Previous Lesson -- Next Lesson
5. Uwe mtiifu kwa mamlaka iliyo juu yako (Warumi 13:1-6)
WARUMI 13:1-6
"1 Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu. 2 Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu. 3 Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake; 4 kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu. 5 Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri. 6 Kwa sababu hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika kazi iyo hiyo.“
Wengi huteseka kutokana na mashindano kati ya vyama tofauti tofauti, kwa ajili ya udanganyifu wa watumishi, kwa ajili ya serikali isiyotenda haki, na pia kwa ajili ya fitina ya upofu. Kwa jumla hakuna mamlaka iliyo kamili duniani mle, maana hakuna mtu asiye na dhambi katika dunia hii. Kwa hiyo basi, uvumilie serikali yako, jinsi Mungu anavyokuwa radhi na wewe na familia yako.
Mtume alikuwa amefunuliwa kwamba, hakuna serikali inayotawala juu ya watu wake, isipokuwa imepangwa na Mungu mwenyewe na kutiwa nguvu naye. Kwa hiyo, itawajibika kwa Mhukumu wa milele. Hivyo basi, watu watumiao rushwa, nao wanastahili kuwa na serikali inayotumia rushwa.
Ukichimba chini sana ndani ya maneno ya mtume wa Mataifa, utakuta matamko mageni sana:
Mtume Paulo huita serikali kuwa ni „wahudumu wa Mungu“ mara mbili. Kwa hiyo, inapoimarisha taratibu za kweli na haki, Mungu ataibariki na kuijazi pamoja na raia zake. Lakini ikipinda kweli au kupokea rushwa, ndipo Mungu ataiadhibu. Watumishi wa serikali, kufuatana na wito wao, ni watumishi wa Mungu, nao watatambua ulinzi wa Mungu, au hukumu na maadhibio yake.
Yesu naye alikuwa amesema jambo hilo kwa habari ya wajibu wa raia kwa mambo ya ushuru na kodi alipotamka: „Mlipeni Kaisari yalyo ya Kaisari na Mungu yaliyo ya Mungu“ (Mathayo 22:21). Kwa tamko hilo Kristo aliwaonyesha watu wajibu wao kwa kufanya iwapasavyo kwa upande wa serikali bila kuchelewa; na kwa wakati uo huo aliiwekea mipaka mamlaka ya serikali. Kwa hiyo, ikiwa mamlaka yoyote inakwenda kinyume cha Mungu wa kweli na amri alizoziweka, au ikiwa inaagiza kuabudu mungu mwingine tofauti na Mungu wa kweli, basi ingewapasa watu kukataa mamlaka ya namna hii. Maana „imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu“ (Matendo ya Mitume 5:29b), hata kama kukataa hivyo, kwa sababu ya imani yake, inaweza kumletea kufukuzwa, kuteswa au hata kuuawa. Nchi zinazozunguka Bahari ya Kati zimenyweshwa na damu ya wafia dini, ambao walikuwa ni askari wa maombi kwa ajili ya serikali zao, ila walikataa kufuata maagizo yao yaliyokuwa kinyume cha Roho wa Kristo.
Biblia takatifu inatueleza kwamba, siku za mwisho mshindani mkuu wa Kristo atainuka kuwa na mamlaka juu ya watu wote wa dunia, naye atawaagiza wote kumwabudu yeye badala ya Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Inasema pia kwamba, yeyote atakayeomba kwa Mungu, atahesabiwa kuwa mpinga wa maagizo ya yule mshindani mkuu wa Kristo, ambazo ni kinyume cha Mungu, na mtu huyu atakufa kifo cha maumivu mengi. Hata hivyo, itakuwa ni bora kwa mtu yeyote kuteseka kwa muda mfupi kuliko kupotea kwa milele.
Pia ni wajibu wetu wa kiroho kufanya sala wakati wa uchaguzi wa serikali yetu na katiba yake, na pia kwa ajili ya kufaulu kuweka haki zake, maana viongozi wa serikali hawawezi kutenda yaliyo mema, isipokuwa kwa neema ya uaminifu wa Mungu.
SALA: Ee Bwana Yesu, wewe ulimtii Baba yako kuliko kuwatii watu, na kwa sababu hiyo ulipata kusulibiwa. Utusaidie kuomba kwa ajili ya serikali yetu itende yaliyo mema, na utujalie ujasiri ya kuikataa, ikiwa inatutaka kutulazimisha kutokuamini au kutenda yaliyo maovu.
SWALI:
- Mipaka ya mamlaka ya kila serikali ni ipi, na kwa nini inatupasa kumtii Mungu kuliko watu?