Previous Lesson -- Next Lesson
3. Mbatizaji anamshuhudia Yesu kama Bwana Arusi (Yohana 3:22–36)
Baada ya kushuhudia kwa unyenyekevu na kutokeza furaha yake juu ya kukua kwa mwamko wa kikristo, Mbatizaji alikiri ukuu wa Kristo na ujumbe wake usio na mfano akitamka:
YOHANA 3:31
31 “Yeye ajaye toka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni wa dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”
Wanadamu ni wa duniani wakihitaji kuzaliwa kwa upya. Yesu pekee alikuwa wa mbinguni, akawa mwanadamu, ili atukaribie sana na kutuokoa. Yesu wa Nazareti anawazidi manabii wote, pia na wanafilosofia na viongozi, kiasi jinsi mbingi ilivyo juu kuliko dunia. Uvumbuzi wa watu unashangaza, ila bado unatumia vitu ambavyo Mungu aliviumba. Mwana ndiye uhai na nuru naye ni sababu ya sisi kuwepo. Hakuna chochote cha kufanana naye. Mwana ametokana na Baba kabla ya enzi zote kuwepo. Yeye ni mkamilifu, akizidi viumbe vyovyote.
YOHANA 3:32-35
32 “Yale aliyoyaona na kuyasikia ndiyo anayoyashuhudia, wala hakuna anayekubali ushuhuda wake. 33 Yeye aliyeukubali ushuhuda wake ametia muhuri ya kwamba, Mungu ni kweli. 34 Kwa kuwa yeye aliyetumwa na Mungu huyanena maneno ya Mungu; Kwa sababu hamtoi Roho kwa kipimo. 35 Baba ampenda Mwana, naye amempa vyote mkononi mwake”.
Mwanadamu Yesu ndiye ashuhudiaye kwa macho kweli zote za mbinguni. Yeye kweli alimwona Baba na kusikia maneno yake. Anafahamu mawazo na mipango yake. Yeye ndiye Neno la Mungu, akitokea kifuani mwa Baba yake. Mafunuo yake ni kamili. Mafunuo yaliyokuja na manabii hayakukamilika. Yesu afunua mapenzi ya Mungu kikamilifu na ya mwisho. Yeye ndiye shahidi mwaminifu, aliyepata kutoa uhai wake kwa ajili ya ushuhuda huo. Ndiye aliyemtukuza Baba, ila kwa huzuni twaona kwamba, bado watu wengi wanakataa ushuhuda wake. Hawamhitaji Mungu aliye karibu, maana hilo lingehitaji kubadilisha mwenendo wa maisha. Huwa wanakataa Uwana wa Yesu na Ubaba wa Mungu mwenyewe.
Bwana asifiwe sana kwamba, sio wote wanaomchukia Mungu na Roho yake. Kuna kundi lililochaguliwa, ndilo lina watu wanaomwona Mungu ndani ya Mwana, nao wanakubali sadaka yake iliyo kamili. Yeye anayeamini ufunuo wake na ukombozi wake, anamheshimu Mungu Baba. Mungu hawezi kusema uongo naye Mwana ndiye ukweli nafsini mwake. Baba hakufunua kiini cha mawazo yake akiyajumlisha ndani ya kitabu, lakini ndani ya nafsi ya Yesu. Yeyote aliye wazi kwa Roho ya neno lake, atapata kuwa mtu mpya. Kristo hakuiti tu kusema kweli, bali kuishi kufuatana na kweli na kuifanya iliyo kweli. Hivyo Injili yake itakuwa inaishi ndani yako.
Yesu hakuongea mambo ya kimawazo tu, au yasiyo na uhakika, au yaliyotamanika tu. Maneno yake ni yenye kuumba mambo , yenye uwezo na hata hivyo yaliyo wazi kabisa. Mungu mwenyewe alikuwa akisema ndani ya mwana wake. Roho ndani yake haina mipaka. Baba alimkabidhi hekima yote, pia na enzi yote ya milele.
Mungu Baba alimpenda kabisa Mwana na kuweka mikononi mwake mambo yote. Upendo wa Baba ni zawadi, naye Mwana anamheshimu Baba yake. Hamna swali kuulizia, nani ni mkubwa, Baba au Mwana. Maswali kama hayo yatoka kwa Shetani. Kila nafsi ya Utatu Utakatifu inatukuza wenzake na kuwaheshimu kwa usawa. Yeye akataaye taratibu hii basi anamkataa Bwana. Baba hakuwa na hofu kunyang’anywa enzi yake na Mwana, maana Baba alielewa unyenyekevu wa Mwana, utiifu wake na kwamba alikubali kabisa kujiweka chini ya utawala wa Baba. Hata hivyo Yesu anatawala juu ya yote akisema: “Enzi yote imekabidhiwa kwangu mbinguni na duniani, nikimheshimu Baba aliyenikabidhi”
YOHANA 3:36
36 “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.”
Yohana Mwinjilisti anatufundisha kanuni inayookoa: Yeye amtegemeaye Mwana yuna uzima wa milele. Sentenso hii fupi inajumlisha INJILI kikamilifu. Yeyote anayekaribia umoja huo wa upendo unaojionyesha katika Baba na Mwana, anakaribia upendo wa Mungu uliodhihirishwa msalabani. Anategemea Mwana Kondoo wa Mungu, akifahamu kwamba, Kondoo huyo ameondoa uchafu wetu. Kwa uhusiano huo na Kristo tunatambua ukweli wa rehema zake katika upendo unaoendelea hata milele. Imani hiyo ndani ya Mwana aliyesulibiwa inatuunganisha na uhai wake wa kweli. Uhai wa milele hauanzi tu wakati tukifa, lakini sasa tunapoanza kupokea imani hii. Roho Mtakatifu atakuja juu ya waumini ndani ya Mwana. Akataaye maneno hayo ya Kristo na kutokuamini Uwana wake na msalaba, anamhuzunisha Roho Mtakatifu. Hatapata utulivu ndani ya dhamiri yake. Asiyejikabidhi kwake Yesu anamkataa Mungu mwenyewe na kuendelea katika hali ya kifo cha kiroho. Dini zote zinazokuwa kinyume cha kanuni za Mwana na msalaba wake zinagongana na ukweli wa Mungu. Anayekataa upendo wake anachagua ghadhabu yake.
Paulo naye anathibitisha msimamo huo wa Yohana: Ghadhabu ya Mungu inadhihirishwa juu ya uasi wote na uovu. Maana wote wametenda dhambi na kuwa kinyume cha ukweli kwa makosa yao. Tambua kwamba, ghadhabu ya Mungu inayoangamiza itamwagika juu ya wanadamu wote.
Jinsi yule nyoka wa shaba ilivyoinuliwa jangwani, ndivyo Msulibiwa amekuwa ishara ya wokovu wetu kutuondolea hasira ya Mungu. Mwana ametufungulia ugawaji wa neema. Yeyote anayezuia neema yake mbali na msalaba kwa kusudi, anadumu chini ya hukumu. Shetani hupata nafasi ndani yake.Watu wasio na Kristo wataharibika. - Eti, lini utaanza kumwombea mtu mmoja mmoja unayemfaham, ili naye apate kumwamini Mwana na kuokoka? Lini utawazungumzia kwa taratibu na upendo marafiki zako, ili nao wapate kuelewa na kupokea uhai wa Mungu kutokana na ushuhuda wako?
SALA: Bwana Yesu, tunakuhimidi kwa ajili ya upendo na ukweli wako. Tunakuabudu, tukiomba tupewe moyo wa utii, iliyoimarishwa katika imani na kwa kumheshimu Baba. Kwa tumaini letu tunatamka kwamba, wewe na Baba ni Mmoja. Wahurumie wale wanaokukataa kwa kutokutambua. Wajalie wafunuliwe ushuhuda wa neno lako. Utusaidie sisi tuwatafute wale, ambao wewe unatutuma kwao, ili tuwaeleze habari zako na kazi yako kwa ajili yetu.
SWALI:
- Jinsi gani tunapokea uzima wa milele?