Previous Lesson -- Next Lesson
6. Jumlicho la sheria au amri za kuhusu watu (Warumi 13:7-10)
WARUMI 13:7-10
"7 Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru; astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima. 8 Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. 9 Maana kule kusema, usizini, usiue, usiibe, usitamani; na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. 10 Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.“
Utawala na wizara ya fedha ya Serikali ya Kirumi hazikuwa jambo muhimu kwa waumini wakati wa mtume Paulo, maana Wakristo walikuwa ni kundi ndogo, wala hawakuwa na nguvu kwenye utoaji wa sheria za serikali. Kwa hiyo, mtume aliwaagiza Wakristo walipe kodi na ushuru bila kudanganya au kupinda hayo maaagizo, watii pia amri na taratibu, na waheshimu idara za serikali, wakijua kwamba, kuomba kwa ajili ya wenye dhambi na wenye mamlaka ndiyo wajibu wao ili kwamba, maofisa wa serikali watende kwa taratibu na busara. Lakini basi, mambo yakaenda vingine, mbali na taratibu za kawaida ndani ya Serikali ya Kirumi. Wao wakawa kinyume cha Kristo, hata wakatoa maagizo ya kuua wakristo wote, ambao hawakumwabudu Kaisari, nao wakawatupa mbele za wanyama wakali wawaue hadharani ndani ya viwanja vyao vya michezo.
Paulo mwenyewe alizaliwa akiwa raia wa Kirumi. Yeye alijiona kuwa na wajibu mbele za serikali yake yenye enzi, naye alitaka yatumika maneno ya Kristo: „Timiza kwake Kaisari mambo yaliyo yake, na upande wa Mungu pia mambo yaliyo ya Mungu.“ Ila kuhusu Kanisa alifahamu kwamba, sheria ya Kristo inakuwa juu ya kanuni zote za kidunia, maana Yesu alisema: „Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi“ (Yohana 13:34-35).
Kila Mkristo apendaye jinsi Yesu alivyopenda wanafunzi wake na kuwahudumia, basi atakuwa ametimiza agizo la Yesu. Upendo huo tukufu ndiyo kanuni na mwenendo wa kawaida wa kanisa, naye Roho Mtakatifu ndiye enzi inayotakiwa na kiini cha kutimiza kanuni hiyo. Pamoja na hayo, Kristo hakufuta amri ya Musa: „Umpende jirani yako kama nafsi yako“ (Mambo ya Walawi 19:18).
Paulo alieleza amri hiyo kwa njia ya sehemu ya pili za Amri Kumi, akisema: Usiwe na chuki, au usimwue mtu yeyote. Usizini. Usiishi kwa uchafu. Usiibe, bali fanya kazi kwa bidii. Usiwe na wivu na mtu kwa sababu ya mali yake, bali uridhike na vipawa ambavyo Mungu amekujalia. Kwa kutimiza maagizo hayo utakamilisha amri ya kumpenda jirani yako.
Mtume hakusema kwa shauku au kwa ufasaha, lakini alikaza kwamba, kujizuia na uzinzi ndiyo hatua ya kwanza na muhimu ya kuishi kwa upendo wa kweli. Alidai kwamba, upendo tukufu, yaani agape, ishinde upendo wa kutwaana, yaani eros.
Upendo wa kweli hausimami kwenye hali ya kujiona, lakini kwenye shabaha ya kuwaangalia wenye haja na kuwahudumia kwanza. Tunaposhiriki kwenye shida, matatizo na mateso ya wengine, basi inatupasa tusitokeze shida, matatizo au mateso kwa yeyote, bali tumsaidie katika magumu yake, tumfariji katika shida zake, pia na kumwimarisha katika haja zake.
Hilo swali, „Nani ni jirani yangu?“ lilikuwa limeisha kujibiwa na Kristo. Linalomaanishwa sio jamaa zetu za damu, za ukoo, bali yeyote aliye karibu nawe unayekutana naye na kumwona kwamba, anatazamia neno la faraja kwako. Jambo hilo lajumlisha pia kueneza ujumbe wa injili kwa wengine, maana „Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo“ (Matendo ya Mitume 4:12).
SALA: Ee Bwana Yesu Kristo, tunakuabudu kwa sababu ulilipatia kanisa lako amri mpya, na ulilijalia nguvu ya Roho Mtakatifu liweze kulitimiza. Utusamehe kama tumeenda kwa haraka haraka na mioyo migumu. Tusaidie kuwaelewa vizuri rafiki zetu, ambao tunawaombea, wabariki na kazi, ili waweze kujipatia ridhiki za kila siku. Pia utufundishe kuwahudumia wote kila mahali walipo.
SWALI:
- Jinsi gani Paulo alieleza kwa kihalisi hiyo amri: „Umpende jirani yako kama nafsi yako“?