazi zako zilizopigwa picha, na makusudi yako yaliyochafua, nawe utatetemeka kwa matisho na utanyamaza. Wewe u mwenye dhambi. Wewe ni mchafu mahali pa ndani ya moyo wako. Uyaungame maovu yako mbele za watu, na kwa vyovyote usimdharau mtenda dhambi mwingine. Pengine jirani yako ni mwovu sana. Lakini juhudi yako dhidi ya maovu yake haithibitishi kwamba wewe ni bila kosa. Wewe utafia dhambi zako mwenyewe, maana wewe unawajibika kwa ajili yako mbele za Mungu. Kwa sababu hizo, jitambue utu wako wa kuvunja sheria ndani ya nuru ya utakatifu kamili wa Mungu.

Pengine hutaki kukubali maneno hayo magumu, au ungetaka kujadiliana na hayo bila kuvunjika ndani ya kiburi chako, wala kumwaga moyo wako katika ungamo wa kweli mbele ya Bwana wako. Kama ni hivyo basi angalia kwamba, kule kutokutambua hali yako haitakuokoa na hukumu tukufu. Ile haki ya milele itakupeleka kortini na kukupatilizia ya haki. Dini zote kuu za ulimwengu zinafahamu habari ya siku ya hukumu. Baadhi yao zinaiita siku ya ufufuo, Al-Quari’ah, au siku ya mwisho wa ulimwengu. Wale tu wasioamini wanakataa kusimama siku moja mbele za Mungu aliye hai. Basi saa ile, siri zako zote, mawazo, maneno na machukizo yaku yatafunuliwa mbele za wote, nawe utatakiwa kutoa hesabu kwa kila neno ovu ulilosema, kwa kila senti ulilotapanya, na kwa kila dakika ambalo hukulitumia kwa kumtukuza Mungu; maana wewe u mwakilishi wa zawadi za Mungu, naye atakaa na kuhesabu nawe kwa kila jambo ambalo alikukabidhi. Miali ya nuru ya utukufu wa Mungu itaingilia hadi mahali pa ndani kabisa ya moyo wako na yote yaliyopita maishani mwako, na yote yaonekana wazi na ya ndani kabisa kuliko picha ya X-Ray au vifaa vingine vinavyojulikana hospitalini. Pale utasimama bila funiko lolote lile.

SALA: Ee Mungu Mtakatifu, wewe ndiwe wa milele na mwenye haki kabisa, na mimi ni mwenye makosa na dhambi. Nisamehe bidii zangu zote za kuonyesha kicho, na uifungue moyo wangu, ili uchafu wote uweze kutoka kwa nuru yako. Nayakiri makosa yangu yote mbele zako, nami nakuomba unijalie Roho wa upendo wako, ili nisirudie kukataa, kuhukumu au kuchukia mtu yeyote, bali nikue ndani ya upendo na busara. Mimi ni wa kwanza katika watenda dhambi wote. Nihurumie mimi , ee Mungu, kufuatana na wema wako wa upendo, na uvunje mabaki ya mwisho ya kiburi changu na ya hali ya wepesi kuona unyeti, ili nipate kuwa mwenye kupendwa moyoni.

SWALI:

  1. Jinsi gani mtu anajipatiliza mwenyewe anapomhukumu mwingine kwa jambo lolote?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on November 15, 2022, at 02:51 AM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)